16 Feb 2011




Habari kutoka Dar es Salaam zinaeleza kuwa milipuko kadhaa imetokea maeneo ya Gongo la Mboto.Hata hivyo habari nyingine zinadai kuwa milipuka hiyo imetokea maeneo ya Kisarawe

Bado hakuna taarifa rasmi kuhusu eneo na chanzo cha milipuko hiyo japokuwa habari zilizopo zinadai milipuko hiyo imetokea kwenye kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Mtandao wa Jamii Forums umemnukuu Mnadhimu Mkuu wa JWTZ Brigedia Jenerali Abdulrahman Shimbo akisema "Hali ni mbaya Kikosi namba tano maghala yamelipuka ni hatari, watu wahame, maghala yako karibu karibu sana, tunaomba wananchi wahame sasa hivi, tunajitahidi kuzuia moto unaotokana na hilo unaweza kwenda mbali sana hadi Kilomota kumi, wananchi walioko karibu na maghala ya kikosi Gongo la Mboto wasogee mbali sasa hivi."

Hadi sasa hakuna taarifa kamili kuhusu idadi ya majeruhi japokuwa picha zilizotumwa na baadhi ya watumiaji wa huduma ya mtandaoni ya Twitter zinaonyesha majeruhi wakiwa katika hali mbaya



Tukio hili la kusikitisha linatokea wakati Serikali ikiwa haijaweka hadharani ripoti ya vyanzo vya milipuko iliyotokea kwenye Kambi ya JWTZ Mbagala mwezi Aprili na Mei mwaka juzi.

Wakati huo,aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Dokta Hussein Mwinyi aliahidi kuwa angewajibika iwapo ingebainika amezembea.Lakini simulizi hizo ziliishia hapo baada ya vile Serikali kupitia Wizara inayoongozwa na Mwinyi kuamua kuiweka ripoti hiyo 'kapuni'

Wakati tovuti hii inaendelea kukusanya habari za uhakika kuhusiana na milipuko hiyo ni muhimu kwa Watanzania kudai haki zao za msingi za usalama wa maisha yao na mali zao.Haiyumkiniki kuona 'intelijensia' ya vyombo vya dola ikiwa na 'ufanisi mkubwa' katika kukandamiza haki za kikatiba za wananchi lakini ikishindwa kuepusha majanga kama haya.

Upatikanaji wa taarifa sahihi unakuwa mgumu hasa kutokana na vyombo 'rasmi' vya habari nchini Tanzania kutowajibika ipasavyo kuwajulisha wananchi kinachoendelea.Tovuti zote za magazeti 'makubwa' hazina breaking news hadi wakati naweka habari hii.

(Video kwa hisani ya Dedichjr na Picha kwa hisani ya Jamii Forums)

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.