27 Dec 2007


Mwanasiasa mahiri na Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistani,Benazir Bhutto ameuawa baada ya kupigwa risasi mjini Rawalpindi,karibu na mji mkuu wa nchi hiyo Islamabad.Mwanamama huyo ambaye alirejea nchini humo hivi karibuni akitokea kwenye hifadhi ya kisiasa,alipigwa risasi mbili,moja ya shingoni na nyingine ya kifuani,baada ya kumaliza kuhutubia mkutano wa hadhara.Aliyemuua alijilipua kwa bomu la kutoa mhanga baada ya shambulio hilo.Angalau watu 20 waliuawa pia katika shambulio hilo linalotarajiwa kuiingiza Pakistan katika machafuko.
-------------------------------------------------------------------
NANI ANAHUSIKA NA MAUAJI HAYO? (Uchambuzi wa kiuanafunzi)
Jibu jepesi ni YEYOTE.Kifo hicho kinaweza kuwa ni mkakati wa Al-Qaeda kuhakikisha Pakistan inaendelea kuwa "unstable" hivyo kuweka mazingira mazuri ya kustawi kwa "cells" za kikundi hicho cha kigaidi.Pia mauaji hayo yanaweza kuwa kazi ya kikundi chochote kile chenye msimamo mkali wa kidini (ambacho pengine hakina mahusiano na Al-Qaeda).Kwanini wamuue?Sababu kuu ni kwamba mwanamama huyo alikuwa akiwakilisha yale yote yanayopingwa na vikundi vyenye msimamo mkali:demokrasia,haki za akinamama,mahusiano mazuri na Marekani na nchi za Magharibi bila kusahau sapoti yake kwa vita dhidi ya ugaidi.Lakini pia,Bhutto anaweza kuwa ameuawa na "elements" flani ndani za mfumo wa siasa za nchi hiyo (majenerali walio madarakani na wastaafu,mashushushu,nk).Baadhi ya hawa wanaweza kuwa maadui aliowatengeneza kipindi cha utawala wake,lakini wengine wanaweza kuwa wale ambao hawakuwa radhi kumwona mwanamama huyo akirejea kwenye upeo wa kisiasa wa nchi hiyo.

Mmoja wa wasaidizi wa Bhutto anadai kuwa aliandikiwa barua na mwanasiasa huyo hivi karibuni ambapo aliwataja watu watatu walio kwenye serikali ya Rais Pervez Musharaf ambao alidai wana mpango wa kumkwamisha katika harakati zake za kisiasa.Lakini pia Oktoba 18 mwaka huu,Bhutto alinusurika kuuwawa katika shambulio lililogharimu maisha ya mamia ya wafuasi wake.Kwa mtazamo wa mbali zaidi,kidole kinaweza kuelekezwa kwa Ramzi Yousef (ambaye kwa sasa yuko gerezani nchini Marekani kwa kuhusika kwake na mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11,2001).Mwezi Julai mwaka 1993,Ramzi alijaribu kumuua Bhutto kwa bomu lakini hakufanikiwa.Ilifahamika baadae kwamba gaidi hiyo alikuwa akitekeleza mpango ulioandaliwa na "elements" flani ndani ya Pakistan,katika baadhi ya nchi za Ghuba na kamanda mmoja wa vikundi vya Afghanistan aliyekuwa na "connection" na Saudi Arabia.

Kama nilivyosema mwanzoni,YEYOTE kati ya makundi hayo niliyoyataja,anaweza kuwa mhusika.Ukweli unabaki kuwa uamuzi wa mwanamama huyo kurejea Pakistan kutoka kwenye hifadhi yake ya kisiasa ulikuwa ni sawa na kujiandikia hukumu ya kifo kwani alikuwa na maadui wengi,ndani na nje ya Pakistan.Bhutto mwenyewe alikiri kufahamu kwamba uamuzi wake wa kurejea Pakistan ulikuwa ukihatarisha maisha yake,na hilo linaweza kumfanya akumbukwe kwa ujasiri wa kutoogopa kuuawa (japo sasa ameuawa) kwa minajili ya kuwatumikia Wapakistani.

PS: Huu ni uchambuzi wangu binafsi kama mwanafunzi wa Siasa za Kimataifa,jisikie huru kunikosoa.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube