10 May 2010

Jambo moja nililojifunza kutoka kwa hawa wenzetu wa nchi zilizoendelea ni kile kinachoelezeka vizuri kwa kimombo kama not settling for less.Yaani,kwa tafsiri isiyo rasmi,ni kutokubali kuridhishwa na pungufu ya matarajio kamili.Kama ni mwanasiasa na wananachi wanaona 'unawazingua' basi usitarajie kuwa wataendelea 'kukulea'.Kama ni kwenye soka,wenye timu hawatarajii pungufu ya ushindi.

Baada ya matokeo yasiyoridhisha kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Alhamisi iliyopita,tayari 'bundi' mbaya ameshaanza kukiandama chama cha Labour.Baadhi ya wanasiasa ndani ya chama hicho wamejitokeza hadharani kutaka Gordon Brown atoswe kwa madai kuwa yeye ndio hasa chanzo cha matokeo mabaya kwenye uchaguzi huo ambapo Labour iliambulia nafasi ya pili nyuma ya chama cha wahafidhina (Conservative Party).

Japo hadi sasa Brown hajatamka kama ataachia ngazi uongozi wa chama hicho lakini dalili ni kwamba presha ikiendelea kuongezeka hatokuwa na jinsi zaidi ya kujiuzulu.Hapa sizungumzii u-waziri mkuu bali hali ya mambo ndani ya chama cha Labour.

Kukurejesha nyuma kidogo,Labour imekuwa na makundi mawili 'yasiyoiva' kwa kitambo kirefu sasa.Kwa upande mmoja ni wale wanaofahamika kama Blairites,ambao wanamhusudu Waziri Mkuu wa zamani Tony Blair,na kwa upande mwingine ni Brownites,ambao wanamhusudu Gordon Brown.Inasemekana kuwepo kwa makundi hayo kumechangia kwa kiasi flani matokeo mabaya ya chama hicho katika uchaguzi uliopita.Inadaiwa kwamba mmoja ya watu wenye nguvu kubwa ndani ya Labour,Lord Mandelson,alitumia kampeni za Brown na Labour kumuimarisha David Miliband,'Waziri' wa Mambo ya Nje wa Uingereza na chaguo la Blairites kumrithi Brown.Inaelezwa kwamba wakati Labour wanazindua kampeni zao kwa ajili ya uchaguzi huo,Mandelson (maarufu kama Malaika wa Giza-Angel of Darkness-ndani ya Labour)alifanikisha safari ya Miliband kwenda Marekani kwa mazungumzo na Rais Obama,fursa ambayo wachambuzi wa siasa wanaamini ingemwezesha Brown kuonekana kama kiongozi mwenye nguvu katika siasa za kimataifa.

Inadaiwa pia kuwa kampeni ya Brown iligeuzwa na Mandelson kuwa 'makao makuu ya Miliband' kwa maana kuwa ilikuwa ikitumika kwa namna flani kumpromoti mwanasiasa huyo (Miliband) ambaye bado ana ukaribu mkubwa na Blair.Hata meya wa zamani wa jiji la London,Ken Livingstone ameligusia hilo katika makala yake aliyoandika kwenye gazeti moja la Daily Mail.

Kwa sasa,harakati zinazoendelea chini chini ndani ya Labour ni za kumrithi Brown.Yani imekuwa kama ndugu za mgonjwa wanapoanza kugombania urithi kabla mgonjwa huyo hajaaaga dunia.Alosema siasa ni mchezo mchafu hakukosea.Baadhi ya majina yanayohusishwa na mpambano huo ni pamoja na akina Miliband,yaani David na mdogo wake Ed,ambaye ni waziri wa mazingira,Ed Ball- 'waziri' wa elimu na 'waziri' wa mambo ya ndani Alan Johnson.

Na akina Miliband  wanazua mvutano ambao unavuka anga za siasa kwa vile wakati David (pichani kushoto) ni Blairite,mdogo wake (kulia) ni Brownite.Inaelezwa kuwa tayari Ed ameshamfahamisha mama yao kuwa anadhamiria kupambana na kaka yake kwenye kinyang'anyiro cha kuiongoza Labour.Hata hivyo,inaelezwa pia kuwa bado yuko njia panda kwa vile kwa upande mmoja Brownites wenzie wanamwona kama chaguo mwafaka kwa nafasi hiyo,lakini kwa upande mwingine 'damu ni nzito kuliko maji' na anatafakari kama pengine itakuwa jambo la busara kumsapoti kaka yake.

Tukiachana na mvutano huo wa kifamilia,'vita' kubwa inatarajiwa kuwa kati ya kaka yake (David) na (Ed) Balls.Wakati David anasifika kwa upeo na akili ya hali ya juu (ni Mwingireza mwenye asili ya Kiyahudi huyu) na ufahamu wake wa siasa za kimataifa hasa kutokana na wadhifa alionao sasa,Balls ana sapoti kubwa kwenye vyama vya wafanyakazi ambavyo kimsingi vina nguvu ya kutosha kwenye chama cha Labour.Kadhalika,wakati David anaonekana kama mtu wa 'tabaka la juu' Balls yuko karibu zaidi na wana-Labour wa ngazi za chini.

Tukiweka kando kidogo matatizo yaliyo ndani ya Labour kwa sasa,huko kwa wahafidhina nako mambo si shwari sana.Kuna wanaomuona mgombea wa chama hicho,David Cameron, kama amewaangushwa kwa kushindwa kwake kupata ushindi wa jumla (overall majority).Upinzani wa chini chini dhidi ya Camron haukuanza kwenye uchaguzi huu tu bali tangu alipoweka bayana dhamira yake ya kukibadilisha chama cha Conservative kutoka mwonekano wake kama 'chama kibaya' (nasty party) kwenda chama chenye kujumuisha makundi mbalimbali katika jamii.Kabla ya harakati za Cameron,chama hicho kimekuwa kikitafsiriwa kama 'cha Waingereza Weupe wa tabaka la juu' na kinachokumbatia zaidi mabwanyenye kuliko watu wa kawaida.

Cameron amefanikiwa kwa kiasi flani kubadili taswira hiyo japo si sana.Katika uchaguzi uliopita alihamasisha uteuzi wa baadhi ya wagombea kutoka makundi ambayo kimsingi 'hayamo kwenye akili za chama hicho' kwa mfano wagombea kutoka jamii ndogo za wasio weupe (ethnic minority),shoga na mabinti kadhaa.Japo baadhi ya wagombea hao wameshinda,wengi wao wamefanya vibaya na tayari baadhi ya wahafidhina wanamlaumu Cameron kwa uamuzi huo wa 'kuwapigia debe wageni wa tamaduni za chama hicho'.

Jingine linalomwandama Cameron ni mchango wa kundi dogo la washauri wake wanaofahamika kama 'wana-Eton wa zamani' (ex-Etonian),yaani marafiki zake wa karibu aliosoma nao katika shule ya Eton yenye hadhi ya juu kabisa na chaguo la 'wateule wachache' kwa hapa.Hao ni pamoja na Kansela ('waziri wa fedha') kivuli George Osborne na mwanamikakati anayesifika kwa akili nyingi Oliver Letwin (ambaye pia ni 'waziri' kivuli).Wengine wanaotuhumiwa 'kumshika akili' Cameron ni pamoja na kiongozi wa zamani wa Conservative,William Hague,na Mkurugenzi wa Mawasiliano,Andy Coulson (ambaye kabla ya kuchukua wadhifa huo alikuwa mhariri wa gazeti maarufu kwa udaku la News of The World).Coulson anafahamika kwa uwezo wake katika 'kutengeneza fitna,majungu na kummaliza mtu' (maeneo yanayolipa umaarufu News of the World).

Washauri hao wa Cameron wanatuhumiwa 'kumshauri vibaya' mgombea hasa katika wazo la 'jamii kubwa' (Big Society) ambalo inaelezwa kuwa liliasisiwa na Letwin.Wakosoaji wanadai kuwa wazo hilo halikueleweka kwa wapiga kura na wengine wanakwenda mbali zaidi na kulieleza kama 'wazo muflisi'.Vilevile,inaelezwa kuwa  Lord Ashcroft,'kibopa' aliyemwaga fedha nyingi kwa minajili ya Conservative kushinda uchaguzi huo,hajaridhishwa na matokeo ya uchaguzi huo,sambamba na 'kushindwa' kwa Cameron kusimama kidete kumtetea mhafidhina huyo tajiri (Ashcroft) alipoandamwa na skandali ya 'hadhi ya raia asiyelipa kodi kutokana na ukazi wake nje ya nchi' (non-domicile status).Lord Ashcroft anaamini kuwa suala hilo limechangia kupunguza kura za chama chao na anaamini kuwa Cameron angeweza kumtetea vizuri zaidi ya alivyofanya.Kadhalika,tajiri huyo anadaiwa kutopendezwa na wazo la Cameron kushiriki midahalo ya uchaguzi kwenye runinga,ambapo anaona kuwa ilisaidia kumuimarisha mgombea wa chama cha Waliberali (Liberal Democrats) Nick Clegg na hivyo 'kula' kura za Conservatives.

Nitaendelea kuwahabarisha kinachojiri kwenye anga za siasa za hapa kadri muda utavyoruhusu.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.