Riyadh,Saudia,April 16
Wafanyabiashara wa Saudi Arabia wameiomba Tanzania kama wanaweza kukodi hekta nusu milioni (500,000) za ardhi inayofaa kwa kilimo hususan cha mpunga na ngano kama sehemu ya mpango wa kujitosheleza kwa chakula kwa falme hiyo ya jangwani.
Maofisa waandamizi wa chemba ya biashara ya jiji la Riyadh walitoa ombi hilo wakati wa ziara ya Rais Jakaya Kikwete katika falme hiyo.
"Tanzania ipo tayari kufanya biashara nanyi.Kuna heka milioni 100 (hekta milioni 40.5)za ardhi nzuri yenye rutuba",Kikwete aliwaambia wafanyabiashara hao.
Samir Ali Kabbani,mkuu wa kamati ya kilimo ya chemba hiyo alisema kwamba wamepata majibu mazuri sana."Kikwete ametuambia kwamba Tanzania inaweza kutukodisha ploti ambazo kila moja ina ukubwa wa hadi hekta 10,000 kwa kipindi cha miaka 99",Kabbani alilieleza Shirika la Habari la Reuters baada ya mkutano huo na Kikwete.
Maofisa na wafanyabiashara wa Kisaudi walitrajiwa kuitembelea Tanzania wiki chache baada ya mkutano huo.
"Wanaweza kukodi ardhi kutoka serikalini",January Makamba,msaidizi wa Rais Kikwete,aliieleza Reuters."Lakini inabidi tuhakikishe kuwa hatuishii kwenye hali kama ile ya Nigeria:hifadhi kubwa ya mafuta lakini foleni kubwa kwenye vituo vya kuuzia mafuta",alisema Makamba.
Maafisa wa Saudia wanaiona Tanzania kama sehemu mwafaka kutokana na mazingira ya kijiografia,kisiasa na wingi wa maji na ardhi ya kilimo.Makampuni kadhaa ya nchi hiyo tayari yameanza kuwekeza katika miradi ya kilimo huko Indonesia na Ethiopia.
Agosti mwaka jana Indonesia ilisema kuwa mjumuiko wa makampuni ya Bin Ladin ya Saudi Arabia unatarajia kuwekeza dola bilioni 4.3 katika hekta 500,000 za kilimo cha mpunga.Mahitaji ya ngano kwa Saudia kwa mwaka yanakadiriwa kufikia tani milioni 2.5,na mwaka juzi nchi hiyo iliagiza kutoka nje karibu tani milioni 1 za mchele,kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya Marekani.
CHANZO: Reuters