Mwandishi Wetu
Aprili 14, 2010
Ni fedha za stimulus package alizozitetea Kikwete bungeni
Gavana BoT aruka kiunzi, amtupia mpira msaidizi wake
Rais Kikwete Aota kujenga safu ya vijana katika uongozi wa kitaifa
Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Mrisho Kikwete ameahidi kuwa kama akijaliwa kupata kipindi cha pili cha kuliongoza taifa la Tanzania, atafanya jitihada kubwa kuubadilisha uongozi wa Tanzania kuwa uongozi wa vijana.Rais Kikwete akizungumza juzi, mjini Dar es Salaam na vijana kutoka nchi mbali mbali za Afrika wanaoshiriki katika Mpango wa Kulea Uongozi wa Afrika wa African Leadership Initiative, Rais Kikwete alisema kuwa anauthamini Mpango huo.Alisema kuwa vijana ndiyo Tanzania ya kesho, na kama Tanzania haikuwekeza vya kutosha katika vijana na maendeleo yao, basi itakuwa haiwekezi katika hali yake ya baadaye.Aliwaambia vijana hao ambao wanashiriki katika Mpango huo unaodhaminiwa na Askofu Mkuu (mstaafu) wa Kanisa la Anglikan Desmond Tutu wa Afrika Kusini kuwa kwa kadri miaka inavyokwenda ni lazima rika la wazee lipishe lile la vijana....INAENDELEACHANZO: Mwananchi
Wenyeviti wastaafu wa CCM waonya
Wenyeviti wastaafu wa mikoa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamevunja ukimya na kuwataka viongozi wa chama hicho wanaotaka kuyatumia mapambano dhidi ya rushwa kama mtaji wa kisiasa na kujipatia umaarufu, kuacha mara moja. Sambamba na hilo, wazee hao wametaka mapambano dhidi ya rushwa yasiwe kichaka cha kuficha ubovu wa uongozi na kushindwa kuwajibika. Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wastaafu wa chama hicho Dar es Salaam jana, Mwenyekiti mstaafu wa Mkoa wa Dodoma, Pancras Ndejembi alisema mapambano dhidi ya rushwa ni ya CCM na si mwanachama binafsi au kikundi cha wanachama wachache.
“Tunashuhudia baadhi ya viongozi wa CCM kurushiana maneno wenyewe kwa wenyewe kwa kutaka kuonyeshana nani zaidi na nani ni vinara kuliko wengine katika mapambano dhidi ya rushwa, hii si sawa,” alisema Ndejembi aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Tanzania. “Tusingependa kuona mapambano haya yanatumiwa kama njia ya kujipatia umaarufu binafsi, mwenyekiti wetu Rais Kikwete ambaye ndiye jemedari wa mapambano haya humsikii anafanya hivyo na sisi wengine tusifanye hivyo…. kama wewe ni kiongozi na hutekelezi wajibu wako kwa wapiga kura wako wakikuuliza uko wapi, usisingizie kupigwa vita na mafisadi,” walionya.
Ndejembi aliyeambatana na wenyeviti wastaafu Hemed Mkali (Dar es Salaam), Tasil Mgoda (Iringa) na Jumanne Mangara (Pwani), alisema wazee hao wamesikitishwa na malumbano ya hadharani baina ya viongozi wa CCM ambao wengine wa ngazi ya juu ya uongozi ndani ya chama. Alisema tabia inayoonyeshwa na viongozi hao ya kushutumiana, kunyoosheana vidole, kuwekeana visasi, kuonyeshana ubabe na kuwekeana nadhiri ya kupambana baina ya viongozi, kunadhoofisha na kukipunguzia heshima chama hicho.
“Lakini pia kufanya hivyo hadharani, kwa nia ya kutaka kuungwa mkono katika shutuma na visasi hivyo kunajenga chuki, uhasama na migawanyiko katika jamii, viongozi hatupaswi kuwajaza watu chuki na uhasama ndani ya mioyo yao,” alisema Ndejembi kwa niaba ya wenzake na kutaka neno ufisadi lisitumiwe kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwakani. Alisema kumuita mtu fisadi kwenye vyombo vya habari haitoshi katika kushinda mapambano dhidi ya rushwa, bali watu waipigie kelele serikali iimarishe taasisi na vyombo vya kupambana na rushwa kama Polisi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mahakama ambako watuhumiwa wanafikishwa.
Licha ya kuwapo malumbano baina ya viongozi hao wa CCM, wastaafu hao walisema kuhitilafiana ni kitu cha kawaida na kamwe watu wasitarajie chama hicho kitameguka. Wastaafu hao walieleza kumuunga mkono Rais Jakaya Kikwete iwapo atagombea tena urais mwakani na kutaka watu wengine wamuunge mkono, kwa maelezo kuwa anafaa kuongoza nchi. Walitoa sababu za kumuunga mkono kuwa ni kukubalika na anaowaongoza, anawapenda watu wote, mvumilivu, mkereketwa wa maendeleo ya wananchi na hana jazba.
Wazee hao walisema wameamua kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo hayo ili ujumbe uwafikie viongozi, wanachama na mashabiki wa CCM, lakini yote hayo waliyoyaeleza wameshayawasilisha kwenye vikao wanavyoshiriki vya matawi na mashina na wamezungumza na viongozi wa sasa wa chamahicho. Ingawa wastaafu hao hawakuwataja kwa majina viongozi wa CCM waliolumbana hadharani, lakini hivi karibuni Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye ni mwanahisa wa Kampuni ya kuzalisha umeme wa upepo ya East Africa Power Pool, amelumbana na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.
Dk. Mwakyembe anadai Rostam anatumia vyombo vyake vya habari kumchafua huku Rostam akitaka mbunge huyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mwandishi wa habari, kuelezea mgongano wa maslahi wakati alipochaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini. Mbali na wazee hao, pia Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM Tanzania Bara ambaye ni Mbunge wa Mtera, John Malecela alitaka malumbano hayo yakome, kwani hayana faida kwa mwananchi na wahusika watumie vyombo husika vya chama kufikisha malalamiko yao.
CHANZO: HabariLeo
CCM yamjibu Dk. Kitine
na Edward Kinabo
SIKU moja baada yaMkurugenzi mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa nchini, Dk. Hassy Kitine, kudai nchi inaendeshwa kienyeji na kukilalamikia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuendelea kuwakumbatia wanachama wake wanaokabiliwa na kesi za ufisadi, chama hicho
kimesema hakiwezi kuwavua nyadhifa hizo, kwa sababu kesi zao bado ni tuhuma tu.
Sambamba na hilo, CCM imesema kauli ya Dk. Kitine kwamba nchi inaendeshwa kienyeji ni maoni yake binafsi, kwani hayana ukweli. Msimamo huo wa CCM ulitolewa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati, alipozungumza na Tanzania Daima, akijibu shutuma nzito zilizotolewa juzi na Dk. Kitine dhidi ya serikali.
“Sisi tunasema, yeye kama raia ana haki ya kutoa mawazo yake, na hiyo ndiyo demokrasia. Lakini si lazima kila anayetoa mawazo yake yawe sahihi. Mtu anaweza kujiuzulu nafasi yake kupisha uchunguzi ufanyike, hiyo haimaanishi kwamba hilo jambo amelifanya kweli.
“Uchunguzi unapofanyika kuna mambo mawili yanaweza kutokea, la kwanza huyo mtu anaweza kubainika alifanya hicho kitu na la pili anaweza kuonekana hana hatia.
“Hatuwezi kuwavua watu uanachama au nyadhifa zao ndani ya chama kwa sababu hiyo tu. Yeye aliyesema hivyo atutajie ni kiongozi gani wa serikali ambaye pia ni kiongozi wa chama, ameshathibitika kuwa hana maadili halafu kama chama tumeendelea kumwacha. Atuambie…..hakuna,” alisema Chiligati.
Alipoulizwa kwanini CCM isiwafukuze uanachama na kuwavua nyadhifa zao za kichama na ubunge, baadhi ya viongozi wake, ambao tayari serikali ya chama hicho ilisharidhika kwamba walikiuka maadili ya uongozi kwa kutumia vibaya madaraka yao, hata ikaamua kuwafungulia kesi, alisema: “Hatuwezi kuwachukulia hatua kwa sababu kesi zao bado ni tuhuma tu. Wakithibitika kama kweli walifanya hivyo, hatutawaacha,” alisema Chiligati.
Chiligati alipinga madai ya nchi kuongozwa kienyeji na kusisitiza kuwa kauli ya Dk. Kitine, haina ukweli wowote.
Alisema nchi inaongozwa vizuri kwa kufuata utawala wa sheria na mihimili yote ya dola, ikiwemo utawala, Bunge na Mahakama, inafanya kazi zake vizuri. Alibainisha kuwa kielelezo kuwa nchi haiongozwi kienyeji, ni amani na utulivu vilivyopo nchini, kwani kama nchi ingekuwa inaongozwa kienyeji kusingekalika.
“Kwa mfano, hilo alilosema nchi inaongozwa kienyeji, maana yake nini? Nchi kuongozwa kienyeji maana yake hakuna mfumo wa utawala kabisa, hakuna utawala wa sheria. Mahakama hazipo wala Bunge halipo…serikali haipo.
“Kungekuwa na hali hiyo, ingekuwa sawa na kusema nchi inaongozwa kienyeji. Lakini sisi hatujafikia hatua hiyo. Bunge lipo, Mahakama ipo, Serikali ipo. Utawala wa sheria. Nchi haiongozwi kienyeji, ndiyo maana kuna amani na
utulivu,” alisema Chiligati.
Mbali ya CCM kutoa kauli hiyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), aliunga mkono kauli ya Dk. Kitine.
“Mzee Kitine ameongea jambo ambalo ninaliongea kila siku kwamba, kuna tatizo kubwa serikalini. Tuhuma za ufisadi zimeshamiri sana, watendaji hawachukui maamuzi, wanasiasa wenye nyadhifa serikalini wamejaza nafasi na hawako tayari kuwajibika. Tunahitaji muafaka wa kitaifa kwenye mambo mengi,” alisema Zitto. Alisema ili mambo yaende vizuri, Tanzania inahitaji kelele za wazee wastaafu kama Dk. Kitine, wasimamie kunena na kushauri na hata kukemea na wananchi wawapigie kura wabunge wengi wa upinzani ili Bunge liwe na meno.
Juzi, Dk. Kitine alisema taifa linakabiliwa na tatizo la uongozi, ambalo halijawahi kutokea katika historia ya nchi. Kada huyo wa siku nyingi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyewahi kuwa mbunge wa Makete, mkoani Iringa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, chini ya uongozi wa Rais mstaafu Benjamin Mkapa, alisema nchi imekuwa ikiendeshwa kienyeji, kwa sababu ya kuporomoka kwa maadili ya uongozi.
“Hali tuliyofikia si nzuri, tena niseme ni mbaya sana. Kuna kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa maadili ya uongozi. Na hii nawaambia, nchi haijawahi kuwa katika hali mbaya huko nyuma kama ilivyo sasa. Kwa hali tuliyofikia ni ngumu kurekebisha maadili ya uongozi."
“Tatizo kubwa ni viongozi kukosa integrity (uadilifu). Kwanza ni integrity ya viongozi wenyewe, pili ni commitment (wito), tatu ni nationalism (utaifa). Haya ndiyo yalikuwepo wakati wa Mwalimu,” alisema Dk. Kitine. Alisema baadhi viongozi wa serikali wamepoteza sifa kuu tatu za uongozi ambazo ni kuwa na uadilifu, wito na kuweka mbele
utaifa, sifa ambazo alisema ndizo zilikuwa nguzo ya uongozi wakati wa Serikali
ya Awamu ya Kwanza, chini ya Baba wa Taifa, hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Alisema uteuzi mbaya wa viongozi hususan uteuzi wa mawaziri, umechangia
kupatikana kwa viongozi wasio waadilifu, wengi wao wakijihusisha na vitendo vya rushwaCHANZO: Tanzania Daima
IFUATAYO NI HABARI ILIYOBEBA MATAMSHI YA DR KITINE.![]()
MKURUGENZI Mkuu mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk. Hassy Kitine, amesema taifa linakabiliwa na tatizo kubwa la uongozi, ambalo halijawahi kutokea katika historia ya nchi.
Kitine ambaye aliiongoza idara hiyo nyeti kwa karibu miaka 30 zama za Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili, alisema ukosefu huo wa uongozi umesababisha nchi iongozwe kienyeji.
Kachero huyo namba moja kwa miaka mingi, ambaye alilazimika kujiuzulu wadhifa wa uwaziri wa nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) wakati wa utawala wa Benjamin Mkapa, mwishoni mwa miaka ya 1990 kutokana na kuhusishwa na kashfa ya mkewe kufuja fedha za umma kiasi cha shilingi milioni 40, alirejea kutoa kilio chake cha miaka mingi cha kuporomoka kwa maadili ya uongozi nchini.
Kitine ambaye aliwahi pia kuwa Mbunge wa Makete kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alitoa matamshi hayo mazito katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam jana, alipozungumza na waandishi wa vyombo kadhaa vya habari.
“Hali tuliyofikia si nzuri, tena niseme ni mbaya sana. Kuna kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa maadili ya uongozi.Na hii nawaambia, nchi haijawahi kuwa katika hali mbaya huko nyuma kama ilivyo sasa. Kwa hali tuliyofikia, ni vigumu kurekebisha maadili ya uongozi.
“Tatizo kubwa ni viongozi kukosa integrity (uadilifu). Kwanza ni integrity ya viongozi wenyewe, pili ni commitment (wito), tatu ni nationalism (utaifa). Haya ndiyo yalikuwepo wakati wa Mwalimu,” alisema Dk.Kitine.
Akizungumza kwa kujiamini kama ilivyo kawaida yake, Kitine alisema viongozi wengi wa serikali wamepoteza sifa kuu tatu za uongozi ambazo ni kuwa na uadilifu, wito na kuweka mbele utaifa, sifa ambazo alisema ndizo zilikuwa nguzo ya uongozi wakati wa Serikali ya Awamu ya Kwanza, chini ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
“That was possible (hilo liliwezekana) chini ya Mwalimu. Kama alikuwa akifanya kosa, basi kosa hilo lilikuwa likitokea tu wakati akifanya jambo kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania. "
“Philosophy (falsafa) ya Mwalimu, ilikuwa kwanza Mungu, pili Tanzania, halafu yeye binafsi. Kila kiongozi anayetofautiana na Mwalimu tu hulifikisha taifa hili kubaya, if you differ with him, utaishia kubaya,” alisema Dk. Kitine akionyesha hali ya masikitiko.
Alisema uteuzi mbaya wa viongozi, hususan ule wa mawaziri, umechangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa viongozi wasio
waadilifu, wengi wao wakijihusisha na vitendo vya rushwa. “Haiwezekani viongozi wakateuliwa kwa misingi ya mitandao …sijui, kwa msingi wa politics of division (siasa za makundi) ndani ya chama. Haiwezekani nchi ikaendeshwa kienyeji. Integrity should be number one (uadilifu unapaswa kuwa kitu cha kwanza kuzingatiwa). "
“Mtu anajiuzulu, anafukuzwa uwaziri kwa sababu ya kashfa, kwa sababu ya kukosa maadili, halafu anabakia kuwa mbunge na mjumbe wa kamati kuu ya chama, nini hii? Hii haifai. Waziri akikosa uadilifu anatakiwa aondolewe mara moja nyadhifa nyingine zote alizobakiwa nazo. Nadhani hii itasaidia,” alisema Dk. Kitine pasipo kutaja jina la kiongozi yeyote.
Kitine ambaye wakati wote wa mazungumzo yake alisema alikuwa anataka kujadili masuala muhimu na si watu, alieleza namna asivyo na imani na hatua zinazochukuliwa na serikali katika kukabiliana na tatizo la rushwa kubwa. Kwa mujibu wa kachero, mwanasiasa na mwanazuoni huyo, hatua hizo ambazo zinahusisha baadhi ya watu wenye majina makubwa kufikishwa mahakamani, zimechukuliwa kwa ajili tu ya maandalizi ya uchaguzi ujao.
“Nilikuwa kiongozi wa kwanza kuzungumzia rushwa kubwa miaka 10 iliyopita. Nilisema ndiyo inayovuruga uchumi kuliko hata rushwa ya
nesi, hakimu, polisi,.… hakuna hata mkubwa mmoja aliyekamatwa. Ilinigharimu sana, na mimi nilipata adhabu ya kuzuiliwa kikao kwa miezi miwili, kama huyu nani huyu, Zitto (Kabwe). Wakati huo ilikuwa ndani ya CCM".
“Mimi nadhani hatua hizi zinazochukuliwa hazilengi kukomesha tatizo la rushwa, ni siasa tu za uchaguzi,” alisema Dk. Kitine.
Alipoulizwa nini kifanyike ili kukabiliana na tatizo hilo la uongozi mbaya, pamoja na mambo mengine, alielekeza changamoto zake kwa Idara ya Usalama wa Taifa.
“Usalama wa Taifa should be completely clean (unapaswa kuwa safi kabisa). Idara hii inatakiwa kuwa, juu ya mambo ya rushwa, iwe safi kabisa. Usalama wa Taifa ndiyo unayoteua viongozi, ndiyo inayoshirikiana na rais kwa kumshauri katika kuteua mawaziri. Sasa kama Usalama wa Taifa ukiwa mchafu ndio tunapata viongozi wala
rushwa. Nafikiri vigezo vinavyotumika kuteua viongozi pia vina matatizo,” alisema Dk. Kitine.
Kada huyo wa CCM ambaye kitaaluma ni mchumi na mwanasheria, akizungumzia hali ya uchumi nchini, alisema kwa kiasi kikubwa uchumi umeshikiliwa na wageni kuliko wazawa, na kuelezea kusikitishwa kwake juu ya kuwepo kwa pengo kubwa kati ya matajiri na maskini.
Akitoa mfano alisema, miongoni mwa mambo yanayoonyesha kuparaganyika kwa mambo ni kukithiri kwa idadi ya ombaomba mitaani. “Mwalimu asingeruhusu watu hawa waombeombe barabarani. Kazi za Watanzania ni udereva teksi, daladala, mabasi, kazi ya uboi ndani ya nyumba na kazi ya kufagia barabarani. Hizi ndizo kazi za Watanzania na hawa ndio wenye mali."
“Uchumi huu wa Watanzania si wa kwao. Watanzania ambao ni matajiri hawazidi hata watano. Hakuna sera bora za kusaidia kutumia
maliasili zetu ili zitupe fedha ya kujenga shule, madaraja, hospitali…..”
alisema Dk. Kitine. Akizungumzia utendaji wa kazi wa Bunge katika kusimamia utendaji wa serikali, Kitine alisema kazi inayofanywa na taasisi hiyo hivi sasa ni kubwa kuliko ilivyopata kuwa wakati wowote huko nyuma.
Hata hivyo katika kuusifia utendaji wa kazi wa Bunge, aliupongeza mchango mkubwa na muhimu wa wabunge wa upinzani katika kuiimarisha taasisi hiyo muhimu. “Ni Bunge zuri kuliko lilivyowahi kuwa huko nyuma. Linaonyesha kila dalili za uhuru. Upinzani unafanya kazi nzuri. Bunge liko wazi zaidi na wabunge wanatoa michango mingi yakinifu, yenye manufaa kwa taifa. Likiendelea hivi tutafika mahali pazuri,” alisema.CHANZO :Tanzania Daima