13 Dec 2009


Mara Sophia Simba dhidi ya Anne Kilango,mara Rostam Aziz dhidi ya Mwakyembe,mara tunaambiwa Kamati ya Mwinyi nako "hakieleweki",na sasa watendaji wakuu na wateuliwa muhimu wa Rais,Mkurugenzi wa TAKUKURU Dr Edward Hosea na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Eliezer Feleshi nao wameingia kwenye malumbano,kama linavyoripoti jarida la Mwananchi

DPP amvaa Dk Hoseah, ataka mdahalo majalada kesi za kifisadi

Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah ambaye jana alidai kuwa DPP amekalia kesi 60 tuhuma za rushwa

James Magai

KWANZA ilikuwa ni ndani ya chama tawala CCM, lakini malumbano baina ya vigogo sasa yamehamia serikalini baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi kujibu mashambulizi ya mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah, akitaka uitishwe mdahalo baina ya wawili hao ili ajibu tuhuma dhidi yake.

Pendekezo hilo la Feleshi limekuja wakati malumbano baina ya viongozi wa CCM hayajapoa baada ya kutuhumiana kwa ufisadi na wivu wa nafasi mbalimbali zilizotokana na uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

Dk Hoseah, ambaye amekuwa akirusha makombora kwa taasisi tofauti, juzi alitoa tuhuma nzito alipokaririwa na gazeti moja akisema kuwa ameshawasilisha kesi zaidi ya 60 za tuhuma za rushwa kwa DPP na akashangaa sababu za mteule huyo mwenzake wa rais kukalia mafaili hayo badala ya kufungua kesi dhidi ya watuhumiwa.

Lakini jana Feleshi alikuwa mbogo na akasema kuwa ili ukweli uwekwe bayana kuna haja ya kuandaa mdahalo baina yake na Hoseah.

DPP Feleshi, akizungumza na gazeti dada la Mwananchi la The Citizen baada ya hafla ya mafunzo ya kamati ya kitaalamu ya mawakili wa serikali iliyofanyika Kunduchi jijini Dar es Salaam, alisema njia pekee ya kuweka sawa rekodi ni kuwepo kwa mdahalo huo wa wazi.

"Ninataka mdahalo na Hoseah katika masuala haya yanayoendelea hata kama utakuwa wa simu tena iwekwe ‘loud speaker (kipaza sauti)’ ili tujadili masuala haya na kumaliza kiu ya wananchi," aliweka msimamo DD Feleshi.

"Kama mtu anasema kuna majalada 60 ofisini kwangu, then (kisha) tunamuuliza yamefika lini? Yeye pia atajibu, kwa kufanya hivyo tutatoa mwanga mzuri kwa wananchi ambao ofisi hizi zipo kwa ajili yao tu."

DPP Feleshi alisema anataka mdahalo huo ufanyike mbele ya waandishi wa habari ili jamii ijue masuala mbalimbali yanayoelekezwa ofisini kwake.

Hoseah pia aliwahi kuirushia kombora mahakama akisema inaendesha taratibu kesi za ufisadi, hivyo kupunguza kasi ya taasisi hiyo kushughulikia watuhumiwa wa rushwa.

Miongoni mwa kesi ambazo zilifunguliwa kwa wingi hivi karibuni na Takukuru ni pamoja na kesi zaidi ya 20 zinazohusu wizi kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), matumizi mabaya ya madaraka na uzembe na tuhuma za kula njama na kuisababishia hasara serikali.

Hata hivyo, mwenendo wa kesi nyingi umekuwa wa kasi ndogo kutokana na upande wa mashtaka kutokamilisha ushahidi.

Akizungumzia madai hayo ya Hoseah, Feleshi aliweka bayana kwamba hayajui majalada hayo na anachojua ni kwamba ofisini kwake kuna majalada ya kesi ambayo yanaingia na kutoka kila siku na anayashughulikia kwa mujibu wa sheria.

Feleshi, ambaye aliwahi kurejesha Takukuru baadhi ya majalada kutokana na kuonekana udhaifu katika ushahidi, alimtaka Dk Hoseah kutoa ufafanuzi kwa kueleza ni majalada gani yanayokaliwa na ofisi yake na yamefika lini.

Alifafanua kwamba ofisi yake haiwezi kukalia majalada kwa kuwa inafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kwa maslahi ya umma na kusisitiza hayajui majalada hayo 60 anayodai Dk Hoseah kwamba yamekaliwa ofisini hapo.

"Hayo mafaili (majalada) ya vigogo mimi siyajui. Ninachojua ni kwamba tuna majalada yanaingia kila siku ya Watanzania wanaotuhumiwa. Tunapokea na kuyafanyia kazi... na hatubagui kuwa haya ni ya PCCB (Takukuru) , TRA( Mamlaka ya Mapato) au ya Polisi. Katiba ya nchi inatoa haki sawa kwa wote kufikishwa mbele ya sheria ili kupata haki," aliongeza DPP.

"Tunafanya kazi kwa maslahi ya umma na tunaendesha shughuli zetu kisheria wala si kwa kuzingatia jambo lolote kwa kuwa hatuna maslahi yoyote kumshtaki mtu bila kuwa na ushahidi wala hatuna maslahi yoyote kumwachia mtu kama kuna ushahidi. Ndiyo maana nasema hakuna kukalia majalada."

Feleshi, ambaye ana mamlaka ya kufunga au kufungua mashtaka kwa watuhumiwa, alisema katika hali hiyo ni vigumu kusema kuna majalada yana muda mrefu kwani hajui hayo yanayosemwa yaliingia lini ofisini kwake.

"Labda kama angekuwepo mwenyewe (Dk. Hoseah) angeeleza zaidi hayo majalada anayodai tumeyakalia. Ni vema mkamuuliza hilo," alisema.

Hizi ni dalili za wazi kwamba kuna ombwe la uongozi wa kitaifa.Yaani kila mtu anaropoka anavyopenda hasa kwa vile mwenye jukumu la kukemea yuko usingizini fofofo.Nidhamu imekuwa zero kwa vile anayepaswa kuwaadabisha watovu wa nidhamu yuko bize na mambo mengine yasiyo na umuhimu kwa taifa.

Tunaelekea pabaya japo Watanzania wengi hawaonekani kuguswa na hali hii.

Ni vema tukaamua kuchukua maamuzi mazito kabla hali haijafikia mahala tusipoweza kurekebisha.Tusipoziba ufa tujajenga ukuta.Unfortunately,baada ya ukuta kuanguka kutokana na nyufa zilizopo tunaweza kushindwa kujenga ukuta huo baada ya matofali yote na tanuru zima kuuzwa na mafisadi.

2010 INAKUJA.IT'S THEN OR NEVER!

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.