27 Nov 2008

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), amezuia kupelekwa mahakamani aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi. 

Karamagi anatuhumiwa kutumia madaraka vibaya katika kusaini mkataba wa mgodi wa madini wa Buzwagi. 
Imedaiwa kuwa, DPP alichukua hatua ya kuzuia kufikishwa mahakamani kwa Karamagi kutokana na ushahidi dhidi ya tuhuma zinazomkabili kutojitosheleza. 

Kesi dhidi ya Karamagi, ilikuwa iwasilishwe katika Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kukamilisha kazi yake. 

Habari kutoka ndani ya kikao watendaji wa serikali na wafadhili wanaochangia bajeti ya serikali kilichofanyika Dar es Salaam jana, zilisema kuwa Takukuru walikwisha baini matumizi mabaya ya madaraka katika sakata zima la Buzwagi, lakini DPP akakataa kesi dhidi ya Karamagi isifunguliwe. 

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mabalozi wote ambao nchi zao zinachangia bajeti kuu ya serikali na Makatibu Wakuu wa wizara mbalimbali. 

Chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya kikao hicho, kilieleza kuwa, wafadhili walielezwa kuwa, Takukuru ilipeleka majalada ya kesi mbili kwa DPP, ikiwemo inayowahusu mawaziri wawili wa zamani, Basil Mramba na Daniel Yona ambayo ilitajwa juzi katika Mahakama ya Kisutu pamoja na la Buzwagi. 

Ilielezwa kuwa, liliporudi jalada la mawaziri hao wawili wa zamani, lilipitishwa kwa ajili ya kupelekwa mahakamani, lakini la Buzwagi DPP alisema hakuna ushahidi wa kutosha kuifikisha kesi hiyo mahakamani, hivyo kulifunga. 

Inadaiwa kuwa, uamuzi huo wa DPP, umeikasirisha Takukuru, ambayo ndiyo iliyokuwa ikikusanya ushahidi ili kesi hiyo iweze kufikishwa mahakamani kwa kuanza kusikilizwa. 

Chanzo hicho cha habari cha kuaminika, wafadhili walielezwa kwamba, majalada ya kesi nyingine nne kubwa, zikiwemo zinazoihusu kampuni ya uchimbaji madini ya Meremeta na Deep Green, bado yapo kwa DPP yakisubiri uamuzi wake. 

Pia Mabalozi hao waliwaomba kushawishi nchi za Ufaransa, Uswisi, Afrika Kusini, Mauritius, Hong Kong kutoa ushirikiano ili kesi hizo tatu ziweze kukamilika. 

Ilidaiwa kuwa, nchi hizo zimekuwa hazionyeshi ushirikiano mara maaofisa wa Takukuru wakihitaji taarifa. 

Jitihada za Nipashe za kumpata DPP, Elieza Feleshi jana ziligonga mwamba, kwani baada ya kuwasiliana naye alieleza kuwa, yupo kwenye kikao na kutaka apigiwe baada ya nusu saa. 

Lakini baada ya muda huo kupita na kupigiwa, alipokea msaidizi wake ambaye alieleza kuwa, bado yupo kwenye kikao na hadi gazeti hili linakwenda mitamboni, kikao hicho kilikuwa bado kikiendelea. 

Nipashe ilipowasiliana na msemaji wa Wizara ya Katiba na Sheria, Omega Ngolle kuhusiana na suala hilo, alisema angeeleza kwa undani suala la jalada la Buzwagi, lakini hakufanya hivyo alipopigiwa simu baadaye. 

Sakata la mkataba wa Buzwagi kusainiwa nje ya nchi kwa mara ya kwanza liliibuliwa Bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini. 

Zitto alidai kuwa, waziri huyo wa zamani alikwenda kusaini mkataba huo, London nchini Uingereza, kwa kutumia mfumo wa mikataba wa zamani wakati serikali ikiwa inajadiliana na wawekezaji kurekebisha mikataba ya madini nchini. 

Suala hilo alilieleza katika mkutano wa nane wa Bunge mjini Dodoma, ambapo alihoji hatua ya Nazir Karamagi kusaini mkataba huo nje ya nchi. 

Baadaye, Zitto aliwasilisha hoja binafsi bungeni, akiomba kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge, kuchunguza hali hiyo. 

Zitto alieleza kushangazwa na uamuzi wa Karamagi kusaini mkataba wa madini kati ya serikali na kampuni maarufu ya madini hapa nchini ya Barrick Gold Mine kwa ajili ya mgodi ya Buzwagi nchini Uingereza badala ya Dar es Salaam. 

Mbali ya kuhoji uhalali wa Karamagi kusaini mkataba huo, kinyume cha maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete ambaye aliagiza kupitiwa upya kwa mikataba yote mipya ya madini, Zitto alikielezea kitendo hicho kuwa kinaongeza wasiwasi wa kuwepo kwa ushawishi wa rushwa. 

Hata hivyo, hoja hiyo ilitupiliwa mbali na Bunge na hatimaye Zitto aliishia kusimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa kile kilichoelezwa amelidanganya Bunge kuhusiana na madai yake hayo. 

Alipewa adhabu hiyo kwa madai ya kutoa kauli ya uongo Bungeni dhidi ya Karamagi, inayohusu kusaini mkataba na kampuni ya Barrick, juu ya mradi wa Buzwagi, jijini London nchini Uingereza.

CHANZO: Nipashe

1 comment:

  1. sijui nasema sijui lakini sijui hata sijui kwanini sijui. Hivi kama kumkingia kifua huyu jamaa wa chama cha CHAI CHAPATI MAHARAGE itakuwaje sijui itakuwaje, kwani inawezekana kabisa wakimkingia wajua sababu za kumkingia ni kuficha yale anayoweza kusema ambayo wao walifanya? ndiyo kama hawakushirikiana naye katika kusaini mkataba hotelini, inakuwaje jamani inakuwaje.
    SAWA LAKINI NIMEKUKOSA SANA MAKALA ZAKO KATIKA JARIDA LETU LA RAIA MWEMA=RAIA MWEMA UGHAIBUNI.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.