4 Mar 2010


Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi,Rais Jakaya Kikwete alieleza kwa undani matarajio yake kuhusu ufanisi wa Sheria mpya ya Uchaguzi.Pamoja na mambo mengine,sheria hiyo inatarajiwa kuziba mianya ya rushwa kwa wanasiasa wanaowania uwakilishi wa wananchi katika Bunge.Hata hivyo,pamoja na nia njema na umuhimu wa kuwa na sheria hiyo,ushahidi wa kimazingira unaashiria kuwa itabaki kuwa sheria tu kama zilivyo nyingine nyingi pasipo kuzaa matunda yanayokusudiwa


Tatizo la nchi yetu halijawahi kuwa ukosefu wa sheria bali usimamizi na utekelezaji wake.Mifano ni mingi,lakini kwa vile sheria hii ya Uchaguzi inalenga kudhibiti mianya ya rushwa,ni vema tukaangalia kwanza ufanisi wa sheria nyinginezo zilizopo ambazo kwa hakika zingeaidia sana kupunguza tatizo la rushwa laiti zingetumika ipasavyo.

Kinachokwaza zaidi usimamizi na utekelezaji wa sheria zetu nyingi ni ukosefu wa uzalendo miongoni mwa waliokabidhiwa dhamana ya kuzisimamia na kuzitekeleza.Ni kichekesho kusikia miongoni mwa taasisi zinazotarajiwa kuwa na dhamana ya hali ya juu katika usimamizi na utekelezaji wa sheria hiyo ni TAKUKURU,chombo ambacho wengi wetu tunaamini kuwa kimeshindwa kazi yake.Hivi TAKUKURU iliyoshindwa sio tu kuchukua hatua dhidi ya wezi wa Richmond bali pia kutengeneza ripoti feki ya kuwasafisha watuhumiwa itawezaje kusimamia na kutekeleza sheria hiyo mpya ya uchaguzi?

Ikumbukwe pia kuwa kwa kiasi kikubwa vyombo vyetu vya dola bado vina fikra ya zama za chama kimoja ambapo "madhambi" ya wana-CCM yanachukuliwa kama "ubinadamu" na hivyo vyombo hivyo kusuasua kuchukua hatua zinazostahili.Kwa baadhi ya taasisi za dola,hata kukemea maovu yanayotendwa na baadhi ya vigogo wa CCM ni kama na kuvunja sheria za nchi!

Kwa mwenendo huu,ni dhahiri basi sheria hiyo inaweza kutumika kuvibana vyama vya upinzani huku wana-CCM wakiendeleza libeneke la takrima kana kwamba imehalalishwa.Sheria hii imeletwa na serikali ya CCM ambayo rekodi yake katika mapambano dhid ya rushwa ina walakini mkubwa.Iweje chama kilichounda serikali kiendelee kuwa na mwenyekiti wa kamati yake ya maadili (Andrew Chenge) ambaye ana tuhuma katika suala la rada?

Pengine badala ya kupoteza muda kwa kuja na sheria mpya,ungefanyika mchakato wa kupitia sheria zilizopo na kuhakikisha zinasimamiwa na kutekelzwa ipasavyo.Vinginevyo,itakuwa ni hadithi ileile ya kuja na sheria mpya zenye kuleta matumaini mithili ya kauli-mbiu "mAisha Bora kwa Kila Mtanzania" huku matokeo yake yakibaki sifuri.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.