20 Jun 2009


Ahadi tupu za kiwete zaelekea kutengeneza kitanzi cha CCM 2010

Na Mwandishi Wetu

IKIWA imesalia takriban miezi 18 kabla ya Uchaguzi Mkuu Oktoba mwakani, sasa ni dhahiri kuwa Rais Jakaya Kikwete ana kibarua kigumu cha kukamilisha ahadi lukuki alizotoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005.

Mazingira hayo pia yanawaweka njiapanda wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika kutetea tena nafasi zao.

Baadhi ya wabunge tayari wameliona hilo na miongoni wamelisema bungeni wakiwashutumu mawaziri ambao wamekuwa wakilimbikiza miradi ya maendeleo kwa upendeleo kwenye maeneo yao bila kuzingatia vipaumbele vya taifa, hata baadhi yao walifikia hatua ya kutishia kukwamisha bajeti iliyopitishwa Alhamisi iliyopita.

Kauli kali zaidi ilitoka kwa Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii aliyeomba dua kwa Mungu awalaami mawaziri hao.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, ahadi kadhaa alizozitoa Rais Kikwete bado hazijatekelezwa na kwa kipindi kilichosalia ni vigumu kufanya hivyo.

Miongoni mwa ahadi alizotoa Rais Kikwete na hazijaonekana matunda yake dhahiri ni zile zilizoandamana na kaulimbiu yake ya Ari Mpya, Nguvu Mpya, Kasi Mpya na mpango wa ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania’.

Kigogo mmoja ndani ya CCM amelieleza gazeti hili kwamba ahadi hiyo ya maisha bora ndiyo ilimpatia Kikwete kura za kishindo na isipotengenezewa mkakati maalumu inaweza kuwa ndio kitanzi chake na wabunge wengi wa CCM.

Alisema ahadi hiyo imesababisha baadhi ya vigogo wa chama na serikali kubadili kauli, na kusema kwamba maisha bora hayatawafuata wananchi kama hawafanyi kazi kwa bidii.

Kwa mujibu wa watu mbalimbali waliozungumza na Mwananchi Jumapili, na hata kauli za wabunge wanapochangia bungeni, Watanzania walio wengi bado wana hali duni ya kimaisha, jambo ambalo litakuwa gumu kulieleza kwa wapigakura hapo mwakani.

Kutokana na ahadi hiyo serikali ilitoa Sh30 bilioni ambazo zilipewa jina la mabilioni ya Kikwete, lakini hazikufika kwa maskini walio wengi kutokana na masharti yake kuwa magumu, na kuangukia kwenye mikono ya wasio wajasiriamali wadogo, hivyo kukwamisha mpango huo wa rais.

Ahadi nyingine zinazoelekea kushindikana ni ya mwafaka wa kisiasa wa Zanzibar ambao Rais Kikwete aliuweka kwenye kipaumbele, lakini hadi sasa hakuna mafanikio yoyote na tayari Chama cha Wananchi (CUF), kimetangaza kujitoa katika mazungumzo.

Ahadi nyingine ni ujenzi wa madaraja ya Kilombero mkoani Morogoro na Kigamboni, jijini Dar es Salaam ni miongoni mwa ahadi kubwa alizotoa Kikwete na hadi sasa hakuna dalili zinazoweza kuashiria kuwa ipo nia ya utekelezaji.

Hata hivyo, Waziri wa Miundombinu, Dk Shukuru Kawambwa alipoulizwa alisema kwamba daraja la Kilombero limetengewa fedha katika bajeti ya mwaka 2009/10.

Kuhusu daraja la Kigamboni, alirudia kauli za muda mrefu kuwa hilo limo kwenye mkakati wa kuanza kujengwa wakati wowote chini ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kushirikiana na wahisani mbalimbali.

Ahadi nyingine ambazo hazijatekelezwa, zimeelezwa kuwa ni kilio cha mahakama nchini juu ya suala la masilahi ya watumishi na vifaa vya kazi.

Hivi karibuni, Jaji Mkuu, Augustino Ramadhan alisikika akilalamika kuwa kiwango cha mafungu yanayoahidiwa kutengwa kwa mahakama hufika kwao kikiwa pungufu.

Suala jingine limeelezwa kuwa ni uboreshaji wa mashirika ya umma ambayo bado yako mikononi mwa serikali, lakini kila kukicha yamekuwa na matatizo na kuzua malalamiko mengi.

Kwa upande wa barabara ambazo ziliahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami na ambazo bado ni Tabora-Nzega, Bunda-Ukerewe na Marangu-Mkuu Rombo-Tarakea-Kamwanga.

Aliahidi pia kulifanya jimbo la Rorya mkoani Mara kuwa wilaya, lakini utekelezaji wake umekuwa ukisuasua.

Mambo mengine ilikuwa ni kupambana na rushwa, lakini pamoja na hali hiyo kuonekana kuzaa matunda kwa mambo mengi yaliyokuwa yamejificha kuchimbuliwa na kuwekwa hadharani, malalamiko yanayoibuka ni baadhi ya watuhumiwa kutofikishwa mahakamani.

Rais Kikwete pia aliahidi kuondoa kero nyingi za Muungano lakini licha ya kuunda kamati ya kuzijadili na kuzishughulikia chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, zipo dalili za baadhi ya wananchi kutoridhika.

Tatizo kubwa linalojitokeza ni baadhi ya Wazanzibari, wakiwamo viongozi wa SMZ kutoa kauli zinazoonyesha dalili za waziwazi kwamba wanadhulumiwa ndani ya Muungano.

Pamoja na hali hiyo, Rais Kikwete atajivunia kwa kutekeleza ahadi yake ya kulifanya Bunge kuwa huru kwani limeonyesha dhahiri kuwa na meno kwa kufichua udhaifu wa baadhi ya vigogo serikali bila kuwa na woga.

Ameonyesha mafanikio pia katika ahadi yake ya kuendesha dola kwa misingi ya utawala bora na uwajibikaji; utawala wa sheria unaoheshimu na kulinda haki za binadamu.

Hata hivyo, katika kipengele hicho kuna manung’uniko kadhaa kama vile baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa kuendelea na nyadhifa zao wakati taratibu za utumishi wa umma ziko wazi kwamba wangepaswa kusimamishwa au kupewa likizo ama kuhamishiwa sehemu nyingine, ili uchunguzi huru ufanyike.

Mafanikio mengine ni kutekeleza ahadi ya kuongeza nafasi za elimu ya juu baada ya kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma.

Ahadi nyingine ambayo Rais Kikwete ameonekana wazi kuivalia njuga ni kuboresha kilimo; na tayari mikakati kadhaa ikiwepo ya pembejeo za kilimo imewekwa, ingawa kuna malalamiko ya pembejeo kutofika kwa wakulima na wakulima wa karafuu na kahawa kutokuwa huru kutafuta masoko yao nje ya nchi.

Nguvu kubwa ya serikali yake kuielekeza kwenye kilimo imechagizwa na mtikisiko wa uchumi duniani ambao umetishia uchumi wa nchi nyingi hasa maskini ambazo zinategemea chakula kutoka nje.

Licha ya mafanikio hayo, serikali ya Kikwete inakabiliwa na changamoto kadhaa hasa za wananchi kutoridhika na mambo mbalimbali yanayotendwa na serikali yake.

Lingine ni wananchi kuona kuwa bado serikali ina matumizi makubwa ya fedha na wakati huo huo inawabidi kufunga mkanda ili kuihudumia huku wakikabiliwa na mazingira magumu ya kipato.

Malalamiko mengine ni baadhi ya watendaji serikalini kuendelea kutumia magari ya kifahari na kutenga Sh19 bilioni kwa ajili ya chai maofisini.

CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.