5 Mar 2010

 (Picha kwa hisani ya Mjengwa.)
MATUMIZI mabaya ya serikali na kuendelea kupanda kwa mfumuko wa bei za bidhaa kwa zaidi ya mara mbili katika kipindi cha kati ya mwaka 2005 na sasa ni chanzo cha maisha magumu ya wananchi, Tanzania Daima limebaini.
Katika wakati ambapo wananchi wapatao milioni nane wanalala au kushinda njaa kwa sababu ya ugumu wa maisha, serikali jana ilikiri kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Ramadhan Kijjah, imekuwa inatumbua shilingi mbili, wakati ina uwezo wa kukusanya shilingi moja

Akitoa tathmini ya serikali kuhusu hali ya uchumi kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, Kijjah alisema mapato ya serikali kwa mwaka ni sh trilioni tano, lakini matumizi ya serikali ni Sh trilioni 10.

Akijadili tathmini hiyo, mchumi na mwanasiasa, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema matumizi hayo makubwa ya serikali yanaathiri vibaya Watanzania wa kawaida, kwani yanachochea mfumuko wa bei unaosababisha gharama za maisha kuwa za juu.

Wakati Kijjah akikiri kwamba kimsingi, mapato ya serikali yamepanda kutoka Sh trilioni 2.167.6 mwaka 2005/06 hadi Sh trilioni 5.096 mwaka 2009/10, Profesa Lipumba alisema kama serikali ingekuwa makini, kulingana na ulaji mkubwa inaoonyesha, makusanyo ya sasa yangekuwa makubwa zaidi na yangekusanya kwa nidhamu.

Alisema serikali inawaachia watu fulani fulani (hakuwataja) na makampuni makubwa yasilipe kodi.

Kwa sababu hiyo, Profesa Lipumba alisema uchumi wa nchi unayumba na kufanya maisha ya Mtanzania yazidi kudorora.

“Hakuna ukusanyaji mzuri wa kodi; watu wanaachiwa, makampuni yanayochimba madini hayalipi kodi ya kutosha….hilo lina athari,” alisema Profesa Lipumba.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mwaka 2004/05 wakati utawala wa Rais Benjamin Mkapa ukielekea ukingoni matumizi ya serikali yalipanda kutoka Sh trilioni 2.1 hadi Sh. trilioni 2.7 mwaka 2005/06 wakati Rais Jakaya Kikwete anaingia madaraka.

Mbali ya hilo taarifa hiyo ya Kijjah ilionyesha kwamba mfumuko wa bei umepanda kwa zaidi ya mara mbili katika kipindi cha kati ya mwaka 2005 ulipokuwa ni asilimia 5 hadi kufikia asilimia 12.2 Desemba mwaka jana kabla ya kushuka kidogo na kuwa asilimia 10.9 Januari mwaka huu.

Hata hivyo Kijjah, alisema serikali imechukua hatua ili kukabiliana na matumizi hayo makubwa. Alisema imeongeza idadi ya wahasibu na wakaguzi wa ndani katika ngazi zote kuanzia wizara hadi serikali za mitaa.

“Kuanzishwa kwa kitengo cha ufuatiliaji wa matumizi ya umma (bajeti) katika miradi iliyoidhinishwa: Ofisi ya Mkaguzi Mkuu (CAG) imeongezewa nguvu za kisheria kuweza kufanya kazi zake bila kuingiliwa na taasisi yoyote.”

Katibu mkuu huyo ambaye alikuwa amefuatana na naibu wake, John Haule, aliongeza ili kupunguza matumizi makubwa ya serikali, yanahitajika marekebisho katika Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004 ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa watendaji wake.

“Sera ya mapato ya mwaka 2009/10 inalenga kukusanya mapato ya ndani yasiyopungua sh milioni 5,096,016 sawa na asilimia 16.4 ya pato la taifa,” alisema.

Kuhusu thamani ya fedha, Kijjah alisema, shilingi iliendelea kuporomoka kutoka wastani wa shilingi 1,195.75 kwa dola ya Kimarekani mwaka 2008 hadi kufikia shilingi 1,318.71 mwaka jana.

CHANZO: Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.