5 Jun 2010

Mwezi Februari mwaka huu,Rais wa Kampuni ya Toyota (ya Japan) Akio Toyoda aliomba rasmi msamaha kwa wateja wa kampuni hiyo nchini Marekani ambao walikumbwa na matatizo ya kiufundi kwenye magari yao.Mwezi kama huo mwaka jana,mabosi wa mabenki ya RBS na HBOS ya hapa Uingereza nao waliomba msamaha kwa wateja wao na umma kwa ujumla kutokana na uzembe uliopelekea benki hizo kukwamuliwa na serikali kwa pauni bilioni 37 fedha za walipakodi wa hapa. Na hivi majuzi,Waziri Mkuu wa Japan,Yakio Hatoyama, ametangaza kuwa atajiuzulu kufuatia kutotimiza ahadi aliyotoa wakati wa kampeni zake za uchaguzi kuwa angeondoa vikosi vya jeshi la majini la Marekani katika visiwa vya Okinawa.


Lakini wakati hayo yakitokea,serikali ya CCM imewaamuru mawaziri wake kuzunguka mikoani kueleza mafanikio ya Awamu ya Nne katika harakati za wazi kuelekea Uchaguzi Mkuu.Tuweke ushabiki pembeni,hivi kweli mawaziri hawa hawakustahili kuzunguka huku na huko kuomba msamaha kwa mlolongo wa madudu tunayoendelea kuyashuhudia tangu mwaka 2005 (na pengine madudu zaidi yanayoendelea kufanywa na CCM miaka nenda miaka rudi)?


Msanii mkongwe wa hapa Uingereza (na duniani kwa ujumla),Sir Elton John aliwahi kuimba wimbo wenye jina SORRY SEEMS THE HARDEST WORD (yaani 'samahani inaelekea kuwa ni neno gumu').Na hakukosea,japo hakuwa analenga siasa za nchi zetu za Dunia ya Tatu,hususan Afrika,na hasa Tanzania.Watawala wetu ni wepesi sana katika kugeuza lawama kuwa pongezi,na wakibanwa katika hilo hugeuka mbogo na kuja na vitisho lukuki.

Labda nikukumbushe kidogo kwanini naamini ziara za mawaziri zingekuwa na maana zaidi kama zingetumika kuomba msamaha kwa wananchi badala ya kuelezea mafanikio ambayo kimsingi yanabaki kwenye takwimu zaidi kuliko uhalisia.Kwanza,Awamu ya Nne ilitufahamisha kuwa inafahamu kilio cha Watanzania,na ikaja na kauli mbiu ya kasi mpya,ari mpya na nguvu mpya.Naamini mie si pekee niliyesahau kuhusu kauli mbiu hiyo kwa vile wala haisikiki tena.Lakini kama hiyo haitoshi,kukaongezwa kibwagizo cha Maisha Bora kwa Kila Mtanzania (Yanawezekana).Japo sote tunatambua kuwa watawala wetu wanaishi kama wako peponi lakini hiyo sio excuse ya kuwafanya wasielewe kuwa maisha bora yamewezekana zaidi kwa mafisadi kuliko kwa wananchi walalahoi wa kawaida.Kwahiyo kama viongozi hawa wangekuwa na nidhamu kwa wapiga kura waliowaweka madarakani hapo 2005 basi angalau wangetuambia nini kinachopelekea maisha bora kubaki haki ya mafisadi wachache huku walalahoi wakizi kuwa walalawima.

Baada ya kuingia madarakani,Awamu ya nne ilitueleza kuwa ili kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania kunahitajika baraza kuuuubwa la mawaziri.Binafsi niliona kuna mantiki katika hoja hiyo japo sikuwa na uhakika kuwa "mwalimu anaweza kumudu darasa lenye wanafunzi wengi" kama ilivyokuwa kwenye kabineti ya JK.Bila kuuma uma maneno,kwa kifupi ukubwa wa baraza la mawaziri haujafanikiwa kwa chochote katika ku-meet matarajio ya Watanzania.Sanasana wengine walilazimika kujiuzulu baada ya kutuingiza mkenge kwenye ishu kama za utapeli wa Richmond.Ungetegemea kujiuzulu huko kungeandamana na hatua za kisheria lakini waliojiuzulu waliishia kupongezwa huku wakikumbushwa kuwa yaliyowakumba ni ajali tu za kisiasa na si ajabu siku moja wakarejea madarakani.

Mkuu wetu wa nchi akatuambia kuwa anawafahamu wala rushwa ila anawapa muda wa kujirekebisha.Binafsi,hapo ndipo nilipoanza kuhisi kuwa sikuwa sahihi kuamini kwamba tumepata mrithi halisi wa Mwalimu (Nyerere) in the form of JK.Tangu lini mwizi akapewa deadline?Kama wala rushwa walikuwa wanajulikana kwa Rais kilichopaswa kufanywa ni yeye kukabidhi orodha hiyo kwa taasisi husika ili wachukuliwe hatua stahili.Unajua,laiti JK angekabidhi orodha ya wala rushwa anaowajua kwa vyombo vya usalama kisha wakakamatwa na kuepwa deadline,pengine by now tusingekuwa tunajiuliza wenye Kagoda ni akina nani.Ni muhimu wak Watanzania kumhoji Rais wetu mpendwa kuhusu hao wala riushwa anaowafahamu,na lini hiyo deadline ita-expire.Tunachohitaji ni majina na sio idadi,na hata kama ni idadi basi tuambiwe lini watashughulikiwa.

Tuaambiwa kuwa matatizo ya umeme yangepatiwa ufumbuzi wa kudumu only miezi michache baadaye kufahamu kuwa ufumbuzi wenyewe unahusisha matapeli wenye kampuni ya briefcase (Richmond).Shahidi muhimu katika sakata la EPA akahifadhiwa mpaka Maulana akachukua uhai wake (kuna wanaodai kuwa bado yuko hai au huenda kafanyiwa plastic surgery) halafu wenye nchi wakagoma katakata kutuambia mwizi mkubwa wa fedha za EPA (Kagoda ni nani).

Tuaaambiwa kuwa ziara za mara kwa mara za Rais wetu huko nje ni muhimu kuitangaza nchi yetu na yeye kujitambulisha,kabla ya kuaminishwa kuwa Mkutano wa Sullivan na huu wa majuzi wa Economic Forum utalinufaisha taifa hasa katika sekta ya utalii,only for tuliorogwa sie kulipa mabilioni ya shilingi kuialika timu ya taifa ya Brazil huku kukiwa na ngonjera zilezile za "ziara hii itasaidia kuitangaza Tanzania".Kama ziara za Rais huko nje na rundo la wafanyabiashara (plus mikutano kama ya Sullivan na huo wa Economic Forum) imeshindwa kuzaa matunda,dakika 90 za mechi na Wabrazili zitaweza?

Majuzi wafadhili wametangaza kupunguza misaada yao kwa sababu ya ufisadi (putting it straightforward) na Waziri wetu wa Fedha Mustapha Mkulo bila aibu anasema hiyo isitupe hofu kwa vile serikali itakopa benki ya Stanbic!Nasema "bila aibu" kwa vile sio tu kukopa sio sifa hususan kwa serikali iliyoingia madarakani na mkwara wa maisha bora kwa kila Mtanzania bali pia deni hilo litabebwa na walalahoi haohao wanaoendelea kubebeshwa mzigo wa mahela yanayokwibwa na mafisadi kila kukicha.

Haya,tukaambiwa tena kuwa kwa vile kuna mtikisiko wa uchumi wa dunia basi na hohehahe sie lazima tuyanusuru makampuni yetu katika kile kinachofahamika ki-uchumi kama "stimulus package".Hivi kwa mwenye akili timamu,ukitangaza kuwa kuna hela za bure somewhere unatagemea nini kama sio vigogo kuunda kampuni hewa na kuiba fedha hizo?Hadi leo hatujaambiwa mafanikio ya stimulus package hiyo, na kama ilivyokuwa kwenye ripoti ya mabomu ya Mbagala usitarajie kuambiwa lolote la maana zaidi ya takwimu za kizushi.

Halafu Mkuu wetu wa nchi akatupa presha kwa kuamua kuhutubia Bunge kuhusu sakata la EPA (pamoja na mambo mengine).Tunaloweza kukumbuka zaidi kwenye hotuba hiyo ni kauli yake kuwa anathamini sana haki za binadamu ikiwa ni pamoja na za mafisadi.Kumbukumbu nyingine ni angalizo kutoka kwa Spika wa Bunge,Samweli Sitta,kuwa haki za binadamu za walalahoi ni muhimu zaidi kuliko za hao mafisadi.

Nimejitahidi kuorodhesha machache yanayopaswa kuombewa radhi na mawaziri wa serikali ya Awamu ya Nne badala ya "kueleza mafanikio".Unless wanataka kutuaminisha kuwa kukua kwa ufisadi ni sehemu muhimu ya mafanikio yao.Natambua kuwa "SAMAHANI" ni neno gumu kama alivyosema Elton John lakini uungwana ni kitu cha bure.Hizo fedha za walipa kodi wanazotumia kuzunguka huku na kule zingeweza kutumika vizuri zaidi kwa kila Waziri kuomba msamaha kwa madudu aliyofanya katika miaka hii mitano.Kaulimbiu kuwa "mlitutuma, tumetekeleza, tumerudi kuwaelezeni tulivyotekeleza na kuwasikiliza" ni matusi ya nguoni kwa vile hakuna Mtanzania mwenye akili timamu aliyeituma serikali kuingia mikataba ya kitapeli na wazushi wa EPA,au kukomalia kutotaja Kagoda ni mdudu gani,plus madumu mengineyo.Tulichowatuma ni kutukomboa kutoka katika lindi hili la umasikini sambamba na kuboresha hali za maisha yetu.Hatukuwatuma kuuza kila kilichopo kwa bei ya kutupa wala hatukuwatuma kung'ang'ania kununua samani kutoka nje na hatimaye kukumbuka dakika za majeruhi kuwa ununuzi huo hauendani na umasikini wetu.

Japo nakerwa na ziara hizi za mawaziri zinazozidi kuwabebesha mzigo walipa kodi walalahoi lakini nakereka zaidi napoona watu hawa wanapotufanya wajinga kiasi cha kutuzushia kuwa TULIWATUMA KULEA UFISADI.

Tumia kura yako vizuri,ukiendekeza ushabiki utazidi kuumia.Hakuna miujiza inayoweza kuondoa ufisadi hata kama watu watakesha kwenye nyumba za ibada (na huko wanakutana na "wabishi" kama Askofu Kilaini ambao wanaendelea kung'angania mtizamo wao finyu kuwa JK bado ni chaguo la Mungu.Askofu muogope Mungu wako unayemtumikia,please!).Nia pekee ya kuondokana na ufisadi ni kuwaondoa mafisadi.Kumbuka kuwa ufisadi ni kitendo kinachofanywa na mafisadi,na as long as wanaendelea kuwepo basi inakuwa mithili ya kupe au mbung'o na damu.Watanyonya hadi tone la mwisho.

AMKA!

9 comments:

 1. Kuhusu ziara za JK nchi za nje, napenda kusema kuwa mkurugenzi wa kituo cha uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Center), Mheshimiwa Ole Naiko, amesema na kurudia kuwa ziara za JK nchi za nje zimeleta faida nchini, kwa upande wa uwekezaji na biashara. Kwa mfano, miezi kadhaa iliyopita aliongelea jinsi kiwango cha uwekezaji kutoka Marekani ulivyopanda mara dufu kutokana na ziara za JK. Hivi karibuni, Ole Naiko ameongelea manufaa ya ziara ya JK na wafanyabiashara wa Tanzania huko Uturuki. Ole Naiko amesema wazi kuwa wanaobeza ziara za JK nchi za nje hawana takwimu, na hawaitakii nchi mema. Maneno yake hayo yako huko mtandaoni pia.

  Mimi si mtaalam wa masuala hayo, bali nileta tu hii taarifa kuhusu kauli za mkurugenzi wa TIC.

  ReplyDelete
 2. Profesa,laiti takwimu tunazopewa na watawala wetu zingekuwa sio tu za kuaminika bali pia zinaendana na hali halisi "mtaani" basi yayumkinika kusema kuwa leo hii tusingekuwa "taifa la dunia ya tatu".Ni dhahiri kuwa laiti ziara hizo zingekuwa zimeleta ufanisi kiasi anachotuaminisha Mheshimiwa Ole Naiko basi nchi wahisani wasingepunguza sehemu ya msaada wao kwa kigezo cha "uzembe" na urasimu kwenye eneo hilohilo la uwekezaji.Na huyo Ole Naiko na TIC yake ingekuwa inawajibika ipasavyo tusingelazimika kuwalipa Wabrazili mabilioni ya shilingi kwa minajili ya "kuitangaza Tanzania" kwa dakika 90.

  Takwimu nyingi zimekuwa za kuleta matumaini sana,na majuzi Mkulo ametuambia kuwa uchumi unakua huku akitoa takwimu za kupendeza.MKUKUTA,MKURABITA,MWEMKWA,nk nk zinafanya vizuri in terms of takwimu,lakini hali ya Watanzania inazidi kuwa duni.

  ReplyDelete
 3. Hivi wewe Profesa Mbele unategemea huyo Naiko anaweza kumkosoa JK...Hivi unataka nini kiongelewe ndiyo ufahamu hiyo serikali ya JK ni ya ubabaishaji...wala rushwa wote ambao ushahidi umetolowa na magazeti makini kabisa kama the Guardian and na taasisi SFO..na kesi zingine nyingi na hizo zote zipo ndani ya uwezo serikali ya JK anashindwa kuchukua hatua zozote kama Rais wa Jamhuri...na kushindwa kwake kuchukua hizo hatua ndiyo inaonesha wazi kuwa hao Mafisadi na wala Rushwa ndiyo maswahiba wake au wanaisa wenzake. Hivyo tunapenda uwe muwazi kama maandishi ya ripoti ndiyo maendeleo ya Tanzania ingekuwa mbali sana kwenye kuondoa umaskini na hata wewe Profesa Mbele ungekuwa unafundisha vyuo vya Tanzania...Tunaomba acaha kutetea uzembe wa serakali hii...tusiposema na kukosoa uozo wa serikali hii kama wewe Profesa hatutafika popote.....Big up Dr Chahali kwa mawazo yakinifu yenye dira halisi ya kuleta uwazi bila kificho katika madudu ya serikali ya JK.

  ReplyDelete
 4. Mimi ni mjumbe. Nimeleta msimamo wa TIC. Nashangaa kuwa kwa kufanya hivyo, nasemwa kuwa ni mtetezi wa serikali ya JK na kadhalika.

  Ukweli kama mimi ni mtetezi wa serikali ya JK au la ummejaa katika kitabu changu kuhusu masuala ya siasa na jamii ya Tanzania enzi hizi za JK. Bofya hapa.

  Nikisema kuwa wa-Tanzania watasoma kitabu changu nitakuwa nawapa sifa ambayo hawastahili. Ni wachache sana wanaosoma vitabu.

  Nimeshatamka tena na tena, kwenye blogu yangu na blogu za wengine, kuwa wa-Tanzania ni wazembe inapofika kwenye suala la kununua au kusoma vitabu. Wanaona ni kero, labda viwe vitabu vya udaku.

  Kuhusu ufisadi ni kuwa wa-Tanzania wenyewe wanaulea na kuuenzi ufisadi, kuanzia vijijini hadi mijini, shuleni, viwandani, hospitalini, maofisini, na kadhalika. Nimeshatamka kuwa wa-Tanzanai wanapolalamikia ufisadi miongoni mwa vigogo serikalini au kwenye mashirika wanafanya usanii. Bofya hapa.

  Huwa sioni sababu ya kujibizana na "anonymous." Sijui kama ni woga au usanii unaowafanya watu wajifiche kwenye malumbano. Bofya hapa.

  "Anonymous" wa hapo juu analeta mpya kwa jinsi anavyomalizia ujumbe wake kwa kupigia debe "uwazi bila kificho" wakati yeye mwenyewe yuko mafichoni. Ndio usanii ninaokataa mimi huo.

