13 May 2010

Ndoa ya Mkeka.Haya ni mambo ya pwani zaidi kuliko 'bara'.Kule kwetu Ifakara hakuna vitu kama hivyo,lakini maeneo kama Tanga,Dar,Bagamoyo,nk ndoa za mkeka 'zinakula sahani moja' kwa umaarufu kama ndoa 'za kawaida'.Actually,ilikuwa almanusra 'nipigwe ndoa ya mkeka' wakati nilipoishi Tanga kwa takriban miaka 15 ilopita.Unajua tena mambo ya ujana...ukiyaangalia wakati huu wa utu uzima inabaki kichekesho.Anyway,kwa kifupi ndoa ya mkeka ni mithili ya fumanizi kati ya wanaovunja amri ya sita pasipo minajili ya kuwa wanandoa,na 'katika kuwapa one-stop fundisho na ufumbuzi' wanafungishwa ndoa ya chap-chap.It's like "si mnapenda kuvunja amri ya sita kisirisiri?Okay,sasa tunawahalalishia mtende manyotenda for the rest of your lives"...lol!Tatizo ni kwamba ni nadra kwa ndoa za mkeka kudumu kwa vile huwa ni'za kulazimisha'.Yani hazina tofauti na stori kama binti 'anayejiachia' na kupata ujauzito ili aolewe na mpenziwe.It rarely works!


Well,makala hii inazungumzia 'ndoa ya mkeka ya kisiasa' kati ya chama cha wahafidhina (Conservatives) na kile cha Waliberali (Liberal Democrats) ambao kwa pamoja wameunda serikali ya mseto hapa Uingereza. 

Uamuzi wa kiongozi wa Conservatives kuunda serikali ya mseto na Liberal Democrats umepokelewa kwa hisia tofauti huku watu wengi wakitabiri kuwa mseto huo hauna maisha marefu.Kikubwa kinachopelekea utabiri huo ni itikadi za vyama husika sambamba na tofauti zao katika sera zao.Japo tumeambiwa kuwa moja ya sababu zilizopelekea kufanikiwa kwa mseto huo ni kwa kila chama "kukubali matokeo" kwa aidha kuelegeza au kuachana kabisa na baadhi ya misimamo yao,hiyo haimaanishi kuwa misimamo hiyo imepotea 'vichwani' mwa wafuasi wa vyama hivyo.

Wakati wahafidhina wanafahamika kwa mrengo wao wa kulia na kati-kulia (right wing or centre-right politics) waliberali ni maarufu zaidi kwa mrengo wa kushoto na kidogo kati-kushoto (left wing or centre-left politics).Pengine hili sio rahisi sana kueleweka kama tukichukulia siasa zetu huko nyumbani kama mfano,kwani nadhani tunaweza kukubaliana kwamba nafasi ya mrengo katika siasa zetu huko Afrika ni ndogo sana.Yayumkinika kabisa kusema kuwa fedha za kukiwezesha chama au mgombea kununua kura ni muhimu zaidi kwenye siasa zetu kuliko mrengo wa chama au mgombea husika.Na hili ni tatizo kwa vile chama (au mgombea) kisicho na mrengo (au msimamo) ni sawa na bendera inayoweza kuelekea upande wowote ule kulingana na mvumo wa upepo.

Wenye hofu kuhusu 'ndoa ya mkeka' kati ya wahafidhina na waliberali wana sababu za msingi kwa vile mseto kati ya siasa za mrengo wa kulia na zile za mrengo wa kushoto hauko mbali sana na jitihada za kuchanganya maji na mafuta.Wakati chama cha Conservatives kinafahamika zaidi kwa siasa zake za kuwakumbatia matajiri huku zikiwakalia kooni 'walalahoi' kwa kudi kubwa (tayari kuna taarifa za 'kiama' cha kodi) waliberali wanafahamika zaidi kwa siasa za kuwa karibu na jamii huku vitu kama haki za binadamu,uvumulivu na ushirikiano vikiwa na umuhimu mkubwa.

Wakati Liberal Democrats walikuwa na sera ya msamaha (amnesty) kwa wahamiaji 'haramu' (illegal immigrants) huku wakisisitiza kuwa hatua kali dhidi ya wahamiaji hao si ufumbuzi kwa vile 'zinazidi kuwaficha msituni',chama cha Conservative kiliweka bayana msimamo wake wa kupunguza idadi ya wahamiaji kwa kuweka ukomo (cap) katika idadi ya wanaoingia/kuhamia Uingereza,sambamba na sheria kali za uhamiaji.Na katika hatua inayoweza kuwagharimu Liberal Democrats,chama hicho kimekubali kuachana na sera yake ya msamaha kwa 'wahamiaji haramu' na badala yake kimeafiki hatua ya Conservatives kuweka ukomo kwenye idadi ya wahamiaji wanaoingia nchini hapa.

Kuna tofauti ya kimtizamo kuhusu umoja na ushirikiano wa Ulaya.Wahafidhina wanasifika kwa upinzani wao dhidi ya suala hilo huku waliberali wakipendelea kuona ushirikiano huo ukisambaa zaidi ikiwa ni pamoja na wazo la Uingereza kutumia sarafu ya Euro badala ya Pound Sterling.Katika kufanikisha 'ndoa' yao,Liberal Democrats wamekubali kusitisha mipango yao kuhusu kukuza ushiriakiano wa Ulaya,jambo linaloweza kuwaudhi waumini wa siasa za chama hicho.

Lakini tayari kuna dalili za mpasuko kwenye 'ndoa hiyo ya mkeka' baada ya taarifa kwenye baadhi ya magazeti ya hapa kwamba 'Waziri' mpya wa fedha ((Kansela) George Osborne (wa Conservatives) amepinga vikali wazo kwamba 'Waziri' wa biashara (Business Secretary) Vince Cable (wa chama cha Liberal Democrats) ndiye atakayekuwa na dhamana ya kufanya mabadiiko kwenye mfumo wa mabenki (kwa minajili ya kudhibiti na kuzuwia uwezekano wa mtikisiko wa kifedha/kiuchumi kutokana na 'uzembe' wa mabenki katika utekelezaji wa sheria za fedha).Badala yake,hazina chini ya Osborne ndio itakayoshikilia dhamana ya utekelezaji wa sera ya mabenki na sekta ya fedha kwa ujumla.


Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kuna hofu kuwa chama cha Liberal Democrats kitakimbiwa na idadi kubwa tu ya wafuasi wake kufuatia uamuzi wake wa kushirikiana na Conservatives.Hali hiyo sio tofauti sana kwa upande wa wahafidhina kwani kuna idadi kubwa tu miongoni mwao wanaoona 'ndoa hiyo ya mkeka' kuwa jambo lisilofaa.Pengine tatizo kubwa kwa vyama vyote viwili ni wale walio 'mwisho wa upande' wa mrengo wa vyama hivyo,yaani wenye mrengo wa kulia kabisa kwa upande wa Conservatives na wa mrengo wa kushoto kabisa kwa upande wa waliberali.Hawa ni watu wanaoongozwa na imani na itikadi,na haiwaingii akilini kuona mambo hayo ya msingi yakiwekwa rehani kwa minajili tu ya kuunda serikali.

Lakini kuna wanaoona kuwa 'ndoa hii ya mkeka' kati ya David Cameron na Nick Clegg inaweza kudumu kwa vile kimsingi viongozi hao wawili wana mambo kadhaa yanayoshabihiana.Wote walisoma shule 'za bei mbaya',wanatoka familia zenye uwezo mkubwa kifedha na,kimsingi, wanaishi katika tabaka tawala.Kwa minajili hii,baadhi ya wachambuzi wanatabiri kuwa mfanano wa haiba za Cameron na Clegg,na sio tofauti katika itikadi zao,utafanikisha kudumu kwa serikali hiyo ya 'ajabu' kati chama chenye siasa za mrengo wa kulia (conservatives) na kile cha mrengo wa kushoto (Liberal Democrats).

Pamoja na yote hayo,siasa ni mchezo usiotabirika.Siku chache zilizopita ingekuwa jambo lisilofikirika kwa wahafidhana na waliberali kushirikiana katika uongozi wa serikali,lakini leo hii 'habari ndio hiyo'.Basi kwa minajili hiyohiyo,haitokuwa ajabu kwa 'ndoa hii ya mkeka' kudumu muda mrefu kuliko inavyotarajiwa.

Muda utatanabaisha (time will tell).

1 comment:

  1. Hiyo makala kaka ingekuwa huyo tunayempigia kura halafu anawaita wanaosemekana wazee na kututukana sisi tunaompigia kura na wengi wakifikiria wazandiki, wanafiki....nk ni wale viongozi wa chama wafanyakazi...na ndiyo hao raia wa Tanzania na pia wenyekuendesha hao wasioajiriwa katika familia zao. Basi kingetokea ni kwamba ungetafutwa hata kufungiwa kwa kuandika haya maoni binafsi yakinifu

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.