28 Mar 2009


Aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge (61), amewekwa chini ya ulinzi katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam, kwa zaidi ya saa saba baada ya kuhusishwa na ajali ya gari na bajaj ambayo imeua watu wawili. Waliokufa ni wanawake wawili ambao ndugu amejitokeza na kudai kuwa wote ni wageni, waliwasili juzi Dar es Salaam kutoka Mwanza na mmoja alikuwa njiani kwenda Zanzibar kuolewa. Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, ajali hiyo ilitokea saa 10 alfajiri usiku wa kuamkia jana wakati Chenge akiendesha gari namba T 512 ACE aina ya Toyota Hilux na kuigonga bajaj hiyo namba T 736 AXC iliyokuwa na abiria hao wawili wanawake.

Chanzo hicho kilidai kuwa baada ya ajali hiyo, Chenge alikwenda kwanza nyumbani kwake na kuripoti kituoni hapo saa moja asubuhi jana na kuwekwa chini ya ulinzi na kuhojiwa hadi saa saba mchana, huku nje akisubiriwa na ndugu zake. Gazeti hili lilimshuhudia mbunge huyo wa Bariadi Magharibi akiingizwa kwenye gari la Polisi namba PT 0217 na kwenda eneo la tukio karibu na shule ya msingi ya Oysterbay katika makutano ya barabara za Karume na Haile Selassie, ambako alieleza namna ajali hiyo ilivyotokea.

Wakati mbunge huyo akitolewa katika kituo cha Polisi, kulitokea vurugu baina ya ndugu zake na waandishi wa habari, ndugu hao wakitaka kuzuia Chenge kupigwa picha, hali iliyosababisha kusukumana na kurushiana maneno makali. “Ninyi mmezidi kumwonea huyu kwani ni lazima mumpige picha ndio muuze? Hebu tokeni hapa,“ alisikika mwanamke ambaye alikuwa mstari wa mbele kusukuma waandishi, huku akilia na almanusra wapigane na mmoja wa wapigapicha waliokuwa kazini.

Hata hivyo, vurugu hizo zilimalizika baada ya waandishi kuwazidi nguvu ndugu hao na kung’ang’ania kumpiga picha mbunge huyo ambaye awali alikuwa akifunikwa magazeti na nduguze, lakini aliyatoa na kupisha waandishi wampige picha vizuri. Akiwa katika eneo la tukio, Chenge alimwelezea Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Peter Kivuyo, namna ajali hiyo ilivyotokea na alidai ilitokea baada ya bajaj hiyo kutaka kupita gari jingine kwa kasi.

“Bajaj ile ilikuwa inataka kupita gari jingine lililokuwa likitoka Morogoro Stores, bahati mbaya kukawa na gari lingine linakuja, ile bajaj ikabana upande wangu na mimi nilikuwa katika mwendo wa kati ya kilometa 80 hadi 100 kwa saa,“ alidai Chenge. Alidai kuwa baada ya kuona bajaj ile inakwepa gari la mbele wasigongane uso kwa uso, alirudi upande wa kulia ndipo alipoigonga ubavuni kushoto. "Gari la nyuma lingesimama, dereva wake angeweza kueleza vizuri, ila baada ya ajali nikasikia watu wanaita 'Chenge! Chenge!’ nikajua niko salama, nikashuka,“ alidai.

Aliendelea kudai kuwa aliposhuka, alikuta abiria wawili wanawake wakiwa bado wanapumua ingawa kwa shida, lakini walipofika trafiki hali zao zilizidi kuwa mbaya na katika kipindi hicho chote, dereva wa bajaj alikuwa haonekani. Naye askari wa usalama barabarani aliyefika katika ajali hiyo, Mustafa Salum, alimweleza Kivuyo juu ya tukio hilo, ambapo alisema alipata taarifa za ajali hiyo saa 10.30 alfajiri na alipofika eneo la tukio, alikuta tayari abiria hao wawili wameshafariki dunia. “Niliipeleka miili ya marehemu hospitali ya Mwananyamala, ila kwa mujibu wa watu waliokuwa eneo la tukio, waliowaona marehemu hao wawili katika ukumbi wa Maisha Club,“ alisema.