  ReplyDelete
 5. Kwa Profesa Mbele,
  Kuwa mjumbe wa TIC ni jambo jema kufanya hivyo lakini taarifa zilizopo tuu kwenye maandishi na siyo kielelezo katika maisha halisi ya mtanzania. Mimi ni Mtanzania niliyopo hapa Tanzania. Tunatambua kuwa huko mlipo ninyi watanzania wenzetu mliyopo huko ughaibuni mnaona na kushuhudia mengi katika maarifa na matukio ya uchumi duniani.
  Hivi tunapozungumzia utalii tunalenga mataifa ya makubwa ya magharibi na kwa sababu hiyo. JK anatumia nafasi kwenda nchi za magharibi anakosema yeye anatangaza utalii wakati watu wenyewe anaowatangazia wanamatatizo ya uchumi!!!!!!.Safari za nje Kama hapa ilivyofafanuliwa hapa na DR Chahali...Je huyo waziri wa mambo nje anafanya nini na balozi Tanzania anafanya nini? This is very strange to be defended from you Prof. Mbele...I can’t understand you at all means to be like this!!!!!
  Sasa hizo takwimu za kusema utalii kuongezeka zinatoka wapi!? Ni ukweli kwamba watu wa magharibi watu makini sana linapokuja suala la matumizi ya pesa wanapokuwa katika kipindi kigumu kwenye uchumi wao...Sasa hao watalii unaosema wametoka wapi!!!!????
  Iwapo wewe ungekuwa makini na upendo na watanzania husinge weka utaratibu wa ununuajia wa kitabu chako kwa asilimia mia moja kutegemea teknolojia ambayo sisi watanzania tupo chini asilimia moja wanaojua jinsi ya kutumia computer mbaya zaidi kuna uhalifu mkubwa katika intanet ambayo unahitaji elimu na maarifa kuutambua huo.
  Sasa unaposema tununue kwa pesa ipi tuliyokuwa nayo. Na pesa zote wamechukua maswahiba wake huyo unayeshindwa kumkosoa waziwazi mpaka sisi tununua haya mawazo yako. Sasa tofauti yako wewe na hao mafisadi ni ipi!??
  Hizo habari za udaku zinaandikwa na vyanzo vipi vya habari....iwapo kama ni magazeti ni mangapi kwa idadi...Wewe unafikiri magazeti yote ya udaku yana-nafasi sawa katika jamii hii ya kitanzania. Sisi ndiyo tunamatatizo idadi yetu ni milioni arobaini.
  Nategemea wewe unaangalia kundi la watu milioni nne ndiyo watanzania wote. Sisi ni watanzania milioni arobaini wenye sifa kuishi kwa siku chini ya dola moja kwa siku, hivyo basi kati yetu kutumia hiyo £10 au nane kununua kitabu chako ni sawa na kipato chetu cha miezi mitatu. Sasa tukae bila kula, kuoga, kuandaa mashmab yetu, kununua kalamu kwa ajili ya familia zetu kwenda shule, bila matibabu ndiyo tutaweza kununua kitabu chako.
  Maneno yako yanatukumbusha msemo wa Kiswahili unaosema aliyeshiba hamfahamu aliyelala njaa. Na hii inathibitisha mara nyingi katika maoni yako kushindwa kuikosoa serikali ya JK kuwa serikali hii ni zuga.

