Showing posts with label BRITISH ELECTION 2010. Show all posts
Showing posts with label BRITISH ELECTION 2010. Show all posts

13 May 2010

Ndoa ya Mkeka.Haya ni mambo ya pwani zaidi kuliko 'bara'.Kule kwetu Ifakara hakuna vitu kama hivyo,lakini maeneo kama Tanga,Dar,Bagamoyo,nk ndoa za mkeka 'zinakula sahani moja' kwa umaarufu kama ndoa 'za kawaida'.Actually,ilikuwa almanusra 'nipigwe ndoa ya mkeka' wakati nilipoishi Tanga kwa takriban miaka 15 ilopita.Unajua tena mambo ya ujana...ukiyaangalia wakati huu wa utu uzima inabaki kichekesho.Anyway,kwa kifupi ndoa ya mkeka ni mithili ya fumanizi kati ya wanaovunja amri ya sita pasipo minajili ya kuwa wanandoa,na 'katika kuwapa one-stop fundisho na ufumbuzi' wanafungishwa ndoa ya chap-chap.It's like "si mnapenda kuvunja amri ya sita kisirisiri?Okay,sasa tunawahalalishia mtende manyotenda for the rest of your lives"...lol!Tatizo ni kwamba ni nadra kwa ndoa za mkeka kudumu kwa vile huwa ni'za kulazimisha'.Yani hazina tofauti na stori kama binti 'anayejiachia' na kupata ujauzito ili aolewe na mpenziwe.It rarely works!


Well,makala hii inazungumzia 'ndoa ya mkeka ya kisiasa' kati ya chama cha wahafidhina (Conservatives) na kile cha Waliberali (Liberal Democrats) ambao kwa pamoja wameunda serikali ya mseto hapa Uingereza. 

Uamuzi wa kiongozi wa Conservatives kuunda serikali ya mseto na Liberal Democrats umepokelewa kwa hisia tofauti huku watu wengi wakitabiri kuwa mseto huo hauna maisha marefu.Kikubwa kinachopelekea utabiri huo ni itikadi za vyama husika sambamba na tofauti zao katika sera zao.Japo tumeambiwa kuwa moja ya sababu zilizopelekea kufanikiwa kwa mseto huo ni kwa kila chama "kukubali matokeo" kwa aidha kuelegeza au kuachana kabisa na baadhi ya misimamo yao,hiyo haimaanishi kuwa misimamo hiyo imepotea 'vichwani' mwa wafuasi wa vyama hivyo.

Wakati wahafidhina wanafahamika kwa mrengo wao wa kulia na kati-kulia (right wing or centre-right politics) waliberali ni maarufu zaidi kwa mrengo wa kushoto na kidogo kati-kushoto (left wing or centre-left politics).Pengine hili sio rahisi sana kueleweka kama tukichukulia siasa zetu huko nyumbani kama mfano,kwani nadhani tunaweza kukubaliana kwamba nafasi ya mrengo katika siasa zetu huko Afrika ni ndogo sana.Yayumkinika kabisa kusema kuwa fedha za kukiwezesha chama au mgombea kununua kura ni muhimu zaidi kwenye siasa zetu kuliko mrengo wa chama au mgombea husika.Na hili ni tatizo kwa vile chama (au mgombea) kisicho na mrengo (au msimamo) ni sawa na bendera inayoweza kuelekea upande wowote ule kulingana na mvumo wa upepo.

Wenye hofu kuhusu 'ndoa ya mkeka' kati ya wahafidhina na waliberali wana sababu za msingi kwa vile mseto kati ya siasa za mrengo wa kulia na zile za mrengo wa kushoto hauko mbali sana na jitihada za kuchanganya maji na mafuta.Wakati chama cha Conservatives kinafahamika zaidi kwa siasa zake za kuwakumbatia matajiri huku zikiwakalia kooni 'walalahoi' kwa kudi kubwa (tayari kuna taarifa za 'kiama' cha kodi) waliberali wanafahamika zaidi kwa siasa za kuwa karibu na jamii huku vitu kama haki za binadamu,uvumulivu na ushirikiano vikiwa na umuhimu mkubwa.

Wakati Liberal Democrats walikuwa na sera ya msamaha (amnesty) kwa wahamiaji 'haramu' (illegal immigrants) huku wakisisitiza kuwa hatua kali dhidi ya wahamiaji hao si ufumbuzi kwa vile 'zinazidi kuwaficha msituni',chama cha Conservative kiliweka bayana msimamo wake wa kupunguza idadi ya wahamiaji kwa kuweka ukomo (cap) katika idadi ya wanaoingia/kuhamia Uingereza,sambamba na sheria kali za uhamiaji.Na katika hatua inayoweza kuwagharimu Liberal Democrats,chama hicho kimekubali kuachana na sera yake ya msamaha kwa 'wahamiaji haramu' na badala yake kimeafiki hatua ya Conservatives kuweka ukomo kwenye idadi ya wahamiaji wanaoingia nchini hapa.

Kuna tofauti ya kimtizamo kuhusu umoja na ushirikiano wa Ulaya.Wahafidhina wanasifika kwa upinzani wao dhidi ya suala hilo huku waliberali wakipendelea kuona ushirikiano huo ukisambaa zaidi ikiwa ni pamoja na wazo la Uingereza kutumia sarafu ya Euro badala ya Pound Sterling.Katika kufanikisha 'ndoa' yao,Liberal Democrats wamekubali kusitisha mipango yao kuhusu kukuza ushiriakiano wa Ulaya,jambo linaloweza kuwaudhi waumini wa siasa za chama hicho.

Lakini tayari kuna dalili za mpasuko kwenye 'ndoa hiyo ya mkeka' baada ya taarifa kwenye baadhi ya magazeti ya hapa kwamba 'Waziri' mpya wa fedha ((Kansela) George Osborne (wa Conservatives) amepinga vikali wazo kwamba 'Waziri' wa biashara (Business Secretary) Vince Cable (wa chama cha Liberal Democrats) ndiye atakayekuwa na dhamana ya kufanya mabadiiko kwenye mfumo wa mabenki (kwa minajili ya kudhibiti na kuzuwia uwezekano wa mtikisiko wa kifedha/kiuchumi kutokana na 'uzembe' wa mabenki katika utekelezaji wa sheria za fedha).Badala yake,hazina chini ya Osborne ndio itakayoshikilia dhamana ya utekelezaji wa sera ya mabenki na sekta ya fedha kwa ujumla.


Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kuna hofu kuwa chama cha Liberal Democrats kitakimbiwa na idadi kubwa tu ya wafuasi wake kufuatia uamuzi wake wa kushirikiana na Conservatives.Hali hiyo sio tofauti sana kwa upande wa wahafidhina kwani kuna idadi kubwa tu miongoni mwao wanaoona 'ndoa hiyo ya mkeka' kuwa jambo lisilofaa.Pengine tatizo kubwa kwa vyama vyote viwili ni wale walio 'mwisho wa upande' wa mrengo wa vyama hivyo,yaani wenye mrengo wa kulia kabisa kwa upande wa Conservatives na wa mrengo wa kushoto kabisa kwa upande wa waliberali.Hawa ni watu wanaoongozwa na imani na itikadi,na haiwaingii akilini kuona mambo hayo ya msingi yakiwekwa rehani kwa minajili tu ya kuunda serikali.

Lakini kuna wanaoona kuwa 'ndoa hii ya mkeka' kati ya David Cameron na Nick Clegg inaweza kudumu kwa vile kimsingi viongozi hao wawili wana mambo kadhaa yanayoshabihiana.Wote walisoma shule 'za bei mbaya',wanatoka familia zenye uwezo mkubwa kifedha na,kimsingi, wanaishi katika tabaka tawala.Kwa minajili hii,baadhi ya wachambuzi wanatabiri kuwa mfanano wa haiba za Cameron na Clegg,na sio tofauti katika itikadi zao,utafanikisha kudumu kwa serikali hiyo ya 'ajabu' kati chama chenye siasa za mrengo wa kulia (conservatives) na kile cha mrengo wa kushoto (Liberal Democrats).

