TAMKO LA TAASISI YA MASHEIKH NA WANAZUONI WA KIISLAMU TANZANIA KUFUATIA KAULI YA MAASKOFU KUINGILIA MADARAKA YA BUNGE NA KULITAKA LISIJADILI JUU YA MAHAKAMA YA KADHI
--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA KUHUSU MUSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA MBALIMBALI WA MWAKA 2014
Sisi Maaskofu, wajumbe wa jukwaa la Wakristo Tanzania, tuliokutana tarehe 20 Januari 2015, Dar es salaam, tumepata fursa ya kutafakari, kujadili na kujielimisha kwa kina yaliyomo katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya 2014 unaopendekeza, pamoja na mambo mengine, marekebisho ya Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka 1964. Mswaada huu unapendekeza kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi. Baada ya mjadala wa kina tunatoa maoni yetu kama ifuatavyo:
Mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu ni mapendekezo makubwa yatakayokuwa na athari kubwa na nzito; kwani yanahoji msingi wa dola ya Tanzania kama dola isiyokuwa ya kidini. Kwa sababu hiyo, mapendekezo hayo yanaibua mambo mazito ya kikatiba ambayo hayawezi kuamuliwa na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali. Kama ambavyo tumesema mara nyingi, masuala yanayohusu imani za dini na kujiingiza kwa Serikali katika masuala yanayohusu imani hizo yanahitaji mjadala mpana na maridhiano ya kitaifa.
Kwanza, Muswada huu unapendekeza kuanzisha Mahakama za Kadhi, licha ya sababu na madhumuni ya Muswada kusema kuwa lengo ni kutambua mahakama hizo. Kwa utaratibu wa sasa wa kisheria, Mahakama za Kadhi hazipo. Kwa hiyo, hoja ya kutambua uwepo wa mahakama hizo si sahihi. Kama inavyofahamika, Mahakama za Kadhi, pamoja na Mahakama za Wenyeji (Native Courts), zilizokuwepo wakati wa ukoloni zilifutwa na Sheria ya Mahakama za Mahakimu (Magistrates Courts Act) ya mwaka 1963. Tangu wakati huo,mahakama hizi hazipo na hazitambuliwi na sheria yoyote. Hivyo, mapendekezo ya Muswada huu yakipitishwa ndiyo yatazianzisha.
Pili, kwa mapendekezo haya, Serikali inachukua jukumu la kuanzisha yenyewe taasisi za kidini kinyume na utaratibu wa kikatiba ambapo Serikali imekuwa haijishughulishi na uanzishwaji na uendeshaji wa taasisi za kidini. Hii ni kwa sababu Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu haikuanzisha mahakama au taasisi nyingine yoyote ya kusimamia Sheria hiyo bali iliweka utaratibu wa mahakama za kawaida kuitambua na kuisimamia Sheria hiyo.
Tatu, mapendekezo haya yanampa Waziri (ambaye ni kiongozi wa Serikali) mamlaka ya kutunga kanuni za utekelezaji wa maamuzi, hukumu na amri za Mahakama za Kadhi. Maana yake ni kwamba dola ya Tanzania, sio tu inakusudia kuanzisha mahakama ya kidini, bali pia kuweka utaratibu wa kutekeleza maamuzi, hukumu na amri za mahakama hizo.
Nne, mapendekezo haya yanafuta utaratibu ambao umekuwepo kwa zaidi ya miaka hamsini ambao unatambua matumizi ya sheria za dini zisizokuwa za Kikristo katika masuala ya hadhi ya mtu, mirathi, ndoa na talaka kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa, Mirathi na Talaka (Waasia wasio Wakristo), yaani “The Marriage, Succession and Divorce (Non- Christian Asiatics) Ordinance, Cap. 112”. Chini ya utaratibu huo, mila na desturi za watu wa imani zisizokuwa za Kikristo, mfano Wabahai, Wabudha, Wahindu, Khoja, n.k, zilikuwa zinatambuliwa kisheria. Chini ya mapendekezo ya Muswada huu, mila na desturi hizo zinafutwa na kunaingizwa utaratibu utakaotambua na kusimamia masuala na maslahi ya Waislamu peke yao. Ni wazi kuwa utaratibu unaopendekezwa ni wa kibaguzi na kinyume na matakwa/masharti ya Katiba ya sasa.
Tano, kwa mapendekezo ya Muswada huu, hatuna hakika kama mamlaka za mahakama za sasa za kusikiliza na kuamua masuala ya hadhi ya mtu, mirathi na ndoa kwa mujibu wa Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu itaendelea kuwepo. Aidha mapendekezo ya Muswada huu yako kimya juu ya uhusiano wa Mahakama za Kadhi na mahakama za kawaida. Kwa mfano, haieleweki (haikuwekwa wazi) kama kutakuwa na utaratibu wa rufaa, marejeo na mapitio ya maamuzi ya mahakama hizo. Endapo, kwa mfano, mtu hataridhika na maamuzi ya Mahakama ya Kadhi, je, atakuwa na haki ya kukata rufaa? Kama atakuwa na haki hiyo, rufaa hiyo itapelekwa kwenye mahakama au chombo gani? Sita, mapendekezo hayo hayo, pamoja na kwamba wadaawa wataenda kwa hiari yao, yako kimya juu ya kesi zinazohusu Waislamu na watu wa imani nyingine. Na hata kwa wadaawa ambao ni Waislamu, ikiwa upande mmoja (tuseme wa Mdai) unakwenda kwa hiari ila upande mwingine (wa Mdaiwa) unataka shauri lisikilizwe na mahakama ya kawaida, Muswada hautoi jibu nini kifanyike.
Saba, kwa ufahamu wetu, baadhi ya madhehebu na taasisi za Kiislamu hazikubaliani na mamlaka ya Mufti kwenye masuala yao. Hivyo, kumpa Mufti mamlaka ya kutunga kanuni zitakazotumika katika Mahakama za Kadhi na kuwateua makadhi wenyewe kunaweza kusababisha migongano na migogoro ndani ya jamii za Waislamu.
Nane, haturidhiki na hoja kwamba mahakama hizi hazitatumia fedha za umma. Kwa mfano, Waziri atakapokuwa anatunga kanuni atatumia fedha na rasilimali mbalimbali za umma. Vile vile, utekelezaji wa amri na hukumu za mahakama hizi utahitaji polisi na madalali wa mahakama ambao wanalipwa kwa fedha za umma. Tunatambua kwamba suala la Mahakama ya Kadhi lilikataliwa na Bunge Maalumu wakati wa kupitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa. Tunaelewa kwamba hiyo Katiba Inayopendekezwa imetamka wazi kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi “… isiyofungamana na dini yoyote….” Aidha, Katiba hiyo imetamka wazi kuwa “shughuli ya uendeshaji wa jumuiya za dini itakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya serikali”. Hivyo, tunashangazwa na kufadhaishwa na suala hili kuibuka kwenye Muswada huu baada ya kuwa limekataliwa kwa namna hii na Bunge Maalumu.
Kwa sababu zote hizo hapo juu, sisi viongozi wa Makanisa wanachama wa Jukwaa la Wakristo Tanzania tunaamini kwamba sababu zilizopelekea kufutwa kwa mahakama hizi mwaka 1963; yaani, kujenga umoja wa kitaifa, kuondoa ubaguzi katika mfumo wa kisheria na utoaji haki sawa, bado ni halali na za msingi leo hii. Kwa sababu hiyo, kwa heshima kubwa, tunashauri kwamba Serikali iondoe Muswada huu Bungeni ili kuepusha kuvunja misingi ya Taifa hili kama taifa lisilo la kibaguzi na lisilo fungamana na dini
MTAZANO WANGU:
Chanzo cha tatizo hili ni hadaa iliyofanywa mwaka 2005 na Mtandao wa Rais Jakaya Kikwete na CCM kwa Waislam: kuahidi kuwapatia Mahakama ya Kadhi pasipo maandalizi stahili. CCM, chama maarufu kabisa kwa akuahidi lolote lile na chochote kile ili ishinde, ilifanikiwa kwa kiwango kikubwa kuwaaminisha Waislam kuwa sio tu ingewapatia Mahakama ya Kadhi bali pia ingeshughulikia kilio chao cha muda mrefu kuhusu masuala ya elimu na ajira.
Lakini katika hili, ndugu zangu Waislam nao wanastahili lawama, kama ilivyo kwa wenzao Wakristo. Dini zetu hizi kuu, yaani Waislam na Wakristo haziwezi kukwepa lawama katika mwendelezo wa mlolongo wa matatizo yanayoikabili nchi yetu. Pengine si sahihi kuzilaumu dini badala ya viongozi wake au taasisi mbgalimbali za dini hizo. Kwa muda mrefu viongozi na taasisi hizi zimejenga ukaribu na CCM na viongozi wake hata pale ilipobainika wazi kuwa chama hicho kinakwenda kinyume na msalahi ya waumini wa dini hizo. Ninaamini wengi mnakumbuka kauli ya Askofu Mkuu Methodius Kilaini kuwa Kikwete ni chaguo la Mungu. Mtumishi huyo wa Mungu wala hakuona umuhimu kuwaeleza waumini iwapo kauli hiyo ilitokana na mapono kufuatia sala/mfungo au ni mtizamo wake binafsi.
Ndugu zangu Waislam wanafahamu vyema historia ya 'unyanyasaji' dhidi ya dini yao, tangu zama za kupigwa marufuku EAMWS na serikali ya TANU kuipigia chapuo BAKWATA ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa na imeendelea kuwa kama wakala wa serikali badala ya taasisi huru ya uwakilishi wa Waislam. Sasa kama TANU ambayo kwa kiwango kikubwa ilithamini maslahi ya wananchi haikuweza kuyapatia ufumbuzi matatizo ya Waislam, kipi kilichowafanya kuamini ahadi hewa za Mtandao wa Kikwete mwaka 2005?
Mtandao huo ulitumia hadaa ya kuwaahidi Waislam kuwa ingewapatia Mahakama ya Kadhi sambamba na kushughulikia malalamiko yao, ikiwa ni pamoja na suala la kujiunga na jumuiya ya OIC. Lakini kwa vile lengo lilikuwa ni kupata sapoti na hatimaye kura za Waislam, Mtandao huo wala haukujihangaisha kufanya uchambuzi wa kina kuhusu uwezekano na hatimaye utendaji kazi wa Mahakama ya Kadhi.
Suala hilo limekuwa likijitokeza mara kadhaa sasa, na hivi karibuni tu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alirejea hadhaa za CCM Bungeni kwa kudai suala hilo lingeshughulikiwa pasipo kutoa maelezo ya kina.
Sasa limeibuka tena wakati tunaelekea kwenye Kura ya Maoni kuhusu Marekebisho ya Katiba. Pasipo kutanguliza mbele maslahi ya taifa, suala hili linaweza kuzua balaa kubwa. Tayari dalili za wazi zinaonyesha kukosekana kwa mwafaka kati ya taasisi kubwa za uwakilishi wa Waislam na Wakristo, kama inavyoonekana hapo juu.
Suala hili haliwezi kumalizwa kwa hadaa, wala ahadi zisizotekelezeka. Hadi sasa, pamoja na ishara hizo hapo juu zisizopendeza, suala hilo bado ni kama jini linalohangaika kutoka nje ya chupa. Likishatoka, hakuna wa kulizuwia.
Binafsi siku zote nimekuwa nikiamini kuwa Mahakama za Kadhi zinaweza kurejeshwa, lakini si kwa minajili ya ksiasa au mashinikizo ya kidini bali kwa kuzingatia utendaji kazi wa mahakama hizo kwingineko, kwa mfano huko Zanzibar na Kenya.
Wakati nikiwa na matarajio kwamba suala hili litamaliza kwa amani, ni muhimu kwa Watanzania kutokubali kuhadaiwa kirahisi na wahuni wa kisiasa kama ilivyofanywa na Mtandao wa Kikwete na hatimaye kuingizwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho mwaka 2005.
Kwa kumalizia, hivi hawa watu waliotangaza nia ya kutaka urais baadaye mwaka huu mbona wapo kimya sana kwenye masuala muhimu kama hili (na lile la unyama wa polisi kwa CUF) ambayo kwa hakika ni kipimo kizuri cha uongozi wa taifa katika nyakati za mashaka kama hizi? Kwa mtizamo wangu, watu hawa hawana jipya na ni wafungwa wa kiitikadi. Hawawezi kusema lolote muda huu ambapo wanategemea huruma ya CCM kuwapitisha ili waweze kugombea. Mwisho wa siku hapo Oktoba, uamuzi wa mwisho unabaki kwako mpira kura: kukubali 'kuingizwa mkenge' tena kama ilivyokuwa katika miaka 10 ya Kikwete au kujaribu kuwa na Tanzania Mpya itakayoongozwa na watu tofauti kabisa, na ambao kwa ucache wao bungeni ni rahisi kuwawajibisha pindi wakikosea.
MUNGU IBARIKI TANZANIA