17 Mar 2011


"Tiba ya Babu" imeibua kila aina ya vimbwanga.Nikianza kuviorodhesha vimbwanga hivyo basi tutakesha kwani kila kukicha kuna mapya.Mara tusikie wagonjwa waliotoroka mahospitalini "wamefumaniana" na madaktari waliotorokwa na wagonjwa hao,huku wote-wagonjwa na madaktari wakiwa kwenye foleni kusbiri "tiba ya Babu"

Lakini siui kama msomaji mpendwa umebaini "mpasuko wa kimtizamo" kati ya maswahiba wawili maarufu,Rostam Aziz na Edward Lowassa.Wakati Rostam alinukuliwa akiiponda "tiba" hiyo,swahiba wake-Lowassa-sio tu alitinga kwa "Babu kupata kikombe" bali pia inaelezwa amewalipia wapiga kura wake gharama za usafiri kwenda kupata "tiba" hiyo.

Je hii ni dalili ya mwanzo ya mpasuko kati ya wanasiasa hawa ambao majina yao ni kama synonymous na ufisadi?Au wanatuzuga tu mind games?You decide

Rostam aponda tiba ya Mchungaji Loliondo
Tuesday, 15 March 2011 21:22

Shija Felician, Igunga
WAKATI Watanzania wengi wakimiminika kwenda wilayani Loliondo, mkoani Arusha kupata dawa inayodaiwa kutibu magonjwa sugu, Mbunge wa Igunga (CCM), Rostam Aziz ameibuka na kusema tiba hiyo haina lolote akidai kwamba ndugu zake watano wameitumia lakini hawajapona.

Akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara wa kuwashukuru wapigakura uliofanyika kwenye Viwanja vya CCM wilayani Igunga, Tabora mbunge huyo alisema haiamini dawa hiyo kwa kuwa ana ushahidi kwa ndugu zake hao ambao anadai kwamba wanaendelea kuugua kisukari licha ya kutumia dawa hiyo siku saba zilizopita.

Aliwataka wale watakaokwenda Loliondo ambao wanatumia dawa za hospitalini kuendelea kuzitumia badala ya kuzipuuza na kuzitupa... “Ndugu zangu wananchi wa Igunga, mimi mjomba wangu Hassan mnamfahamu karibu wote hapa mjini ni mgonjwa wa siku nyingi wa kisukari. Ameshakunywa dawa hiyo lakini mpaka sasa ni mgonjwa kama mnavyomuona sasa hiyo dawa inaponyesha nani?”

Hata hivyo, aliwataka wananchi wote wenye imani juu ya dawa hiyo waende huku akiwasisitizia kutopuuza ushauri wa madaktari kwani.

Wakati Rostam akipinga dawa hiyo, wilayani Kahama, mamia ya wafanyabiashara wamefunga shughuli zao na kukimbilia Loliondo kwa Mchungaji Mwasapile kunywa dawa hiyo huku baadhi ya waliorejea baada ya kuinywa wakidai kuwa hali zao sasa ni nzuri.

Wafanyabiashara hao wengi wao wanaondoka kwa siri wakidai wanakwenda Dar es Salaam katika shughuli zao, lakini siri imefichuka baada ya baadhi yao kuoneka katika runinga wakiwa katika foleni wakisubiri kupatiwa huduma hiyo.

Mbali ya kuzungumzia suala hilo la tiba ambalo limegusa hisia za wananchi wengi wa Afrika Mashariki, mbunge huyo aliwapa pole wananchi wa Igunga ambao nyumba zao zimeezuliwa na upepo uliosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha wiki iliyopita ambazo ziliathiri kaya 19. Aitoa msaada wa Sh500,000 kwa kila kaya iliyokumbwa na maafa hayo.
CHANZO: Mwananchi

Lowassa apata kikombe Loliondo
Tuesday, 15 March 2011 23:47

Waandishi Wetu

WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa juzi alipata tiba ya magonjwa sugu inayotolewa na Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile katika Kijiji cha Samunge, Tarafa ya Sale, Loliondo, mkoani Arusha.Lowassa alifika katika eneo hilo mchana akiwa na viongozi kadhaa wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na Serikali kisha kupata kikombe kimoja chenye dawa kinachotolewa na mchungaji huyo kwa ajili ya tiba.

Tofauti na viongozi wengine, Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli (CCM), Jimbo linalopakana na Kijiji cha Samunge, alikwenda huko akiwa na viongozi mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini na baadhi ya wapigakura wake.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Lowassa alithibitisha kwenda Loliondo na kuwataja viongozi wa dini alioambatana nao katika msafara wake kuwa ni Askofu Msaidizi wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini, Dk Frederick Shoo na Mkuu wa Jimbo la Masai Kaskazini, Dayosisi ya Kaskazini Kati (Arusha), Mchungaji John Nangole.

Katika ramani ya utendaji kazi ya KKKT, Jimbo la Masai Kaskazini ndipo kilipo Kijiji cha Samunge ambako ni makazi ya Mchungaji Mwasapile.“Ni kweli, nimekwenda pale na wapigakura wangu pamoja na viongozi wa dini, Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dk Shoo na Mkuu wa Jimbo la Masai Kaskazini, Mchungaji Nangole,” alisema Lowassa na kuuliza: “Kwani hiyo nayo ni habari jamani?”

Baada ya Lowassa kufika katika kijiji hicho akiwa na ujumbe wake, aliongoza moja kwa moja hadi kwa Mchungaji Mwasapile na kuzungumza naye kisha akapata kikombe cha tiba na kuondoka.

Kabla ya Lowassa kwenda kupata tiba, amekuwa akitoa msaada wa nauli kwa wagonjwa mbalimbali wa jimbo lake kwenda kwa mchungaji huyo ambaye dawa yake inadaiwa kutibu magonjwa ya saratani, kisukari, pumu, shinikizo la damu na Ukimwi.Lowassa ni miongoni mwa wanasiasa maarufu nchini ambao wameshafika kwa mchungaji huyo kupata tiba hiyo wakiwamo mawaziri, naibu mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya.
CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.