31 Jul 2009


Ushaskia kuhusu political conmanship?Hebu soma kwanza habari ifuatayo kisha tujadili
Spika Sitta aomba ulinzi zaidi, adai nguvu ya mafisadi inahatarisha maisha yake

Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muuangano wa Tanzania sasa anahofia maisha yake kutokana na vitisho vya mafisadi

Spika Sitta aomba ulinzi zaidi, adai nguvu ya mafisadi inahatarisha maisha yake

Kizitto Noya, Dodoma na Boniface Meena

SPIKA wa Bunge Samuel Sitta ameiomba Serikali kumwongezea ulinzi kwa kuwa mafisadi wameongeza nguvu ya vita dhidi yake.

Spika Sitta alisema hayo alipokuwa akizungumzia tuhuma dhidi yake, zilizoripotiwa jana na baadhi ya vyombo vya habari (sio Mwananchi) kuwa anafanya njama kuchoma nyaraka za Bunge.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Spika anadaiwa kula njama ili kuchoma ofisi ya mhasibu wa Bunge ili kuharibu nyaraka muhimu zinazomhusisha na ubadhirifu wa fedha za Bunge.

Lakini Spika Sitta alijibu tuhuma hizo bungeni akisema taarifa hizo zina mkono wa wabaya wake, wenye lengo la kumchafua katika utendaji wake.

“Hivi kama kweli nataka kuficha faili la Bunge nani anaweza kunizuia humu ndani?” alihoji Spika Sitta na kuongeza:

“Hizi ni taarifa za wabaya wangu, wanachofanya ni kuziweka kwenye internet kwanza halafu wanazisambaza kwenye vyombo vyao maalum, magazeti manne; gazeti la Tazama, Tanzania Daima na mengine mnayoyaona," alisema Spika na kuongeza:

“Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba mnipe ulinzi zaidi, hii vita ni ngumu na kubwa sasa. Ulinzi mnaonipa naona hautoshi,” alilalamika Spika Sitta na kuwaponda wanaomwandama kuwa hata iweje, ataendelea kushinda ubunge jimboni kwake na kuwa Spika kama bado atakuwa hai mwakani.

Alifafanua kuwa fedha wanazopeleka maadui zake jimboni kwake Urambo zinasaidia kuimarisha maendeleo, lakini hazitomng’oa madarakani.

"Wananchi wangu wanajua ninachokifanya jimboni kwangu, hata wakipeleka pikipiki bado nitashinda," alisema Sitta.

Mara kwa mara Spika Sitta amekuwa akidai kwamba anaandamwa na mafisadi ambao wanataka aache kufichua maovu yao.

Spika Sitta alisema hayo muda mfupi baada ya kumaliza kutoa mwongozo kwa mbunge wa Micheweni (CUF), Shoka Khamis Juma, kwamba chama fulani kina tabia ya kununua shahada za kura wakati wa chaguzi.

Katika mwongozo wake, Spika alimtaka mbunge huyo kufuta kauli yake bungeni kwa kuwa ushahidi aliotoa kuthibitisha kauli hiyo ni dhaifu.

“Madai ya Shoka ni tuhuma kama tuhuma zozote zinazotolewa na wanasiasa wengine,” alisema.

Akifafanua kuwa Shoka ameshindwa kuthibitisha tuhuma zake kwa kuwa ametoa ushahidi wa magazeti ambayo sio yote yanaweza kuaminika.

“Magazeti yanaweza kuwa chanzo cha taarifa kwa wabunge katika kuchangia hoja zao, lakini sio kigezo pekee cha kumwezesha Spika kutoa mwongozo,” alisema Sitta na kuendelea:

“Hivyo mheshimiwa Shoka hawezi kulindwa na kifungu namba 63 (2), kwa mantiki hiyo namtaka kwa kanuni namba 63 (1) afute kauli yake humu bungeni kabla ya kumalizika kikao hiki cha Bunge”.

Juni 12 mwaka huu mbunge huyo wa CUF alitamka bungeni alipokuwa akiuliza swali la nyongeza kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimekuwa na tabia ya kuiba shahada za kupigia katika maeneo ambayo kinaona hakiungwi mkono.

Naibu Spika Anne Makinda ambaye alikuwa anaongoza kikao cha Bunge siku hiyo, alimtaka mbunge huyo athibitishe kauli yake, naye alifanya hivyo Juni 17, mwaka huu kwa kuwasilisha kwa Spika nakala za magazeti yaliyoripoti uchaguzi wa Jimbo la Busanda.

Hata hivyo, Spika Sitta alisema kwa kuwa hakuna ushahidi wa hukumu kuhusu tuhuma hizo, madai ya Shoka ni tuhuma kama tuhuma zingine zinazotolewa na wanasiasa majukwaani, hivyo kumtaka afute madai yake.
CHANZO: Mwananchi

Nadhani sasa kuna umuhimu wa kuangalia kama Spika huyu wa Viwango na Spidi bado anastahili kuendelea na wadhifa wake ambao ni wa nne kitaifa.Natoa hoja hiyo kwa vile kuna kila dalili kuwa Spika Samwel Sitta sasa anaogopa kivuli chake mwenyewe.
Ni hatari kwa kiongozi wa kitaifa kama Spika kutoa madai mazito namna hiyo pasipo kuwa na uthibitisho wowote.Hivi hao mafisadi wanaohatarisha maisha yake ni akina nani?Nauliza hivyo kwa vile kwa mujibu wa maelezo yake inaonyesha anawafahamu hata kwa majina.Sasa tunapokuwa na kiongozi wa kitaifa ambaye pindi maisha yake yanapokuwa hatarini (kama unaamini anachosema) anakimbilia kuomba aongezewe ulinzi hadharani,then hapo kuna mushkeli.Ni hatari zaidi kumsikia Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,taasisi tukufu yenye jukumu la kutunga sheria za nchi,akiuliza bila aibui wala uoga "Hivi kama kweli nataka kuficha faili la Bunge nani anaweza kunizuia humu ndani?” You can't be serious,Mzee wa Spidi na Viwango!Yaani unatuambia kuwa kwa wadhifa wako unaweza kuficha nyaraka muhimu za Taifa (mfano faili la Bunge) na hakuna mwenye uwezo wa kukuzuia?Nadhani unatafsiri vibaya madaraka yako.Uspika ni nafasi inayoongozwa kwa taratibu na sheria,za nchi na za Bunge unaloongoza.Sasa unapotuambia kuwa hakuna wa kukuzuia ndani ya Bunge kuficha faili (ukijiskia kufanya hivyo) unatuaminisha kuwa aidha huelewi mipaka ya kazi yako,au unadhani Uspika ni kuwa juu ya sheria za nchi na Bunge,au kulewa madaraka.Tukiwa hapohapo kwenye hoja yako ya "hakuna wa kukuzuia...",na tukiamini kuwa ni kweli hakuna wa kukuzuia,je utalalamika kuwa mafisadi wanakuwinda wakikuzushia zengwe kwamba umeficha nyaraka muhimu zaidi ya faili la Bunge?Sawa utasema wanakuandama lakini ushawapa hoja kwamba "ukitaka kuficha faili la bunge hakuna wa kukuzuia".Well,wao wanaweza kuja na tuhuma kubwa zaidi ya kuficha faili.Laiti busara zingetumika,ungeishia tu kukanusha tuhuma za kwamba una mpango wa kuchoma moto ofisi za bunge,na sio kukurupuka kudai una uwezo wa kuficha faili la bunge pasipo kuwapo wa kukuzuwia.Ni rahisi kwa Spika kuomba aongezewe ulinzi (kwa kigezo kuwa ulinzi alionao sasa hautoshi) kwa vile gharama za kuongezewa ulinzi zitabebwa na walipa kodi na si kutoka mfukoni mwa Spika.Hoja hii ya Spika Sitta pia inaweza kufanya tujiulize iwapo licha ya nafasi yake ya Uspika,Mheshimiwa Sitta pia ni mtaalam wa mambo ya ulinzi wa viongozi,na review aliyofanya katika protection anayopewa hivi sasa imempelekea kuhitimisha kuwa ulinzi alionao hautoshi.Hii ni sawa na kuwadharau professionals wenye jukumu