23 Feb 2010

Angalia "mchemsho" huu  wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Samuel SITTA.Anarusha tuhuma nzito dhidi ya wanaharakati wanaokusudia kuandamana kupinga "mahitimisho ya mjadala wa Richmond bungeni" ilhali katika habari husika ameshindwa kuthibitisha tuhuma hizo.Kibaya zaidi,yeye mwenyewe aliporushiwa tuhuma kama hizo aligeuka mbongo.Hebu soma kwanza habari husika (hasa maneno ya rangi nyekundu)

Salim Said
SPIKA wa Bunge Samuel Sitta amewashukia wana-mtandao wa asasi za kiraia zinazotetea usawa wa jinsia, haki za binadamu na maendeleo ya ukombozi wa Wanawake, akisema wanatia mashaka na kwamba wanaendeshwa na utashi binafsi wa wajanja wachache, huku wenyewe wakisema maandamano yapo palepale.
Wanaharakati hao, walitangaza maandamano makubwa ya amani yatakayoendeshwa nchi nzima kupinga kuvungwavungwa kwa hoja za mikataba ya Richmond, TICTS, TRL, taarifa ya uchafuzi wa mazingira kwa kemikali za sumu katika mgodi wa North Mara na ukiukwaji wa haki za binadamu, Loliondo.
Akizungumza na Mwananchi jana Spika Samuel Sitta alipingana vikali na madai ya wanaharakati hao, kuhusu Bunge na kueleza kwamba mtu yeyote akitaka kupima uwezo na uzuri wa bunge katika maamuzi na kusimamia serikali aangalie rekodi ya kazi za bunge kuanzi mwaka 2005 hadi sasa.
'Mimi sikubaliani na wanaharakati hawa hata kidogo. Maandamano ni haki yao na waandamane, lakini hawawezi kupima kazi za bunge kwa kuangalia kipindi cha mitafaruku ," alisema Spika Sitta.
Spika Sitta alisema kuimarisha Bunge si kazi ya lele mama, bali ni mapambano yanayohitaji ujasiri wa hali ya juu.
"Mimi naamini kwamba bunge letu limeimarika katika kuisimamia serikali ukilinganisha na lilikotoka, wanaharakati wanapaswa kujua pia kuimarisha bunge ni mapambano," alisema Spika.
Kuhusu suala la bunge la mfumo shirikishi wa demokrasia, Spika Sitta alisema hilo ni kinyume na katiba, lakini aliwataka wanaharakati hao wajaribu kujenga hoja.
"Mimi naona mfumo wa demokrasia ya uwakilishi bungeni ni mzuri tu, kwa sababu unapatikana kupitia uchaguzi ambayo ni ridhaa ya wananchi, lakini mfumo shirikishi utapatikana wapi.
"Huwezi kushirikisha mashirika au taasisi hizo katika bunge, kwanza zinamwakilisha nani, kwanza haziwawakilishi wanawake ni utashi tu wa baadhi ya wajanja," alihoji Spika Sitta.
Alisema mitandao hiyo inatia mashaka kwa wahisani kwani baadhi ya taasisi zinakula fedha bila ya kupeleka mrejesho kwa wahusika.
"Mambo yote ya bunge yanajadiliwa hadharani na kila mtanzania anayetaka anasikia, lakini je mambo ya hawa wanaharakati na mitandao yao yanajadiliwa na nani," alihoji Spika Sitta.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Concern for Development Initiatives in Africa (ForDIA), Bubelwa Kaiza alisema ujumbe wao mkubwa katika maandamano hayo, ni kwamba hoja hizo zimevungwavungwa na bunge halitambui nguvu na mamlaka liliyopewa kikatiba, badala yake linafanya kazi kwa maslahi ya vyama vya siaasa na sio wananchi.
"Wapo wanaotaka tusiandamane, lakini huo ni woga wao tu, maandamano yapo palepale nchi nzima, tuna sababu za msingi za kuandamana kwani bunge halikuwajibika katika kushughulikia hoja mbalimbali katika kikao cha 18, badala yake limezivungavunga hoja hizo kwa maslahi ya vyama vyao vya siasa.
"Sisi pamoja na wananchi hatukuridhika kuhusu hoja zile zilivyohitimishwa, hakuna pia aliyewajibishwa, kwa hiyo tunaitaka serikali iachane na mfumo wa demokrasia wakilishi na ianzishe mfumo wa demokrasia shirikishi wa bunge ili wabunge waweze kuwajibika moja kwa moja kwa wananchi," alisema Kaiza.
CHANZO: Mwananchi

Tatizo kubwa linalomkabili Spika wetu Samuel Sitta ni uropokaji,yaani kuongea bila ktafakari athari zinazoweza kusababishwa na matamshi yake.Kama kiongozi mkuu wa chombo chenye dhima ya kutunga sheria za nchi,Sitta alipaswa kutambua kuwa baadhi ya kauli na tuhuma alizotoa dhidi ya wanaharakati ni za kihuni.Na bahati yake ni kwamba wanaharakati hao hawana muda wa kumburuza mahakamani kuthibitisha kashfa alizotoa dhidi yao.

Hivi Spika Sitta anaweza kuuthibitishia umma kuwa mitandao inatia mashaka kwa vile baadhi ya taasisi zinakula pesa bila kurejesha fedha kwa wahusika?Ameyajuaje hayo?Hivi hao wanaotoa fedha zao (wanaofadhili mashirika hayo) wamekuwa wajinga kiasi gani cha kutohitaji taarifa za matumizi ya fedha wanazotoa?

Sitta ni mropokaji kwa vile yeye alipotuhumiwa kukumbatia ufisadi katika ofisi ya Bunge aliwaka kama nini akidai ni njama za mafisadi dhidi yake.Iweje leo akurupuke kuwatuhumu wanamtandao kwa vile tu wameonyesha nia ya kuandamana kupingana na ubabaishaji wa Bunge linaloongozwa na Sitta?

Sitta asijione Mungu-mtu.Kila Mtanzania ana haki kama yeye Sitta kutoa mawazo yake hadharani alimradi havunji sheria za nchi.Kama Sitta anaona Bunge analoongoza limefanya vizuri katika utendaji kazi wake,si lazima kwa kila Mtanzania kuona hivyo au kukubaliana na mtizamo wa aina hiyo.Na ni vigezo vipi anavyoweza kutuonyesha Mheshimiwa Sitta kuwa Bunge lake limewajibika ipasavyo?Huko kutuzuga kwa zaidi ya miaka miwili kuwa yeye na wenzake ni wapambanaji dhidi ya mafisadi kisha kusalimu amri kama kondoo walionyeshewa mvua?

Na hata kama Bunge analoongoza Sitta linawajibika akama anavyotaka tuamini,si ndio kazi yake?Na si kazi ya kawaida kwani kwa mshahara wa mamilioni na kiinua mgongo cha mamilioni mengine kwanini waheshimiwa hawa wasiwajibikie kwa kiwango cha juu?

Sitta anakasirika kwa vile alitangaza kuwa "mjadala umefungwa",na kwa jinsi anavyojihisi ni Mungu-mtu anaona kitendo cha wanaharakati "kuendeleza mjadala" ni kama "wanavunja amri ya Mungu".Katika habari husika hapo juu,Sitta anathibitisha ubinafsi wake kwa kurudiarudia kutumia neno "MIMI".Anaweza kuwa sahihi katika mtazamo wake binafsi,lakini jamii hailazimiki kuafikiana nae wala kushurutishwa kutenda atakayo yeye.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube