16 Oct 2009


NDUGU YANGU Mpayukaji Msemaovyo anasema:

Naitwa Mchumiatumbo mwana wa Tapeli.

Ingawa wakati naandika waraka huu vijana wenzangu wapatao 166 wamo wakimenyeka toka Mwanza hadi Butiama, kama ishara ya kumbukizi ya safari yako adhimu ya ukombozi ukiliungua mkono marehemu azimio la Arusha, mimi sitafanya hivyo.

Nina sababu. Kwanza mimi ni mnafiki wala mjamaa kama wewe. Nina roho nyepesi hasa nionapo vitu kama pesa madaraka na sifa.

Mimi ni mbabaishaji na muongo; au msanii kama washikaji wasemavyo. Ni fisadi through and through. Ninanuka kiasi cha kutostahili hata kukaribia kaburi lako achia mbali nyumba yako, wanao, mkeo, watu wako hata taifa lako. Nisingependa walevi na wazinzi kufagia makaburi ya mitume mwalimu. Hivyo, kwanza nakuwa mkweli kwa nafsi yangu na kwako na umma wako.

Tatu, nitaunga mkono azimio lipi iwapo ninaoona wamenizunguka wakiwaibia watu wako ni wale wale walioliua azimio la Arusha? Nitaadhimisha vipi iwapo miiko ya uongozi na usawa wa binadamu vimetoweka na nafasi yake kuchukuliwa na ufisadi, ujambazi wa mchana, ubabaishaji na uongo?

Nne, mwalimu, sitaki kujidanganya na kukudanganya. Kile ulichopigania kwa sasa hakuna. Ulipigania uhuru na maendeleo. Sasa kuna utumwa na kuporomoka. Ulitekeleza ujamaa na kujitegemea. Sasa tuna uhujumaa na kujimegea. Ulipigania mstakabali wa nchi toka kwa wakoloni wawe wavumbuzi, wamisionari na watawala. Sasa mstakabali huo umo mikononi mwa wawekezaji, na wafadhili wa makuadi wao. Ulipigania ardhi ya Tanzania kabla haijaingia mikononi mwa vijifalme vya kifamilia. Nitakuenzi kwa udhu upi iwapo kila nipitapo Loliondo nakaribishwa kwenye falme za kiarabu utadhani hapa ni uarabuni?

Nitapata wapi mshipa wa kukuenzi wakati nakung’ong’a? Je mwalimu una habari? Yale madini uliyosema vizazi vijavyo vingeyaendeleza na kufaidika nayo yaliuzwa na jamaa yako Tunituni uliyempigia debe usijue jizi.

Tano, mwalimu siwezi kukuenzi wakati nakuchukia na kukudharau. Ningekupenda na kukuheshimu ningeshika urithi wako na kuheshimu wosia wako wa kupendana na kutohujumiana. Nakumbuka wakati ukianga dunia ulikuwa ukiwalilia watanzania wako baada ya kugundua makosa uliyofanya kuwaweka mikononi mwa nunda wala watu. Nami ni mmojawapo.

Je una habari mkoani mwako watu wameishamiminiwa risasi za moto kutokana na kukatiza kwenye ardhi ya mwekezaji na si mtanzania? Una habari mkoani mwako uchafuzi wa mazingira unatishia maisha ya ndugu zako? Hapa kweli nina sababu ya kukuenzi? Je kukuenzi ni matendo au maneno mwalimu?

Ingawa ukiwa kuzimu bado unaliletea sifa taifa langu, sifichi wala kuchelea kukwambia kuwa waliohai wanaliletea aibu na fedheha baada ya kulibinafsisha huku wakibinafsisha hata akili na roho zao. Mwalimu nilikufahamu sana . Ulikaa madarakani kwa kitambo kirefu ukiacha nyuma familia isiyo na ukwasi zaidi ya utu. Uliowawezesha wamefikia hata kuchukua ule mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira uliozawadiwa na rafiki yako Mao Tse Tung.

Mwalimu, vinyamna mwitu na mbwa hawa walitutenda kweli. Walitudanganya kuwa uwekezaji ndiyo sera na njia pekee ya kutukomboa tusijue walikuwa wakimaanisha kinyume. Wengine walituahidi maisha bora kwa wote tusijue wote ni wao washirika zao, watoto zao na wake zao hata nyumba ndogo zao. Tupo msambweni mwalimu wakati huu tunapozidi kuuzana na kuhadaana. Je unaweza kuamini kuwa kwa sasa hakuna tofauti ya polisi na kibaka? Nina ushahidi. Juzi polisi aliuawa kama kibaka na wananchi wenye hasira na kukata tamaa huku polisi tena wakubwa wakiwapiga risasi wafanyabiashara wakidai ni vibaka!

Wakati wa uongozi wako matupinkele au zeruzeru kwa lugha rahisi walikuwa salama. Baada ya kuingia pepo la utajiri usioulizwa ulivyopatikana, maskini hawa wanatolewa kafara na wanganga njaa wa kienyeji. Hivyo ndugu zetu hawa wanauawa hata zaidi ya swala mwalimu na hawana mtetezi zaidi ya vijikesi viwili vitatu vya kuondolea lawama. Tembo kwa sasa wana ulinzi madhubuti zaidi ya ndugu hawa.

Zama zako uliongoza. Uongozi ulikuwa utumishi wa umma na si uchumia tumbo na utumikishaji na uhujumu wa umma. Ikulu ilikuwa mahali patakatifu siyo pa deal. Uongozi ulikuwa uongozi na si uongo kama sasa. Siasa ilikuwa baraka si balaa kama sasa.

Wale watoto wa wachunga mbuzi na maskini wa kunuka uliowatoa kwenye umaskini na kuwasomesha sasa ni matajiri wa kutupwa. Yupo mpumbavu mmoja jizi aliyewahi kuita shilingi bilioni moja vijisenti ukiachia mbali wengine uliowaachia laana kuwa walikuwa wamejilimbikizia chumo la wizi. Na kweli maneno yako hayakuanguka. Kwani wezi wenzao waliwabeba na kuwakweza hatimaye tamaa zao na upofu vikawadondosha.

Mwalimu sitakuenzi,. Siwezi kujidanganya na kuidanganya dunia. Nitakuenzije iwapo kipato changu kinatokana na rushwa, uwekezaji, uuzaji mihadarati, uongo, ahadi hewa, uhujumu na mengine mengi yapinganayo na dhamira ya dira yako mwalimu?

Hivi kweli panya anaweza kumuenzi paka zaidi ya kufaidi ‘uhuru’ baada ya paka kuondoka? Je nune aweza kuishi nje ya kinyesi cha ng’ombe zizini? Si haki nune kuwa mwalimu wa usafi wakati mlo wake na makazi yake ni kwenye uchafu hata anenepe na kunawiri vipi.

Mwalimu naogopa kuja Butiama au kusimama mbele ya kadamnasi ya maadhimisho yako na kukupamba wakati nilisha kuvua nguo. Naogopa. Maana mama Maria hata wanao wananijua. Inawezekana nikakulamba uchogo na kukupaka mafuta kwa mgongo wa chupa kiasi cha kumkera mmojawapo akaamua kunizodoa na nikazidi kudhalilika ingawa niliishadhalilika muda mrefu.

Mwalimu ulikuwa na akili inayochemka. Yangu mimi ni bongolala. Ulikuwa msafi na mwadilifu. Mie ni mchafu sina mfano. Mkeo hakuwa akitumia ofisi yako kuubia umma. Mie wangu nami wote tu wezi. Nikiiba huku yeye anaibia kule. Hata watoto nimewaingiza. Nataka hata ikibidi wawe marais kama siyo mawaziri. Je hapa mwalimu nitakuwa na cha kukuenzi?

Mwalimu ulileta elimu bure kwa wote. Mie nashabikia kuchangia gharama ingawa kimsingi hakuna gharama za kuchangia zaidi ya kutunisha mfuko wa walaji wakubwa. Ulipigania ardhi. Mie natamani niwe rais niiuzie mbali nipate changu nifiche ughaibuni. Mwalimu ulichukia wafanya biashara wezi. Mie hawa ndiyo washitili wangu.

Mwalimu ulisisitiza usawa wa binadamu. Mie naamini binadamu si sawa wala si mfano wa Mungu kama wachungaji wasemavyo. Usawa ni mambo ya kizamani. Kwangu, heshima ya binadamu haitokani na ubinadamu wake bali pochi lake. Hukusikia wahenga wakisema mwalimu kuwa aso kitu si mtu bali kinyama mwitu? Mtu chake bwana. Kwa imani yangu mie si mfano wa Mungu bali mfano wa shetani kutokana na uroho na roho mbaya vyangu. Mungu si mwizi wala muongo wala mbabaishaji kama mimi mwalimu.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.