10 Nov 2008

Na Mwandishi Wetu, Dodoma 

MKURUGENZI wa kampuni ya Shivacom Tanzania, Bw. Tamir Sonaiya ametoa jumla ya sh. milioni 400 kwa Umoja wa Vijana ya CCM (UVCCM) kwa ajili ya kugharamia Mkutano Mkuu wa Umoja huo unaotarajiwa kufanyika kabla ya Desemba 15, mwaka huu. 

Kati ya fedha hizo sh. milioni 150 zitakuwa ni posho za wajumbe 1,000 wa mkutano huo ambapo kila mmoja atalipwa sh. 50,000 na kiasi cha milioni 250,000 zimetumika katika kutengenezea fulana, mikoba, kofia na bendera za chama kwa ajili ya mkutano huo. 

Fedha hizo zilikabidhiwa jana makao makuu ya CCM mjini hapa mbele ya Rais Jakaya Kikwete. 

Akikabidhi fedha hizo, Bw. Sonaiya alisema kuwa ameamua kujitolea kusaidia chama chake kwa kuwa yeye ni kada mwaminifu wa CCM na vifaa vyote alivyotoa vimetengenezwa kutoka katika kiwanda chake. 

Kwa upande wa Rais Kikwete alimpongeza Mkurugenzi huyo kwa kujitolea fedha hizo na kuwataka makada wengine wa CCM wenye uwezo kusaidia chama hasa kwa wakati huu wa kuelekea uchaguzi Mkuu ambapo fedha nyingi huhitajika ili kugharamia maandalizi ya mikutano hiyo. 

“Kinachosumbua sana kwenye mikutano ni namna ya kupata fedha za kuhudumia mikutano hiyo hivyo kwa hatua iliyofanywa na Umoja wa Vijana itasaidia kuondokana na tatizo la fedha lililokuwa likiwakabili katika maandalizi ya mkutano wao,” alisema Rais Kikwete. 

Fedha hizo zimepatikana kupitia uhamasishaji uliofanywa na kamati iliyoteuliwa na Baraza Kuu la Umoja huo kwa ajili ya kufanya maandalizi ya mkutano huo ikiwa chini ya Waziri wa Nishati na Madini, Bw. Willium Ngeleja, Waziri wa Mambo ya Ndani, Bw. Laurence Masha na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Willium Lukuvi.

CHANZO: Majira


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.