HII ya Yanga haijapata kutokea kwenye historia ya soka ya Ligi Kuu Tanzania Bara. Ndio kauli nyepesi unayoweza kuitumia kama ukipata nafasi ya kupita karibu na kambi ya Yanga jijini Dar es Salaam.
Yanga imeweka kambi kwenye Hoteli ya Lamada Ilala, jijini Dar es Salaam chini ya ulinzi mkali wa askari ambao haujapata kutokea kwa timu yoyote ya Tanzania pengine tangu Ligi Kuu Bara ianzishwe.
Ulinzi huo ambao wachezaji wa Yanga wamesema kwamba hawajapata kuuona, unadaiwa kuwekwa na mdhamini mkuu wa klabu hiyo, Yusufu Manji kutokana na kikosi hicho kukabiliwa na pambano gumu dhidi ya Simba Jumapili kwenye Uwanja Mkuu wa Tanzania jijini Dar es Salaam.
Walinzi hao wengine wakiwa na silaha ambao wametapakaa kila kona mpaka kwenye korido za kwenda vyumbani, walimwagwa hotelini hapo juzi Jumapili jioni wakati mechi baina ya Yanga na Polisi Dodoma ikiendelea kwenye Uwanja wa Taifa. Yanga ilishinda 3-1.
"Tuliporudi tu ile jioni tukashangaa mazingira yamebadilika ghafla, kila kona ina walinzi na wengine wamebeba silaha na wengine wana virungu pamoja na baadhi ya wanachama ambao walikuwa wanapitapita huku na huko kutulinda," alidokeza mchezaji mmoja.
"Sijapata kuiona hali hii, mpaka wachezaji tunashangaa kwa jinsi walinzi walivyomwagwa huku nje wapo kama 12, kwenye korido za vyumbani wapo na kwenye ngazi za kushukia pia wapo.
"Huruhusiwi kutoka nje ya geti na hata ukikaa nje mazungumzo yako yanafuatiliwa kila hatua, yaani mpaka wageni wanaoingia wanaulizwa maswali kama ni mtu mwenye chumba chake lazima waende mpaka chumbani wakahakikishe kama kweli ana chumba.
"Sisi wenyewe wakati unatoka chumbani unaulizwa unakwenda wapi, ukitoka nje kwenye ngazi unawakuta pia hawa walinzi wanafanana na wale wa ile kampuni inayolinda kule ofisni kwa Manji."
Mchezaji mwingine alisema; "Huku ni mitutu tu kila upande bwana, hata kama unaenda nje kununua vocha au kitu chochote kuna walinzi.
"Kwa jinsi palivyo huku utafikiri tunacheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika tena na Real Madrid, ni kasheshe tupu ndugu yangu lakini ndio soka," alisema mchezaji mwingine.
Mwanaspoti ilipojiri kwenye kambi ya timu hiyo jana, askari hao walicharuka mithili ya mbogo wenye njaa na hawakutaka kusikiliza chochote.
"Unakwenda wapi? Wewe ni mteja hapa au unakwenda kuwaona wachezaji wa Yanga?" Walisema walinzi hao wakiwazuia waandishi wa Mwanaspoti kuingia ndani ya hoteli hiyo.
"Huwezi kuingia humu hotelini mpaka upate kibali cha Yanga, wasiliana na mwenyekiti au meneja wa timu," alisema askari mmoja wa kampuni ya Group 7 Security aliyekuwa ameshika rungu.
"Ondokeni eneo hili haraka, usije ukatusababishia matatizo makubwa au tukakufanya chochote baadaye ikawa matatizo, ondoka bwana kwa usalama wako," alisema mlinzi mwingine aliyekuwa amekunja sura.
Waandishi wa Mwanaspoti wamekuwa wakienda mara kwa mara katika hoteli hiyo kufanya mahojiano na wachezaji wa timu hiyo, lakini kila kitu sasa kimebadilika na mawasiliano pekee yaliyobaki ni kwa njia ya simu.
Yanga ambayo imekuwa ikinyanyaswa na Simba kwenye Ligi Kuu Bara kwa takribani miaka saba sasa, inaonekana kujizatiti na kutaka kulipiza kisasi na hasa kutokana na hali kutokuwa shwari ndani ya Simba.
Viongozi wa Yanga wameapa kufanya mauaji makubwa Jumapili kwa madai kuwa dalili za kuimaliza Simba zilianza mwishoni mwa wiki wakati Toto wenye urafiki na Yanga walipoifunga Simba mabao 4-1
0 comments:
Post a Comment