15 Apr 2009


SAKATA la halmashauri ya Karatu, kugomea kulipia malazi ya Makamu wa Rais, Dk Ali Mohamed Shein na ujumbe wake limechukuwa sura mpya baada ya aliyekuwa kaimu mkurugenzi wakati wa ziara hiyo, Majid Myao kutakiwa kutoa maelezo.

Myao aliitwa na mkuu wa wilaya ya Karatu, Mathew Sedoyeka hivi karibuni ili akatoe maelezo juu ya suala hilo hasa kutokana na halmashauri hiyo kugoma kulipa kiasi cha Sh2milioni ambazo ni malipo ya kulala siku moja na chakula kwa ujumbe huo, katika hoteli ya Bougain Villea ya mjini Karatu.

Kwa mujibu wa maelezo ya maandishi ya Myao, yaliyopo katika barua yake ya Machi 3, 2009 yenye kumbukumbu namba kdc/ded/cv.3/1/121, Myao amejitetea kuwa uamuzi wa kutolipiwa ziara hiyo, umetokana kamati ya fedha ya madiwani kukataa kuidhinisha fedha hizo.

Alisema kutokana na kutoidhinishwa malipo hayo, aliona angekiuka sheria namba tisa ya mwaka 1982 ambayo inahusu masuala ya matumizi ya fedha za halmashauri na maamuzi ya kamati ya fedha.

“Kama mimi ningetoa malipo hayo ni wazi ningekiuka sheria za serikali za mitaa hasa ikizingatiwa madiwani katika kikao chao halali ndio waligomea,”alieleza Myao.

Akizungumzia sakata hilo, mbunge wa jimbo la Karatu,
Dk Wilbroad Slaa alisema ni halali kwani walikuwa hawana bajeti ya malipo hayo na aliomba mtendaji yoyote wa halmashauri hiyo asiwajibishwe kwa suala hilo.

CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.