hilo,ambao naamini wangetambua mapungufu hayo kabla hata ya Spika Sitta kutamka hadharani.Lakini twende mbali zaidi kwenye hili la "ulinzi alionao Spika hautoshi"Je anaweza kututhibitishia japo tukio moja linaloashiria kutotosha kwa ulinzi alionao hivi sasa?Yaani kutuhumiwa kuwa anataka kuchoma moto ofisi za bunge, na "maadui zake kumwaga fedha jimboni kwake" vimekuwa matishio ya kiusalama yanayotosheleza kufikia uamuzi wa kumuongezea ulinzi?Kichekesho ni kwamba wakati Spika akimtaka Mbunge wa Cuf (Mheshimiwa Shoka Hamis Juma) afute kauli yake kwa kuwa "ushahidi aliotoa-katika madai kuwa kuna chama flani kinanunua shahada wakati wa chaguzi-ni dhaifu",yeye mwenyewe anafanya kilekile cha kutoa madai dhaifu kuwa nguvu ya mafisadi inahatarisha usalama wake ilhali hajaweza kutoa uthibitisho wowote zaidi ya "kauli za kisiasa" kuwa maadui zake wanapeleka pesa jimboni kwake ili asirejee bungeni.Ana uhakika gani kuwa hao anaowaita maadui zake si wananchi wenye dhamira ya kuleta maendeleo katika jimbo hilo pasipo kuwa na ajenda za kisiasa?Au Spika Sitta anataka kutuambia kuwa ni yeye tu aliye na hatimiliki ya kupeleka misaada katika jimbo hilo?Jamani,yaani hadi maendeleo ya jimbo yanafanywa kuwa mithili ya maamuzi ya mtu binafsi!?Kuna mengi ya kujadili kuhusu kauli za Spika Sitta,lakini lililo wazi ni kwamba nafasi anayojipachika ya ukinara wa mapambano dhidi ya ufisadi ni sawa na political conmanship.Kwa lipi hasa?Sio Sitta huyu aliyempa "kifungo" Zitto Kabwe kwa "kosa" la kumkalia kooni Karamagi kuhusu Buzwagi?Sio Spika Sitta huyu aliyetishia kumfungulia mashtaka Dkt Wilbroad Slaa pale mbunge huyo wa Karatu aliposhikilia bango kuhusu ishu za ufisadi?Ni lipi alilofanya Samweli Sitta,kama Spika wa Bunge la Jamhuri au Mbunge wa Urambo linaloweza kumjumuisha kwenye kundi la vinara wa mapambano dhidi ya ufisadi?Yaani Watanzania wenzake kutamani jimbo la Urambo imekuwa ufisadi?Au mtu kutamani nafasi ya uspika imekuwa ufisadi?Lakini kwa vile siasa zetu kwa sasa zinaruhusu mambo ya ajabu kabisa kutokea,kauli hizi za Spika Sitta hazitawahangaisha wenye dhaman ya uchambuzi wa kauli hatari kama hizi na kuchukua hatua za haraka.Ni business as usual,kauli imetolewa,siku imepita,and life goes on!Na kwa vile magazeti yetu yako bize zaidi kuripoti habari badala ya kuchambua mantiki ya habari husika,yayumkinika tutasikia makubwa zaidi ya kauli hizi za wanasiasa wanaoogopa vivuli vyao wenyewe.Na kwa vile kilio,kicheko,kuchafua hewa na hata kukoroma kwa mwanasiasa kunatosha kuwa leading news kwenye magazeti yetu,basi tutarajia vimbwanga zaidi.Trust me,tutashuhudia vituko vingi zaidi na zaidi kadri siku zinavyoyoyoma kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010.By the way,si ndio tunaelekea kile kipindi cha usanii wa kisiasa ambapo watu wazima hupiga magoti majukwani na wengine kutoa shikamoo hata kwa watoto wadogo alimradi wahakikishiwe kura?
1 comment:

  1. hello... hapi blogging... have a nice day! just visiting here....

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube