1 May 2011Ansbert Ngurumo

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinajitapa kwamba kinajivua gamba. Lakini sasa imeanza kudhihirika kwamba badala ya kujivua gamba kinajichuna ngozi. Kitakufa!

Bahati mbaya, kama baadhi yetu tulivyowahi kuandika huko nyuma, CCM kinashindwa kuwaaminisha watu wenye akili timamu kwamba kikiwafukuza ujumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu watu watatu – Andrew Chenge, Edward Lowassa na Rostam Azizi – kitakuwa safi. Kinajidanganya!

Taarifa zinaonyesha kuwa wanaoshabikia igizo hili la kujivua gamba ni Mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, na kundi linalofuata mkumbo kwa unafiki na woga.

Lakini wapo wana CCM wengi wenye akili timamu, na wananchi wengine, wanaosema wazi kwamba hata hao watatu wakiondoka, CCM haiwezi kuwa safi tena. Wala haitamsaidia Rais Kikwete kuonekana mwema kwa Watanzania. Na haitakifanya chama hicho kirejeshe mng’aro wake kwa umma.

Ni wazi, jitihada za Rais Kikwete na wenzake zinatokana na ukweli unaomuuma yeye binafsi kutokana na CCM kufanya vibaya katika uchaguzi mkuu uliopita.

Na ingawa kuna ukweli kwamba ufisadi umechangia kukifanya CCM kichukiwe na wananchi, hoja hiyo haiishii kwa watatu hawa. Mafisadi CCM ni wengi. Nimesema huko nyuma, kwamba hata Rais Kikwete mwenyewe, alitajwa kuwa miongoni mwao.

Hata jana alitajwa upya katika mkutano wa Mchungaji Christopher Mtikila na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, akimhusisha rais na utajiri wa ghafla wa mtoto wake.

Ufisadi huu wa rais unamnyima makali ya kuwashughulikia mafisadi wenzake. Na zaidi ya hayo unapanua wigo wa adui zake, maana sasa anagombana na watu wanaomfahamu vema; waliomsaidia na kumjenga, wakambeba hadi Ikulu.

Woga wake ni kwamba baadhi ya hawa waliombeba hadi Ikulu wana uwezo wa kutumia nguvu zile zile kumwondoa ama Ikulu au kwenye chama. Anachofanya sasa ni kuwashughulikia mapema ili kujinusuru.

Lakini nina hakika jitihada hizi hazitakinusuru chama chake. Na ingawa ameaminishwa kwamba mafisadi hawa ndio waliokifanya chama chake “kishindwe” uchaguzi mwaka jana, wapo wanaosema yale asiyotaka kusikia.

Anajiuliza zilikokwenda kura zake mwaka 2010, anapolinganisha na mwamko wa 2005. Anatafuta wachawi, lakini anasahau mambo kadhaa.

Kwa mfano, serikali imeshindwa kukidhi matakwa ya wananchi kama ilivyoahidi mwaka 2005. Kwa nini waipe CCM kura nyingi hata kama inawahonga mashati, kanga, kofia, pesa na pombe?

Wananchi walimsikia Rais Kikwete mwenyewe akiwaambia wafanyakazi ”sitaki kura zenu!” Wengi walikuwa waaminifu kwa kauli yake; wakamnyima. Si wao tu, bali hata rafiki zao, ndugu zao na wajuani wao, walikaa upande wa wafanyakazi. Kwa nini atarajie kura za CCM ziongezeke?

Mara kadhaa, Rais Kikwete alijikuta akigombana na baadhi ya viongozi wa dini kubwa zenye ushawishi kwa umma. Aliwadanganya Waislamu kuhusu Ofisi ya Kadhi Mkuu. Wamedai hadi wakakata tamaa. Hatimaye akawapatia ufumbuzi usioendana na ahadi yake. Wana sababu ya kumwamini na kumpa kura nyingi?

Serikali yake, kupitia kwa wasaidizi na washauri wake kadhaa, na hata yeye binafsi, ilijiingiza katika mzozo usio wa lazima na madhehebu kadhaa ya Wakristo, ikikerwa na jitihada zao za kukuza elimu ya uraia, na kuwahamasisha kuchagua viongozi waadilifu.

Sasa kama alikerwa na kampeni ya kuchagua viongozi waadilifu, tutamwaminije leo katika vita dhidi ya ufisadi? Na anapata wapi ujasiri wa kupiga vita mafisadi wale wale ambao alifika kwenye majimbo yao akawamwagia sifa na kuwanyanyua mikono kuwaombea kura?

Na kumbukumbu zinaonyesha kwamba katika wote, kama tunarejea ile orodha ya mafisadi ya awali (ambamo naye yumo), walishinda wote isipokuwa mmoja – Basil Mramba.

Zaidi ya hayo, walishinda wa kura nyingi. Maana yake ni kwamba wanakubalika katika majimbo yao, na hata nguvu yao inapenya katika vikao vya juu vya chama.

Ndiyo maana baadhi yao (kwa mfano Lowassa) wamefanikiwa hata kupata uongozi katika kamati za Bunge. Anajua nguvu yao ya ushawishi. Ndiyo inayomtisha.

Zaidi ya hayo, CCM kimetumia mabilioni ya shilingi kwa ajili ya “kununulia kura,” kinyume kabisa cha sheria ya gharama za uchaguzi. Ni mbunge gani wa CCM anaweza kujitapa kuwa amepita bila nguvu za ufisadi? Sasa rais na wenzake wanapiga vita ufisadi gani wakati wenyewe wamepita kifisadi, na chama kimejaa wabunge waliopita kifisadi?

Ndiyo maana sisi wengine tunakwenda mbali. Tunasema katika igizo la sasa la kujivua gamba, Rais Kikwete na wenzake, kama wana ujasiri wa kutosha, wasiishie tu kuwafukuza kwenye vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu.

Wawavue na ubunge. Wapoteze kila kitu. Tuanze upya. CCM igombee majimbo hayo bila nguvu ya rushwa. Je, CCM ina ujasiri huo?

Wapo wanaodokeza pia kwamba hata udhaifu binafsi wa rais kiafya ulichangia kupunguza imani na matumaini ya watu. Kwa mfano, madaktari wake walijaribu kufunika funika kwa taarifa zenye utata, lakini walishindwa kumzuia kuanguka hadharani mara kadhaa. Wanadhani hiyo ilikuwa mbinu ya kumwongezea kura?

Hizi ni chache tu, lakini zipo sababu nyingi za kuanguka kwa CCM katika uchaguzi uliopita. Hata maisha magumu yanayowakabili wananchi sasa hivi, ni kigezo kingine cha kuwahamasisha wananchi waichukie serikali na chama chake.

Ndiyo maana wenye akili wanapotazama kampeni hii ya kuvuana magamba wanasema bila woga kwamba tatizo la CCM si watu fulani, bali mfumo. Chama kimejikita katika mfumo wa ufisadi, kinaongoza kwa mazoea, kinakumbatia udikteta wa rais na mwenyekiti, na kinaogopa mabadiliko.

Mtu mmoja amenidokeza kwamba haikuwa kwa bahati mbaya Pius Msekwa kuteuliwa makamu mwenyekiti wa CCM. Ni Msekwa huyu aliyekuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa CCM mwaka 1977.

CCM haina muono mpya, au damu mpya za kushika nafasi ya Msekwa katika chama? Maana yake ni kwamba CCM iko nyuma ya wakati kwa miaka 34.

Hii ndiyo CCM inayoshabikiwa na kina Nape waliozaliwa ndani ya kipindi cha u-CCM wa Msekwa?

Ndiyo maana wanashindwa kujivua gamba, maana wao wenyewe ni magamba manene yaliyoshikamana na nyama za chama. Wakidiriki kuyavua, wataondoka na mnofu wa CCM.

Lakini hili haliwezekani kwa sababu CCM bila ufisadi, haiwezi kudumu. Ninachoona ni kwamba, ingawa wanaogopa kujichuna ngozi ili wasife, jitihada wanazofanya sasa ni sawa na kunywa sumu kali ambayo haiwezi kuwaepusha na mauti ya kisiasa. Wanalijua hilo?


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.