  ReplyDelete
 6. Inaendelea kwa ajili ya Profsa Mbele,
  Nikukumbushe tuu mwalimu ama kiongozi yeyote ni kielelezo cha jamii kama wewe uliyemkufunzi wa chuo kikuu huko unakoishi na kuja kututembelea hapa kwa muda mfupi na kuondoka kwenda peponi na kutuacha sisi hapa motoni na baadae kutoa hayo maoni ya kuogofya(shocking).
  Hivyo basi iwapo wewe ni kiongozi katika jamii basi ni rahisi sana kuisaidia jamii hii ama kuingamiza. Na hiyo dhana inayotumika na CCM na serikali ya Kikwete kuiangaamiza jamii yetu na wewe Profesa Mbele ukishirkia kwa kujiita Mjumbe wa TIC.
  Kukuthibitishia hayo kashfa ya rada, kagoda na hao dada zake, Richmond na dada zake, migodi kuuzwa, mashirika ya umma, Menejiment ya kuingoza TANESCO iliyoingizwa madarakani kwa mtutu kwa Baraka za Kikwete wahusika wake wangekuwa jela hivi sasa na pia kufilisiwa ndiyo ungesema kwamba watanzania wote katika ngazi zote wanaweza kuwa hai kupambana kuondoa ufisadi hivi sasa haiwezekana kwa sababu kuanzia ngazi juu(Rais angalia kauli zake kutoka ughaibuni blog) kabisa yenye uwezo na mamlaka kupambana na Rushwa na ufisadi ndiyo wanabariki huu uhalifu. Tunatambua kwamba wewe ni miongoni watu walilelewa na CCM na pia hata kusomeshwa bila kukopeshwa mpaka elimu ya chuo kikuu hivyo unaona dhambi kama vile kuikosoa serikali ya CCM ni sawa na kuhua mtu vile.
  Kujificha kwangu inatokana na watu kama wewe profesa Mbele..baada kuongelea suala la muhimu unaleta masihara katika mtoa maoni sababu kuwa na status of an anonymous...these are just options available from Dr Chahali Blog kwa sisi tunaogopa kufahamika kwa mtu kama wewe. Kimsingi naweza kukuita wakala wao hao tunaotaka haki itendeke ili tuendeshe Taifa letu tunalolipenda.
  Nategema utakuwa umeelewa wewe mtu wa namna gani ili uweze kujitafakari iwapo unayo nia ya kufanya hivyo kuwa nje ya TANZANIA incorrupt network.
  Nikukumbushe tuu mwalimu ama kiongozi yeyote ni kielelezo cha jamii kama wewe uliyemkufunzi wa chuo kikuu huko unakoishi na kuja kututembelea hapa kwa muda mfupi na kuondoka kwenda peponi na kutuacha sisi hapa motoni na baadae kutoa hayo maoni ya kuogofya(shocking).
  Hivyo basi iwapo wewe ni kiongozi katika jamii basi ni rahisi sana kuisaidia jamii hii ama kuingamiza. Na hiyo dhana inayotumika na CCM na serikali ya Kikwete kuiangaamiza jamii yetu na wewe Profesa Mbele ukishirkia kwa kujiita Mjumbe wa TIC.
  Kukuthibitishia hayo kashfa ya rada, kagoda na hao dada zake, Richmond na dada zake, migodi kuuzwa, mashirika ya umma, Menejiment ya kuingoza TANESCO iliyoingizwa madarakani kwa mtutu kwa Baraka za Kikwete wahusika wake wangekuwa jela hivi sasa na pia kufilisiwa ndiyo ungesema kwamba watanzania wote katika ngazi zote wanaweza kuwa hai kupambana kuondoa ufisadi hivi sasa haiwezekana kwa sababu kuanzia ngazi juu(Rais soma kauli zake kutoka ughaibuni blog) kabisa yenye uwezo na mamlaka kupambana na Rushwa na ufisadi ndiyo wanabariki huu uhalifu. Tunatambua kwamba wewe ni miongoni watu walilelewa na CCM na pia hata kusomeshwa bila kukopeshwa mpaka elimu ya chuo kikuu hivyo unaona dhambi kama vile kuikosoa serikali ya CCM ni sawa na kuhua mtu vile.
  Kujificha kwangu inatokana na watu kama wewe profesa Mbele..baada kuongelea suala la muhimu unaleta masihara katika mtoa maoni sababu kuwa na status of an anonymous...these are just options available from Dr Chahali Blog kwa sisi tunaogopa kufahamika kwa mtu kama wewe. Kimsingi naweza kukuita wakala wao hao tunaotaka haki itendeke ili tuendeshe Taifa letu tunalolipenda.
  Nategema utakuwa umeelewa wewe mtu wa namna gani ili uweze kujitafakari iwapo unayo nia ya kufanya hivyo kuwa nje ya TANZANIA incorrupt network.

  Big up Dr Chahali for showing us your nationalism spirit.

  ReplyDelete
 7. Profesa,binafsi sina tatizo na wewe mwalimu wangu kutukumbusha ujumbe wa TIC lakini tatizo langu lipo kwa hao TIC wenyewe na utendaji wao kwa ujumla.
  Japo naafikiana nawe Profesa kuwa kusoma machapisho ni tatizo miongoni mwa Watanzania wengi lakini kwa upande mwingine tatizo ni kilichomo katika machapisho husika.Hivi katika mazingira ya sasa ambapo Watanzania wengi wako hoi kiuchumi,haiyumkiniki kubashiri kuwa machapisho yenye kuelemea zaidi kwenye takwimu pasipo kujali hali halisi yatapuuzwa?Nachomaanisha hapa ni tabia iliyojengeka miongoni mwa waandishi wengi kuandika kama “watazamaji” au “waangalizi” walio nje ya jamii wanayoilenga badala ya kuwa sehemu ya jamii hiyo.Ni dhahiri,kwa mfano,kitabu kinachodai kuwa uwekezaji umeinufaisha Tanzania kitaonekana kama “kamusi ya matusi” kwa “watu wa kawaida mtaani”.

  Halafu kuna tatizo la lugha inayotumika katika mengi ya machapisho hayo. Kuna tofauti kati ya mhadhara kwenye warsha au darasa la wanafunzi wa chuo kikuu..Pengine hicho kinachochea baadhi ya watu kupendelea zaidi machapisho ya udaku kuliko “hayo ya maana” kwani hawaoni umuhimu wa kupoteza muda kusoma kitu kisichoeleweka au kinachoelezea mambo tofauti na uhalisia (kana kwamba mwandishi anaishi sayari tofauti na wasomaji wake).

  Kuhusu wanaotoa mawazo yao kama “anonymous” (kama huyo mchangiaji hapo juu) binafsi sina tatizo sana kwa vile la muhimu zaidi kwangu ni uzito na mantiki ya hoja zao na si majina yao.Kadhalika,naheshimu haki za kibinadamu za watoa maoni wanaoamua kutotumia majina yao wanapotoa maoni yao.Ni kama katika filamu ambapo wahusika wengi hutumia majina bandia na kinachoifanya filamu ivutie sio jina la mhusika bali ubora (na pengine ujumbe) wa filamu husika.Na hata baadhi ya waandishi maarufu wamekuwa wakitumia majina bandia (kwa mfano James Hadley Chase) lakini haikuzuwia machapisho yao kuwa world bestsellers.Hata hivyo,binafsi napenda kutumia jina langu halisi kila napoweka comments mahala flani.Kwanini?Kubwa zaidi ni uamuzi wangu tu.

  Japo naafikiana nawe Profesa kuwa Watanzania hawawezi kukwepa kabisa mchango wao katika kushamiri kwa ufisadi,natofautiana nawe kidogo kwa sababu hii: Kwa uelewa wangu mdogo,mahusiano mbalimbali katika jamii yanategemea sana umiliki wa nyenzo za uzalishaji mali na mahusiano ya nguvu za uzalishaji mali (power relations).Ni rahisi kulilaumu tabaka tawaliwa kwa “kuzembea” kuliwajibisha tabaka tawala iwapo anayelaumu haangalii namna tabaka tawala linavyojizatiti kudumisha nafasi yake.Kwahiyo,ni rahisi kuwalaumu walalahoi “wanavyolea ufisadi” iwapo tunafumbia macho mazingira yaliyotengenezwa na tabaka tawala dhidi ya “wanaopinga ufisadi”.

  Hivi katika mazingira ya sasa ambapo ni rahisi zaidi kumweka madarakani mbunge (kwa njia halali za kidemokrasia) kuliko kumtoa madarakani hata kama amebainika kupata ubunge huo kwa kugushi sifa zake za kitaaluma (rejea suala la Mheshimiwa Chitalo),au katika mazingira ya sasa ambapo rais ni mithili ya mungu-mtu kutokana na nguvu lukuki alizolimbikiziwa (na kwa bahati mbaya au makusudi zimeishia kwenye kutuambia tu “wala rushwa wanajulikana,nawapa muda wa kujirekebisha...”),mtu wa kawaida mtaani afanyeje?Na je katika mazingira haya ambapo mara nyingi mksanyiko “halali” ni wa kusikiliza hotuba za viongozi wa chama tawala,na madamano “halali” ni ya kupongeza kauli flani za watawala wetu na sio kupingana nazo,mwananchi wa kawaida anapata wapi nafasi ya kuwawajibisha watawala?Na hapo tunaweka kando lawama tunazopaswa kutumiwa sie tuliobahatika “kuona ndani ya darasa”-au tabaka la kati kwa ujumla pamoja na civil society-kwa namna tunavyojiweka karibu zaidi na tabaka tawala na kulitelekeza tabaka tawaliwa.

  Nyerere alitufundisha kuwa ili tuendelee tunahitaji watu,ardhi,siasa safi na uongozi bora,na kwa vile hakuna mtu anayependa kuwa fukara au kunyonywa,na pia ardhi tunayo ya “kumwaga”,kwa hakika kinachotukwamisha ni mapungufu katika siasa na uongozi,au kwa ufasaha zaidi, siasa za kifisadi na uongozi wa kizushi.

  ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube