8 Jun 2010

Rais Kikwete akikabidhi zawadi ya kinyago kwa mchezaji wa Brazil,Kaka,huku mtoto wa Rais,Ridhiwani Kikwete (kulia kwa Rais),akishuhudia na "tabasamu la haja" (Picha kwa hisani ya Ankal Michuzi)

Niite mzandiki,mkosoaji wa kila kitu,au hata mpuuzi.Yote sawa.Lakini haihitaji upeo hata wa mtoto mchanga kutambua kuwa uamuzi wa "kununua" kipigo cha mabao matano kutoka kwa Wabrazili ilhali tumegubikwa na matatizo lukuki ya kiuchumi ni,well,upuuzi.

Nilishabashiri awali kuwa baada ya mechi kati ya Taifa Stars na Wabrazili itakuja mechi kali zaidi kuhusu faida au hasara za mechi hiyo.Na hapa nazungumzia fedha.Kwa mujibu wa tovuti ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC),mechi hiyo ilifanikishwa na mkopo wa benki flani kwa Shirikisho letu la Soka chini ya uongozi wa Leodgar Tenga.Inaelezwa kuwa TFF walitarajia mpambano huo ungeingiza takriban dola milioni tatu ambazo zingerejesha gharama zinazokisiwa kuwa dola milioni mbili unusu (zaidi ya shilingi bilioni tatu)walizotumia "kununua" mechi hiyo.Kwa akili ya Tenga na wenzake,walitarajia uwanja wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000 ungefurika na pengine kuzalisha faida kubwa zaidi ya hizo dola milioni tatu zilizokisiwa.Sijui ni kufumbia macho umasikini unaowakabili Watanzania wengi au ni ubishi tu,TFF wakaweka viingilio vya juu na vitakavyoingia kwenye vitabu vya historia ya soka la Tanzania.

Sidhani kama tutafahamisha gharama halisi za mechi hiyo wala kuelezwa hasara kamili.Na si kwamba tutafichwa kwa sababu ya aibu ya waandaaji bali kuna "wajanja" (isomeke MAFISADI) watakaoongeza ukubwa wa hasara hiyo kwa kujirejeshea gharama wasizostahili.Lakini pamoja na usiri huo,tovuti ya BBC imemnukuu Waziri wa Habari na Michezo George Mkuchika akisema kuwa serikali haikuchangia chochote katika "ununuzi" wa mechi hiyo,na akatupa "kigongo" kingine kwa kudai TFF walikopa fedha kutoka benki kumudu gharama hizo.

Lakini kauli ya Mkuchika inakinzana na kauli ya awali iliyotolewa na Tenga,ambapo kwa mujibu wa tovuti ya gazeti la Daily Nation,alinukuliwa akieleza kuwa (nanukuu) "Tuliongea na Rais wetu (Jakaya Kikwete),na ni yeye ndiye aliyewezesha mechi hii kuwezekana".Tenga alisema (nanukuu tena) "(Rais) alivutiwa tangu mwanzo na kuhakikisha kila uwezo wa dola (serikali) unawezesha mechi hiyo".

Sasa sijui nani anasema ukweli kati ya Mkuchika na Tenga.Na pengine swali la muhimu zaidi ni nani atayebeba mzigo wa deni hilo kama si mlipakodi wa Tanzania.Na ni mzigo kweli kwani dalili za wazi za uzembe wa waandaaji wa pambano hilo tunaloaminishwa kuwa litaitangaza Tanzania ni matangazo mengi ya makampuni ya kigeni badala ya vivutio vya taifa letu.Well,unatarajia nini kutoka kwa wazembe walioshindwa hata kuwa na CD  ya uhakika ya wimbo wa taifa letu?

1 comment:

 1. Kuna mdau mmoja kutoka chakarika spot naye alielezea kuhusu mechi hiyo siku saba kabla ya mechi na kuieleza TFF....

  Kuchanganywa kwa taarifa na matamko kwa serikali ya awamu ya nne siyo ajabu kwa sababu haina utaratibu katika utendaji ndiyo sababu wanamtegemea Sheikh Yahya katika kuendeshasha serikali na wenzetu wa magharibi wanatumia sayansi, sheria na teknolojia.

  Sifa nzuri ya mwandishi kuandika habari yeyote iwe nzuri ama mbaya kwa muhusika...

  Iwapo JK serikali inafanya madudu ni halali kukosolewa na kama itatokea ikafanya vyema inastahili kusifiwa pia...

  Ingawa kwa sasa hakuna hata chembe ya sifa bora, zote mbaya kwa serikali ya JK

  ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube