29 Jul 2010

TANZANIA imetajwa katika ripoti ya Kipimo cha Hali ya Rushwa Afrika Mashariki (EABI), kuwa na taasisi zinazoongoza kwa rushwa kwa nchi za Afrika Mashariki.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mratibu wa sekretarieti ya Jukwaa la Wazi (TRAFO), Kaiza Buberwa, alisema kuwa utafiti huo ulifanywa kwa kushirikisha sampuli 10,469 na watu 3,231 walihojiwa kwa Tanzania.

Alisema kuwa katika utafiti huo uliofanyika chini ya wataalamu wa nchi husika, ulifanyika Febrauari na Machi ambapo nchi za Kenya, Burundi, Tanzania, Rwanda na Uganda zilihusishwa.


. Buberwa alisema taasisi zinazoongoza kwa rushwa katika Afrika Mashariki ni Jeshi la Polisi, Mahakama, Jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa, Wakala ya Usajili wa Vifo na Vizazi (RITA), Magereza, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi katika kutoa huduma kwa wananchi, sambamba na ajira.


Alisema kuongoza kwa taasisi hizo ni kutokana na sampuli hiyo ya watu hao, ambao walizitaja taasisi zilizokithiri kwa rushwa wakati wa kupata huduma za kijamii.

Buberwa alisema kwa kuongoza kwa rushwa katika idara nyeti za serikali kwa Afrika Mashariki, Jeshi la Polisi limechukua nafasi ya tano kwa asilimia 65.1 na Mahakama kuwa nafasi ya 10 kwa asilimia 56.4 katika utoaji wa huduma katika misingi ya rushwa.

Aidha, alisema kuwa katika ripoti hiyo haisemi Tanzania hakuna rushwa wala rushwa kidogo, ripoti inasema kwamba ni kwa kuzingatia idadi ya matukio ya vitendo vya rushwa katika idara kadhaa za umma wakati wa kutoa huduma kwa wananchi ikilinganishwa na nchi za Burundi, Kenya, Uganda na Rwanda.

Buberwa alisema kuwa baadhi ya Watanzania asilimia 85.8 wanaamini kuwa hali ya rushwa Tanzania ni mbaya, wakati asilimia 40.6 wanaamini serikali hatimizi wajibu wake katika kuondoa rushwa na kuimarisha utawala bora.

Alisema taasisi nyingine zinazofuata katika rushwa kwa utoaji wa huduma kwa jamii ni Jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa (JKT) asilimia 74.2, Wakala ya Usajili wa Vifo na Vizazi (RITA), asilimia 66.2, Magereza asilimia 61.9, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) asilimia 46.8, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi asilimia 47.9.

CHANZO: Tanzania Daima

.

1 comment:

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube