16 Jun 2009

Miongoni mwa nukuu muhimu kuhusisna na Mwenyekiti Mao wa China ni hii: usiseme kitu kama hujakitafiti (tafsiri yangu isiyo rasmi kwenye usemi no research,no right to speak).Sasa sijui tumweleweje huyu Sekulu MUSTAFA MKULO anapodai kwamba kuna baadhi ya taasisi za dini zimekuwa zikitumia vibaya misamaha ya kodi,lakini hakuweza kutaja angalau jina la taasisi moja.Hizi ni dalili za ubabaishaji na uoga.Uoga huo wa kutaja hadharani watumishi wa Mungu wanaotuhumiwa kuvunja sheria unasababishwa na mtoa tuhuma kutokuwa mkamilifu.Ni mithili ya mama anayechelea kutaja madhambi ya bintie kwa kuwa naye yumo katika mchezo huohuo.



Kama kuna wachunga kondoo wa Bwana walikuwa wakitumia misamaha ya kodi vibaya lakini hawakuchukuliwa hatua,inamaanisha chombo kinachoitwa Mamlaka ya Mapato kiko kwenye usingizi wa pono.Kwanini wahusika hawakuchukuliwa hatua?Au kulikuwa na utatu usio mtakatifu wa vigogo serikalini,wafadhili ughaubuni na watumishi wa Mungu?

Hata kama tukiafikiana na maelezo za Mheshimiwa Mkulo kuhusu hako kamchezo kasikopendeza ,ni dhahiri kwamba vitendo vya watenda dhambi hao wachache havimaanishi kuwa dhehebu lote analotoka mtenda dhambi nalo lina makosa.Kuwepo kwa viongozi kadhaa wa dini ambao wamekuwa wakitumia vibaya misamaha ya kodi hakumaanishi kwamba mantiki nzima ya mpango huo imepoteza maana.


Na lini utaratibu huu wa "akikosea mmoja basi wamekosea wote" ulianza?Mbona hapo Benki Kuu palipozaliwa ufisadi wa EPA na nduguye wa Maghorofa Pacha bado wahusika wameendelea "kupeta"?Kama Ballali ndio kinara cha wizi huo,kwanini basi wasaidizi wake (ikiwa ni pamoja na huyu gavana wa sasa) wameachwa kuendelea na kazi?Je Liyumba anapotuhumiwa kufanya ubadhirifu wa fedha za Maghorofa Pacha,kwanini basi menejimenti yote ya Benki Kuu nayo isipandishwe kizimbani kwa vile,kwamujibu wa Mkulo,akikosea mmoja basi wamekosea wote!Mbona Mattaka kalikoroga ATCL kapelekwa NIC,Peter Noni anahusishwa na EPA kapewa ulaji TIB,Mzee wa Vijisenti na mabilioni yake visiwani Jersey bado yuko kwenye kamati ya maadili ya chama tawala!

Kwa madhambi haya,dnio maana hutosikia yeyote akidiriki kutaja jina la kiongozi wa dini anayetuhumiwa kufuja misamaha ya kodi (kama yupo).Mtu asiye msafi hawezi kuonyesha uchafu wa mwenzie.

Lakini binafsi natafsiri kuwa hatua hii ina ajenda mbalimbali zilizofichika ikiwa ni pamoja na kuonyeshana nani mwenye nguvu zaidi: mamlaka za kidunia au za kiroho.Usisahau kauli za hivi karibuni kutoka kwa madhehebu mbalimbali ya Kikristo kwamba mafisadi wameteka nchi....na kuandaa mkakati wa kupata viongozi bora katika uchaguzi mkuu wa 2010.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.