30 Apr 2011Kuna wapuuzi wanajaribu kutuminisha usanii unaoitwa "kujivua magamba" kwa chama tawala CCM kilichozaa serikali iliyopo madarakani.Lakini hata tukiweka kando ukweli kwamba nyoka anayejivua magamba anakuwa hatari zaidi kuliko awali,porojo hizi za kuchefua za CCM ni miongoni tu mwa jitihada zake kuwapumbaza Watanzania kuhusu matatizo ya msingi yanayotishia uhai wa taifa letu.

Wakati akili za Watanzania zimeelekezwa Samunge "kwa Babu wa Loliondo" na "magamba" ya akina Lowassa,Chenge na Rostam,mafisadi wanaitumia vizuri nafasi hiyo kubaka uchumi wetu kwa kasi ya kimbunga.Hebu angalia habari zifuatazo ambazo ni mwendelezo tu wa mkakati wa kuiflisi Tanzania yetu.

CAG abaini ufisadi wa Sh50 bilioni serikalini

Saturday, 30 April 2011 10:00

Boniface Meena

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amebaini ufisadi wa Sh50.6 bilioni serikalini ukiwamo wa malipo yanayotia shaka ya Sh15.7 bilioni katika kipindi cha mwaka wa fedha 2009/2010.

Katika ripoti yake ya ukaguzi iliyoishia Juni, 30, 2010, CAG amesema fedha nyingi zilitumika kufanya ununuzi bila kufuata taratibu.

Katika ripoti yake, amesema wizara, idara, wakala na sekretarieti za mikoa, zilitumia fedha katika kipindi cha mwaka 2009/2010 kufanya ununuzi ambao haukuwa kwenye mpango wa mwaka.

Alisema matumizi hayo ni kinyume cha kifungu cha 45 cha Sheria ya Ununuzi ya Umma ya mwaka 2004 kinachozitaka taasisi za ununuzi kuweka mpango wa mwaka kwa lengo la kuepuka ununuzi wa dharura, kupata thamani ya fedha, kupunguza gharama za matumizi na kufanya ununuzi sahihi kwa njia ya kandarasi.

"Ukaguzi umebainisha kwamba katika mwaka wa fedha 2009/2010, taasisi zilizoonyeshwa hapa chini zilifanya ununuzi yenye thamani ya Sh50.6 bila kufuata kifungu cha sheria," imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya fedha hizo, Sh650.7 milioni zilitumika katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, kununulia samani kwa maofisa wanaoishi katika nyumba binafsi

Wizara nyingine ni Nishati na Madini, Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Maliasili na Utalii, Habari, Vijana na Michezo na Tume ya kurekebisha Sheria.

"Ununuzi wa samani kwa maofisa hao ulikuwa si sawa kwa kuwa hawana stahili ya kununuliwa vitu hivyo na ni kinyume cha waraka wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma (Utumishi) Na. C/CA/134/213/01/G/69 wa Januari 30, 2006, unaohusu malipo ya posho ya nyumba na ununuzi wa samani kwa nyumba za Serikali kwa maofisa wenye stahili," imesema ripoti hiyo.

CAG ameeleza pia kuwa eneo jingine ambalo fedha hizo zimetumika vibaya ni matengenezo ya magari ya serikali na taasisi zake ambako Jumla ya Sh176.7 milioni zimeliwa.

Alisema wakati kanuni ya 5 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma (mali, kazi, huduma zisizo za ushauri na uuzaji wa mali ya umma kwa zabuni) ya mwaka 2005, ikitaka wizara, idara, wakala na sekretarieti za mikoa kutengeneza magari yake Temesa (Wakala wa Ufundi na Umeme), au kupeleka katika karakana zilizoidhinishwa na wakala huyo, magari mengi yalikuwa yanatengenezwa kwenye karakana binafsi.

"Magari hayo yametengezwa kwenye karakana hizo bila kuwa na kibali kutoka Temesa kama sheria inavyotaka."

CAG amebaini pia kuwa serikali na taasisi zake imetumia Sh13.8 bilioni kulipia mali na vifaa ambavyo hata hivyo, havikupokewa au vilipokewa pungufu.

"Hii ni kinyume na kanuni ya 122 ya kanuni za Ununuzi ya Umma (mali, kazi, huduma zisizo za ushauri na uuzaji wa mali ya umma kwa zabuni) ya mwaka 2005," alisema.

Taarifa hiyo ilisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2009/2010, wizara, idara, sekretarieti za mikoa mitatu zilifanya malipo yenye shaka yanayofikia Sh15.7 bilioni.

Malipo hayo yalikosa viambatanisho ambavyo vingeonyesha taarifa za kina pasipo kuacha shaka yoyote kuhusiana na usahihi wa malipo hayo.

CHANZO: Mwananchi

Mamilioni yafujwa Mambo ya Nje

na Mwandishi wetu

WIZARA Ya Mambo ya Nje na Ushirikinao wa Kimataifa imegumbikwa na ufisadi mkubwa wa upotevu wa mamilioni ya dola katika ubalozi wake wa heshima nchini Israel na ubalozi wa Marekani.

Imebainika kuwa dola za Marekani milioni 615 zimeyeyuka katika ubalozi wake Israel na hivyo jana kuifanya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kumuweka kiti moto Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Hayo yalibainika jana katika kikao cha pamoja cha Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), kilichoketi chini ya mwenyekiti wake, John Cheyo, ambaye alihoji matumizi ya fedha hizo ambayo yalipingana na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Cheyo, alisema mwaka 2008/2009 imeonekana katika ubalozi huo kupotea kwa kiasi hicho cha fedha hasa katika utoaji wa viza na kutotolewa risiti kwa wahusika.

“Hapa inaonyesha Balozi wa heshima Madam Rinit Hershkovity wa Israel alitumia fedha za serikali vibaya na kamati yetu inahitaji kupata maelezo ya kina inakuaje kiasi cha dola milioni 615 za Marekani kupotea katika mazingira ya kutatanisha.”

“Hii kamati si ya kuchezea hasa katika kudai matumizi ya fedha za walipa kodi wa nchi hii sasa tunahitaji majibu mazuri na hatua zilizochukuliwa juu ya mtu huyu aliyefanya ufisadi wa aina hii,” alisema Cheyo.

Akijibu maswali hayo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya nje na ushirikiano wa Kimataifa, John Haule, alisema serikali ilipogundua ubadhirifu huo ililazimika kuufunga ubalozi huo toka Februari 2, mwaka 2009 na kumtaka balozi huyo kurejesha fedha hizo.

Haule, alisema kwa kuwa yeye ni mgeni katika wizara hiyo amegundua kukabiliwa na changamoto ya kuweka mahesabu sawa ikiwemo kupambana na matumizi mabaya ya fedha za umma.

“Mwenyekiti mimi ni mgeni toka niripoti wizarani; nina siku 21, lakini hivi sasa tumefanikiwa kuufunga ubalozi wa heshima wa Israel; hata hivyo bado ninakiri kuwa nina kazi ya kurekebisha mifumo ya fedha na utendaji wa kazi,” alisema Haule.

Majibu hayo ya Katibu Mkuu Haule, yalimuinua Mbunge wa Kibiti, Abdul Marombwa (CCM), ambaye alitaka kufahamua matumizi ya kiasi cha cha dola za Marekani 7,600,000 zilizotolewa kwa ajili ya kununua jengo la ghorofa sita nchini Marekani kwa kiasi cha dola 10.4 milioni.

Alisema ripoti ya watalaamu ilionyesha kuwa badala ya kufanya kazi hiyo wizara iliagiza kutumika kiasi cha dola milioni 151.0 huku kukiwa hakuna haja ya kufanya hivyo.

“Ripoti hiyo ilibainisha kazi iliyofanyika sio ukarabati bali ni kukata vyumba… sasa kwa hili tunahitaji maelezo ya kina, na hatua zote hizo hakuna kibali kilichothibitisha matumizi ya fedha hizo wala uhalali wa matumizi hayo,” alisema Marombwa.

Hata hivyo hali hiyo ilimfanya katibu mkuu wa wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa kumwachia naibu katibu Mkuu wake kutoa maelezo ya kina kwa kamati hiyo ambaye alisema kuwa hivi sasa wanalazimika kuzifunga balozi nyingi za heshima kutokana kutokuwepo udhibiti.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inaonyesha kuwa zaidi ya euro 144,202 hazijalipwa kwa mujibu wa jalada namba TZBR/A.20/11 la Agosti 26, 2009 na kuonyesha kuwa deni hilo bado halijalipwa hadi sasa.

Balozi ambazo zimekumbwa na upotevu wa fedha na kuthibitishwa na CAG ambazo hadi sasa hazijatoa maelezo ya kina kuhusu matumizi yake ni pamoja na Italia waliotakiwa kurejesha kiasi cha sh 6,060,519.00 ambapo wahusika walitakiwa kufanya hivyo.

Mbali na upotevu wa fedha hizo kati ya mwaka 2007/2008 ubalozi ulitakiwa kuwasilisha kibali cha ukaguzi na kufanya matuzi ya sh 517,741,802 zilizotumika kinyume cha sheria


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube