12 Apr 2011


Nimekumbana na habari ifuatayo katika gazeti la Tanzania Daima ambapo inaelezwa kuwa mwekezaji mmoja mwenye asili ya Kiasia amemchoma moto mwanamke mmoja kwa kosa la kuingia hotelini mwa mwekezaji husika bila kulipa kiingilio.

Kinachojidhihirisha katika habari husika ni dalili kwamba jeshi la pilisi linasuasua kumtendea haki mwananchi huyo.Nimewasiliana na bloga mwenzangu ambaye pia ni mwandishi mwandamizi wa gazeti moja la jamii huko nyumbani kumwomba tushirikiane kulipigia kele suala hili hadi haki ya mwananchi mwenzetu ipatikane.Kwa sie Watanzania tulio nje tunashuhudia namna raia wa nchi za wenzetu wanavyothaminiwa na sheria zao lakini kwetu ni hadithi tofauti hususan linapokuja suala la hao wanaoitwa wawekezaji.

Uwezo wa kifedha isiwe sababu ya kunyanyasa wananchi wasio na uwezo.Natoa wito kwa kila Mtanzania atakayeguswa na habari hii kuchangia kwa namna moja au nyingine kudai haki itendeke na ikiwezekan mwekezaji husika atimuliwe kabisa nchini.Hatuhitaji wababaishaji wanaoifanya nchi yetu kama pori lisilo na sheria.

Habari husika ni hii:

Mwekezaji amchoma moto raia Darna Hellen Ngoromera
RAIA wa Kiasia anayehusishwa kumiliki hoteli moja maarufu iliyopo Kigamboni anadaiwa kumjeruhi kwa kumchoma moto mkazi wa Mjimwema, Lila Hussein (25), baada kuingia hotelini hapo bila kulipa kiingilio.

Akizungumza na Tanzania Daima jana, ndugu wa majeruhi huyo, Abdullah Saiwaad,alisema tukio hilo lilitokea Jumamosi majira kati ya saa 5:00 na 6:00 usiku.

Alisema kabla ya kuchomwa moto, Lila ambaye amelazwa wodi namba 7 katika Hospitali ya Temeke akiwa hajitambui, alivuliwa nguo kisha kumwagiwa mafuta ya petroli na kwamba amejeruhiwa vibaya kuanzia sehemu za magotini hadi shingoni.

Alisema chanzo cha tukio hilo ni Lila kuingia kwenye muziki hotelini hapo bila kulipa kiingilio.

“Hali ni tete, Lila yupo hospitali ya Temeke akipigania maisha yake baada ya kuchomwa moto na mhindi ambaye ni mmiliki wa hoteli ya South Beach, ameungua vibaya tunamwomba Mungu anusuru maisha yake,” alisema Saiwaad.

Alisema baadaye aliokolewa na wafanyakazi wawili baada ya kuamua kupeleka taarifa kijijini Mjimwema.

Kutokana na tukio hilo wanakijiji wametishia kuchoma moto hoteli hiyo na kwamba hali hiyo imesababisha mkuu wa kituo cha Kigamboni kupeleka askari wa doria kusimamia usalama hotelini hapo.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Davis Misime, alikiri kuwepo kwa taarifa hizo na kuahidi kuzifuatilia kwa kina.

Kwa mujibu wa Misime, usiku askari walipata taarifa kuwa kuna mtu amechomwa moto hotelini hapo ndipo walipokwenda na kumchukua majeruhi na kumpeleka katika kituo cha afya Kigamboni kisha baadaye kupelekwa Temeke.

Hata hivyo, habari zinapasha zaidi kwamba baadaye jioni ya jana, Lila alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutokana na hali yake kuwa mbaya.

CHANZO: Tanzania Daima

1 comment:

  1. Mbona ndiyo zao hawa wahindi! wabaguzi wa rangi, tena ndani ya nchi yetu wenyewe.Mtikila hakukosea kuwaita magabachori!

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube