Usiniite mnafiki,au mpindisha maneno.Uthibitisho kuwa hata Rais Jakaya Kikwete hana imani na TAKUKURU upo katika habari ifuatayo (ANGALIA MAANDISHI MEKUNDU)
Rungu la Kikwete lilimwokoa Siyoi |
Monday, 05 March 2012 09:17 |
NAPE, WASSIRA WADAIWA KUSIMAMA KIDETE ATOSWE, JK AKATUMIA 'RUNGU' KUZIMA HOJA,WABUNGE WOTE CHADEMA KUHAMIA ARUMERU Joseph Zablon, Dar na Moses Mashalla, Arusha USHINDI wa Siyoi Sumari kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, unadaiwa kuitesa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, baada ya baadhi ya wajumbe kukuna vichwa kuhusu mbinu na mikakati ya kutengua ushindi alioupata katika duru ya pili dhidi ya William Sarakikya. Katika Mkutano Mkuu wa jimbo hilo uliofanyika, Februari 20 ulimchagua Siyoi ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, marehemu Jeremiah Sumari kwa kura 361, akifuatiwa na Sarakikya aliyepata kura 259. Hata hivyo, CC ya CCM iliyoketi Februari 27, iliagiza kurejewa kwa upigaji kura kati ya wagombea hao. Katika duru hilo la pili la uchaguzi uliofanyika Machi Mosi mwaka huu, Siyoi alipata ushindi wa kishindo wa kura 761 na kumtupa mbali mpinzani wake, Sarakikya aliyepata kura 361. Juzi katika kikao hicho cha CC, ushindi huo wa mara ya pili wa Siyoi uliipasua tena kamati hiyo kuu yenye mamlaka ya juu ya uamuzi ndani ya chama hicho, baada ya baadhi ya wajumbe kudaiwa kutaka atoswe na apitishwe Sarakikya kutokana na tuhuma za matumizi makubwa ya fedha wakati wa kampeni. Vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka katika kikao hicho cha CC, vilifafanua kwamba waliosimama kidete kutaka Siyoi atoswe ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira. Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Nape alipinga Siyoi kurejeshwa akizingatia matukio mbalimbali ya tuhuma za matumizi makubwa ya fedha yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya watu ili wamchague mgombea huyo, kitu ambacho hakikupaswa kuvumiliwa. Hoja hiyo ya Nape iliungwa mkono na Wassira ambaye naye alitaka Siyoi atoswe kutokana na tuhuma hizo za matumizi makubwa ya fedha kutoka kwa baadhi ya wapambe wake waliotaka mgombea huyo achaguliwe. Lakini inadaiwa kuwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alisema kikao hicho kisingeweza kumkata Sumari kwa sababu tu ya tuhuma hizo za rushwa zilitolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mkoani humo. Chanzo kingine kilimnukuu mwenyekiti huyo akisema kwamba, Arusha ni mkoa wenye siasa za aina yake hivyo ni muhimu kuwa makini kwani siku za nyuma kuliwahi kuibuka tuhuma za rushwa kwa wabunge wa CCM kukamatwa lakini, mahakama ikawaachia huru. Chanzo hicho kiliongeza kwamba, Rais Kikwete alisisitiza kuwa hata tuhuma za rushwa zilizotolewa zilikuwa zikigusa wengine kwani iliwahi kupendekezwa kwamba Elishalia Kaaya ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), ndiye apitishwe na wengine wang'olewe. Katika kikao hicho, Rais Kikwete pia alinukuliwa akihoji kuwa endapo Siyoi angekatwa jina kungekuwa na uhakika wa chama kushinda kwa kumsimamisha Sarakikya? Hakupata jibu kama mgombea huyo wa pili angeweza kushinda kiti hicho. Hata hivyo, chanzo hicho kilisema baada ya mwenyekiti kutumia rungu kumpitisha Siyoi alimpa angalizo: “Basi na wewe usiende kutamba huko mitaani kwamba umeangusha watu, fanya kampeni, ushinde jimbo tuangalie mambo mengine mbele.” Ilielezwa zaidi kwamba Rais Kikwete aliungwa mkono na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, aliyeeleza kuwa haoni sababu ya kumwondoa Siyoi katika kinyang'anyiro hicho kwani ushindi wake ulikuwa mkubwa. |
Chanzo na Kwa habari Kamili: Mwananchi