Pamoja na yote hayo,siasa ni mchezo usiotabirika.Siku chache zilizopita ingekuwa jambo lisilofikirika kwa wahafidhana na waliberali kushirikiana katika uongozi wa serikali,lakini leo hii 'habari ndio hiyo'.Basi kwa minajili hiyohiyo,haitokuwa ajabu kwa 'ndoa hii ya mkeka' kudumu muda mrefu kuliko inavyotarajiwa.

Muda utatanabaisha (time will tell).

10 May 2010

Jambo moja nililojifunza kutoka kwa hawa wenzetu wa nchi zilizoendelea ni kile kinachoelezeka vizuri kwa kimombo kama not settling for less.Yaani,kwa tafsiri isiyo rasmi,ni kutokubali kuridhishwa na pungufu ya matarajio kamili.Kama ni mwanasiasa na wananachi wanaona 'unawazingua' basi usitarajie kuwa wataendelea 'kukulea'.Kama ni kwenye soka,wenye timu hawatarajii pungufu ya ushindi.

Baada ya matokeo yasiyoridhisha kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Alhamisi iliyopita,tayari 'bundi' mbaya ameshaanza kukiandama chama cha Labour.Baadhi ya wanasiasa ndani ya chama hicho wamejitokeza hadharani kutaka Gordon Brown atoswe kwa madai kuwa yeye ndio hasa chanzo cha matokeo mabaya kwenye uchaguzi huo ambapo Labour iliambulia nafasi ya pili nyuma ya chama cha wahafidhina (Conservative Party).

Japo hadi sasa Brown hajatamka kama ataachia ngazi uongozi wa chama hicho lakini dalili ni kwamba presha ikiendelea kuongezeka hatokuwa na jinsi zaidi ya kujiuzulu.Hapa sizungumzii u-waziri mkuu bali hali ya mambo ndani ya chama cha Labour.

Kukurejesha nyuma kidogo,Labour imekuwa na makundi mawili 'yasiyoiva' kwa kitambo kirefu sasa.Kwa upande mmoja ni wale wanaofahamika kama Blairites,ambao wanamhusudu Waziri Mkuu wa zamani Tony Blair,na kwa upande mwingine ni Brownites,ambao wanamhusudu Gordon Brown.Inasemekana kuwepo kwa makundi hayo kumechangia kwa kiasi flani matokeo mabaya ya chama hicho katika uchaguzi uliopita.Inadaiwa kwamba mmoja ya watu wenye nguvu kubwa ndani ya Labour,Lord Mandelson,alitumia kampeni za Brown na Labour kumuimarisha David Miliband,'Waziri' wa Mambo ya Nje wa Uingereza na chaguo la Blairites kumrithi Brown.Inaelezwa kwamba wakati Labour wanazindua kampeni zao kwa ajili ya uchaguzi huo,Mandelson (maarufu kama Malaika wa Giza-Angel of Darkness-ndani ya Labour)alifanikisha safari ya Miliband kwenda Marekani kwa mazungumzo na Rais Obama,fursa ambayo wachambuzi wa siasa wanaamini ingemwezesha Brown kuonekana kama kiongozi mwenye nguvu katika siasa za kimataifa.

Inadaiwa pia kuwa kampeni ya Brown iligeuzwa na Mandelson kuwa 'makao makuu ya Miliband' kwa maana kuwa ilikuwa ikitumika kwa namna flani kumpromoti mwanasiasa huyo (Miliband) ambaye bado ana ukaribu mkubwa na Blair.Hata meya wa zamani wa jiji la London,Ken Livingstone ameligusia hilo katika makala yake aliyoandika kwenye gazeti moja la Daily Mail.

Kwa sasa,harakati zinazoendelea chini chini ndani ya Labour ni za kumrithi Brown.Yani imekuwa kama ndugu za mgonjwa wanapoanza kugombania urithi kabla mgonjwa huyo hajaaaga dunia.Alosema siasa ni mchezo mchafu hakukosea.Baadhi ya majina yanayohusishwa na mpambano huo ni pamoja na akina Miliband,yaani David na mdogo wake Ed,ambaye ni waziri wa mazingira,Ed Ball- 'waziri' wa elimu na 'waziri' wa mambo ya ndani Alan Johnson.

