1 Jul 2009


CCM wafanya mkutano kanisani, wampiga kiongozi wa kigango

Na Frederick Katulanda, Biharamulo

WAFUASI wa CCM juzi walivamia Kanisa Katoliki, Kigango cha Nyantakara kilicho Kata ya Lusahunga na kufanya mkutano wao, huku wakimshambulia na kumjeruhi katibu wa kanisa hilo baada ya kuwaamuru watoke.

Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 3:00 asubuhi wakati wafuasi hao wa wanawake wa CCM, wakiongozwa na mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la John, walipoingia kanisani humo kwa madhumuni ya kuchukua viti kwa ajili ya mkutano wao. Badala ya kuchukua viti, waliamua kutotoka na kufanyia mkutano huo kanisani.

Akizungunza na Mwananchi katekista wa kigango hicho ambacho kipo katika parokia ya Kaniha, jimbo la Kahama, Faustine Damas alisema wafuasi hao wa CCM waliingia kanisani na kuchukua meza ya kuendeshea ibada na kuigeuza kuwa meza ya wageni wao na baadaye kuendesha mkutano wao.

Alieleza kuwa alipofika kanisani alistaajabu kusikia nyimbo wa 'Tieni, tieni' ukiimbwa na baada ya kuingia ndani alikuta wakiwa wanaendelea na mkutano wao huku wakitumia meza kuu ya ibada, jambo ambalo lilimfanya ampigie simu katibu wa kigango hicho, Festus Masumbuko ambaye baada ya kuwaomba waondoke na kuwanyang'anya meza hiyo ya ibada, wafuasi hao wa CCM walianza kumpiga.

"Waliamua kugoma kuondoka na ndipo alipowanyang'anya meza ya ibada, lakini wakamvamia na kumpiga mateke na ngumi. Wamemjeruhi vibaya na pia wamemchania shati," alieleza katekista huyo.

Alisema kutokana na hali hiyo alilazimika kupiga kelele na ndipo wananchi walipofika na kumwokoa. Lakini wakati hali hiyo ikiendelea, mfuasi mmoja wa CCM alipiga simu polisi na kuwaeleza kuwa walikuwa wakifanyiwa vurugu na ndipo polisi walipoenda eneo hilo na kuwakamata wananchi waliokuwa wanataka kumuokoa katibu.

Wananchi hao wanashikiliwa na polisi kwa kufanya vurugu katika mkutano huku wana CCM wakiachiwa huru na kuondoka zao.

Kutokana na hali hiyo paroko wa parokia ya Kaniha, Padri Isaya Bahati ambaye pia ni msaidizi wa askofu wa jimbo la Kahama, alisema muda mfupi baadaye akiwa polisi kuwa amesikitishwa na vurugu hizo na kusisitiza kuwa kanisa kama nyumba ya ibada inapaswa kuheshimika kwa vile si uwanja wala ukumbi wa mikutano.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, naibu katibu mkuu wa CCM, George Mkuchika alisema hana taarifa ya vurugu za wafuasi wake kanisani na kwamba kwa kuwa amepokea taarifa hizo, atazifuatilia kwa kina.

“Ngoja nifuatilie kwa kina kujua ni nini kimetokea,” alieleza Mkuchika.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera Henry Salewi alisema kuwa hakuwa kwenye eneo la uchaguzi na kumtaka mwandishi awasiliane na kamishina Telesphol Anaclet ambaye ndiye amekuwa akishughulikia masuala hayo. Hata hivyo, kamishna huyo alisema jeshi la polisi linaendelea na masuala yake hivyo lipewe nafasi ya kufanya kazi.

“Naomba mtuache tufanye kazi yetu sina cha kukueleza kwa sasa,” alisema kamishina huyo wa oparesheni maalumu ya uchaguzi na akakata simu.

Waliokamatwa na jeshi hilo la polisi wametajwa kuwa ni Evarist Dotto, Semen Elias, Mosha Makoye, Batista na Timetheo ambao walitambulika kwa jina moja.

CHANZO: Mwananchi

HITIMISHO LISILOHITAJI TAFAKURI YA KINA NI KWAMBA CCM IMEFILISIKA KISIASA,NA KATIKA KUTAPATAPA KWAKE IKO TAYARI HATA KUWEKA REHANI AMANI NA UTULIVU WA TAIFA LETU.

NA KWA JINSI ILIVYOSHINDWA KUJINASUA NA TUHUMA KWAMBA INAKUMBATIA UFISADI NA MAFISADI,NI DHAHIRI KAMPENI ZA 2010 ZITASHUHUDIA MAZINGAOMBWE,UHUNI NA UPUUZI ZAIDI YA HUU.DINI NI KITU HATARI KINAPOTUMIWA KWA MINAJILI YA UBINAFSI WA KISIASA JAPO BINAFSI SINA KIPINGAMIZI NA KUCHANGANYA DINI NA SIASA ALIMRADI WAHUSIKA WAWE MAKINI KUTENGANISHA LIPI LA KAIZARI NA LIPI LA KIROHO.

2 comments:

 1. Mie naomba na kuomba na kuomba maana hata sijui uozo huu wa nchini tunaupeleka wapi. Yaani ni kama kila kitu kimeoza. Inasikitisha saana. Lakini NAJUA kuwa kinachotuua ni MFUMO ambao umejengwa kwenye MSINGI WA RUSHWA NA KUTHAMINI PESA ukisaidiwa na KUJUANA.
  Tunahitaji "mkatili" wa viongozi ili kutusaidia kuinyanyua (kama sio kuifufua) nchi yetu.
  Really Sad
  Thanx for it Brother.

  ReplyDelete
 2. Kidumu chama cha mapinduzi...kidumu!
  Na kitaendelea kudumu ndani ya ufisadi!

  Zidumu fikra za watuhumiwa wote wa ufisadi!
  Zidumu!...na wataendelea kupeta katikati ya tuhuma wazi za ufisadi!

  (kwa masikitiko makubwa nadhani ccm itashinda kwa kishindo mwakani)

  ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube