Showing posts with label MAISHA BORA. Show all posts
Showing posts with label MAISHA BORA. Show all posts

19 Jul 2010

Foleni za magari ni maisha bora-JK
Monday, 19 July 2010 05:33
*Asema watakakamatwa kwa rushwa CCM haitawatetea

Na Peter Mwenda

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Kikwete ametamba kuwa chama hicho kwa miaka mitano iliyopita kimeinua maisha ya Watanzania akitoa mfano wa Jiji la Dar es Salaam kuwa foleni za magari zinatokana na wananchi kuwa na maisha bora.

Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na CCM Mkoa wa Dar es Salaam kwa ajili ya kumpongeza Rais Kikwete kuchaguliwa kuwa mgombea pekee wa urais kwa asilimia 99.16, Dkt. Ali Mohammed Shein kuchaguliwa kuwa mgombea wa Urais Zanzibar na Dkt. Mohamed Gharib Bilal kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais.

"Hapa Dar es Salaam taabu ya msongamano wa magari inaonesha hali ya maisha ni bora, sasa tunahangaika jinsi ya kuondoa msongamano, kuanzia mwakani tutaanza kujenga barabara za juu," alisema Rais Kikwete.

CHANZO: Majira

Hivi kumbe maendeleo yanapimwa kwa msongamano na foleni za magari!Vipi kama foleni hizo ni matokeo ya mindombinu isiyoendana na mahitaji?Vipi kama wingi wa magari hayo ni matokeo ya ufisadi-aidha ya wizi na ubadhirifu wa mali ya umma na ukiukwaji wa taratibu mbalimbali eg ukwepaji kodi stahili bandarini na TRA?

Na je,foleni hizo za magari zinaendana vipi na idadi ya Watanzania wanaumudu mlo wao kila siku?Je wingi wa magari unaendana na idadi ya wamiliki wa magari?Nauliza hivyo kwa sababu wengi tunafahamu kuwa wakati kuna wachache wenye msururuwa magari na majumba ya kifahari kuna wengine wengi tu ambao hata fedha ya kununulia baiskeli hawana,achilia mbali uhakika wa nauli ya daladala.

Na je inawezekana Rais hajafahamishwa na wasaidizi wake kuhusu ongezeko la 'TZ ELEVEN' i.e. watembea kwa miguu ambao hawafanyi hivyo kama sehemu ya mazoezi ya viungo mbali ukosefu wa nauli?Au hawajamwambia kuhusu idadi ya 'mikweche' ambayo licha ya kusababisha foleni inachangia uwezekano wa ajali?Na inawezekana pia wasaidizi wake hawajamfahamisha kuwa mingi ya 'mikweche' hiyo iko barabarani baada ya wamiliki kutoa 'kitu kidogo' kwa askari wa usalama barabarani?

KAMWE MAJIBU RAHISI KWENYE MASWALI MAGUMU HAYAWEZI KULETA UFUMBUZI WA MATATIZO YETU!SINTOSHANGAA TUKISKIA HATA KUONGEZEKA KWA WENYE VITAMBI (INCLUDING WALE WENYE VITAMBI VYA KWASHAKOO) NAKO NI DALILI YA MAISHA BORA!

5 Mar 2010

 (Picha kwa hisani ya Mjengwa.)
MATUMIZI mabaya ya serikali na kuendelea kupanda kwa mfumuko wa bei za bidhaa kwa zaidi ya mara mbili katika kipindi cha kati ya mwaka 2005 na sasa ni chanzo cha maisha magumu ya wananchi, Tanzania Daima limebaini.
Katika wakati ambapo wananchi wapatao milioni nane wanalala au kushinda njaa kwa sababu ya ugumu wa maisha, serikali jana ilikiri kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Ramadhan Kijjah, imekuwa inatumbua shilingi mbili, wakati ina uwezo wa kukusanya shilingi moja

Akitoa tathmini ya serikali kuhusu hali ya uchumi kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, Kijjah alisema mapato ya serikali kwa mwaka ni sh trilioni tano, lakini matumizi ya serikali ni Sh trilioni 10.

Akijadili tathmini hiyo, mchumi na mwanasiasa, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema matumizi hayo makubwa ya serikali yanaathiri vibaya Watanzania wa kawaida, kwani yanachochea mfumuko wa bei unaosababisha gharama za maisha kuwa za juu.

Wakati Kijjah akikiri kwamba kimsingi, mapato ya serikali yamepanda kutoka Sh trilioni 2.167.6 mwaka 2005/06 hadi Sh trilioni 5.096 mwaka 2009/10, Profesa Lipumba alisema kama serikali ingekuwa makini, kulingana na ulaji mkubwa inaoonyesha, makusanyo ya sasa yangekuwa makubwa zaidi na yangekusanya kwa nidhamu.

Alisema serikali inawaachia watu fulani fulani (hakuwataja) na makampuni makubwa yasilipe kodi.

Kwa sababu hiyo, Profesa Lipumba alisema uchumi wa nchi unayumba na kufanya maisha ya Mtanzania yazidi kudorora.

“Hakuna ukusanyaji mzuri wa kodi; watu wanaachiwa, makampuni yanayochimba madini hayalipi kodi ya kutosha….hilo lina athari,” alisema Profesa Lipumba.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mwaka 2004/05 wakati utawala wa Rais Benjamin Mkapa ukielekea ukingoni matumizi ya serikali yalipanda kutoka Sh trilioni 2.1 hadi Sh. trilioni 2.7 mwaka 2005/06 wakati Rais Jakaya Kikwete anaingia madaraka.

Mbali ya hilo taarifa hiyo ya Kijjah ilionyesha kwamba mfumuko wa bei umepanda kwa zaidi ya mara mbili katika kipindi cha kati ya mwaka 2005 ulipokuwa ni asilimia 5 hadi kufikia asilimia 12.2 Desemba mwaka jana kabla ya kushuka kidogo na kuwa asilimia 10.9 Januari mwaka huu.

Hata hivyo Kijjah, alisema serikali imechukua hatua ili kukabiliana na matumizi hayo makubwa. Alisema imeongeza idadi ya wahasibu na wakaguzi wa ndani katika ngazi zote kuanzia wizara hadi serikali za mitaa.

“Kuanzishwa kwa kitengo cha ufuatiliaji wa matumizi ya umma (bajeti) katika miradi iliyoidhinishwa: Ofisi ya Mkaguzi Mkuu (CAG) imeongezewa nguvu za kisheria kuweza kufanya kazi zake bila kuingiliwa na taasisi yoyote.”

Katibu mkuu huyo ambaye alikuwa amefuatana na naibu wake, John Haule, aliongeza ili kupunguza matumizi makubwa ya serikali, yanahitajika marekebisho katika Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004 ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa watendaji wake.

“Sera ya mapato ya mwaka 2009/10 inalenga kukusanya mapato ya ndani yasiyopungua sh milioni 5,096,016 sawa na asilimia 16.4 ya pato la taifa,” alisema.

Kuhusu thamani ya fedha, Kijjah alisema, shilingi iliendelea kuporomoka kutoka wastani wa shilingi 1,195.75 kwa dola ya Kimarekani mwaka 2008 hadi kufikia shilingi 1,318.71 mwaka jana.

CHANZO: Tanzania Daima

14 Sept 2008



Rais Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kutambua kuwa njia pekee itakayowakwamua kiuchumi na kuwaletea maisha bora ni kujishughulisha na shughuli mbalimbali za maendeleo na si kukaa tu vijiweni na kulalamika. 
Kauli hiyo aliitoa jana wakati akijibu malalamiko ya wananchi wa kijiji cha Nyumba ya Mungu, kilichopo katika kata ya Lang`ata, tarafa Msitu wa Tembo, wilayani Simanjiro, ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara yake ya kikazi mkoani Manyara. 

Wananchi hao waliokuwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali, walimweleza Rais Kikwete kuwa bado wanashindwa kuishi maisha bora kama walivyokuwa wametarajia na badala yake wanakabiliwa na matatizo sugu ya kupata huduma bora ya afya na mitaji ya biashara na ukosefu wa ajira. 

Rais Kikwete alielezwa hayo na wananchi wa kijiji cha Lemkuna, muda mfupi kabla ya kuzindua bonde la umwagiliaji la kijiji hicho, ambapo pia walilalamikia bei kubwa ya pembejeo za kilimo na umbali wa upatikanaji wake, hasa mbolea. 

Akizungumza mara baada ya kuwasikiliza wananchi hao, Rais Kikwete, aliwaeleza kuwa wanapaswa kujiajiri wenyewe kupitia utaratibu wa kupata mikopo na kujiunga kwenye vikundi vya kuweka na kukopa (SACCOS) ili waweze kuanzisha miradi ya maendeleo. 

``Jamani msitarajie maisha bora kama yatadondoka kutoka juu, utaratibu uliopo ni wa mikopo tuliyoianzisha ili muweze kufanya shughuli za maendeleo, awamu ya kwanza imekwishapita wengine wamepata wengine hawajapata ila tutaendelea kuhakikisha kuwa mikopo zaidi inatatolewa ili wale ambao hawajapata waweze kupata`` alisema. SOURCE:ippmedia.com

Kauli hiyo inashabihiana na hii iliyotolewa na Waziri Mkuu wa zamani,Edward Lowassa

2007-05-10 15:55:28 
Na Radio One Habari

Waziri Mkuu, Mheshimiwa Edward Lowassa amesema maisha bora kwa kila Mtanzania hayawezi kuja kwa kukaa vijiweni na kunywa kahawa bali kwa kufanyakazi kwa bidii na hasa kuendeleza kilimo. 

Amefafanua kuwa maisha bora kwa kila Mtanzania yanayosemwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ni matokeo ya kazi na hayaji kwa kukaa vijiweni kutwa nzima kunywa Kahawa na kutaka wananchi wa Pwani wafanye kazi kwa bidii kujiletea maendeleo. 

Akihutubia mkutano wa hadhara kijijini Maneromango Wilayani Kisarawe Mkoani Pwani Waziri Mkuu amesema watu wa mkoa huo lazima wabadili pato la mwaka la kila mtu ili liwe kubwa kama katika mikoa mingine. 

Aidha ameagiza mashambapori yaliyopo Kisarawe na wilaya nyingine Mkoani Pwani yaorodheshwe, yapelekwe Wizara ya Ardhi ili hatimaye yafikishwe kwa Rais yatwaliwe na kuwagawia vijana wafanye kazi za kilimo. 
Waziri Mkuu anakamilisha ziara yake ya siku sita ya Mkoa wa Pwani leo kwa kutembelea Wilaya ya Bagamoyo. 
SOURCE: Radio One


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.