29 Apr 2010

JIJI la Tanga limfeunikwa na simamzi kuu kufatia wanafunzi 18 wa Chuo cha Kiislamu cha Shamsil-Maariff kufa papo hapo na wengine 125 kujeruhiwa vibaya, baada ya lori walilokuwa wakisafiria kutoka kwenye sherehe za maulidi kupinduka.

. Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Adolphina Kapufi aliliambia gazeti hli jana kuwa ajali hiyo ilitokea saa 5:30 usiku wa kuamkia jana katika eneo la njiapanda kuu ya Mabanda ya Papa jijini hapa.

Kapufi aliwataja baadhi ya waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Twalib Kunemu, Juma Idd, Faraji Habib, Jahshi Rashid, Hussein Bakari, Hajji Athumani naYussuph Hussein na kwamba, kazi ya kuwatambua maiti wengine bado inaendelea.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Paschal Kanyinyi alisema kazi ya kuwatambua waliokufa na majeruhi waliolazwa katika hospitali hiyo wodi ya Galanosi inaendelea.

Kanyinyi aliwataja majeruhi waliotambuliwa kuwa ni Jumaa Salim ambaye ameumia mbavu, Makame Ahmed, Ahmed Shehe, Selemani Said na Juma Akida.

Aliwataja majeruhi ambao hali zao ni mbaya, hivyo waliokimbizwa katika Hospitali Taifa ya Muhimbili, jijini Dar essalaam kuwa ni Hemed Shaaban na Hassan Adam.

Kanyinyi alifahamisha kuwa kati majeruhi 125 walifikishwa katika hospitali hiyo usiku wa kuamkia jana baada ya kupata ajali, 70 walipata matibabu na kuruhusiwa kurejea chuoni kwao.

Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu huyo, majeruhi 55 wanaendelea kupata matibabu katika hospitali hiyo kwa msaada wa timu maalumu ya waganga na wauguzi waliokusanywa kutoka hospitali na vituo mbalimbali vya afya mkoani Tanga kwa ajili ya kutoa huduma hiyo.

Mwananchi ilifika katika Hospitali hiyo ya Bombo na kukuta idadi kubwa ya wananchi waliokusanyika katika hospitali hiyo kwa lengo la kutambua miili ya waliokufa na majeruhi.

Mwalimu wa zamu wa Chuo hicho, Ustaadh Ajali Ramadhan, alisema kuwa wanafunzi hao walikuwa wakitokea Kijiji cha Kibafuta ambako walikwenda
kuhudhuria sherehe za kuzaliwa kwa Mtume Mohamad S.A.W.

Hata hivyo, Ustaadhi Ramadhan alisema anashangaa kuona idadi kubwa ya wanafunzi waliopata ajali, kwani aliowaruhusu kutoka chuoni hapo walikuwa 60 tu.

“Nashangaa sijui ni nini kimetokea, kwani niliowaruhusu kuondoka na gari
hilo ni wanachuo 60 tu, lakini idadi ya waliopata ajali imekuwa kubwa. Sijui walipandia wapi…,” alisema mwalimu huyo wa zamu.

Kanyinyi alimshukuru Mkurugenzi wa Kampuni ya Raha Leo, Seleman Abdallah kwa kutoa dawa kwa ajili ya kuwatibu majeruhi wa ajali hiyo.

“Tunashukuru Mkurugenzi wa Raha leo, ametusaidia sana kwa kutoa dawa za
kuwatibu majeruhi na pia vifaa kwa ajili ya kusaidia kuhifadhia miili ya waliokufa,” alisema Kanyinyi.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Meja Jenerali Mstaafu Said Kalembo alifika hospitalini hapo saa 5 .30 asubuhi na kuwapa pole ndugu wa wanafunzi waliokufa katika ajali hiyo.

Akiwa, akiwa katika wodi ya Galanosi Mkuu wa Mkoa huyo alimuagiza Kaimu Mganga Mkuu kuwaita waganga na wauguzi kutoka vituo vyote vya afya vya jijini hapa ili kuongeza nguvu, kwa vile waliopo katika Hospitali ya Bombo walikuwa wmezidiwa na kazi ya kuwahudumia majeruhi.

Katibu wa Bakwata wa Mkoa wa Tanga, Mohamed Riami alisema huo ni msiba
mkubwa uliwakumba Waislamu na Watanzania kwa ujumla, hivyo akaomba msaada wa hali na mali kuokoa maisha ya majeruhi waliopata ajali hiyo.

Ajali hii ni muendelezo wa ajali mbaya za barabarani zinazoendelea kutokea na kuua watu sehemu mbalimbali nchini hivi sasa.

Moja ya ajali hizo mbaya ni iliyotokea jijini Dar es Salaam mwezi uliopita na kuua watu zaidi ya 10 papo hapo baada ya lori la mafuta ya taa kuigonga na kulalia daladala maneo ya Kibamba katika Barabara ya Morogoro.

Katika ajali hiyo iliyotokea alfajiri, daladala ilisagawa na kuwa kama chapati; na miongoni mwa waliokufa ni mama mjazito aliyekuwa anakwenda kujifungua hospitalini akiwa pamoja na mumewe.

CHANZO: Mwananchi
.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.