Na akina Miliband  wanazua mvutano ambao unavuka anga za siasa kwa vile wakati David (pichani kushoto) ni Blairite,mdogo wake (kulia) ni Brownite.Inaelezwa kuwa tayari Ed ameshamfahamisha mama yao kuwa anadhamiria kupambana na kaka yake kwenye kinyang'anyiro cha kuiongoza Labour.Hata hivyo,inaelezwa pia kuwa bado yuko njia panda kwa vile kwa upande mmoja Brownites wenzie wanamwona kama chaguo mwafaka kwa nafasi hiyo,lakini kwa upande mwingine 'damu ni nzito kuliko maji' na anatafakari kama pengine itakuwa jambo la busara kumsapoti kaka yake.

Tukiachana na mvutano huo wa kifamilia,'vita' kubwa inatarajiwa kuwa kati ya kaka yake (David) na (Ed) Balls.Wakati David anasifika kwa upeo na akili ya hali ya juu (ni Mwingireza mwenye asili ya Kiyahudi huyu) na ufahamu wake wa siasa za kimataifa hasa kutokana na wadhifa alionao sasa,Balls ana sapoti kubwa kwenye vyama vya wafanyakazi ambavyo kimsingi vina nguvu ya kutosha kwenye chama cha Labour.Kadhalika,wakati David anaonekana kama mtu wa 'tabaka la juu' Balls yuko karibu zaidi na wana-Labour wa ngazi za chini.

Tukiweka kando kidogo matatizo yaliyo ndani ya Labour kwa sasa,huko kwa wahafidhina nako mambo si shwari sana.Kuna wanaomuona mgombea wa chama hicho,David Cameron, kama amewaangushwa kwa kushindwa kwake kupata ushindi wa jumla (overall majority).Upinzani wa chini chini dhidi ya Camron haukuanza kwenye uchaguzi huu tu bali tangu alipoweka bayana dhamira yake ya kukibadilisha chama cha Conservative kutoka mwonekano wake kama 'chama kibaya' (nasty party) kwenda chama chenye kujumuisha makundi mbalimbali katika jamii.Kabla ya harakati za Cameron,chama hicho kimekuwa kikitafsiriwa kama 'cha Waingereza Weupe wa tabaka la juu' na kinachokumbatia zaidi mabwanyenye kuliko watu wa kawaida.

Cameron amefanikiwa kwa kiasi flani kubadili taswira hiyo japo si sana.Katika uchaguzi uliopita alihamasisha uteuzi wa baadhi ya wagombea kutoka makundi ambayo kimsingi 'hayamo kwenye akili za chama hicho' kwa mfano wagombea kutoka jamii ndogo za wasio weupe (ethnic minority),shoga na mabinti kadhaa.Japo baadhi ya wagombea hao wameshinda,wengi wao wamefanya vibaya na tayari baadhi ya wahafidhina wanamlaumu Cameron kwa uamuzi huo wa 'kuwapigia debe wageni wa tamaduni za chama hicho'.

Jingine linalomwandama Cameron ni mchango wa kundi dogo la washauri wake wanaofahamika kama 'wana-Eton wa zamani' (ex-Etonian),yaani marafiki zake wa karibu aliosoma nao katika shule ya Eton yenye hadhi ya juu kabisa na chaguo la 'wateule wachache' kwa hapa.Hao ni pamoja na Kansela ('waziri wa fedha') kivuli George Osborne na mwanamikakati anayesifika kwa akili nyingi Oliver Letwin (ambaye pia ni 'waziri' kivuli).Wengine wanaotuhumiwa 'kumshika akili' Cameron ni pamoja na kiongozi wa zamani wa Conservative,William Hague,na Mkurugenzi wa Mawasiliano,Andy Coulson (ambaye kabla ya kuchukua wadhifa huo alikuwa mhariri wa gazeti maarufu kwa udaku la News of The World).Coulson anafahamika kwa uwezo wake katika 'kutengeneza fitna,majungu na kummaliza mtu' (maeneo yanayolipa umaarufu News of the World).

