10 Mar 2010

TAkukuru
Katika toleo jana la gazeti la Mwananchi kuna habari kwamba Mbunge wa Nyang’hwale,James Musalika, alilazimika ‘kuingia mitini’ kuwakwepa makachero wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) waliokwenda katika ‘hafla’ kati ya mbunge huyo na wapiga kura.Kwa mujibu wa Mwananchi,hatua hiyo ya wanadola wa TAKUKURU ni katika utekelezaji wa ‘ruhusa’ waliyopewa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete ‘kudhibiti wanasiasa wanaotoa rushwa kwenye chaguzi’.
Wakati gazeti la Mwananchi limeishia kuripoti tu tukio hilo pasipo kwenda mbali zaidi ya kungalia ‘upande wa pili wa tukio hilo’ blogu hii inatafsiri tukio hilo kama dalili za waziwazi za dhihaka inayoikumba Sheria mpya ya Uchaguzi kabla hata haijashika kasi.
Kwa upande mmoja,tukio hili linaendelea kuthibitisha kuwa TAKUKURU ni taasisi hafifu na isiyojua wajibu wake katika kulitumikia Taifa kwa ufanisi.Uzito mkubwa katika habari hii ni kushindwa kwa taasisi hiyo kufanikisha rungu walilopewa na Rais kuwadhibiti wanasiasa wanaonunua uongozi kwa rushwa.Kwanza TAKUKURU haikuhitaji kusubiri maelekezo kutoka kwa Rais ili waanze kuwashughulikia wala rushwa kwa vile hilo ndilo jukumu na madhumuni ya kuwapo kwa taasisi hiyo dhaifu.
Rais nae hawezi kukwepa lawama kwa vile badala ya kuendelea kuwafundisha TAKUKURU namna ya kutimiza wajibu wao,alipaswa kuwawajibisha kwa kushindwa kutekeleza majukumu waliyokabidhiwa.Kwanini kila jambo lisubiri maagizo ya Rais ilhali ana baraza kubwa la mawaziri linalopaswa kumsaidia katika uongozi wa Taifa letu?
Kwa wenye ufahamu wa tasnia ya ukusanyaji taarifa za siri na namna ya kuzitumia ipasavyo (na hicho ni kipaumbele katika utendaji kazi wa kila siku wa TAKUKURU) ni dhahiri kwamba taasisi hiyo ilishindwa kupata taarifa sahihi katika wakati mwafaka.Wanadola hao walipaswa kufahamu shughuli inbgefanyikia wapi kisha kupenyeza maafisa wao katika kundi la wahudhuriaji kama sio kuvamia wakati wahusika wakiwa katikati ya shughuli husika.Kwa kifupi,TAKUKURU hawako proactive bali wanazembea hadi ishu inatokea kisha,pasipo aibuwanaujulisha umma kuwa walifanya hili na lile lakini haikuwa vile.Kwa lugha nyingine, wanatusomea rambirambi baada ya kufeli kwao.
Kwa upande mwingine pia, tukio hilo ni kielelezo cha dhihaka inayotawala Sheria hii mpya ya kupambana na rushwa katika siasa.Kama nilivyowahi kuandika huko nyuma,tatizo sio sheria au haja ya kuwa na sheria mpya, bali usimamizi na utekelezaji wa sheria zilizopo.Tunaweza kuja na sheria milioni dhidi ya rushwa lakini tusifanikiwe hata kidogo hasa tukizingatia udhaifu na ubabaishaji wa taasisi kama TAKUKURU.
Musalika amefanikiwa kutuonyesha namna gani sheria hii ianvyoweza kukwepeka. Na ujumbe mkubwa zaidi kwa Rais Kikwete na TAKUKURU ni kwamba sheria hii inakwepeka kirahisi kwa kutumia mgongo wa ‘shughuli za chama’. Kadhalika, tukio hili linapaswa kuwafumbua macho Watanzania kuwa ni vigumu sana kutenganisha rushwa na utawala wa CCM. Uhusiano wa rushwa na CCM ni kama ule wa mbu na malaria au ukimwi na HIV.Sasa inapotokea Mwenyekiti wa chama kinacholea rushwa anapojaribu kupambana na na sehemu muhimu wa uhai na ustawi wa chama hicho, ni dhahiri kuwa mafanikio yatabaki kuwa hadithi zaidi kuliko ufanisi.
Hivi kama Rais yuko serious na rushwa kwenye siasa, hawatolei macho hao ‘wanaovikwa ukamanda wa vijana’ ambapo yayumkinika kusema kuwa ‘ukamanda huo’ umegeuka kama nafasi ya wagombea watarajiwa kujinadi kwa wapiga kura? Hii ni rushwa ambayo hata kama TAKUKURU isingekuwa dhaifu ingepata wakati mgumu sana kupambana nayo kwa vile ni sehemu ya taratibu za kichama.
Na Musalika ameweka bayana kuwa yeye kama Mbunge hayuko tayari “kuombwa msaada wa saruji nikakataa eti kwa sababu ya sheria...” bali atatoa “maana huko ni kutekeleza ilani ya chama”.
Kwa lugha nyingine, “kutoa rushwa ni kutekeleza ilani ya CCM”.He couldn’t put it more precisely,I suppose!
Kaazi kweli kweli!

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.