KATIKA matoleo mawili yaliyopita ya jarida hili maridhawa, safu hii imekuwa ikijadili vurugu za kidini zilizojitokeza hivi karibuni nchini.
Katika makala hii, nitaanza sehemu ya kwanza ya kuhitimisha mjadala huo (na sehemu ya pili ya hitimisho itakuwa katika toleo lijalo).Ni matarajio yangu kuwa mfululizo huu wa makala hizi utafungua mjadala mpana zaidi kuhusu hali ya dini nchini Tanzania, nafasi ya dini katika kujenga au kubomoa amani, na hatimaye mapendekezo ya nini kifanyike kudumisha umoja, upendo, amani na mshikamano miongoni mwetu.
Mwamko ulioonyeshwa na makundi mbalimbali ya kijamii katika kulaani na kuzungumzia suala hili unatoa picha chanya kuwa wengi wetu tunatamani kuiona Tanzania yetu ikiendelea kuwa “kisiwa cha amani” (japo neno ‘amani’ lina tafsiri pana, na linaweza kuzua mjadala mwingine mpya. Lakini kwa minajili ya mada hii, tuitafsiri amani kama hali ya utulivu na maelewano miongoni mwa jamii).
Katika makala zilizotangulia, nilijikita zaidi kubainisha sababu ambazo kwa uelewa wangu zilichangia kuleta vurugu hizo za kidini. Nimejaribu kurejea historia ya nchi yetu, kabla na baada ya uhuru, na kuonyesha sababu zilizozalisha manung’uniko ya Waislam, hususan katika maeneo makuu mawili ya upatikanaji (access) wa fursa ya elimu na ajira.
Kwa kuangalia michango mbalimbali ya wanajamii katika mjadala kuhusu vurugu hizo, moja ya hoja inayoonekana kupewa uzito mkubwa ni ile inayodai kuwa chanzo cha vurugu hizo si dini.
Naomba niweke bayana msimamo wangu kuwa binafsi ninazitafsiri vurugu hizo ZINA SABABU ZA KIDINI japokuwa si DINI PEKEE bali pia kuna mwingiliano wa sababu nyingine.
Ninachomaanisha hapa ni kwamba si kweli kuwa vurugu hizo hazihusiani kabisa na dini bali dini ni moja ya sababu za vurugu hizo.
Kwa kuwa katika makala zilizotangulia nimeelemea zaidi katika sababu hizo ‘zisizo za kidini kwa asilimia 100,’ katika makala hii ya mwanzo wa hitimisho nitajaribu kujadili ‘eneo hatari’ la dini kama moja ya chanzo cha vurugu hizo.
Ninasema ‘eneo hatari’ kwa sababu yayumkinika kuhisi kuwa baadhi ya wasomaji hawatopendezwa na uthibitisho nitakaoweka wazi, na ambazo ni lazima tuziongelee ili si tu tuweze kuwa na mjadala wa maana kuhusu suala hili, bali pia tuweze kuwa katika nafasi ya kusaka ufumbuzi.
Kama ilivyo mahala kwingineko (kwa maana ya si Tanzania pekee), uchambuzi kuhusu dini si tu unaweza kuzua hisia hasi (kama vile kuhisi mwandishi Mkristo haruhusiwi kukosoa Uislam, au kinyume chake), lakini pia unakabiliwa na tatizo la msingi la vigezo vingine vinavyoathiri dini husika, kama vile tofauti kati ya mjini na vijijini, idadi ya wakazi katika sehemu husika, historia ya sehemu husika, nk.
Kwa kifupi-na huu ni mfano tu-inaweza kuwa na ugumu wa namna fulani kuuchambua Ukristo kwa kutumia mikoa miwili ya Kilimanjaro na Kaskazini Pemba kama maeneo ya kupata takwimu za kuwezesha uchambuzi husika.
Wakati Kilimanjaro ina idadi kubwa ya Wakristo, Kaskazini Pemba ina idadi kubwa ya Waislamu. Tofauti hizo ‘zisipolindwa vema kwa kuzingatia kanuni za tafiti’ zinaweza kuzua matokeo ‘fyongo.’
Na suala hili la ‘vigezo vingine’ ni moja ya mambo yaliyojitokeza katika utafiti wangu kuhusu harakati za vikundi vya Kiislamu huko nyumbani.
