30 Sept 2010

UTITIRI WA AHADI ZA KIKWETE NI KAMA UTAMU WA PIPI HIZO ANAZOMPATIA MTOTO HUYO PICHANI.PIPI NI TAMU KADRI INAVYOYEYUKA MDOMONI LAKINI SIO TU HAIDUMU BALI HAIONDOI NJAA.

Hebu soma kwanza nukuu hii hapa chini kisha utaelewa kwanini nimeweka kichwa cha habari hicho hapo juu

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete amesema moja ya kazi kubwa itakayofanywa na serikali yake katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni kumsaidia mkulima wa Tanzania aweze kulima kwa kutumia trekta badala ya jembe la mkono.
Rais Kikwete aliyasema hayo alipokuwa akiwahutubia wakazi wa kata ya Lyabukande, jimbo la Solwa wilayani Shinyanga katika moja ya mikutano yake ya kampeni iliyofanyika jana.
“Katika miaka mitano ijayo iwapo mtatupa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi hii, tumepanga kumsaidia mkulima ili aweze kuboresha kilimo chake kwa kumwezesha kulima kwa trekta badala ya jembe la mkono alilolizoea enzi na enzi,” alieleza Rais Kikwete.
Alisema iwapo mkulima atasaidiwa katika kilimo chake, ataweza kujikomboa kutokana na umasikini na kumuwezesha kuwa na maisha bora kama ambavyo sera ya CCM inavyoelekeza.
CHANZO: Majira

Sio siri,inaudhi,inakera na inachukiza.Hivi huyu Jakaya Kikwete siye aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 2005 hadi leo hii?Ofkozi,jibu ni ndiyo.Sasa hizi habari za kusema atamsaidia mkulima kuondokana na jembe la mkono kwanini ziwe leo na sio mwaka 2005 au 2006 au 2007 au 2008 au 2009 au hata mapema mwaka huu?



Kwa kweli kama kuna Watanzania bado wanajishauri kuhusu wampigie au wamnyime kura Kikwete basi utitiri wa ahadi anazoendelea kutoa,huku nyingi zikiwa ni marejeo ya alizotoa wakati wa kampeni zake za mwaka 2005 ni sababu moja kati ya maelfu ya sababu ya kustaafisha urais kwa kumyima kura.Tena huyu hapaswi kushindwa kwa tofauti ya kura chache bali stahili yake ni kile kiitwacho anguko la pua.

Hakuna maelezo mengine zaidi ya kuamini kuwa Kikwete anawafanya Watanzania ni wapumbavu maana vinginevyo asingediriki kuongea upuuzi kama huu wa kuahidi kuwakomboa wakulima eti akipewa miaka mingine mitano ilhali hii anayomaliza ameitumia zaidi kuzurura huko nje ya nchi.Na kwa angalizo tu,huyu mtu amezowea sana kusafiri,sasa kwa vile amelazimika kukaa nchini kwa zaidi ya miezi miwili sasa basi wapiga kura mkirogwa tu kumrejesha atafanya utalii wake kwa hasira,perhaps on weekly basis badala ya monthly basis kama tulivyozowea.

Badala ya kuwaomba msamaha wakulima kwa kuwapuuza kwa muda wote aliokuwa madarakani yeye anakuja na hadithi mpya kuwa anadhamiria kuwatoa kwenye kilimo cha jembe la mkono.Hayo matrekta hewa yatanunuliwa kwa fedha zipi ilhali priority ya serikali yake ni ununuzi wa magari ya kifahari na samani za bei mbaya kwa watawala?

Na wakulima wakishapatiwa matrekta,je ziada ya mazao yao itauzwa wapi ilhali vyama vya ushirika vimeendelea kuwa taasisi maalum za kuwafisadi wakulima?Kama kweli alikuwa na nia ya kuona mkulima anaondokana na jembe la mkono kwanini basi zile fedha "zilizorejeshwa" na mafisadi wa EPA hazikutumiwa kwa dhamira hiyo?Lakini kwa kuonyesha kuwa anawazuga tu wakulima,alipotangaza "stimulus package" ya kisanii,waliopewa kipaumbele ni wafanyabiashara huku wakulima wakisahaulika.

Naomba nisiandike zaidi.Kikwete ni mbabaishaji na hana jipya.Haihitaji majini ya Sheikh Yahya kufahamu kuwa ahadi alizokwishatoa hadi sasa zinahitaji awe rais wa maisha ili atekeleze japo nusu ya ahadi hizo.Haiwezekani kutoa ahadi kila kukicha ilhali kuna lundo la ahadi zinazosubiri utekelezaji.

Chonde chonde Watanzania,kumbukeni kuwa kama Kikwete ameweza kufanya masihara katika awamu yake ya kwanza huku akijua fika kuwa mwishoni mwa awamu hiyo angesimama tena majukwaani kuomba ridhaa ya kuchaguliwa tena,pata picha awamu yake ya pili ambapo hatohitaji tena kura itakuwaje!Tafakari maneno haya kwa makini sana kwa sababu pindi mtu huyu akirejea Ikulu basi sote tumeliwa.Kidogo kilichobaki kitakombwa na kukwanguliwa kabisa.Na kwa namna ufisadi ulivyoshamiri katika awamu yake ya kwanza basi yayumkinika kubashiri kuwa pindi akichaguliwa tena (God forbid) basi si ajabu Watanzania kushtukia nchi yetu imeshauzwa na hatuna pa kwenda.

Bahati nzuri,katika uchaguzi wa mwaka huu hatuna tena tatizo lililokuwa likitukwaza hata kufikiria mbadala wa CCM.Zama hizo tulikuwa tunasema "sasa tusipoichagua CCM tukichague chama gani ilhali vyama vyenyewe ni bora ya hiyo CCM".Mwaka huu Mungu amesikiliza kilio chetu na kutupatia ufumbuzi mapemaaa.Tumeletewa Dokta Wilbroad Slaa,mwanasiasa ambaye kwa hakika amejidhihirisha bayana kuwa ana uchungu wa dhati kwa Tanzania na Watanzania.


TANZANIA BILA UFISADI INAWEZEKANA.TANZANIA BILA MAFISADI WANAOLINDWA NA KUPIGIWA KAMPENI NA KIKWETE INAWEZEKANA PIA.MPE KURA YAKO DOKTA SLAA NA MPATIE WABUNGE WA KUTOSHA WA KUUNDA SERIKALI NDOGO YA UFANISI NA YA UKOMBOZI WA MTANZANIA.

5 comments:

  1. Duh! Kikwete kafanikisha kilimo au kusafiri nje na kulinda mafisadi? Kumbe Kikwete anatuchukulia kama mataahira wasio na hata kumbukumbu! Duh! Namma hii inatisha. Kikwete kafanikiwa kujenga ufalme wake ambapo mkewe Salma, mke mdogo Rahma na mwanae Ridhiwani wamemegewa urais kiasi cha kuwa na rais mke wa rais, rais nyumba ndogo ya rais na rais mtoto wa rais kabla ya marais kama Lowassa yaani rais rafiki bila kusahau rais mshirika kama Rostam. Kazi kwenu wapiga kura hasa wabongo mnaoendelea kuteseka chini ya himaya hii fisadi na zandiki iliyosheheni wanafiki na vigeugeu kama Kakobe na Mrema.

    ReplyDelete
  2. Chahali bado nakuambia kwa herufi kubwa kuwa HATUDANGANYIKI...Imba wee mafisadi mara ahadi lakini sisi tumeona na tunakubali yaliyofanyika yamefanyika kulingana na uwezo wa nchi na rasilmali zake. Nahisi umeahidiwa cheo na serikali ya Dr. Slaa ndiyo maana unamkampenia kwa nguvu zote. Ningependa kukupa ushauri wa bure tu kuwa soma alama za nyakati, na rejea chaguzi za serikali za mitaa zilizofanyika hivi punde halafu ufanye tathmini yako.. Kama unakubali kuwa Mbuyu ulianza kama uyoga maana yake ulianzia chini ukakua hadi kuwa mbuyu, vivyohivyo matoe=keo ya chaguzi za serikali za mitaa na vitongoji ndiyo uyoga na uchaguzi mkuu ni mbuyu...je unataka kutudanganya kuwa mbuyu utageuka na kuwa mwebe?...kwa sayansi ipi???? labda ya kumwaga damu kama viongozi wako walivyojinadi majuzi.
    UTAKE USITAKE USHINDI NI WETU CCM...OYEEEEE

    ReplyDelete
  3. Laiza wewe ndiyo kioo cha washabiki wa CCM kwa sababu wanatatizo la kuelewe....Kauli ya kumwaga damu haimaanishi kuwa wanaitakia mabaya Tanzania isipokuwa michezo michafu inayofanywa na CCM ndiyo inatasababisha umwagaji damu. Ushahidi unaonesha hivyo hata nchi jirani ya Kenya kwamba mbinu hizo wanazotumia CCM na wewe Laiza ndizo zitaleta umwagaji damu..Kimsingi Tanzania kama nchi ipo katika sayari ya dunia hii...Hizi mbinu ambazo hivi sasa serikali ya CCM inafanya ndizo zilileta umwagaji damu nchi nyingine pia kaika sayari hii ya Dunia...Hivyo Dr Slaa kutamka haya kunitayazarisha matoke ya mbinu chafu hizo CCM kulazimisha kubaki madarakani....Kuhusu chaguz za serikali za mitaa ni wakati uliopita hivyo tunaongelea hivi sasa kwa sababu serikali ya CCM imethibitisha haipo tayari kutekeleza utawala wa sheria kazi yake ni kukamata na kusmubua watu wadogo na kuleta madaraja katika kuhukumu watu kwa mujibu sheria....Kuhusu Bwana Chahali kumuunga mknono Dr Slaa siyo kwa sababu ya kuahidiwa cheo kama wewe unavyofikiria...Mtanzania yeyote mwenye uchungu na utaifa wake ni lazima atashabikia kiongozi anaonesha utaifa wa kweli na siyo wa maneno kama yako wewe Laiza na haoa unaowashabikia. Uchafu na uvunjaji wa sheria umefikia kikomo...Husiogope sheria kwa sababu pengine pia wewe laiza Fisadi isipokuwa tegemea kuanzia Novemba mwaka huu kufikisha mahakamni na pia kufilisiwa kwa sheria inayotokana wazalendo wa kwweli kam Dr Slaa...Tena na mashaka na uwezo wa akili yako wewe Laiza..Ushauri wa bure nenda hospitali kafanyiwe uchunguzi wa akili yako..

    ReplyDelete
  4. Tena na tena nimewalalamikia wa-Tanzania, kuwa ni wazembe, hasa kwenye suala la elimu. CCM inaweza kutamba hivi kutokana na umbumbumbu uliokithiri miongoni mwa wa-Tanzania.

    Kwa mfano, wangekuwa si wazembe, wangesoma aliyoandika Mwalimu Nyerere kututahadharisha kuhusu CCM, na wengi wangeiogopa CCM badala ya kuikumbatia.

    Mimi ni raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa, ila daima nimeiona CCM kuwa tatizo na kikwazo kwa maendeleo ya kweli kama alivyoyafafanua Mwalimu Nyerere. Soma hapa.

    ReplyDelete
  5. Kiukweli kuna watu wana makengeza hata ya akili,yaani matatizo yameanza kwa JK tuu au toka enzi za JKN junior yalikuwepo??? hivi mbona huyu jamaa anawakera sana? chukueni hiyo!! mafisadi wote walianza kazi na Nyerere wakaja kwa Mwinyi Wakafurumuka kwa Mkapa Wameumbuka kwa Kikwete mnataka iweje??sijui kupiga debe lakini Tanzania ya 2010 ina agenda za kimaslahi fulani bahati wasomao alama za nyakati hujua mapema.sometime unaweza kumuweka baba yako mahali pa mtu ambaye unamtukana halafu mkaribishe rafiki yako amtukane kama utajisikia vizuri Hizo Siasa za MAJI TAKA.Kwetu huyaelekeza mchambawima.Jamani mlozaliwa miaka ya 80 acheni kusema,watu tuliishi 3/4 ya jehannam miaka ya JKN

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.