Showing posts with label YUSUPH MAKAMBA. Show all posts
Showing posts with label YUSUPH MAKAMBA. Show all posts

22 Jan 2011


Imagine wale vibaka wanaowanyima raha pale mtaani wasingekuwepo!

Imagine baba au mama mwenye nyumba angeheshimu mkataba mlowekeana kuhusu jengo unalopanga kwake,na kutambua kuwa kodi unayolipa ina-cover uhuru na haki zako kama mpangaji!

Imagine waandaaji wa filamu za kibongo wangezingatia zaidi uwezo na vipaji vya waigizaji badala ya maumbile au "jina kubwa" (kama sio rushwa za ngono)!

Imagine vituo vya redio vinavyojigamba kuwa vinawalenga vijana vingeachana na watangazaji vilaza wanaojifanya kuifahamu siasa (na hivyo kujipachika wadhifa wa political analysts/commentators) japo wanatambua uwezo wao ni zero,zilch,nada,sifuri,kaput!

Imagine ajira na promosheni makazini vingezingatia ujuzi na uwezo badala ya kujuana plus undugunazesheni (not forgetting rushwa za ngono)!

Imagine baadhi ya wachunga kondoo wa Bwana wangetambua kuwa wanamkasirisha Muumba kwa "kugeuza kondoo wake kuwa vitoweo vya bure" japo wakiwa madhabahuni wanakemea kwa nguvu zote ubanjuaji wa Amri ya Sita!

Imagine na sie mabloga tungejifunza kutoka kwa kampeni ya Rais Obama na,kwa hivi karibuni kabisa,Tunisia,na kuwekeza nguvu zetu katika matumizi ya social media ku-address matatizo yanayoikabili nchi badala ya hali ilivyo sasa ambapo baadhi yetu wako bize zaidi kujikomba kama sio kuripoti tu matukio (na hapa tunaweka kando wenzetu ambao wako bize zaidi na "flani kafanya hili au lile" badala ya nini kifanyike kuikomboa jamii yetu)!

Imagine vyombo vya habari vinavyoendeshwa kwa fedha za walipa kodi vingetambua kuwa kazi ya kupigia debe CCM inapaswa kuachwa kwa Uhuru,Mzalendo na Redio Uhuru pekee!

Imagine Kamati Kuu ya CCM ingekuwa na wazalendo wa kutambua kuwa hata kichaa akiporwa hawezi kumlipa aliyempora,sembuse wao watu wenye akili timamu na wenye dhamana ya kutuongoza lakini wanaendekeza ufisadi na kuhalalisha malipo kwa majambazi wa Dowans!

Imagine....Imagine...Imagine...Too much imagination

And imagine,fani ya siasa Tanzania ingeachwa kwa wenye wito,uwezo na uzalendo badala ya hali ilivyo sasa ambapo kila Tom,Dick and Harry anayeweza kununua wapiga kura anaweza kulala jambazi akaamka mbunge,kama sio waziri au mkurugenzi wa hovyo hovyo!

Na imagine ulimwengu wa siasa za Tanzania ungekuwaje laiti baadhi ya viumbe wangetambua umuhimu wa co-ordinationa kati ya ubongo na mdomo kabla ya kuropoka lolote hadharani.Kwa hakika dunia ingekuwa mahala bora sana pa kuishi laiti baadhi ya wanasiasa wasemaovyo,vichwa maji,vichwa makabati matupu,nk wasingepewa fursa ya kuongoza hata kundi la mifugo,let alone kuongoza wananchi.

Yes,dunia ingekuwa mahala bora kabisa laiti watu kama Yusuph Makamba na Tambwe Hiza wasingeruhusiwa kutamka lolote hadharani hadi itakapothibitika kuwa watakachoongea hakitazidi kuisogeza Tanzania yetu kuelekea kwenye mshikemshike kama wa huko Ivory Coast, au mahala kwingine kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Talking of Tambwe Hiza,nimeshindwa kujizuwia kupaliwa na kicheko baada ya kukutana na habari ifuatayo:

Tambwe Hiza alazwa

na Betty Kangonga

SIKU moja baada ya kumshambulia Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, kaimu katibu mkuu wa kitengo cha propaganda wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Richard Hiza, amelazwa katika Hospitali ya Regency akisumbuliwa na maradhi ya pumu.

Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu mmoja wa ndugu wa karibu ambaye hakupenda jina lake litajwe kwa kuwa si msemaji wa familia, alisema Hiza alilazwa kwa mara ya kwanza katika Hospitali ya Mbagala Kizuiani akisumbuliwa na maradhi hayo.

Alisema Hiza alizidiwa usiku wa juzi muda mfupi baada ya kurejea kutoka kazini na kukimbizwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Alisema baada ya vipimo vya kiuchunguzi Hiza alibainika kusumbuliwa pia na shinikizo la damu hivyo kulazimu kumhamishia Hospitali ya Regency kwa matibabu zaidi.

“Kwa kweli hali yake haikuwa nzuri na alikuwa hawezi kuzungumza; maana tatizo lake limemuanza ghafla sana ingawa ana tatizo la pumu kwa muda mrefu lakini tumeshangaa hali yake kuwa hivi,” alisema.

Hiza ameugua ikiwa ni siku moja tu baada ya kukaririwa na gazeti moja la kila siku siyo Tanzania Daima akidai Dk. Slaa ana wazimu, amebakiza kuvua nguo na kwamba ni mfa maji anayetapatapa.

Hiza alitoa kauli hiyo akidai kwamba Dk. Slaa ana hofu ya kufungwa kwani serikali ya CCM imepania kufanya hivyo ili kumnyamazisha.

Akitumia lugha ya matusi, Hiza alinukuliwa akisema, “Ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba kiongozi huyo amepandwa na wazimu, alichobakiza ni kuvua nguo tu…amechanganyikiwa na ndiyo maana anatapatapa kutafuta lolote la kusema.

CHANZO: Tanzania Daima
Lol!Mchimba kisima katumbukia mwenyewe kisimani.Jitu zima ovyooo!Linaropoka tu,na kujipachika udaktari wa magonjwa akili to an extent of kum-diagnose Dkt Slaa na maradhi ya akili,kumbe lenyewe lina matatizo makubwa ya afya.Msomaji mpendwa,huhitaji hata dakika moja ya kozi ya utabibu kumaizi kuwa kichaa cha kuzuzshiwa hakifui dafu kwa gonjwa la hatari kama PUMU na SHINIKIZO LA DAMU.

Naomba nisiwe mnafiki kumwombea Tambwe apate nafuu.Ndio,Biblia inatuasa kuwapenda maadui zetu lakini busara katika jamii zinatuasa pia kuwa ADUI YAKO MWOMBEE NJAA (njaa hapo symbolises mambo mabaya kama hayo yalomkuta Msema Ovyo Tambwe Hiza).

Kufungika kwa mdomo mmoja mchafu kunaifanya dunia kuwa mahala bora kabisa kuishi.Sio siri kwamba laiti maradhi yanayomkabili Tambwe yakipelekea kupunguza,kama sio kumaliza,tatizo lake la kuutumia ubongo wake kama matope,kisha kuunyima ubongo huo ushirikiano na mdomo wake,and therefore kupelekea uropokaji usiosahili hata kwenye vilabu vya gongo,siasa za Tanzania zinaweza kuchukua sura mpya.Yaani,siasa minus mbwatukaji mmoja ambaye kauli zake za ovyo ovyo ni maarufu zaidi kuliko madaraka yake.

Ndio maana nimeandika hapo juu kuwa MUNGU SI TAMBWE HIZA.Yeye anajifanya kumsemea ovyo Dokta Slaa,na kumhukumu kuwa ana kichaa,ilhali yeye Tambwe ndiye mwenye matatizo makubwa ya kiafya yanayoweza kabisa kuwa na uhusiano na tabia yake ya kuropokaropoka.

IMAGINE SIASA ZA TANZANIA MINUS UROPOKAJI WA TAMBWE HIZZA!SURELY,THAT WOULD MAKE THE WORLD SUCH A WONDERFUL PLACE TO LIVE...Lol!

15 Jan 2011


Hivi kuna uwezekano kwamba Mwenyekiti wa CCM,ambaye pia ni Rais wa Tanzania,Jakaya Kikwete,hamtakii mema Katibu Mkuu wa chama hicho,Yusuph Makamba,na ndio maana (Kikwete) hamshauri Makamba achunge kauli zake.Kwa vile wengi tunafahamu 'upole' (uzembe?) wa Kikwete katika kuwajibisha watendaji fyongo,labda anasubiri Makamba akutane na tukio la 'mchimba kisima kazama kisimani' ie kauli zake za ovyo ovyo zije kumlipukia mwenyewe.

Hebu soma kwanza stori ifuatayo,kisha tutaijadili kidogo.

Makamba amjibu Askofu Laizer
Thursday, 13 January 2011 21:07

Raymond Kaminyoge


KATIBU Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba, amesema kuwa na uelewa finyu wa biblia si jambo la ajabu kwake kwa sababu yeye siyo askofu.

Makamba aliliambia Mwananchi jana kwa simu, kuwa licha ya uelewa finyu wa biblia, lakini amekuwa akitoa vifungu hivyo kwenye biblia.
Makamba alisema hayo kufuatia, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Thomas Laizer kusema Makamba ana uelewa finyu wa biblia.

Laizer alisema hayo juzi mjini Arusha wakati wa kuwaaga watu wawili waliofariki kwa kupigwa risasi na polisi katika maandamano na Chadema yaliyofanyika Januari 5 mwaka huu.

“ Ni kweli ninauelewa finyu wa biblia kwa sababu mimi siyo askofu, hata Qurani naweza kuwa siifahamu vizuri kwa sababu mimi siyo Sheikh, ndiyo maana kila ninachozungumza kuhusu dini hizo nakariri vifungu kutoka katika vitabu hivyo,” alisema. Makamba alisema alimweleza Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kutoandamana kwa sababu serikali ilipiga marufuku maandamano hayo, wao wakapuuza.

Alimtaka Laizer kutoa tafsiri ya kitabu cha Warumi 13 sehemu ya kwanza hadi ya saba, inayosema kuwa kila mtu hana budi kutii serikali inayotawala kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu.
Alisema kwa hiyo anayepinga mamlaka inayotawala anapinga chombo kilichowekwa na Mungu na watu wanaoasi hujiletea hukumu.

“ Kwa maana watawala hawatishi watu wanaotenda mema bali wale wanaotenda maovu, kama hupendi kuishi kwa kumwogopa mwenye mamlaka basi tenda mema naye atakusifu,” alisema.

“ Laizer anieleze ufinyu wangu katika uelewa wa biblia upo wapi ikilinganisha na tukio lililotokea mkoani Arusha,” alisema.

CHANZO: Mwananchi

Sasa Makamba anaelekea kubaya.Na kama kuna watu wanamtakia mema (angalau ndani ya familia yake) ni vema wakamdhibiti mapema.

Kutumia Maandiko Matakatifu kuhalalisha maovu ni mithili ya matusi kwa waumini wa dini husika.Makamba si Mkristo,na amekiri kuwa uelewa wake wa Biblia Takatifu ni mdogo.Sasa kama ni hivyo,iweje basi aanzishe malumbano na kiongozi wa madehehebu ya Kikristo,achilia mbali kiongozi huyo kuwa ni Askofu Mkuu wa KKKT?

Makamba anaelewa vyema kuwa Maandiko Matakatifu,hayawezi kunukuliwa kwa vipande vipande.Kadhalika,uwezo wa kunukuu haumaanishi uelewa wa nukuu husika.Pia naamini Makamba anafahamu fika kuwa aya aliyotumia kuhalalisha udikteta wa CCM na polisi wake (uliopelekea mauaji ya raia wasio na hatia)haimaanishi kuwa hata mamlaka inayokandamiza watu wasio na hatia iendelee kunyenyekewa.

Kama suala la kutii mamlaka iliyo madarakani,kwanini basi hapo 1979 tulimng'oa Nduli Idi Amini ambaye wakati huo alikuwa Rais halali wa Uganda?Au kwanini basi Hitler nae alivurumishwa ilhali alikuwa kiongozi halali wa Ujerumani?Au kwanini tulisapoti harakati za mapambano dhidi ya makaburu ilhali wabaguzi hao wa rangi walitengeneza "serikali halali"?

Kwa wanaompenda Makamba,ni vema wakamshauri kuwa madaraka aliyonayo,sambamba na kuwa chini ya bosi mwenye huruma kwa wanaoboronga (ie Kikwete),visimfanye apate jeuri ya kuanzisha bifu na Watumishi wa Mungu.Ni vema pia akatambua unyeti wa kutumia Biblia kuhalalisha maovu ilhali yeye ni Muislam.Kiongozi mwenye akili timamu anapaswa kutambua hatari na madhara ya KUDHARAU MAANDIKO MATAKATIFU (kama ambavyo Makamba anavyoichezea Biblia Takatifu mithili ya Manifesto ya Uchaguzi ya CCM-iliyosheheni kila ahadi ya uongo).

Na kama Makamba mwenyewe ameshawahi kusoma blogu hii (which I doubt) basi ushauri wangu mwepesi kwake ni AACHAE KUMCHEZEA MUNGU,hata kama haamini kuwa Mungu ambaye Askofu Mkuu Lazier ni mtumishi wake,ni Mungu wake yeye Makamba.

Na kwa Kikwete,hivi lini utajaribu angalau kuwaonyesha Watanzania kuwa una uwezo japo haba wa kukemea mambo hatari?Ah,yani umekuwa hapo Ikulu kama pambo huku watendaji wako wakizidi kuhangaika kusaka moto na petroli ya kuiunguza Tanzania?

26 Dec 2010





Kwa mara ya kwanza kabisa,nalazimika kumpongeza Mbunge wa Monduli kwa tiketi ya CCM,Edward Lowassa.Tuweke kando ishu nyingine ambazo blogu hii zimepelekea kumshutumu kiongozi huyo mara kwa mara,hadi kufikia hatua ya aliyekuwa Mwandishi wake wa habari (Press Secretary),Bwana Said Nguba,kutoa comments bloguni hapa kumtetea bosi wake wa wakati huo (Lowassa).

Majuzi,Lowassa alitoa wito kwa chama chake cha CCM na Chadema wakae pamoja kutafuta mwafaka kuhusu sakata la umeya wa Arusha.Waziri Mkuu huyo wa zamani alifanya kile kiongozi yoyote anayejali maslahi ya umma anachopaswa kufanywa kwa kuweka kando itikadi za kisiasa na badala yake kutilia mkazo umuhimu wa kupata mwafaka katika sakata hilo la umeya wa Arusha.Lowassa alionya kwamba kama hatua za haraka na za makusudi hazitachukuliwa basi kuna hatari ya kuzalisha 'Ivory Coast nyingine ndani ya Tanzania yetu' akirejea hali tete inayozidi kusumbua katika taifa hilo la Afrika Magharibi baada ya Rais aliyemaliza muda wake na kushindwa uchaguzi mkuu kugoma ''kuachia ngazi".

Lakini wakati baadhi yetu tukivutiwa na uzalendo wa Lowassa,akaibuka mmoja wa wanasiasa wenye rekodi nzuri ya kubwatuka na "kusema ovyo",Katibu Mkuu wa CCM,Yusuph Makamba.Kiongozi huyo mwenye rekodi ya uropokaji alimvaa Lowassa akidai amekosea kusema aliyosema kwani hayo yalipaswa kujadiliwa kwenye vikao vya chama hicho tawala.Sina hakika kama Makambaanatumia kilevi cha aina yoyote lakini mchemsho huu wa safari hii unapaswa kuwa "wake up call" kwa (Mwenyekiti wa Taifa wa CCM),Rais Jakaya Kikwete,kwamba Makamba anastahili kupatiwa msaada wa kuchunguzwa akili yake.Ni mpuuzi asiye na mfano ambaye kwake usalama wa wakazi wa Arusha una umuhimu mdogo kulinganisha na taratibu za chama hicho tawala.Angalizo aloloyoa Lowassa kuwa Arusha inaweza kugeuka Ivory Coast halikuweza kuingia kwenye ubongo wa Makamba,sio kwa vile haelewi umuhimu wa political consensus bali kwa vile kwa akili yake nayohisi ina mapungufu kitendo cha CCM kukaa kitako na Chadema ni sawa na kuvunja Amri ya Mungu.

Mpuuzi huyu amesahau kuwa mgogoro mkubwa wa kisiasa visiwani Zanzibar ulimalizwa baada ya CCM na CUF kuweka mbele maslahi ya taifa na kukaa pamoja kutafuta mwafaka wa kudumu.Na kwa tunaokumbuka kauli za kitoto za Makamba katika nyakati tofauti za jitihada za CCM na CUF kutafuta mwafaka huko Zanzibar,yayumkinika kuamini kuwa suluhu hiyo isingepatikana laiti mwanasiasa huyo "angepewa rungu" la kupitisha maamuzi ya mwisho.

Kwa akili yenye mapungufu ya Makamba,vyama vya upinzani ni mithili ya wanyama wasiopaswa kuwepo nchini.Ni sahihi kusema kuwa laiti CCM ingekuwa ile ya Baba wa Taifa,basi Makamba asingepewa hata fursa ya kuwa Mjumbe wa Nyumba Kumi.Inakuwaje kiongozi wa kitaifa wa chama tawala haoni umuhimu wa kutafuta ufumbuzi wa haraka wa matatizo yanayoendelea huko Arusha?Haihitaji PhD ya Siasa kutambua kuwa anayemlea Makamba ni Kikwete ambaye anakiendesha chama hicho kwa mtindo wa "bora liende".Na Kikwete asipoamka kutambua kuwa CCM inazidi kujiweka mbali na wananchi,si ajabu chama hicho kichovu kikamvunjikia kabla hajamaliza muda wake hapo 2015.Mwenyekiti gani asiye na ujasiri wa kumwambia Katibu wake kuwa achunge mdomo wake?

Enewei,tuweke kando tofauti zetu na tusapoti mawazo ya busara ya Lowassa kuhusu umuhimu wa kutafuta suluhu huko Arusha.Sambamba na hilo,tumpuuze Makamba na pengine tumshauri aruhusu ubongo wake uwe na mawasiliano na mdomo wake kabla hajaropoka jambo lolote lile.

3 Sept 2010

Wenye busara zao wanatuusia kuwa pindi ukiwa unaishi kwenye nyumba ya vioo then sio wazo jema ku-entertain kurusha mawe.Mantiki ya msemo huo ni kwamba kama una ishu zenye utata katika maisha yako then sio wazo jema kuanza kushupalia ishu za watu wengi lest flani akakugeuzia kibao.

Lakini usemi huo umeonekana hauna maana kwa Katibu Mkuu wa CCM,Yusuph Makamba,ambaye kwa siku kadhaa sasa ameamua "kuvalia njuga maisha binafsi ya Dokta Wilbroad Slaa" na kuligeuza suala la ndoa ya mgombea huyo wa Chadema kuwa ajenda ya uchaguzi.

Pengine ni dharau au ujinga,Makamba alijisahau kuwa wakati anamnyooshea kidole Dkt Slaa,yeye mwenyewe (Makamba) alikuwa na doa linaloweza kabisa kumpeleka jela.Kwa mujibu wa taarifa zilizozagaa mtandaoni,Makamba anatuhumiwa kumbaka mwanafunzi wakati akiwa mwalimu mkuu wa shule moja na hatimaye kufukuzwa ualimu.

Hizi ni tuhuma nzito sana kwani licha ya kumtia doa Makamba kama mwanasiasa,ni suala linaloweza kumpeleka jela endapo victim wake atajitokeza hadharani,na kupatiwa msaada wa kisheria.Lakini tukiweka ishu za kisiasa kando,hapa kuna suala la binti asiye na hatia ambaye inadaiwa alibakwa na mtu aliyekabidhiwa dhamana ya kumpatia elimu na mwongozo katika maisha yake,mwalimu wake,lakini akaishi kubakwa.

Blogu hii inatoa ombi maalum kwa yeyote yule anayeweza kuipatia taarifa za uhakika kuhusu binti huyo anayedaiwa kubakwa na Makamba.Lengo si kumkomoa mtuhumiwa bali kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake as well as kutoa reminder kwa watu wengine wanaotumia vibaya dhamana walizokabidhiwa,iwe mashuleni,makazini au hata katika ngazi ya familia.

Je unamfahamu binti anayedaiwa kubakwa na Makamba?Kama jibu ni ndiyo basi tafadhali sana tuwasiliane kwa barua pepe kwa anuani hii [email protected].

3 Dec 2009


Sijui tuiweke CCM katika kundi gani maana kila kukicha ni songombingo moja baada ya nyingine.Of course,migongano ni jambo la kawaida kwani hata ukiweka glasi katika boksi moja zinaweza kugongana kama si kuvunjika kabisa.Ndio maana maboksi yaliyosheheni glasi huwa na tahadhari "handle with care" au "fragile".

Pengine kabla sijaendelea na mada yangu kuhusu utovu wa nidhamu unaoendelea ndani ya chama tawala CCM,huku Katibu Mkuu Yusuph Makamba akitoa kauli zisizoendana na hadhi yake katika jamii,ni vema ukasoma habari ifuatayo kisha tujadili kidogo:

Makamba awatukana wanaoshauri Kikwete asigombee 2010

Rais Kikwete kongamano la Nyerere limemweka katika lawama za kutokuwa na maamuzi na kuwa asipendekezwe kugombea awamu ya pili.

Na Leon Bahati
KATIBU mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, ambaye katika miezi ya karibuni amekuwa akihaha kutoa ufafanuzi, kukanusha au kujibu tuhuma mbalimbali dhidi ya chama hicho tawala, jana alikuwa na kazi nyingine ya kumtetea Jakaya Kikwete baada ya waziri katika serikali ya awamu ya tatu kushauri asiteuliwe kugombea urais 2010 iwapo atashindwa kufanya maamuzi magumu dhidi ya mafisadi.

Safari hii, Makamba alitumia maneno makali kumjibu waziri huyo, Matheo Qares akisema watu wenye fikra kwamba CCM inaweza kumtosa mwenyekiti wake kwenye mbio za urais wakati wa uchaguzi mkuu wa mwakani, "ni wehu".

Qares, ambaye aliwahi kushika wadhifa nyeti wa Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma, alitoa rai hiyo juzi kwenye kongamano la kumuenzi muasisi wa taifa la Tanzania aliposema kuwa CCM haina budi kutafuta mwanachama mwingine wa kugombea nafasi ya urais mwaka 2010 iwapo Kikwete atashindwa kufanya maamuzi magumu dhidi ya mafisadi, ambao alisema hawakijui chama na wengine uraia wao una utata.

Lakini jana, Makamba alisema watu wenye fikra hizo ni wehu kwa kuwa uteuzi wa wagombea ndani ya CCM ni mchakato usiotoa ruhusa kwa mawazo binafsi ya watu.

"Mtu mwenye akili nzuri hawezi kusema kwamba Rais Kikwete ameshindwa kutekeleza wajibu wake. Anayefikiria hivyo, ni mwehu," alisema Makamba alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu kauli hizo.

Alisema ni vyema watu hao wakafahamu kuwa mgombea urais wa CCM anateuliwa kwa mujibu wa taratibu za chama kupitia vikao mbalimbali hivyo, wazo binafsi halina nafasi.

Alipoulizwa kuhusu shutuma zinazoelekezwa kwa Rais Kikwete, Makamba alisema asingependa kujibu hoja zilizotolewa na mjumbe mmoja mmoja kwenye kongamano hilo.

Lakini akaeleza kwamba yupo tayari kutoa maoni yake binafsi baada ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere kuwasilisha kwake mapendekezo waliyofikia kwenye kongamano hilo.

"Mimi mwenyewe sikuwepo kwenye kongamano hilo. Wala sijui mapendekezo yao. Siwezi nikatolea maoni hoja za mtu mmoja mmoja alizotoa kwenye Kongamano hilo. Nitakapopata mapendekezo ya jumla ya taasisi hiyo, nitakawa katika nafasi nzuri ya kutoa maoni yangu."

Katika kongamano hilo, Rais Kikwete amekuwa akilaumiwa kwa kutochukua hatua dhidi ya watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi, wengi wao wakielezwa kuwa ni wafanyabiashara ambao wanatuhumiwa kukiteka chama kwa kutumia nguvu zao za pesa.

Wakati fulani Joseph Butiku, mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere ambayo iliandaa kongamano hilo, alisema Rais Kikwete amezungukwa na mafisadi ambao wanaitafuna nchi.

Akizungumza kwenye kongamano hilo juzi, Qares alisema rais hana budi kufumba macho na kuwashughulikia hao watuhumiwa ambao wanadai Kikwete hakujuana nao barabarani na kama atashindwa basi ashauriwe kuwa miaka yake mitano inamtosha.

Kabla ya Qares, Musa Nkangaa, ambaye aliwahi kuwa waziri kwenye serikali ya awamu ya pili, aliituhumu CCM kuwa imepoteza hadhi na kujikuta ikikumbatia matajiri wachafu.

Kwa mujibu wa Nkangaa, CCM imekuwa si chama cha wakulima na wafanyakazi tena, bali kimebaki kuwa chama cha matajiri.

"Ndiyo maana imekuwa ikiweweseka kuwashughulikia watuhumiwa wa Richmond na Kagoda," alisema akimaanisha kashfa ya utoaji zabuni ya ufuaji umeme wa dharura kwa Richmond Development Company LLC na tuhuma za wizi wa mabilioni ya fedha kutoka BoT.

CHANZO: Mwananchi

Tatizo kubwa la watawala wetu ni yale mazowea waliyojijengea ya kupigiwa makofi na vigeregere hata wanapoongea pumba.Ni katika mstari huohuo,kauli na mawazo mbadala huchukuliwa kuwa ni mithili ya kosa la uhaini.Sidhani kama kuna ubaya kwa wana-CCM kumpa changamoto mwenyekiti wao kama ambavyo Mtanzania yeyote mwenye mapenzi ya dhati anavyostahili haki ya kukemea mwelekeo mbovu wa nchi yetu.

Japo naafikiana na Makamba anapokumbusha wana-CCM wenzie kwamba chama hicho kikongwe kina utaratibu wake wa kumpata mgombea urais lakini hiyo sio sababu ya kuwaziba midomo wale wanaodhani mwanachama mwenzao waliyempitisha kugombea urais katika uchaguzi uliopita,na kushinda,yaani Jakaya Kikwete,ameshindwa kukidhi matarajio ya wana-CCM hao (kama Matheo Qareshi).Sio tusi kutoa mawazo kuwa flani ameshindwa hasa pale kauli kama hiyo inapoambatana na mifano hai kadhaa.

Sidhani kama Makamba anafanya hivyo kwa ile anaamini kuwa Qaresi ni mwehu (ikumbukwe Mtanzania huyo alishawahi kushika nyadhifa za juu ikiwa ni pamoja na uwaziri katika ofisi ya rais) bali ni muendelezo wa kasumba ya kujikomba.Kwa Makamba kumhukumu Qaresi kuwa ni mwehu amekwepa ujasiri wa kujadili hoja badala ya kumjadili mtu.

Ni muhimu tuwe wakweli na wawazi katika kujadili hatma ya taifa letu.Ni dhahiri kuwa vita dhidi ya ufisadi inakwamishwa na mwenye jukumu la kuchukua hatua.Hatuwezi kufanikiwa katika mapambano dhidi ya rushwa (kama yapo at all) ilhali ilishashauriwa kwamba Mkurugenzi wa TAKUKURU,Edward Hosea,ang'olewe madarakani kutokana na kuhusishwa na utapeli wa Richmond.Ushauri huo ulitolewa pia kuhusa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Johnston Mwanyika.Huwezi kuwalaumu Hosea na Mwanyika kwa vile hawakujiteua kushika nyadhifa hizo.Aliyewateua yupo na amesikia yaliyosemwa dhidi yao lakini kaamua kupuuza.

Kwa hakika kama tunataka kuiona Tanzania ikijikomboa kutoka katika lindi la umasikini unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na ufisadi,basi ni dhahiri tunahitaji kuangalia makosa yaliyofanyika mwaka 2005 na kuhakikisha hatuyarudii katika uchaguzi mkuu ujao hapo mwakani.Haya mambo ya kuangalia haiba ya mtu na pasipo kujali kama haiba hiyo inaendana na uwezo wa kazi yameshatufikisha hapa,na tukizubaa yatatupeleka pabaya zaidi,

Kinachisikitisha ni mwamko mdogo mingoni mwa Watanzania wa tabaka la kati (the middle class).Tabaka hili lina nafasi nzuri ya kuunganisha nguvu na tabaka la walalahoi ili kulibana tabaka tawala ambalo so far limeji-identify kama sehemu muhimu ya ustawi wa ufisadi na mafisadi.

Inawezekana kabla hatujachelewa.





6 Oct 2009


NILIWAHI KUBASHIRI HUKO NYUMA KWAMBA KADRI 2010 INAVYOSOGEA NDIVYO TUTAVYOZIDI KUSHUHUDIA VITUKO.LEO HII MAKAMBA NAE AMEJIUNGA KATIKA VITA DHIDI YA UFISADI!HIVI SI BINADAMU HUYU ALIYEWATAKA WATANZANIA KUACHANA NA MIJADALA YA UFISADI KWA VILE BAADHI YA WAHUSIKA WAMEFIKISHWA MAHAKAMANI?

HEBU MSIKIE ALIVYOGEUKA KINYONGA KATIKA HABARI HII HAPA CHINI:

Makamba ahimiza mapambano dhidi ya ufisadi

na Jacob Ruvilo, Kigoma

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusufu Makamba, amesema ufisadi unapaswa kupigwa vita na kila Mtanzania mzalendo, kwani umechangia kwa kiasi kikubwa kudidimia maendeleo ya nchi.

Makamba alisema hayo juzi kwenye semina ya viongozi wa CCM Jimbo la Kigoma Mjini iliyofanyika katika viwanja vya Lake Tanganyika.

Alisema suala la watu kujipatia mali kinyume cha utaratibu na kuhujumu nchi havina uhusiano wowote na CCM, kwani watuhumiwa wote hawakuagizwa na chama kufanya hivyo, bali ni hulka zao binafsi.

Makamba alifafanua kuwa suala la muumini wa dhehebu fulani kwenda kinyume na maadili au amri ya vitabu vya dini, hapaswi kulaumiwa sheikh au mchungaji, badala yake ni muumini husika ambaye mwisho wa siku ndiye atakayepata adhabu kwa Mungu.

Aidha, Makamba alisema suala la vyama vya upinzani kushika bango na kuidhihaki CCM kuwa ni mafisadi kutokana na viongozi wachache wasio waaminifu, halina maana, bali suala la umoja na mshikamano katika kupinga mafisadi hao ni jukumu la watu wote, ikiwamo CCM.

Mbali na hilo, Makamba alikemea baadhi ya viongozi wa chama hicho kutumia uwezo wao wa fedha kutoa rushwa ili kupita katika chaguzi mbalimbali kuwa ni moja ya upatikana wa viongozi mafisadi na wasiofaa kwa jamii.

Alisema Tanzania haikuandaliwa kutawaliwa na wenye nacho na kwamba hali hiyo inaweka tabaka la mwenye nacho na asiyenacho, hali ambayo isipoangaliwa kwa umakini suala la rushwa litabaki kuwa ndoto.


TATIZO LETU WATANZANIA NI UWEPESI WETU KUAMINI KILA KINACHOAHIDIWA.MWAKA 2005 MAKAMBA NA CCM YAKE WALITAMBUA HILO NA KUJA NA AHADI LUKUKI IKIWEMO ILE MAARUFU YA KULETA MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA.SASA WANASEMA KWAMBA SUALA LA MAISHA BORA LILIANZA ZAMA ZA MWALIMU NYERERE,PENGINE KATIKA KUKWEPA KUTUELEZA HAYO MAISHA BORA WALIYOAHIDI ILIKUWA NI KWA MAFISADI PEKEE AU...?MAANA KAMA SUALA HILO LILIASISIWA NA NYERERE BASI WANGETAMKA BAYANA WAKATI ZA KAMPENI ZA 2005 BADALA YA KUIFANYA KAULI-MBIU MUHIMU ILIYOWAZUGA WATANZANIA NA KUTOA USHINDI MKUBWA KWA CCM.

NI MUHIMU KWA WAPIGA KURA KUTAMBUA KUWA WANASIASA WETU WANAWEZA KUAHIDI LOLOTE ILI WAPATE KURA KAMA ILIVYOSANIFISHWA KWENYE WIMBO WA "NDIO MZEE" WA PROFESA JAY.

TUSIREJEE MAKOSA YA 2005,PLEEEEZ!

17 Sept 2009


HIZI SIO HARAKATI ZA SIASA BALI NI UTOTO.NA UTOTO HUU UNAENDELEA KWA VILE CHAMA TAWALA KINA IMANI YA KUTOSHA KUWA WANAOCHEZEWA SHERE (WAPIGA KURA) BADO WAKO USINGIZINI,NA KINACHOENDELEA (UTOTO HUO) NI SAWA NA NJOZI.

HEBU SOMA HII,KISHA TAFAKARI:

Makamba amfuata Spika Sitta Urambo, ampigia magoti

*ASEMA HANA UGOMVI NAYE, ASEMA ALIKUWA MLEZI WA NDOA ZA WANAYE

Na John Dotto, Tabora

KATIKA kile kilichoelezwa kwamba, ni kujisafisha mbele ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta, CCM imesema ipo pamoja naye katika kutekeleza majukumu yake kama Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Yusufu Makamba; ikiwa ni siku chache baada ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kuondoa utata uliotokana na maazimio ya Halmashauri Kuu ya chama hicho ulioonyesha kuwa wabunge wanaopiga kelele dhidi ya ufisadi, wanakichafua chama na serikali yake.

Akizungumza na viongozi wa CCM wilaya ya Urambo kwenye mkutano wa ndani uliohudhuriwa na Spika Sitta, Makamba, alitumia muda mwingi kumsifia Sitta kwamba ni mtu muelewa, asiyetetereka na wala kuyumbishwa na mtu yeyote na kwamba anachokifanya ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho.

Makamba aliwaambia wanaCCM hao kwamba, hana chuki na Sitta, kwani hata alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alimkaribisha katika ndoa za wanawe na akapewa nafasi ya kuzungumza kama baba mlezi, heshima ambayo alisema hataisahau katika maisha yake.

Alisema wana CCM wanatakiwa kupuuza maneno ya watu wanaodai chama kina mgogoro na Spika, kwasababu hakuna kitu kama hicho na yote anayoyatekeleza kwenye Bunge ni kwa niaba ya chama chake.

Hata hivyo, baada ya kikao cha NEC, Makamba alikuwa mstari wa mbele kudai kuwa kikao kile kina uwezo wa kumuhoji mbunge yoyote hata Sitta kama anakwenda tofauti na chama.

Makamba alinukuliwa akisema NEC ni mama na akina Spika ni watoto hivyo ina mamlaka ya kuhoji mienendo yao.

Mara baada ya kikao cha NEC, Sitta alifanya ziara mkoani Tabora na kulalamika kwamba, CCM makao makuu wamewakataza viongozi wa chama hicho mkoani kumpokea.

Hatua ya Makamba kwenda Urambo kuhutubia na Sitta, inatafsiriwa kama njia ya kuweka mambo sawa na kufuta makovu ya huko nyuma baina yake na Spika.

Kwa upande wake, Sitta alimshukuru Makamba kwa kutembelea jimboni kwake na mkoa wa Tabora kwa ujumla.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika baada ya kikao cha ndani kumalizika, Makamba aliwahakikishia wananchi wa Urambo kwamba CCM kipo pamoja na mbunge wao Sitta, ndiyo maana wanatekeleza ahadi zote ikiwemo ujenzi wa barabara ya Urambo Kaliua mpaka Tabora Mjini.

Akizungumzia suala la ufisadi, Makamba alisema kuwa wanaCCM wote kuanzia ngazi ya matawi wanapaswa kuungana na wabunge wanaopiga vita ufisadi, kwani vita dhidi ya rushwa ni ya wanaCCM wote.

Alisema anakerwa na watu wanaosema CCM ni chama cha mafisadi kwani ufisadi wa mtu mmoja si wa CCM na akatoa mfano kuwa dhambi ya Mkatoliki mmoja si dhambi ya Askofu Kilaini wala kanisa lote.

Makamba alimaliza ziara yake jana mkoani Tabora na juzi alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM wakiwemo makatibu wote wa wilaya za Tabora kwenye ukumbi wa mikutano wa CCM mkoa, aliwalaumu viongozi hao kukaa kimya wakati wapinzani wanakishambulia chama hicho kwa kukipakazia maneno machafu.

Aliwataka waamke na kukipigania chama na kuacha kukaa kimya na kusubiri makao makuu ama Makamba kujibu mashambulizi.

Baada ya kikao cha Nec kilichofanyika Dodoma mwezi uliopita, Makamba na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chilligati kwa nyakati tofauti walisema CCM imeunda kamati ya watu watatu, inayoongozwa na Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi kuwachunguza wabunge wenye tabia ya kuishambulia serikali nje ya vikao vya chama.

Habari za ndani ya kikao hicho ambazo baadaye zilivuja kwa vyombo vya habari, zilieleza kuwa Nec ilimweka kitimoto Spika Sitta kwa madai kuwa anaruhusu mijadala inayokichafua chama na serikali, huku baadhi ya wajumbe wakishinikiza anyang'anywe kadi ya CCM kwa madai kuwa anawapa uhuru bungeni watu wanaoishambulia serikali kwa ufisadi.

Hata hivyo, mwanzoni mwa wiki hii baada ya hotuba ya Rais, Chilligati alisema chama hicho hakina ugomvi wala uadui na wabunge wake wanaoongoza vita dhidi ya mafisadi nchini.

Kabla ya hapo, Mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita ambaye alisemekana kumwandama Spika Sitta katika kikao cha NEC na akamwita faru aliyejeruhiwa anayetakiwa kumalizwa kabla hajasababisha madhara zaidi, naye alibadili msimamo na kuwaunga mkono wapiganaji wa ufisadi pamoja na Spika Sitta kwamba, wanatekeleza ilani ya CCM, hivyo wanastahili kuungwa mkono.

Mabadiliko haya ya siasa ndani ya chama hiki tawala na mfululizo wa matukio ya aina hiyo likiwemo la Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile ambaye amekaririwa katika vyombo vya habari akisema hana ugomvi na Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe, anayesemekana kuwa ni hasimu wake kisiasa.

CHANZO: Mwananchi


NA HAWA NDIO TUNAOTARAJIA WAREJEE KUTUTAWALA 2010!

8 May 2009


Na Frederick Katulanda, Busanda

KAMPENI za uchaguzi za CCM katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Busanda jana zilizidi kukumbana na upinzani mkali baada ya makamu mwenyekiti wa chama hicho, Pius Msekwa na makamu mwenyekiti wa zamani, John Malecela, kujikuta wakizomewa wakati walipokuwa wakijinadi katika mkutano uliofanyika Nyarugusu wilayani Geita.

Mbali na vigogo hao wa CCM, mgombea wa chama hicho katika uchaguzi huo mdogo, Lolencia Maselle Bukwimba na mumewe, Maselle Buziku walizomewa wakati walipotambulishwa kwenye mkutano huo wa kampeni.

Tukio hilo limetokea siku moja baada ya chama hicho kujikuta kikiwa na watu wachache wakati wa kuzindua kampeni zake kwenye kata ya Kaseme, tofauti na mikutano ya vyama pinzani vya Chadema na CUF.

Dalili za hali mbaya katika mkutano huo zilianza wakati viongozi hao wakiingia eneo la Nyarugusu ambalo ni maalumu kwa wachimbaji wa dhahabu. Viongozi hao walipokelewa na alama ya vidole viwili kila walikopita. Alama ya vidole viwili hutumiwa na Chadema.

Zomea zomea hizo ziliwakabili viongozi hao wa CCM wakati walipokuwa wakimnadi mgombea wao. Hali mbaya ilianza kwa katibu mwenezi na uhamasishaji, Simon Mangelepa wakati aliposimama jukwaani na kuanza kuwatambulisha wageni walioambatana nao na kufuatiwa na mbunge wa viti maalum mkoani Mwanza, Maria Hewa ambaye alizomewa baada ya kuwaeleza wananchi kuwa wanapaswa kutulia.

Kutokana na hali hiyo mwenyekiti wa CCM mkoani Mwanza, Clement Mabina alisimama jukwaani kabla ya kumkaribisha Malecela ili amnadi mgombea wa chama hicho na kuwaeleza kuwa anazo taarifa kuwa kuna watu ambao wamepangwa hapo kwa ajili ya kuzomea, naye kuzomewa.

Baadaye ikawa zamu ya Malecela ambaye baada ya kusimama jukwaani aliwaeleza wananchi kuwa shutuma za ufisadi hazina nafasi katika kampeni kwa sasa na kuwataka wenye ushahidi wa ufisadi kuupeleka polisi, kauli ambayo iliwafanya wananchi ambao walikuwa wametulia, kuanza kuzomea wakimtaka aondoke huku wakionyesha vidole viwili.

Hata hivyo, Malecela aliwatuliza na kuwaeleza kuwa hiyo ndio njia sahihi ya kushughulikia mafisadi na kuendelea kuwaeleza wananchi kuwa iwapo wataichagua CCM katika uchaguzi huo watapatiwa umeme pamoja na kutengewa maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo.


Nataka kuwaeleza iwapo mtamchagua mgombea huyu, basi serikali italeta umeme eneo hili….na kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo," alisema lakini akakatwa kauli na kelele za wananchi ambao walisema miaka yote wameichagua CCM na kuahidiwa mambo hayo bila ya kufanikiwa.

Kutokana na hali hiyo Malecela aliamua kuwatuliza na kuomba Busanda isigeuke kama Tarime na kwamba wao CCM wanataka kampeni za amani na utulivu.

Ndipo ilipofika zamu ya Msekwa kumnadi mgombea na baada ya kupanda jukwaani alimkaribisha mgombea aliyemsimamisha mumuwe, Maselle Buziku, ambaye naye alipoeleza kuwa iwapo watamchagua mkewe atatumia nafasi yake SEDA kuhakikisha wanapata mikopo, lakini akazomewa na wananchi hao.


Hata hivyo zomea zomea hizo hazikuweza kuhatarisha amani katika mkutano huo na mgombea huyo alijieleza bila ya matatizo na kupiga magoti lakini alipoomba kura, naye akajikuta anazomewa.

Katibu mkuu wa CCM, Yusuf Makamba amekiri kuwa kuna hali ngumu kwenye Jimbo la Busanda na kuwataka viongozi wa chama hicho kupigana kufa au kupona ili kuhakikisha jimbo haliangukii mikononi mwa upinzani kwa kuwa machungu ya kushindwa Tarime anayajua.

Kauli hiyo ilitolewa na Makamba juzi mchana wakati alipokuwa akizungumza na viongozi mbalimbali wa chama hicho katika mkutano wa ndani kwenye ofisi za CCM wilayani Geita baada ya kuwasili kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni wa chama chake zilizofanyika juzi katika kata ya Kaseme.

Makamba alikiri kuwa hali ni ngumu na hivyo kuwaomba kila mmoja kuhakikisha mgombea wa CCM anashinda, akilalamika kuwa makali ya kushindwa alishayaonja Tarime.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho na kuthibitishwa na mmoja wa viongozi wa chama wilayani humo zimeeleza kuwa Makamba aliamua kufanya mkutano huo kwa lengo la kuwekana sawa kutokana na CCM kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wale walioenguliwa katika kura za maoni za kuwania kuteuliwa kuwa mgombea wa chama hicho.

Makamba amesema "jamani kushindwa ni kubaya, mwenzenu Tarime nilionja ubaya wake mpaka ilibidi nitoroshwe na Green Guard ili kuepuka kuzomewa, sasa tusiposhikamana mambo yatakuwa magumu tutoe tofauti zetu,'” alisema mmoja wa wajumbe waliokuwa kwenye kikao hicho akimnukuu Makamba.

Hata hivyo, baada ya kauli hiyo Makamba alishtuka na kuhoji iwapo walikuwemo waandishi wa habari ukumbini humo na kuonya utoaji wa taarifa hizo baada ya kujibiwa hawakuwemo.

Aidha baada ya kujibiwa kuwa hakuna waandishi Makamba alishtuka baada ya kubaini kuwa kulikuwa na mpiga picha wa chama na kumuagiza kuhakikisha mkanda huo anaukabidhi kwa katibu wa CCM wa mkoa.

Makamba alipoulizwa kuhusu suala hilo alijibu kuwa hajawahi kukiri kuwepo kwa hali ngumu kwa vile hana wasiwasi na uchaguzi huo na kusema alikuwa akieleza masuala ya kushikamana.

“Wewe unataka nikueleze mikakati yangu, kama nilikuwa nawahimiza watoto wangu kulima we unakutakia nini,” alihoji katibu huyo wa CCM alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kikao hicho.

Sambamba na hatua hiyo Makamba alimtaka mjumbe wa halmshauri kuu ya chama hicho mkoani Mwanza, Anthony Diallo kutumia uwezo wake kuhakikisha kampeni hizo zinakuwa na hamasa ya kutosha ikiwa ni pamoja na kurusha taarifa zake katika vyombo vya habari.

Uchaguzi katika jimbo la uchaguzi la Busanda umepangwa kufanyika Mei 24 kwa lengo la kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, marehemu Faustine Kabuzi Rwilombe.

Vyama vingine vinavyowania kiti hicho ni Chadema, CUF na UDP.

CHANZO: Mwananchi

WANACHOHITAJI CCM NI BUSARA ZA KI-UTU UZIMA,YAANI KUKIRI PALE WALIPOKOSEA,NA KUAHIDI KUJIREKEBISHA BADALA YA KUENDELEZA AHADI HUKU ZILE WALIZOTOA MWANZO ZIMEENDELEA KUBAKI AHADI TU PASIPO KUZITEKELEZA.WAINGEREZA WANASEMA " A PROMISE MEANS NOTHING UNTIL DELIVERED."
HALAFU HIZI KAULI ZA KIBAGUZI KUWA "ICHAGUENI CCM IWALETEE HIKI AU KILE" (AS IF AWALI ILIYOCHAGULIWA ILIKUWA CHADEMA AU CUF) NI KUWAFANYA WAPIGA KURA WAJINGA AU WASAHAULIFU.KAMA WALIKUWA NA NIA YA KULETA HUO UMEME,SI WANGEFANYA HIVYO WAKATI WAPIGA KURA WALISHAWAPA HESHIMA YA KUMCHAGUA MGOMBEA WA CCM KWENYE UCHAGUZI ULIOPITA?SASA HIZI HABARI KUWA MKITUCHAGUA TENA NDIO TUTAFANYA HIKI AU KILE NI MITHILI YA KUWAHADAA WANANCHI.
I HOPE WAPIGAKURA WA BUSANDA HAWATAISHIA KUFIKISHA UJUMBE KWA CCM KWA KUZOMEA TU BALI PIA KUINYIMA KURA ILI IKIAMSHE CHAMA HICHO KUTOKA USINGIZINI KWAMBA THIS IS 2009,AND SO FAR THE ASSESSMENT OF HOW THE PARTY HAS IMPLEMENTED ITS ELECTION MANIFESTO LEAVES A LOT TO BE DESIRED.KAMA TARIME WALIWEZA,BUSANDA PIA WANAWEZA.NA KAMA WOTE WASIORIDHIKA NA MWENENDO WA CCM WATAAMUA KUWA ENOUGH IS ENOUGH,NO MORE FALSE PROMISES,THEN CHANGE IS NOT ONLY COMING BUT WILL EVENTUALLY BE ACHIEVED.
AS OBAMA SAID,YES WE CAN IF WE BELIEVE IN CHANGE.

17 Apr 2009

KWA MUJIBU WA GAZETI LA Uhuru,KATIBU MKUU WA CCM,YUSUPH MAKAMBA,AMEAGIZA UONGOZI WA CCM NA JUMUIYA ZAKE NGAZI ZA MIKOA KUANDAA MAPAMBANO YA KUMPONGEZA JK NA SERIKALI KWA KAZI NZURI KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA RUSHWA.....
Nadhani muda si mrefu kutakuwa na tangazo jingine la kuagiza maandamano ya kupongeza mafanikio ya kutimizwa kwa ahadi ya MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA sambamba na pongezi za kuwabainisha wamiliki wa Kagoda.
CCM HOYEEEE!!!!!

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI!!!!!

That's all I can say!

Habari nyingine ndani ya gazeti hilo ni pamoja na "UFISADI MALIASILI:Sh Bil 2.4 zayeyuka kiutatanishi;Mil 790 zatumika kununua pikipiki hewa;Watumishi watimuliwa,wachunguzwa"





11 Dec 2008

Na Simon Mhina
Kada machachari wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amesema kauli ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba, kwamba mjadala juu ya mafisadi wa Akauti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ufungwe, inaashiria kuwakumbatia mafisadi. 

Mwanasiasa huyo chipukizi ambaye yupo katika kipindi cha mapambano na makada wenzake ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), kutokana na kuvuliwa uanachama kwa kupinga mradi wa Jengo Jipya la Umoja huo, alisema hatua ya Makamba kuweka mizengwe mapambano dhidi ya ufisadi inawavunja moyo watendaji wa serikali ambao wapo mstari wa mbele kushughulikia tatizo hilo. 

Nape ambaye bado ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), alisema kauli ya Makamba ni sawa na ya mtu anayeogopa kivuli chake. 

Hata hivyo, Nape katika mazungumzo na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, alisema kimsingi Makamba hana uwezo wala madaraka ya kuzuia mjadala juu ya mafisadi. 

Nape alisema ingawa hana uhusiano wowote na watu wanaopiga makelele juu ya ufisadi, lakini anafikiri wanafanya hivyo kutokana na machungu makubwa ya umasikini wanayopata Watanzania kutokana na mafisadi. 
Alihoji: ``Hivi Mzee Makamba mafisadi wakisemwa vibaya yeye anakerwa na nini? 

Hivi kinachomkera ni kipi, mafisadi waliopora fedha za wavuja jasho au wavuja jasho wanaopiga makelele juu ya mafisadi kuwaibia?`` 

Alisisitiza kuwa katika hali ya kawaida, hakuna Mtanzania ambaye atanyamazia ufisadi kutokana na uzito wake. 

Nape alihoji tena: ``Ina maana Mzee Makamba anajua idadi ya mafisadi wote nchini?`` 

Akifafanua, alisema kazi ya kuwashughulikia wahalifu hao ipo chini ya serikali na vyombo vyake vya dola na sio jambo la kisiasa. 

Wakati huo huo, Mbunge wa Moshi Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Philimon Ndesamburo, amesema chama chake `kitafunga mdomo` kuhusu ufisadi, iwapo Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, atakamatwa na kufikishwa mahakamani. 

Alisema Mkapa ni hazina kubwa ya mafisadi nchini na siku akifikishwa kortini janga hilo litakuwa limefikia tamati. 

``Chadema hatutaacha kupiga kelele juu ya ufisadi kama anavyosema Makamba hadi hapo Mkapa ambaye ni hazina ya mafisadi atakapopelekwa kortini, mambo yote yaliyofanyika yalikuwa chini ya utawala wake na alikuwa anayajua na alishiriki, lazima akamatwe,``alisema Ndesamburo. 

Mbunge huyo alisema mafisadi ndani ya CCM na serikali yake, hawajamalizika hivyo lazima waendelee kusakwa. 
Alisema asilimia 10 tu ya mafisadi wote nchini ndio wamekamatwa, lakini asilimia 90 akiwemo `baba lao` bado wapo mitaani. 

Ndesamburo alisema japokuwa Makamba amelenga kuwasaidia baadhi ya mafisadi, lakini kwa hili anatakiwa aone aibu. 

``Yaani wakati huu ambao Rais Jakaya Kikwete ameridhia watu waliokuwa mawaziri wafikishwe Mahakamani yeye anasimama kutetea ufisadi, namuomba angalau aone aibu, hata kama amelambishwa asali,`` alisema. 

Kuhusu Operesheni Sangara, Ndesamburo alisema itaendelea kwa nguvu zote licha ya Makamba kuibeza, kwa vile inalenga kuwafumbua macho Watanzania. 

Alisema operesheni hiyo si uchochezi wala nguvu ya soda, bali Makamba ametoa shutuma hizo, baada ya kushindwa kujibu hoja zinazotolewa na Chadema. 

Makamba alinukuliwa katika vyombo vya habari jana akisema kwamba mjadala wa EPA kwa sasa umefungwa kwa kuwa watuhumiwa wote wamefikishwa kortini. 

Hata hivyo, ukweli ni kwamba bado watuhumiwa wengine wakiwamo wamiliki wa Kagoda Agriculture Ltd hawajafikishwa kortini. 

CHANZO: Nipashe

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.