29 Sept 2010


CHADEMA: Synovate wahini mahakamani
*Slaa asema wanazo nyaraka za utafiti wao.
*Adai kuna mbinu za 'kuchakachua' matokeo.

Na Tumaini Makene

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeivaa kampuni utafiti ya Synovate kikisisitiza kuwa kina matokeo ya utafiti uliofanywa na kampuni hiyo ya kupata matokeo yaliyotoa ushindi wa asilimia 45 kwa chama hicho na mgombea wake wa urais, Dkt. Willibrod Slaa.

Synovate hivi karibuni ilikanusha habari kuwa haijawahi kufanya utafiti wala kuficha matokeo hayo yaliyodaiwa kuipa CCM na mgombea wake Rais Jakaya Kikwete asilimia 41, huku ikitishia kulishtaki gazeti moja liliwakariri viongozi wa CHADEMA wakieleza utafiti huo.

Akizungumzia matokeo hayo jana, Dkt. Slaa alisema "Synovate wakimbie haraka mahakamani, tunazo document (nyaraka), hata gazeti lililotishiwa kushtakiwa lisiwe na wasiwasi, huu ni wakati wa kuvunja heshima ya Synovate kitaifa na kimataifa.

"Walifanya utafiti na katika swali namba GP 06 waliuliza, 'uchaguzi ukifanyika sasa hivi nani utampigia kura kuwa rais wa Tanzania?' na majina yote yaliweka pale ya wagombea, sasa wanakanusha nini, waende haraka sana mahakamani, vinginevyo credibility (heshima) yao tutaivuruga nchi nzima na kimataifa, alisema huku akionesha nyaraka hizo kwa mbali.

Dkt. Slaa alisema katika nchi nyingine taasisi za maoni zinakuwa huru, hazipendelei chama chochote kile.

Katika hatua nyingine, CHADEMA kimemshutumu serikali ya CCM inanyoongozwa na Rais Jakaya Kikwete kikidai kuwa imepanga kutumia mbinu chafu ili kuhujumu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.

Kimesema kuwa kinazo taarifa za uhakika kuwa kati ya mbinu hizo chafu ambazo zinatumiwa au zinataka kutumiwa na serikali kukibeba Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi wa mwaka huu ni kutoa maelekezo kwa Usalama wa Taifa na kujipanga kuchapisha karatasi bandia za kupigia kura nje ya nchi.

CHADEMA kimesema kuwa njama hizo ni aina ya ufisadi kwa kuwa zinahusisha matumizi mabaya ya madaraka na raslimali za nchi kukisaidia chama kimoja cha siasa-CCM, hivyo hazipaswi kuvumiliwa kwani zina lengo la kuingilia maamuzi ya wapiga kura na kuvuruga amani ya nchi.

Kimesema kuwa iwapo mbinu hizo chafu zitafanikiwa kwa kuharibu uchaguzi na kupanga matokeo ya kuipendelea CCM na mgombea wake wa urais, "Rais Kikwete ndiye atabeba lawama na laana zote juu ya yale yatakayotokea. Usalama wa Taifa wakanushe kama hawajapewa maelekezo na kama sasa hawazunguki mikoani."

Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibroad Slaa alipokuwa akizungumza na waandishi ambapo alisisitiza kuwa siku zote chama hicho kimekuwa kikisema kuwa amani ya nchi wakati wa uchaguzi imekuwa ikivurugwa na chama tawala kwa nia ya kutaka kung'ang'ania madaraka, kinyume na maamuzi ya Watanzania.

"Leo tumewaita kuzungumzia juu ya mambo matatu, maamuzi ya Kamati Kuu ya CHADEMA hasa juu ya ubunge wa viti maalumu, uchaguzi mkuu wa mwaka huu na suala la Synovate (kampuni inayojihusisha na kura za maoni ya watu)...juu ya uchaguzi mkuu tunazo taarifa za uhakika kuwa Serikali imetoa instructions (maelekezo) kwa Usalama wa Taifa na sasa wako mikoani wakizunguka nchi nzima, kuhakikisha Kikwete anashinda kwa hali yoyote ile.

"Tunajua mikoa ambayo wamekwisha kwenda mpaka sasa hivi na wanachofanya huko tunakijua...hii ni sawa na ile barua tuliyoikamata hivi karibuni ikiwaelekeza watendaji wa Serikali kuhakikisha CCM inashinda uchaguzi wa mwaka huu kwa hali na mali. Tunatoa angalizo mapema lolote litakalotokea mwaka huu Rais Kikwete atabeba lawama na laana zote za Watanzania.

"Kwa hali wanayoionesha ya kuhangaika mpaka sasa Kikwete ameshashindwa. Ni kigezo tosha kuwa mpaka sasa wameshashindwa uchaguzi. Tunapenda kumwambia kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni uchaguzi wa wananchi, hakuna cha Usalama wa Taifa, hakuna cha JWTZ wala FFU, waache wananchi wafanye maamuzi juu ya nchi yao," alisema Dkt. Slaa.

Dkt. Slaa ambaye pia ni Mgombea urais wa CHADEMA katika uchaguzi wa mwaka huu, lakini jana akitumia kofia yake ya ukatibu mkuu wa chama alisema kuwa wanazo pia taarifa za kina na za uhakika kuwa kuna karatasi za bandia zinachapishwa katika moja ya nchi za nje, ili zije zitumike wakati wa uchaguzi, akidai ni mwendelezo wa mbinu chafu za kuiba kura.

Alisema chama chake na Watanzania wengi wapenda haki hawatakubali mbinu hizo chafu, akisema matumizi mabaya ya madaraka na raslimali za nchi ni aina ya ufisadi ambao CHADEMA kimekuwa kikiupiga vita tangu kilipotangaza orodha ya aibu ya watu mafisadi wapato 11 nchini.

"Wanaonesha dhahiri kuelemewa...sasa wanafanya vitendo vya kuhatarisha amani ya nchi, hawaitakii mema nchi. Tunasema amani ikivunjika Kikwete atabeba lawama, hatuwezi kukubali udikteta na ubabe huu. Kutumia raslimali za serikali na matumizi mabaya ya madaraka ni aina ya ufisadi, ndiyo maana Kikwete tulimweka katika orodha ya mafisadi."

Akiongezea katika suala hilo, Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, Bw. Freeman Mbowe alisema kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu ukivurugika, Rais Kikwete, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini watapaswa kuwajibika mbele ya Watanzania.

Bw. Mbowe alisema kuwa kuna vitendo vinavyofanywa na baadhi ya viongozi hao kwa nia ya kubeba ushindi wa CCM vinaiweka matatani dhana nzima ya demokrasia na kuonekana kiini macho, hali ambayo haiwezi kukubalika.

"Tunapenda kutoa tahadhari kwa Rais Kikwete, kwa NEC na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, yaani kwa Makame (Jaji Lewis, Mwenyekiti wa NEC) na Tendwa (John, Msajili), watu hawa watatu ndiyo wenye mamlaka ya umma na wajibu wa kutoa haki, utulivu na amani katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu.

"Bahati mbaya sana watu hawa watatu wana mikakati ya kuchakachua kura badala ya kutenda haki, wanaliandaa taifa kuchakachua kura...tunatoa angalizo kwa jamii nzima na jumuiya ya kimataifa demokrasia nchi hii ni kiinimacho. Msajili kwa makusudi anabadilisha na kuvunja sheria iliyotungwa na bunge ili kumsaidia Kikwete, halafu hakuna mtu yeyote anayejali wala kuchukuliwa hatua...huu ni uwendawazimu.

"Jana Shinyanga Kikwete kahutubia mpaka saa 1, karibu kila mahali anazidisha muda...tunataka jamii nzima na jumuiya ya kimataifa ituelewe, hawa watu wameshindwa siasa za hoja, wameshindwa siasa za aina zote za maana sasa wanajiandaa kwa siasa za uchakachuaji...mwaka huu kitaeleweka, hapatatosha pale wananchi watakapoamua kulinda maamuzi na kura zao," alisema Bw. Mbowe.

Aliongeza kuwa chama hicho kitaandaa malalamiko ya kuwayawasilisha kwa NEC na Tendwa juu ya vitendo vya kuzidisha muda.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bw. Salvatory Rweyemamu alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo jana, alisema hizi ni tuhuma za kisiasa na zinamhusu mgombea wa CCM, kwa hiyo aulizwe Meneja wa Kampeni wa chama hicho, Bw. Abdulrahaman Kinana.

Bw. Kinana hakupatikana kwenye simu yake ya mkononi ambayo mara kadhaa ilikuwa ikiita bila kupokewa.

Kuhusu suala la uteuzi wa majina ya wabunge wa viti maalumu wanawake ndani ya CHADEMA, Dkt. Slaa alijigamba kuwa chama chake kimeweka historia nchini kwa kuwa chama cha kwanza kutumia njia ya kisiasa na kisayansi kupata wabunge hao, huku akisema sheria ya uchaguzi inayolazimisha vyama vya siasa kuwasilisha majina hayo siku 30 kabla ya uchaguzi ni chanzo cha zoezi hilo kutofanyika kwa ufanisi mapema, hivyo watairekebisha wakipewa ridhaa ya kuongoza nchi.

"Njia ambayo consultant (mshauri) wetu atawaeleza vizuri imeondoa kabisa yale mawazo ya wabunge kutoka upande mmoja wa nchi, dhana ya mchezo mchafu mtu kumweka girlfriend wake, uswahiba na unafiki mwingine, hii ni kwa sababu CHADEMA tumedhamiria kuchukua dola na tunaenda kuchukua dola. Hivyo ilikuwa lazima tujipange vizuri kupata wabunge kutoka nchi nzima, maana hata katika majimbo tumesimamisha wabunge 185," alisema Dkt. Slaa.

Kwa upande wake mtaalamu mshauri aliyepewa kazi ya kuratibu utaratibu wa kuwapata wabunge wa viti maalumu, Dkt. Kitila Mkumbo alisema kuwa kwa uchanganuzi aliofanya kwa kutumia vigezo vya jumla kama vile umahiri, bidii, dhana ya uwakilishi wa wananchi kupitia wabunge wa viti maalumu na kila kanda kupata nafasi, itasaidia CHADEMA kupata wabunge makini kama ilivyokuwa katika bunge lililopita.

"Mbali ya vigezo hivyo vya jumla nilitumia vigezo vingine kwa sayansi ya takwimu ambavyo vilikuwa ni elimu, uzoefu wa uongozi kisiasa, uzoefu wa uongozi nje ya siasa, ugombea ubunge jimboni, mchango wa hali na mali katika shughuli za chama na kampeni zinazoendelea, umri katika chama, ambapo kila kigezo kilikuwa na sehemu ndogondogo tofauti ambavyo ndivyo tulitolea maksi.

"Kwa kweli kwa ukokotoaji wa vigezo hivyo CHADEMA imepata wabunge mchanganyiko wenye sifa mbalimbali kutoka karibu kila eneo la nchi katika kanda mbalimbali, kwa kweli ilikuwa lazima kuzingatia vigezo vingi kwani CHADEMA kinajiandaa kuunda serikali.

1 comment:

  1. Tamaa bila maarifa halali ni hatari kabisa kama ugonjwa wa mlipo wa Kipindupindu au uti wa mgongo...Kama hali yenyewe ndiyo hivyo basi sasa ndiyo tutaona gharama halisi ys ufisadi ni kuhatarisha hiyo amani hapa Tanzania...CCM na viongozi wake kamwe wasikimbie wajibu wa kuvunja amani ya Tanzania kwa Tamaa na kujaribu kuficha Madhambi yao kwa kung'ang'ania kukaa madarakani hata kwa njia chafu

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.