11 Mar 2009


Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi amepigwa kofi na mmoja wa watu waliohudhuria Baraza la Maulid wakati akihutubia katika ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam jana.Mwinyi, ambaye alimwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika Baraza hilo, alikutwa na masaibu hayo baada ya kijana aliyefahamika kwa jina la Ibrahim Said (26) kwenda jukwaani akajifanya fundi na kumpiga kofi la nguvu Rais mstaafu.

Kijana huyo aliyekuwa miongoni mwa umati uliohudhuria baraza hilo, aliinuka wakati Rais mstaafu akizungumzia masuala ya Ukimwi na kwenda hadi jukwaani na kujifanya anarekebisha vyombo vya kupaza sauti vikiwemo na vya televisheni alivyokuwa akitumia kuhutubia.Kijana huyo ambaye alikuwa amevalia suruali ya khaki na shati jeupe, alitumia sekunde kadhaa kujifanya kutengeneza vifaa hivyo akiwa mbele ya Mwinyi na ghafla alimzaba kibao. Kitendo hicho kilisababisha viongozi waliokuwa jukwaani, kusimama ghafla na wanausalama kuingilia kati na kumkata mtama kijana huyo katika juhudi za kumdhibiti asiendelee kuleta madhara.

Miongoni mwa watu waliokuwa katika jukwaa kuu ni pamoja Sheikh Mkuu Mufti Issa Shaaban Simba, Kaimu Mufti Suleiman Gorogosi na Waziri Mkuu mstaafu, Rashidi Kawawa ambao wote walibaki katika mshangao. Baada ya wanausalama kumdhibiti kijana huyo waumini walimwagika na kuanza kumtwanga kwa ngumi na mateke na hivyo wanausalama ikabidi wabadili majukumu na kuanza kumhami. Kutokana na hekaheka hizo shughuli za hotuba zilisimama kwa dakika kama nne.

Pamoja na vurumai hizo, wanausalama walifanikiwa kumuingiza kijana huyo katika gari aina Land Cruiser yenye namba za usajili T 531 AUB na kuondolewa katika viwanja vya Diamond Jubilee na kufikishwa Kituo cha Polisi cha Selander Bridge. Kwa mujibu wa Polisi ambaye hakutaka kutaja jina lake kituoni hapo, alisema katika kumhoji, kijana huyo (Said) alijitambulisha kuwa ni mkazi wa Mabibo Farasi, Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa hizo zilizopatikana kituoni hapo, Said ni mzaliwa wa Mkoa wa Dar es Salaam aliyehitimu kidato cha Sita mwaka juzi katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Tabora. Kijana huyo katika maelezo yake, amejitambulisha kuwa ni Mwalimu wa masomo ya ziada katika Kituo cha Ngome Kongwe, kilichoko Mabibo. Hata hivyo, haikuweza kufahamika sababu za kijana huyo kufanya kitendo hicho kutokana na waandishi kushindwa kupata nafasi ya kuzungumza naye.

Awali, kabla ya kijana huyo kumpiga kofi kiongozi huyo mstaafu wa kitaifa, Mwinyi alikuwa akiwaasa Waislamu kuepukana na ngono zembe zinazochangia ongezeko la Ukimwi. Alisisitiza kwamba ugonjwa huu umekaa mahali pabaya na kuwasihi waumini kuwa ni jukumu la kila mmoja kujilinda. Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mufti Gorogosi, alisema amekuwa akimuona kijana huyo katika mikutano ya dini.

"Hata jana (juzi) katika Maulid usiku alikuwepo, hivyo nashindwa kuelewa kama ana akili nzuri au la," alisema Gorogosi. Alimwomba Rais mstaafu awasamehe Waislamu kwa tukio hilo. Wakati huo huo, Joseph Lugendo anaripoti kwamba Mwinyi amewataka viongozi wa dini nchini kujenga daraja la upendo, baina ya waumini wa dini tofauti badala ya kugeuka kuwa kuta zenye kuwagawa Watanzania katika misingi ya dini.

Aliwataka viongozi hao, wakiwamo masheikh na mapadri, kujenga daraja la upendo na masikilizano baina ya waumini wa dini mbalimbali, ili kuendeleza amani na mshikamano uliopo nchini. Akihutubia mkesha wa Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) usiku wa kuamkia jana Dar es Salaam, Mwinyi alionya viongozi hao wasigeuke kuwa kuta zisizopenyeka zitakazogawa Watanzania kwa misingi ya dini zao.

"Tupo hapa Waislamu na wasio Waislamu kwa kuwa ushirikiano Tanzania ni jadi na mila yetu, sisi huungana kusherehekea siku zote, Waislamu husherehekea na Wakristo siku ya Pasaka na Krismasi na wao hutuunga mkono kwenye Idd zote."Hili ni jambo jema linaloondoa chuki baina ya dini na kuleta mshikamano, mimi napendezwa sana na mwenendo huu na ninatoa mwito kwa mapadri na masheikh kuliendeleza," alisema Mwinyi.

Alisema hawezi kuisemea dini ya Kikristo kwa kuwa haifahamu, lakini miongoni mwa mafunzo yao ni kuwa na subira na kusamehe na kuongeza kwamba mafundisho yao (Wakristo), yamewataka anayepigwa kofi shavu moja ageuze na lingine lipokee kofi la pili. "Huu ni mfano wa kuepusha shari. Lakini na sisi Waislamu pia Mungu katutaka kuwatendea mema na uadilifu ambao hawakupigana nasi wala hawakututoa majumbani kwetu, hakika Mungu huwapenda waadilifu," alisema Mzee Mwinyi huku akinukuu baadhi ya aya kuongeza nguvu katika hoja yake hiyo.

Alisema msingi wa kuishi kwa amani, huanzia katika kaya mpaka jamii na ndio uliosababisha Tanzania kuwa kisiwa cha amani kilichozungukwa na nchi zenye vurugu na kutaja kuwa dini zimechangia kuunda msingi huo. Hata hivyo, alisema kauli hiyo haina maana kuwa nchi zisizo na amani hazina dini, bali malezi ya Watanzania yaliyotekelezwa na viongozi waliotangulia, pia yamechangia sehemu ya amani iliyopo. "Wazee wetu walitandika zulia la utamaduni wa kuishi kwa amani, upendo na utulivu ... katika hali hii ya utu uzima wangu, inanituma kuwausia vijana, tutunze utulivu huu.

"Katu tusiruhusu uondoke tusiwape wenzetu sababu ya kutupa majina mabaya, ya mjahidina na magaidi, vijana nakuusieni tena tusitoe mwanya huo, tumekuwa tukipewa majina na maadui wa nje. "Wanasema dini yetu ni ya fujo, ni wakati wa kushikamana na si wa kulumbana na kama mnajadiliana si mbaya ila kuwepo na staha, heshima na pasiwepo kejeli, ubabe wala dharau dhidi ya dini nyingine," alisema Mwinyi.


CHANZO: Habari Leo


AJALI HUTOKEA,LAKINI LINAPOKUJA SUALA LA ULINZI WA VIONGOZI AJALI ZINAPASWA KUZUIWA KWA GHARAMA YOYOTE ILE.TULISIKIA YALIYOJIRI MBEYA HIVI KARIBUNI AMBAPO KUNDI LA WANANCHI WALIURUSHIA MAWE MSAFARA WA RAIS JK.KWA MTAZAMO MPANA,TUKIO HILO LINGEWEZA KUTAFSIRIWA KAMA SEHEMU YA MAPUNGUFU KATIKA ENEO ZIMA LA ULINZI WA VIONGOZI WETU.NASEMA HIVYO KWA VILE KUNA WATU WENYE JUKUMU LA KUHAKIKISHA USALAMA WA NJIA AU ENEO ATAKALOPITA KIONGOZI,NA NI KWA UHAKIKA KUTOKA KWAO ONLY,NDIPO MSAFARA AU ZIARA YA KIONGOZI ITAENDELEA KAMA ILIVYOPANGWA.THANKS GOD,HAYO MAWE HAYAKUMDHURU YEYOTE,NA PENGINE LA KUSHUKURU ZAIDI NI KWAMBA YALIKUWA MAWE TU NA SIO SILAHA.
SASA TUNASIKIA MZEE MWINYI NAE AMEKUMBWA NA ZAHAMA KAMA INAVYOELEZWA KATIKA HABARI YA HAPO JUU NA PICHANI HAPO CHINI.INAFAHAMIKA KWAMBA ULINZI WA VIONGOZI HUWA MGUMU ZAIDI KWENYE MIKUSANYIKO AU MIKUTANO YA HADHARA LAKINI KWA KAWAIDA UGUMU HUO UNAPASWA KUWA CHANGAMOTO YA MAFANIKIO YA SHUGHULI NZIMA YA KIONGOZI HUSIKA.TUNAPASWA KUMSHUKURU MUNGU KWAMBA ALICHOPIGWA NACHO MZEE MWINYI NI KIBAO TU,LAKINI KAMA TUKIENDELEA NA "BUSINESS AS USUAL" KUNA SIKU ITAKUWA TINDIKALI AU KITU KINGINE CHENYE MADHARA.KAMA MTU HUYO ALIWEZA KUPIGA KIBAO,NI DHAHIRI KWAMBA ANGEWEZA HATA KUCHOMA KISU AU KURUSHA RISASI.KUMKATA MTAMA MHUSIKA WAKATI AMESHAFANYA MADHARA NI SAWA NA KUSOMA RAMBIRAMBI YENYE MANENO MAZURI WAKATI MTU AMESHAPOTEZA UHAI:INALIWAZA LAKINI HAISAIDII.

(Aliyemzaba kibao Mzee Mwinyi akidhibitiwa baada ya tukio.Wajuzi wa mambo ya ulinzi wa viongozi wanaweza kuafikiana nami-kutokana na picha hii-kwamba kuna mapungufu LUKUKI.Picha ya tukio kwa hisani ya MICHUZI Jr)

NI ISHARA NYINGINE KWAMBA KUNA MAPUNGUFU MAHALA FLANI.YAYUMKINIKA KUHISI KWAMBA MAPUNGUFU HAYO NI MATOKEO YA MAZOWEA.KUNA WATU WANATEKELEZA MAJUKUMU YAO KWA MAZOWEA,KWAMBA KWA VILE JANA ILIFANYIKA HIVI BASI HATA LEO ITAFANYIKA HIVYOHIVYO.DHANA YA "HOPE FOR THE BEST EXPECT THE WORST" INAONEKANA KAMA POROJO TU KWA WANAOENDEKEZA MAZOWEA.

TUSIFIKE MAHALA TUKALEWESHWA NA "AMANI NA UTULIVU".KUNA MENGI YANAYOJIRI HUKO MITAANI YANAYOASHIRIA KWAMBA KIWANGO CHA FRUSTRATIONS KWENYE UMMA KINAONGEZEKA.FOR THAT MATTER,KUNA UMUHIMU MKUBWA WA KUENDESHA MAMBO KULINGANA NA HALI HALISI BADALA YA KUONGOZWA NA HISIA AU IMANI ZISIZOZINGATIA REALITY.

IT CAN BE DONE...BUT IF AND ONLY IF SOMEONE OUT THERE PLAYS THEIR PART.2 comments:

  1. Hodi nimekuja kukusalimia. Hapo kazi kwelikweli

    ReplyDelete
  2. Karibu Dada Yasinta.Nashukuru kwa kunitembelea.Nami huwa natembelea pale kwako.Karibu tena.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube