20 Jun 2009


Orodha ya wabunge bubu bungeni yawekwa hadharani

Na Leon Bahati

WAKATI tukielekea mwaka wa lala salama wa Bunge la mwaka 2005-2010, huku baadhi ya wabunge wakiibuka mashujaa kwa kutoa michango mizito inayoitingisha serikali, imebainika kuwa baadhi yao hadi sasa hawajawahi kuuliza hata swali moja wala kuchangia.

Uchunguzi huo umefanywa na Mwananchi Jumapili kwa msaada wa tovuti ya bunge ambako kila mchango wa mbunge hurekodiwa kwa kuonyesha swali la msingi au la nyongeza alilouliza, majibu yake na mchango aliotoa.

Kati ya wabunge 319 walioko katika Bunge la sasa ambao hawajawahi kuuliza maswali ya msingi wanakadiriwa kufikia 50 na wasiouliza maswali ya msingi wala nyongeza ni zaidi ya 30.

Mawaziri na wabunge ambao pia ni wakuu wa mikoa, hawajahusishwa kwenye hesabu hizo kwa sababu wapo upande wa serikali na wote wamekuwa hawaulizi maswali. Wengine ambao hawakuhusishwa kwenye vipengele hivyo ni Spika na Naibu Spika, lakini wote wameonyeshwa kuwahi kuchangia hoja mbalimbali.

Kwa mujibu wa mtandao huo, Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz ndiye pekee ameonyeshwa kuwa hajawahi kuuliza swali lolote wala kuchangia jambo lolote tangu Bunge limeanza.

Wabunge wengine ambao wameonyeshwa hawajawahi kuuliza maswali, lakini wamekuwa wakichangia hoja mbalimbali nao ni Yusuf Makamba (Katibu Mkuu wa CCM); John Shibuda, Harith Mwapachu, Ali Haji Ali, Omar Sheha Musa, Abdallah Sumry, Gideon Cheyo, Juma N’hunga, Nazir Karamagi, Anna Abdalah, Ali Haji Ali, Thomas Mwang’onda, Salum Khamis Salum, Hassan Rajabu Khatibu na Felix Mrema.

Wengine ni Philemon Sarungi, Edward Lowassa, Andrew Chenge, Abdisaalam Issa Khatib, Dk Ibrahim Msabaha, Zakia Meghji, Kingunge Ngombale Mwiru, Salimu Yusufu Mohamed, Salum Ahamed Sadiq, Omar Sheha Mussa, Manju Msambya na Benedict Ole-Nangoro.

Wabunge ambao pia ni wakuu wa mikoa ufanisi wao wa kuchangia bungeni ni mdogo ni Abdul Aziz – Iringa (7); Dk James Msekela – Dodoma (6); Monica Mbega – Kilimanjaro (3); Dk Christine Ishengoma-Ruvuma (4) na William Lukuvi – Dar es Salaam (3). Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba aliwahi kutoa michango bungeni mara mbili tu.

Katika Kundi la wabunge 13 wanaoongoza kwa kuuliza maswali ya msingi linaongozwa na Mgana Msindai (CCM) mwenye maswali 34 na kufuatiwa na William Shellukindo (29); Diana Chilolo (28), Paschal Degera (28), George Lubelege (25), Raphael Mwalyosi (24) na Mhoga Ruhwanya (23).

Wabunge wengine kwenye kundi hilo wana maswali 22 kila mmoja nao ni, James Msalika, Job Ndugai, Zitto Kabwe, Herbert Mtangi, Victor Mwambalaswa na Lucy Owenya.

Wabunge 11 vinara wa kuuliza maswali ya nyongeza ni Dk Wilbrod Slaa (71), Hamad Rashid Mohamed (71), Mgana Msindai (67), Esther Nyawazwa (58), George Lubelege (56), Diana Chilolo (54), Hafidh Ali Tahir (52), Geofrey Zambi (50) na wawili waliofungana kwa kuuliza 49, Jenista Mhagama na John Kilimba (49).

Katika kundi la kutoa michango mbalimbali kwenye vikao vya bunge linaongozwa na Naibu Spika Anne Makinda (495); akifuatiwa na Spika, Samweli Sita (494). Wengine ni Jenister Mhagama (193); Job Ndugai (147); Zitto Kabwe (125); Dk Slaa (106); Andrew Chenge (89); Suzan Lyimo (87); William Shelukindo (77); Geofrey Zambi (73); John Kilimba (69) na mawaziri wawili waliofungana kwa kufikisha michango 67 ambao ni Shamsa Mwangunga, Waziri wa Maliasili na Utalii na Waziri wa Miundombinu, Dk Shukuru Kawambwa.

Mawaziri wengine wanaofuatia ni Dk Mary Nagu (64); Profesa David Mwakyusa (59); William Ngeleja (50); Mwanasheria Mkuu wa Serikali; Johnson Mwanyika (47); Dk Makongoro Mahanga (45); Profesa Jumanne Maghembe (45); Stephen Wasira (41) na John Chiligati (40).

Akizungumzia kuhusu kumbukumbu hizo wiki iliyopita, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema kuwekwa kwa taarifa hizo hakuna maana zaidi ya kuweka kumbukumbu za michango ya wabunge, lakini akasema kulikuwa na marekebisho kwa wakati huo.

Alipotafutwa tena jana, alisema tovuti hiyo ya Bunge imefanyiwa marekebisho makubwa ili wananchi waweze kupata kwa undani kumbukumbu mbalimbali za vikao vya Bunge.

Pamoja na maboresho hayo, Dk Kashililah alisema: "Tuna mpango wa kuongeza maboresho zaidi yakiwepo ya kuwezesha watu kufuatilia vikao vya Bunge kupitia tovuti hiyo."

Licha ya baadhi ya wabunge kuwa na mchango hafifu, Bunge la sasa limeonekana kuwa mwiba mkali kwa viongozi serikalini hususan mawaziri, kutokana na baadhi ya wabunge kuwabana katika mambo mbalimbali ya utendaji mbovu na ufisadi, huku kufupishwa kwake kukipunguza nafasi ya kuuliza maswali na kuchangia kwa baadhi yao ambao walikuwa hawajafanya hivyo.

Katika kipindi hicho miongoni mwa hoja nyingine zilizosisimua ni mjadala wa Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe kuhusu utoaji wa zabuni ya umeme wa dharura iliyotolewa kwa kampuni ya Richmond Development Limited (LLC); na kusababisha Rais Jakaya Kikwete kuvunja baraza la mawaziri baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu pamoja na mawaziri wengine wawili.


CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.