13 Mar 2009


BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limeibua upya hoja za kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga na Jumuiya ya nchi za Kiislamu Duniani (OIC), kwa kuitaka serikali kutafakari kwa kina na hekima juu ya kuridhia kuanzishwa kwa vyombo hivyo.

Kuibuka tena kwa hoja hizo kumekuja miezi michache baada ya Rais Jakaya Kikwete kufunga mijadala hiyo iliyokuwa ikielekea kuwagawa wananchi kwa misingi ya kidini.

Hoja hizo zimeibuliwa juzi kwenye Baraza la Maulid na Naibu Katibu Mkuu wa Utawala wa Bakwata, Suleiman Lolila, ambaye aliitaka serikali iangalie upya na kwa hekima na kama inawezekana iharakishe masuala hayo mawili.

“Tunaipongeza serikali kwa hekima kubwa na jitihada inayoitumia katika kushughulikia masuala ya Mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga na OIC, Waislamu wanangoja kwa hamu na shauku kubwa ridhaa ya serikali, Inshallah, tunaiombea serikali ipate wepesi katika masuala haya maridhawa.

“Tunawaomba Waislamu wadhamirie kwa dhati katika suala hili la OIC na mahakama ya kadhi kwa kutokuruhusu mwanya wowote wa mifarakano miongoni mwetu, kwani mifarakano itakaribisha mgawanyiko na utengano miongoni mwa jamii,” alisema Lolila.

Naibu Katibu Mkuu huyo, akisoma risala ya Bakwata mbele ya Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, alisema ili kuridhiwa kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi na OIC kuna hitaji utulivu wa hali ya juu miongoni mwa waumini wa dini zote mbili (Waislamu na Wakristo) ili kuipa serikali nafasi ya kufanya maamuzi ya busara kwa lengo la kuimarisha umoja wa kitaifa miongoni mwa jamii.

Suala la uanzishwaji wa mahakama ya Kadhi na Tanzania kujiunga na OIC, mwishoni mwa mwaka jana lilizua mjadala mpya nchini, baada ya kufika bungeni na kutishia kuwagawa wabunge kwa itikadi za kidini.

Oktoba mwaka jana katika hotuba yake, Rais Kikwete, hakutaka kuweka wazi ni lini Tanzania itaridhia kujiunga na OIC pamoja na uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, na badala yake aliwatuliza wananchi kwa kuwaambia wavute subira wakati serikali ikilifanyia kazi suala hilo kwa masilahi ya umma.

Rais Kikwete aliweka bayana kuwa ni mapema mno kuanza kutoa uamuzi wa masuala hayo, kwa kuwa bado utafiti haujakamilika pamoja na serikali kutotoa uamuzi wa mwisho, hivyo hakuna sababu kwa wananchi kulumbana.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.