7 Mar 2011


Kwa siku kadhaa sasa kumekuwa na taarifa kuwa Mchungaji mmoja mstaafu huko Monduli,mkoani Arusha anatoa tiba ya Ukimwi kwa gharama nafuu ya shilingi 500.Inaelezwa kuwa maelfu kwa maelfu ya watu wamekuwa wakimiminika kwa Mchungaji huyo Ambilikile Mwasakile kujipatia tiba ya gonjwa hilo hatari .

Japo kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa Ukimwi unadhibitika kwa sasa kutokana na uvumbuzi wa dawa zenye ufanisi zaidi katika kudhibiti athari za ugonjwa huo,tiba rasmi haijapatikana.Hata hivyo,ukweli huu haumaanishi kuwa tiba ya Mchungaji Mwasakile ni feki kwa vile hadi sasa hakuna mtu au taasisi iliyopinga madai yake.

Pia,huwezi kuwashangaa maelfu ya watu wanaofurika kwa Mchungaji huyo kusaka tiba.Kama malaria tu inawafanya watu wakimbilie mahospitalini,sembuse waathirika wa Ukimwi!

Lakini kama kichwa cha habari kinavyohoji,ukimya wa Wizara ya Afya na serikali kwa ujumla kuhusu madai hayo unaweza kuzua zahma kama ile ya upatu maarufu wa DECI.Katika sakata hilo la "kupanda mbegu",watumishi kadhaa wa Mungu walifanikiwa kuhamasisha maelfu kwa maelfu ya Watanzania "kupanda mbegu" zao kwa matarajio ya kuvuna mamilioni.Sote tunajua kilichofuata.

Serikali ilikuwa ikifahamu uwepo wa DECI lakini haikuchukua hatua stahili (kuruhusu au kuharamisha) hadi pale ilipozinduka na kupiga marufuku upatu huo,hatua iliyowaacha wananchi lukuki wakiwa wamepoteza fedha zao "za ngama".

Sasa japo katika suala hili la tiba ya ukimwi,malipo ni shilingi 500 tu,unyeti wa suala hilo na faida au athari zake unalazimisha serikali kutoa kauli rasmi.Tunafahamu ombwe kubwa la uongozi linaloikabili serikali yetu lakini si kwa kiwango cha kushindwa kusema lolote kuhusu suala hili "dogo" japo linaloweza kuwa na athari kubwa kwa jamii.

Hivi kwa mfano tiba ya Mchungaji huyo ni feki,je hiyo haitoathiri watu wanaoweza kusitisha matibabu ya dawa za kudhibiti virusi vya Ukimwi (ARVs?Serikali yoyote yenye kujali watu wake inapaswa kutoa kauli ya mwongozo kwa wananchi wake kuhusu ukweli au uongo wa madai hayo ya kupatikana kwa tiba ya ukimwi.

Japo kujaribu kuhalalisha au kupinga madai hayo si kazi nyepesi,mazingira yafuatayo yanaweza kutoa mwanga japo kidogo:

Kwanza,katika imani za kidini,kuna uwezekano kwa binadamu kujaliwa karama za kufanya miujiza.Nadhani baadhi ya wasomaji wanafahamu kazi za watu kama Father Nkwera na yule mama wa Mikocheni (anadhani alikuwa anaitwa Esther kama sikosei).Kadhalika,wengi wetu tumesikia miujiza ya Sheikh Shariff.

Pili,kuna watu wanaoaminika kuwa na uwezo wa kutibu maradhi mbalimbali kwa kutumia tiba za asili.Katika ukoo wetu,kuna ndugu yangu mmoja ambaye amekuwa akitoa tiba za asili katika eneo la Kiberege huko Morogoro.Kila nilipokuwa namtembelea nilikuwa nashuhudia namna anavyotibu watu wenye matatizo mbalimbali,ya kiafya na kimaisha.Hata hivyo,hapo kwenye "zahanati" yake kuna tangazo kuwa yeye hana uwezo wa kutibu ukimwi.

Tatu,ni rahisi kuzusha jambo na likaaminika miongoni mwa wengi.Na kama jambo lenyewe ni habari njema basi si ajabu "waaminifu" wa awali wakasambaza habari hizo "njema" na kupelekea tetesi zisizo na ukweli kupata uaminifu.Waingereza wana msemo kwamba uongo usipokemea unaishia kupata hadhi ya kuwa ukweli.Sasa ikitokea kuwa madai ya Mchungaji huyo si ya kweli,lakini hakuna anayekanusha,basi madai hayo yanaweza kuchukua hadhi ya "ukweli".

Kinachonipa wasiwasi ni kauli ya Mchungaji Mwasakile kuwa alianza kutoa matibabu hayo mwezi Agosti mwaka jana baada ya kuoteshwa na Mungu.Kwa maana hiyo,kuna watu kadhaa ambao wanaweza kuwa mashuhuda wa ufanisi wa dawa anazotoa kwa wagonjwa wake.Kwanini habari hizo hazikufahamika hadi majuzi,inabaki kuwa muujiza kama habari yenyewe ya tiba.

Pengine unaweza kusema si rahisi mtu kutapeli kwa kutoza shilingi 500 tu.Lakini ukifanya hesabu za chap chap utagundua kuwa laiti wagonjwa 2000 tu wakilipa kiwango hicho,Mchungaji atakuwa ametengeneza shilingi milioni moja.Na kwa mujibu wa taarifa za idadi ya watu wanaoelekea kwa Mchungaji huyo,yawezekana ameshachuma shilingi milioni kadhaa hadi sasa.


Ni mapema mno kubaishiri lolote kuhusu madai hayo.Kwa upande mmoja tiba kwa nguvu za kiroho au dawa asilia inawezekana,japo sina hakika kama ukimwi nao unatibika kwa njia hizo.Lakini,again,katika Mungu yote yanawezekana.

Serikali inaweza kuwasaidia Watanzania kwa kutoa tamko rahisi kuhusu madai hayo.Na licha ya ombwe la uongozi linaloikabili serikali yetu,suala hili linaweza kuwa rahisi zaidi hasa kwa vile taarifa zinaeleza kuwa vigogo kadhaa wameonekana wakielekea kwa Mchungaji huyo kwenda kujipatia tiba.Hawa wanaweza kuwa mashuhuda wazuri katika suala hilo.


Wakati jamii inasubiri uthibitisho wa madai ya Mchungaji huyo ni vema kubaki na msimamo rasmi wa kitabibu kuwa ukimwi hauna tiba.Na kwa waliokwishapewa "tiba" ya Mchungaji huyo,ni muhimu kwao kufanya vipimo vya kitaalamu kuthibitisha kama kweli wamepona.Na kama wakipona basi iwe fundisho kwao badala ya "kurejesha libeneke kwa kasi mpya,nguvu mpya na ari mpya"

Picha zote kwa hisani ya Michuzi

Kwa habari na picha zaidi soma hapa kwa Miss Jestina

4 comments:

  1. Wajinga ndiyo waliwao. Kwa mtu kuamini kuwa kuna tiba ya ukumwi inahitaji moyo, lakini pia kuwaamini hawa manabii wa uongo ni suala lingine. Yangu macho, ipo siku ukweli utajulikana tu.

    ReplyDelete
  2. wewe jamaa acha kuoinga kila kitu maana nakuona unajifanya kila kitu uko right, kumbuka ww ni binadamu na iko cku yatakutokea yanayowatokea hao unaowasema kila cku. kama ni Deci nyingine ww kinakuuma nn? Elimika sasa kaka

    ReplyDelete
  3. Mtoa maoni usiye na ID,toa mchango wako kulingana na mada hapo juu badala ya kujisikia mdhaifu kwa kudhani mimi ninajifanya kujua sana. Hayo ni maneno yako, na kwa mtizamo wangu ni maneno ya mkosaji.Mimi kama binadamu huru ninao uhuru wa kusema mawazo yangu bila kujali itikadi, dini, rangi, elimu, ukabila nk.

    ReplyDelete
  4. Hayo yalikua ni maoni yangu kama wewe ulivyosema ndio maana ukaweka ukurasa wa maon, lakini kama sio mazuri basi unaweza kutoyapublish

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.