14 Dec 2009



Waziri Chikawe asema Kikwete hawezi kuwabana mafisadi
*Asema Rostam, Dk Hoseah hawakamatiki
*Asikitika DPP, DK Hoseah kuparuana

Na Leon Bahati

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe amesema Rais Jakaya Kikwete hana uwezo kutumia mamlaka yake kuwapeleka mahakamani watuhumiwa wa ufisadi kwani hilo ni jukumu la vyombo alivyoviteua kuchunguza na kuchambua nani afikishwe huko baada ya kujiridhisha kwa ushahidi.

"Huu ni utawala wa sheria, Rais Kikwete hawezi kutoa amri za kukamata watu wakati kuna vyombo alivyoviteua kuchunguza na kuchukua hatua." Waziri Chakawe alisema hayo jana alipokuwa katika mahojiano maalumu na gazeti hili ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Alisema kitendo cha baadhi ya Watanzania kumshinikiza Rais Kikwete awafikishe mahakamani watuhumiwa wa ufisadi kinaashiria kuwa wanataka aamuru watuhumiwa hao wapelekwe mahakamani bila kutumia vyombo husika jambo ambalo haliwezekani katika mfumo wa kibepari.

"Enzi zile za mfumo wa ujamaa na chama kimoja cha siasa, hilo lingewezekana lakini wakati huu ambao nchi inatumia mfumo wa kibepari, haiwezekani," alisema Chikawe.

Hivi karibuni, wanasiasa na hata baadhi ya viongozi waliowahi kuwa serikalini awamu zilizopita, wakichangia mada ya mustakabali wa taifa kwenye kongamano la taasisi ya Mwalimu Nyerere, waliitaka CCM imtose Rais Kikwete asigombee tena ili kumalizia ngwe ya miaka mingine mitano, iwapo atashindwa kufanya maamuzi magumu ya kuwachukulia hatua watuhumiwa wa ufisadi.

Alionya kwamba Rais Kikwete akikurupuka katika hilo, kesi nyingi zitakwaa kisiki mahakamani na itabidi hao wanaoitwa mafisadi kulipwa mabilioni ya fedha kama fidia ya usumbufu.

Chikawe alisema mawazo ya namna hiyo yanatokana na watu wengi kuendelea kuwa na mtazamo wa mfumo wa kijamaa na chama kimoja na kusahau kuwa tayari nchi imeingia katika mfumo wa kibepari.

Waziri Chikawe alitumia mfano wa enzi za waziri mkuu, hayati Edward Sokoine alipopambana na wahujumu uchumi kwa kutoa amri ya kukamatwa watu ovyo na kutaifishwa mali zao kuwa moja ya mifano ya uongozi katika mfumo wa ujamaa.

Alisema amri hizo zilikubalika kulingana na mazingira ya wakati lakini, ulipoanza kuingia mfumo wa kibepari waliopoteza mali kupitia operesheni hiyo walidai haki kupitia mahakama na walishinda hivyo serikali ikabidi iwafidie pamoja na usumbufu.

Waziri huyo mwenye dhamana ya kusimamia katiba na sheria za nchi, ambaye amekuwa kimya licha ya kuwepo na mijadala mingi inayokosoa utendaji wa vyombo vya sheria nchini hasa suala la ufisadi, alisema polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wana haki ya kuchunguza makosa ya jinai, lakini pia mkurugenzi wa mashtaka (DPP) ana mamlaka ya kutoruhusu kesi hizo zisiende mahakamani kama hakutakuwa na ushahidi wa kutosha.

Alitoa mfano wa Mbunge wa Igunga, Rostam Azizi (CCM) ambaye wengi wamekuwa wakimtuhumu kwa ufisadi kupitia kashfa ya kampuni tata ya Richmond iliyopewa zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura mwaka 2006, akisema hakuna ushahidi wa kumfikisha mahakamani.

"Wewe jaribu kuipitia ile ripoti ya Kamati Teule ya Bunge ya (Dk Harrison) Mwakyembe, hata uipitie mara 10. Mimi nimeipitia mara nane, sijaona sehemu ya kupata ushahidi wa kumshtaki," alisema Chikawe.

Kuhusu anwani ya barua pepe ya kampuni ya Caspian ambayo inamilikiwa na Rostam kutumiwa na kampuni iliyoirithi Richmond, alisema: "Ni sawa, lakini hadi sasa hakuna mahali popote ambapo kampuni ya Dowans inatuhumiwa. Yenyewe ilipokea jukumu ambalo Richmond ilishindwa lakini wao wakatekeleza. Ingekuwa Dowans wana matatizo, basi hata Rostam angeweza kuhusishwa."

Alizungumzia shinikizo la kutaka Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah awajibishwe kwa madai ya kuficha madhambi ya Richmond ambayo kamati ya Dk Mwakyembe iliyaweka wazi, alisema:

"Takukuru ilichunguza mwenendo wa utoaji wa zabuni kwa Richmond na kwenye ripoti yake ikaeleza haikuona fedha zilizotumika kurubuni mtu yeyote. Na hata kamati ya Dk Mwakyembe haikubaini kitu cha namna hiyo.

"Kamati ya Dk Mwakyembe imebaini udhaifu wa serikali kuchunguza Richmond kabla ya kuingia mkataba na hili ndilo lililofanya Lowassa na wenzake kujiuzulu na Baraza la Mawaziri kuvunjwa."

"Lakini uzuri ni kwamba Rais Kikwete alikuwa ameagiza wasipewe fedha hadi wawe wameleta mitambo nchini na hilo lilifanyika. Kampuni ya Richmond haikuchukua hata senti ya serikali. Kama ilihonga watu kwa siri huko, ilikula kwao. Ila tunachojua walishindwa kuleta mitambo ya kuzalisha umeme wakatoa kazi hiyo kwa Dowans ambao walifanikisha."

Pamoja na hali hiyo, Chikawe alisema Mtanzania yeyote mwenye ushahidi unaoweza kuwashtaki wanaotuhumiwa ni vyema akawasiliana na Mpelelezi Mkuu wa Makosa ya Jinai (DCI) au Takukuru.

Kuhusu majibizano yaliyotokea hivi karibuni baada ya Dk Hosea kumlaumu DPP, Elieza Feleshi kwa kukalia mafaili zaidi ya 60 ya kesi za ufisadi na baadaye Feleshi kumjibu kuwa ni muongo, Chikawe alisema ni jambo ambalo halikumpendeza.

"Kwa kweli imekuwa bahati mbaya vyombo hivi vya serikali kulumbana vyenyewe, lakini nafikiri ilikuwa ni bahati mbaya tu, wakati mwingine hilo halitatokea," alisema Chikawe.

Hata hivyo, alisema huenda lilichangiwa pia na vyombo vya habari kwa kuchokonoa mambo hayo hivyo kuwafanya kutoa kauli ambazo pengine zilionekana kuhitilafiana.

Chikawe ambaye ni Mbunge wa Nachingwea alisisitiza kwamba DPP amekuwa akipelekewa mafaili mengi na anapoona hayana ushahidi wa kutosha huwashauri wahusika mambo ya kufanya na pengine kuwaeleza kwamba hakuna kesi ya kujibu.

CHANZO: Mwananchi

1 comment:

  1. Basi hata kuwaondoa katika nafasi alizowateua yeye mwenyewe au kuwanyangánya kadi za uanachama kwa wale waliokiuka maadili ya ya CCM?

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.