19 Nov 2008


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeendelea kusisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinahusika na wizi wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).

Hayo yalibainishwa juzi na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, alipohutubia wananchi wa Manispaa ya Iringa, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mwembe Togwa.

Alisema CCM inahusika na wizi wa fedha hizo, kwani chama hicho ndicho kilichotoa maelekezo kwa makampuni yanayotuhumiwa kuiba fedha hizo.

Alisema CCM ilitumia makampuni hewa yaliyoanzishwa kughushi na kujipatia fedha hizo kwa ajili ya kugharamia kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, uliomwingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani kwa ushindi wa asimilia 80.

Akitoa mfano Zitto alisema, kutokana na rekodi za kibenki za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), CHADEMA ilibaini CCM iliitumia kampuni hewa ya Deep Green Finance, kuchota sh bilioni 10.4, katika kipindi cha miezi minne kati ya Agosti mosi na Desemba 10 mwaka 2005, na kisha kampuni hiyo kutoweka katika faili la Msajili wa makampuni nchini (BRELA).

Alisema katika kipindi hicho CCM pia iliitumia Kampuni ya Tangold Ltd ambayo haikuwa imesajiliwa kisheria, kujichotea kiasi kingine cha sh bilioni 9 kwa madhumuni hayo hayo ya kugharamia kampeni zake.

Aidha, alisema baadhi ya viongozi wa CCM wana uhusiano wa moja kwa moja na Kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd, ambayo ni moja ya kampuni kadhaa zinazodaiwa kuhusika na wizi huo, na kujipatia fedha kwa ajili ya kampeni, lakini vigogo wa CCM waliohusika na wizi huo hawajafikishwa mahakamani.

Alisema, CCM ilimtumia pia mfanyabiashara mmoja maarufu mwenye asili ya Kiasia (jina tunalo) kujipatia kiasi kingine cha fedha, na licha ya mfanyabiashara huyo kurejesha fedha alizochukua bado alifikishwa mahakamani kwa sababu ya kukataa kurejesha kiasi kingine cha fedha.

Alisema mfanyabiashara huyo aliikatalia serikali ya CCM, kurejesha sehemu ya fedha alizochukua kwa sababu kiasi hicho cha fedha ndicho alichokitumia kuwanunulia viongozi wa CCM magari aina ya Mahandra.

“Kama CCM inabisha kwamba haikufadhiliwa wala kununuliwa magari na mtuhumiwa huyo wa EPA, itoe vielelezo vyote vinavyothibitisha kwamba walinunua wenyewe magari hayo. Itoe risiti zote za usajili wa ....na iseme ilitumia fedha kiasi gani wakati wa kampeni. Iseme ilizipata wapi fedha hizo,” alisema Zitto huku akishangiliwa.

Alisema Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati, hajui chochote kuhusiana na jinsi chama chake kilivyopata fedha za kampeni ndiyo maana amekuwa akitetea.

Alisema Chiligati hajui kwa sababu kampeni za CCM wakati wa uchaguzi mkuu 2005, hazikuratibiwa na viongozi wa makao makuu ya chama hicho, bali ziliratibiwa na kundi maarufu la wanamtandao lililokuwa mstari wa mbele kumuunga mkono Rais Kikwete, tangu katika hatua za awali za uteuzi wa mgombea wa chama hicho.

Alisema kwa mara ya kwanza, sakata la wizi wa fedha za EPA, liliibuliwa bungeni na Mbunge wa Karatu, Dk. Willbrod Slaa, lakini wabunge na viongozi wa CCM walisema Slaa alitumia nyaraka za kughushi na hoja yake ilikuwa ya uongo.

Aliendelea kufafanua kwamba, sakata hilo lilipozidi serikali ililazimika kutumia kampuni kufanya ukaguzi ambayo ilithibitisha kwamba ilikuwa ni kweli.

Alisema suluhisho la msingi la kushughulikia kwa haki watuhumiwa wote wa EPA na kuhakikisha kwamba wizi huo hautokei tena, ni kwa serikali kuanzisha Mahakama Maalumu ‘Tribunal’ itakayohusisha wanasheria na majaji wastaafu wanaoheshimika na kuaminika nchini pamoja na wataalamu wazoefu wa masuala ya fedha, kwa ajili ya kushughulikia tuhuma zote za EPA.

Alisema bilioni 133 zilizoibwa ni fedha za umma na wala wananchi wasikubali kudanganywa kwamba fedha hizo si za serikali.

Katika mkutano huo, aliyekuwa kada maarufu wa Chama cha Wananchi CUF katika manispaa hiyo, Mlaki Mdemu, alitangaza kujiunga na CHADEMA na kukabidhiwa kadi ya uanachama na Zitto.

Wananchi waliohudhuria mkutano huo, waliichangia CHADEMA, takriban sh 300,000 na kukitaka chama hicho kiende kwenye Jimbo la Mbeya Vijijini, ambalo liko wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wake, Richard Nyaulawa, kilichotokea hivi karibuni.

Hata hivyo, Zitto aliwaambia wananchi hao kwamba CHADEMA inakusudia kusimamisha mgombea katika jimbo hilo, lakini kwa sasa haiwezi kufanya lolote, kwa kuwa bado inaomboleza msiba huo.


IWAPO MADAI HAYA YA CHADEMA YANA UKWELI (AND CIRCUMSTANTIAL EVEDIENCE SEEMS TO BACK THEM) BASI HUENDA HATA KESI ZINAZOENDELEA MAHAKAMANI NI CHANGA LA MACHO TU.CCM NEEDS TO COME CLEAN ON THIS.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.