Naye kaka wa mmoja wa marehemu hao, January Constantine, alisema alipata taarifa za kifo cha dada yake, Beatrice Constantine (34) asubuhi na alikwenda kutambua mwili wake hospitalini, lakini kutokana na alivyopondeka alimtambua kwa alama za mwili. Alisema dada yake ni mfanyabiashara na mkazi wa Mwanza na kwamba aliwasili Dar es Salaam, akiwa na rafiki yake huyo na ilikuwa aondoke jana alfajiri kwenda Zanzibar kwa ajili ya harusi ya rafiki yake huyo. Gazeti hili lilishuhudia gari la Chenge kwa mbele likiwa na damu, nywele na mabaki ya ubongo ambao unasadikiwa kuwa wa mmoja wa marehemu hao. Polisi pia iliokota kipande cha fuvu la mtu katika eneo la tukio.

Gari hilo lilikuwa na stika ya Bima ambayo ilikatwa Juni 6, 2006 na kumaliza muda wake Juni 6, mwaka juzi. Naye Theopista Nsanzugwanko anaripoti kuwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema mmiliki wa bajaj hiyo ni Zuwena Nassoro na anatakiwa kuripoti katika kituo chochote cha Polisi huku wakiwa wanamshikilia Chenge Oysterbay ili kuisaidia Polisi. Alisema uchunguzi wa tukio hilo unafanywa chini ya Kivuyo na wataalamu mbalimbali ili kuondoa dhana ya upendeleo kwa kuwa Chenge ni mtu maarufu.

Chenge (62) alijiuzulu uwaziri wa miundombinu Aprili 20 mwaka jana, kutokana na kashfa ya rushwa ya dola milioni moja kutoka kampuni kubwa ya uuzaji vifaa vya kijeshi duniani ya BAE Systems. Alijiuzulu baada ya kudaiwa kupokea rushwa ili kuwezesha ununuzi wa rada ya kijeshi ya pauni milioni 20 za Uingereza na kwamba fedha hizo ziliwekwa katika akaunti yake ya kisiwa cha Jersey.

Baada ya kujiuzulu, alikaririwa akisema pamoja na tuhuma hizo, mapenzi kwa nchi yake na chama chake, ndivyo vilimlazimisha achukue uamuzi huo na kuongeza kuwa fedha zilizokutwa katika akaunti yake hiyo hazina uhusiano wowote na BAE Systems. Tuhuma hizo za rushwa zilichochea kelele pale alipohojiwa na waandishi wa habari na kujibu kuwa fedha anazotuhumiwa nazo ni 'vijisenti (fedha kidogo)'.

CHANZO: HabariLeo

I SMELL DITOPILE-LIKE ADMINISTRATION OF JUSTICE......KWA UBINADAMU WA KAWAIDA TU,GARI LAKO LIKIHUSIKA KATIKA AJALI INAYOPELEKEA HATARI YA MAISHA YA MAJERUHI PRIORITY INAKUWA KWENYE KUOKOA MAISHA YA MAJERUHI HAO (KWA MUJIBU WA HABARI HII MZEE WA VIJISENTI ALIKWENDA ZAKE NYUMBANI HADI SAA 1 ASUBUHI ALIPORIPOTI KITUO CHA POLISI NA KUHOJIWA KWA MASAA 7-(DOES IT REALLY MATTER HOW LONG THE INTERROGATION LASTED WHEN TWO PEOPLE HAD ALREADY LOST THEIR LIVES?).

ANYWAY,LET'S GIVE THE POLICE A BENEFIT OF DOUBT HOPING THAT THIS TIME HAKUTAKUWA NA USANII KAMA KATIKA ISHU YA MAREHEMU DITO.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.