Kwa mfano, baadhi ya wahojiwa wa Kiislamu katika jiji la Dar es Salaam walionekana kuwa na hamasa kubwa kuzungumzia ‘ubaguzi wanaofanyiwa na kile walichokieleza kama Mfumo Kristo,’ wengi wa wahojiwa katika ‘maeneo yasiyo ya mijini (rural areas) walionekana kuelemea zaidi kwenye kero zinazowakabili kila siku katika nyanja kama za afya, elimu na kilimo.
Hata mwanazuoni mmoja wa Kiislamu niliyefanya naye mahojiano alikiri kwamba, (namnukuu) “…kwa huko vijijini haya masuala ya udini hayana uzito kulinganisha na adha zinazowakabili wananchi katika maeneo hayo ambazo kimsingi hazibagui kuwa huyu ni Juma au Petro…”
Tukiweka kando ‘kikwazo’ hicho kinacholeta ugumu fulani katika kuchambua dini, moja ya mifumo (models) ya kuchambua vurugu (ziwe za kidini, kikabila, kisiasa, nk) unaonyesha hali hii (kwa mchanganuo wa jumla): ubaguzi huzua manung’uniko; manung’uniko huzua hamasa; hamasa huzua upinzani ambao waweza kuzua vurugu.
Na moja ya sababu za msingi zinazoelezwa katika model hiyo kuwa zinaweza kujenga hisia ya kubaguliwa ni kupotea kwa hali ya kujiendeshea mambo pasi kuingiliwa (autonomy).
Kufutwa kwa Mahakama za Kadhi kunaweza kuwa mfano mwafaka.
Japo mahakama hizo zilikuwa za kidini lakini kimsingi zilijitosheleza kushughulikia ‘kesi za kidini’ miongoni mwa Waislamu (yaani masuala kama mirathi, nk).
Lakini eneo jingine linaloweza kuingia katika kundi hili ni ushiriki wa baadhi ya Waislamu katika harakati za uhuru. Ushiriki huo haukuwa wa kisiasa tu bali wa kidini kwani moja ya mafundisho ya Uislamu katika kushughulikia jambo baya (kama udhalimu wa mfumo wa ukoloni) ni “kulikemea, kulichukia au kuliondoa” jambo hilo.
Kwa kutafsiri ushiriki wa Waislamu hao ulikuwa na msingi wa kidini (licha ya siasa), kujumuika kwao kuliwapa autonomy ya aina fulani, yaani kuweza kuitumia imani yao ya kidini kukabiliana na jambo baya (ukoloni).
Kama nilivyobainisha katika makala zilizotangulia, hisia kuwa “tulikuwa mstari wa mbele kupambana na mkoloni lakini uhuru ulipopatikana tumeishia kuwa chini ya wenzetu waliomsapoti mkoloni (kwa maana ya ukaribu kati ya ukoloni na Kanisa/ Ukristo)” zinaweza kutafsiriwa kama kupoteza autonomy hiyo.
Lakini pia ni muhimu kuelewa kuwa Uislamu si suala la imani pekee bali ni mfumo kamili wa maisha. Stadi zinaonyesha kuwa pindi mfumo wa kimaisha unapoonekana kuwa hatarini (kwa sababu moja au nyingine) inaweza kuleta mwamko wa kukabili tishio husika.
Kimsingi, dini hutoa mwongozo kwa muumini kuhusu maisha yake kibinafsi na katika jamii. Sasa tukiafikiana kuwa Uislamu kama dini na kama mfumo kamili wa maisha hauridhii aina yoyote ya uonevu, ni wazi hisia kuwa “Waislamu wanabaguliwa” zinaweza kufuata ile model ya ubaguzi – manung’uniko – hamasa – upinzani.
Pengine hili halitowapendeza baadhi ya wasomaji: katika utafiti wangu (na katika baadhi ya stadi nyingine) kuna uthibitisho wa kuwapo kwa vikundi vya Kiislamu vyenye mrengo mkali wa kiimani (Islamic extremists). Naomba ieleweke kuwa uwepo wa vikundi hivyo katika Uislamu haimaanishi kuwa mrengo mkali katika dini ni kwa Uislamu pekee.
Israel kuna Wayahudi wenye mrengo mkali kabisa ambao hawataki kabisa kusikia lolote kuhusu Wapalestina. Huko Marekani kuna Wakristo wenye msimamo mkali kabisa ambao kwa kiasi fulani wanachangia ‘uhasama’ kati ya taifa hilo na Waislamu na Uislamu kwa ujumla (kwa mfano Pasta Terry Jones aliyezua sokomoko duniani kwa kuchoma Kuran Tukufu).
Sasa kwa huko nyumbani, vikundi hivyo vya Waislam wenye msimamo mkali si tu ‘wameteka’ ajenda ya msingi ya manung’uniko (tunayoweza kuafikiana kuwa ni halali) ya Waislamu bali pia wamegeuza ajenda hiyo kuwa nguzo muhimu ya kupambana na wale wote wasioafikiana na mtizamo wao.
Wahanga wa ‘wana-msimamo mkali’ hawa si Wakristo pekee bali hata Waislamu wenzao wanaoonekana ‘kutokuwa na msimamo kama wao.’
Uthibitisho wa hii ni pamoja na vurugu zilizojitokeza nyakati fulani za uporaji wa misikiti. Japo wateka misikiti hao walidai kuwa wanairejesha kwa Waislamu misikiti iliyokuwa chini ya BAKWATA, kuna uthibitisho kuwa lengo lilikuwa kuigeuza misikiti hiyo kuwa ya ‘msimamo mkali.’
Badala ya hoja ya msingi inayohusu manung’uniko ya Waislamu dhidi ya mfumo wanauona kuwa unawakandamiza, vikundi vya Kiislamu vyenye msimamo mkali vinakwenda mbali zaidi kiasi cha kutaka kulazimisha kila mtu afuate imani yao (pasipo kujali ni Muislamu au la).
Uchambuzi wa wasifu wa baadhi ya viongozi wa vikundi hivyo unatoa picha ya waumini ambao ‘si washika dini kihivyo’ lakini ‘wenye hasira kali dhidi ya yeyote asiyeshika dini inavyostahili.’
Kwao, ‘kafir’ si asiye Muislamu tu bali hata Muislamu anayeshirikiana na wasio Waislamu (hata pale ambapo ushirikiano huo hauna madhara kwa Waislamu na dini yao).
Kuna tatizo jingine la msingi. Wakati kumekuwa na jitihada kubwa kwa Wakristo kutafsiri Biblia Takatifu kwa Kiswahili, yayumkinika kusema kuwa jitihada za kuitafsiri Kuran Tukufu kwa Kiswahili hazijaendelezwa vya kutosha.
Sasa, kwa vile ni rahisi kutumia Maandiko Matukufu/Matakatifu kuhalalisha au kuharamisha kitu fulani, kutoa fursa kwa watu wasio na uelewa wa kutosha wa maandiko hayo kuwa viongozi wa dini kunaweza kuwa na madhara.
Kwa uelewa wangu, ijtihad ni jukumu la wanazuoni wa Kiislamu, lakini kuna uthibitisho wa kitaaluma kuwa baadhi ya viongozi wa vikundi vya Kiislamu vyenye msimamo mkali wamejipachika jukumu hilo na kufanya tafsir (exegesis au tafsiri) katika minajili inayoendana na ajenda/matakwa yao (ya ‘msimamo mkali.’)
Japo katika Uislamu ni vigumu kuchora mstari unaotenganisha dini na siasa, tofauti na kwenye siasa ambapo mwananchi yeyote yule anaweza kuwa mwanasiasa, kwenye dini ni tofauti, kwani uelewa wa dini (kwa maana ya maandiko, sheria, nk) ni kigezo muhimu cha kuwa na mamlaka ya kuwaongoza waumini wengine.
Katika toleo lijalo, makala ya mwisho wa mfululizo huu itaangalia vikwazo vya ndani ya Uislamu kupata ufumbuzi wa manung’uniko yao; baadhi ya migongano ya kiimani kati ya Waislamu na Wakristo, na ‘utata’ katika Katiba kuhusu migongano hiyo; mapendekezo ya nini kifanyike kukabiliana na vurugu za kidini huko nyumbani.
ITAENDELEA