26 Apr 2009


KUNA kila dalili kuwa taifa halielekei pazuri hasa baada ya siku za hivi karibuni kuibuka matukio kadhaa ambayo kwa kiasi kikubwa yameishtua jamii kiasi cha kuhoji taifa linakoelekea.

Matukio ya kiongozi wa nchi kudhalilishwa kwenye mtandao wa kompyuta, malumbano ya wabunge juu ya kuvuja kwa siri za serikali na kuanikwa kwa mishahara yao pamoja na hatua ya Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, kutaja majina ya watu anaowatuhumu kuwa mafisadi ‘papa’ hadharani.

Kutokea kwa matukio hayo katika kipindi hiki ambacho taifa linaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwakani kumeelezwa ni mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yanaweza kuliyumbisha taifa.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii wanayaona matukio hayo kama ni mapambano ya hatari yanayowahusisha baadhi ya wafanyabiashara na vigogo wa siasa ambao katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakitumia njia mbalimbali kuhakikisha wanafanikisha mikakati ya kuongoza.

Tukio la Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, kuwataja baadhi ya wafanyabiashara na wanasiasa maarufu hapa nchini kuhusika na kashfa za ufisadi limezua mtafaruku miongoni mwa jamii ambapo baadhi ya watu wanaiona hatua hiyo ni mapambano ya hadharani baina ya pande hizo mbili.

Mapambano hayo ambayo katika siku za hivi karibuni yamefikia hatua mbaya kiasi cha kuanza kuhusisha uandishi wa habari usiozingatia maadili ya fani ya habari umeonekana kutumika kwa ajili ya kukashfu na kudhalilisha utu wa baadhi ya walengwa.

Vita ya pande hizo mbili vinaonekana kuanza kushika kasi na kuna habari kuwa baadhi ya wafanyabiashara waliotajwa na Mengi wamejipanga kujibu mashambulizi hayo kwa gharama zozote zile.

Wakati mapambano hayo yakionekana ni ya pande mbili wanasiasa, wafanyabiashara na wananchi mbalimbali wamejikuta ama wanaunga mkono upande mmoja au mwingine hali inayozidisha utete wa vita hivyo.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii wamebainisha kuwa hali hii ya sasa imekuja hasa baada ya ufisadi wa EPA, Meremeta, Richmond na kadhalika ambao ulisababisha baadhi ya viongozi akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowasa kujiuzulu.

Kujiuzulu kwa viongozi hao na kufikishwa mahakamani kwa baadhi ya watuhumiwa walioshiriki katika kashfa hizo na za matumizi mabaya ya madaraka kumechochea vita dhidi ya ufisadi huku baadhi ya wananchi wakitaka pia Rais wa mstaafu, Benjamini Mkapa, naye aondolewe kinga ili aweze kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.

Hatua ya Mengi kujitokeza hadharani na kutaka majina ya watu anaowatuhumu kwa kashfa za ufisadi na baadhi ya wabunge kuwachachamalia watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi nako kumezidisha joto na hofu ya mapambano hayo.

Wakati mawazo ya watu yakiwa bado katika mzozo huo, limetokea tukio jingine la kusikitisha katika mtandao ambapo kiongozi wa nchi amejikuta akidhalilishwa kwa picha zisizofaa mbele ya jamii.

Tukio hilo kwa kiasi kikubwa linaonyesha ukosefu wa ustaarabu na maadili kwa baadhi ya watu ambao wameamua kutumia vibaya teknolojia ya kisasa hususan upashanaji habari kwa kutumia mtandao.

Jambo hilo kwa kiasi kikubwa limekuwa likihusishwa na mbinu za kuchafuliana majina hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi na kubainishwa kuwa kama hatua za haraka za kuwakamata wanaohusika na mitandao hiyo zisipochukuliwa kuna hatari ya viongozi wengi zaidi kudhalilishwa kupitia mambo mbalimbali.

Moja kati ya tukio la udhalilishaji wa viongozi ni hatua ya kijana mmoja kuamua kumpiga kofi Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, katika sherehe za Maulid zilizofanyika kwenye Ukumbi wa Daimond Jubilee, Dar es salaam.

Sakata jingine ambalo limeonekana kuwagawa zaidi Watanzania na wanasiasa ni kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma, kuwa kuanzia sasa wabunge na watendaji wote watakaovujisha siri za serikali watashughulikiwa ipasavyo.

Kauli hiyo ambayo ilionekana kumlenga Mbunge wa Karatu Dk. Wilbrod Slaa (CHADEMA) na baadhi ya wabunge ambao wamekuwa wakitumia nyaraka mbalimbali zinazodaiwa kuwa za siri kuiumbua serikali sasa watakumbana na mikono ya sheria endapo watakutwa na nyaraka hizo.

Kauli hiyo imeonekana kupingwa na wananchi wengi kwa madai kuwa sasa serikali inataka kuwa ya kidikteta hasa kwa kuficha nyaraka za ufisadi uliofanywa au unaofanywa na viongozi waliopo na waliomaliza muda wao madarakani.

Baadhi ya wananchi wamekuwa wakiihusisha kauli hiyo kama ni njama za kuficha uovu ambao umekuwa ukipoteza fedha nyingi za Watanzania kupitia rasilimali mbalimbali.

Mshangao huo wa wananchi uliongezeka zaidi pale baadhi ya wabunge walimshutumu hadharani Dk. Slaa kwa kubainisha vipato wanavyovipata wabunge na kutaka fedha hizo zipunguzwe ili zitumike kwa maendeleo ya wananchi.

Baadhi ya wabunge walimtuhumu Dk. Slaa kwa kutaka kujitafutia umaarufu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu ujao jambo ambalo limepingwa vikali na wananchi wanaoonekana kukubaliana na ushauri wa Dk. Slaa.

Matukio haya kwa kiasi kikubwa kwa namna moja au nyingine yanaonyesha kuliweka taifa katika sehemu mbaya na iwapo kama hatua za kurekebisha baadhi ya mambo hazitachukuliwa kuna kila dalili za kutokea mpasuko mkubwa miongoni mwa jamii.

Naye Rahel Chizoza anaripoti kutoka Dodoma kuwa sakata la wizi wa nyaraka za serikali na kuwekwa hadharani kwa mishahara minono na marupurupu wanayopata wabunge kulikoibuliwa na Mbunge wa Karatu Dk. Wilbrod Slaa (CHADEMA), hivi karibuni limechukua sura mpya baada ya baadhi ya wabunge kuonyesha kumchukia mbunge huyo.

Hali hiyo imejitokeza jana kwenye semina ya maboresho ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma iliyoendeshwa kwa wabunge ambao baadhi yao walionyesha hali ya kumbeza mbunge huyo aliposimama kwa ajili ya kuchangia hoja.

Hali hiyo ilisababisha mwenyekiti wa semina hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Mpwapwa, George Lubeleje, kuingilia kati na kuwasihi wabunge kupunguza minong’ono.

“Hivi hizi nyaraka zinazodaiwa kuwa ni za siri, kwa nini zinawekwa kwenye makabati ya serikali, naomba Katibu Mkuu aniambie kama ni halali kwa nyaraka za wizi kuwepo katika kabati za serikali,” alihoji Dk. Slaa

CHANZO:Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.