24 Oct 2008


Na Peter Edson
JUMUIYA ya Kikristo Tanzania (CCT) imemuonya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuwa kauli zake kuhusu kujiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Nchi za Kiislamu (OIC) zinaweza kusababisha mgawanyiko wa kitaifa na kumtaka aachane nazo au ajiuzulu wadhifa wake.

Tamko hilo la maaskofu wa makanisa ya Kikristo imekuja baada ya Waziri Membe kukaririwa akisema kuwa hakuna athari zozote kwa Tanzania kujiunga na taasisi hiyo, ambayo madhumuni yake ni kutetea binadamu na hasa Waislamu na sehemu takatifu.

Membe alisema hakuna haja ya kuwa na woga wa kujiunga na taasisi hiyo wakati katika mchakato wake wakristo na waislamu watanufaika na miradi itakayokuwa ikisimamiwa na OIC, na akashangaa ujasiri wa Watanzania wa kupambana na matatizo umekwenda wapi kiasi cha kuogopa nchi kujiunga na jumuiya hiyo.

Suala hilo liliwahi kuibuka mwishoni mwa utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi wakati vyombo vya habari vilipofichua kuwa serikali ilijiunga kinyemela na jumuiya hiyo. Baadaye viongozi wa serikali walikiri kufanya hivyo kabla ya kujiondoa, lakini safari hii upinzani umekuwa mkubwa zaidi.

Wakitoa tamko lao kwa waandishi wa habari jana, maaskofu hao kutokana makanisa ya kiprotestanti walisema kauli ya Waziri Membe ina lengo la kutetea maslahi ya watu wachache.

Maaskofu hao walisema kwa kuwa katiba ya OIC hiyo inaeleza bayana kuwa italinda mila, desturi na tamaduni za kiislamu, kujiunga na jumuiya hiyo itakuwa ni kukiuka katiba ya nchi inayoeleza kuwa dini ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi, na kwamba shughuli ya uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchini.

"Kama serikali ikikubali, kutakuwa ni mwanzo wa kuruhusu kubomoka na kuvunjika kwa amani ya nchi kwa sababu yanagusa hisia na itikadi za wananchi," alisema Askofu Peter Kitula, ambaye ni makamu mwenyekiti wa kwanza wa CCT.

Askofu Kitula, ambaye alisoma tamko hilo la maaskofu, alisema baada ya kutafakari kwa roho ya kiutume na kinabii wameamua kupinga kuanzishwa kwa mahakama ya kadhi pamoja na mchakato wa kujiunga na OIC.

Alisema katiba ya Tanzania ibara ya 19 kifungu cha 2 inaeleza wazi kuwa kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi, na shughuli ya uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchini.

"Ibara hii ni muhimu sana kwa ajili ya kusimamia na kuhakikisha kwamba mambo ya dini yanatenganishwa kabisa na shughuli za uendeshaji wa nchi," alisema.

Alisema sehemu hiyo ya katiba inapingana na ibara ya 1 kifungu cha 11 ya katiba ya OIC kinachosema kuwa jumuiya hiyo inatetea mila, tamaduni na desturi za kiislamu, kuwalinda na kuwaelimisha wananchi kuhusu uislamu nchini, jambo ambalo askofi huyo alisema linaonyesha wazi kuwa kujiunga na IOC itakuwa ni ukiukwaji wa katiba.

Alisema siku za hivi karibuni Bunge la Jamuhuri ya Muungano limekuwa likijadili miswada ya sheria ya kuanzisha au kujihusisha na vyombo hivyo viwili, lakini akasema kuwa kushinikiza kukubalika kwake ndani ya bunge ni kwenda kinyume na katiba.

Naye Owdernburg Mdegela, askofu wa dayosisi ya Iringa ya Kanisa la Kiinjili la Kilutherani Tanzania (KKKT), alisema kitendo cha Waziri Membe kulizungumza jambo hilo bila kulionea haya ni kutetea maslahi ya watu wachache na kuvunja katiba.

Alisema Tanzania ina rasilimali za kutosha hivyo kujiunga na umoja huo kwa lengo la kutafuta misaada ama kutafuta kula na baadaye kupoteza mwelekao wa taifa, ni kujiingiza katika mtego ambao kujinasua kwake kunahitaji gharama ambayo ni kumwaga damu.

"Sisi tunasimama kama viongozi wa kanisa tukimwambia Membe kuwa hafai wadhifa huo, hivyo ni vema akaacha mara moja kutoa kauli zake zisizo na mantiki. Lakini kama hawezi, basi inampasa ajiuzulu," alisema Askofu Mdegela.

Naye askofu wa kanisa pentekoste, Sylivester Gamanywa alisema Waziri Membe anatoa kauli ambazo zina lengo la kuweka hisia binafsi na mgawanyiko wa kitaifa pamoja na kuvunjika kwa amani.

Alisema kitendo cha waziri huyo kusema kuwa serikali inaruhusu fedha chafu na kwamba kama mtu akikuta fedha za shetani inampasa kuzichukuwa, ni kuwadhalilisha Watanzania na taifa lao kwa ujumla.

Naye askofu wa Anglikana, Dk. Stephen Munga alisema kuwa waziri Membe hafai katika kushughulikia masuala ya kitaifa kwani hakuna mamalaka yoyote iliyomuagiza aende kuzungumzia suala la kuaanzishwa kwa OIC.

"Inampasa Waziri Membe afahamu kuwa sisi ni Tanzania na tutafuata mambo yetu na si kuiga masuala ya nje. Anavyosema tuwaige Waganda si jambo sahihi," alisema Dk. Munga.

Alisema kama kanisa msimamo wao ni kuyakataa mambo hayo mawili na kuitaka Serikali na mamlaka zake zote kuacha kuendelea kukaribisha mijadala ya mambo hayo kwani kufanya hivyo ni kupoteza muda wa wenye dhamana ya mamlaka ya nchi hii na rasilimali zake.

"Tunauhakika kuwa yaliyomo ndani ya OIC ni hatari kabisa, kwani endapo yakikubalika katiba ya nchi itakuwa imevunjwa na Watanzania watakuwa wameingia katika migogoro itakayoua maridhiano, mshikamano, utengemano na umoja wa kitaifa," alisema Askofu Kitula.

"Kwa kuzingatia wajibu wetu wa kinabii na kiutume, tunatoa wito kwa bunge kutoruhusu kamwe uanzishwaji wa mahakama ya kadhi kwa kupitia mchakato wa utendaji wa mamlaka ya nchi, pia kutoridhia uanachama wa Tanzania katika OIC."

Akizungumzia tamko la maaskofu, mwenyekiti wa kamati ya msikiti wa Idrissa, Sheikh Ally Basaleh alisema kuwa awali kabla ya kuanza kwa mchakato wa masuala hayo serikali ilishafanya uchambuzi wa kina na kugundua umuhimu wa kuanzishwa kwa vyombo hivyo.

"Kauli za maaskofu hawa na viongozi wa kanisa zinadhihirisha kuwa wanakataa maamuzi yao ya awali kwamba Rais Jakaya Kikwete ni mteule wa Mungu, kwani ndiye anayesimamia masuala haya yote," alisema Basaleh.

Alisema waislamu ni sehemu ya jamii hivyo wao kama viongozi wa dini wanaandaa mchakato wa kutoa tamko litakalokuwa likitoa mchanganuo kuhusu uhalali wa kuanzishwa kwa vyombo vyote hivyo viwili nchini.
CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.