Washauri hao wa Cameron wanatuhumiwa 'kumshauri vibaya' mgombea hasa katika wazo la 'jamii kubwa' (Big Society) ambalo inaelezwa kuwa liliasisiwa na Letwin.Wakosoaji wanadai kuwa wazo hilo halikueleweka kwa wapiga kura na wengine wanakwenda mbali zaidi na kulieleza kama 'wazo muflisi'.Vilevile,inaelezwa kuwa  Lord Ashcroft,'kibopa' aliyemwaga fedha nyingi kwa minajili ya Conservative kushinda uchaguzi huo,hajaridhishwa na matokeo ya uchaguzi huo,sambamba na 'kushindwa' kwa Cameron kusimama kidete kumtetea mhafidhina huyo tajiri (Ashcroft) alipoandamwa na skandali ya 'hadhi ya raia asiyelipa kodi kutokana na ukazi wake nje ya nchi' (non-domicile status).Lord Ashcroft anaamini kuwa suala hilo limechangia kupunguza kura za chama chao na anaamini kuwa Cameron angeweza kumtetea vizuri zaidi ya alivyofanya.Kadhalika,tajiri huyo anadaiwa kutopendezwa na wazo la Cameron kushiriki midahalo ya uchaguzi kwenye runinga,ambapo anaona kuwa ilisaidia kumuimarisha mgombea wa chama cha Waliberali (Liberal Democrats) Nick Clegg na hivyo 'kula' kura za Conservatives.

Nitaendelea kuwahabarisha kinachojiri kwenye anga za siasa za hapa kadri muda utavyoruhusu.

29 Apr 2010

British National Party (BNP),chama cha kibaguzi cha hapa Uingereza,kimetangaza kwamba kitatoa paundi 50,000 kwa kila atakayeafiki kuhama Uingereza.Akiongea katika kipindi cha 'Today' cha kituo cha redio cha BBC4,mwenyekiti wa chama hicho,Nick Griffin (pichani) alisema kuwa mpango huo ni mahsusi kwa Waingereza wasio Weupe (non-White British) na wahamiaji wengine wasio weupe (non-White migrants).

Griffin alieleza kuwa kwa mujibu wa sera ya uhamiaji ya chama chake 'milango ya Uingereza itafungwa' kwa wageni isipokuwa tu kwa wale wenye ujuzi au taaluma maalum."Aidha unazungumzia fundi bomba wa ki-Polish au mkimbizi kutoka Afghanistan,milango ya Uingereza itafungwa kwa sababu nchi hii imejaa",aliongeza kiongozi huyo mbaguzi wa rangi.

Kiongozi huyo wa BNP alitanabaisha kuwa "Idadi ya watakaozuiwa kuingia nchi hii itakuwa yoyote na kutoka popote.Milango itafunguliwa tu pale itapokidhi mahitaji wa Waingereza na Uingereza".Akitolea mfano wa utekelezaji wa sera hiyo,Griffin alisema laiti Uingereza ikiwa na mahitaji ya wataalam wa nyukia basi chama hicho kitaruhusu,kwa mfano,mwanafikizia kutoka Japan.

Alipoulizwa kama sera hiyo itaambatana na kuvunja mikataba ya kimataifa,mbaguzi huyo alijibu: "Kabisa.Mikataba ya kimataifa haikidhi mahitaji ya Uingereza na watu wake.U-kimataifa (internationalism) ni miradi ya tabaka la wanasiasa".

Kuhusu kuwataka wasio weupe kuondoka Uingereza,Griffin alisema:"Tunasema tutatoa posho ya kuhama makazi (resettlement grants) na hili ni suala la hiari .Tunazungumzia takriban pauni 50,000 kwa kwa mtu".Alipoulizwa ni watu wangapi wanaotarajiwa kuhama Uingereza kwa mujibu wa sera hiyo alisema: "180,000 kwa mwaka,kama wataondoka katika nchi hii iliyojaa kupindukia".

Imetafsiriwa kutoka Yahoo! News


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.