Showing posts with label Ansbert Ngurumo. Show all posts
Showing posts with label Ansbert Ngurumo. Show all posts

16 May 2011


Wasaidizi wana nafuu kuliko rais?

Ansbert Ngurumo

BAADHI yetu hatujaelewa ari, nguvu na kasi ya Rais Jakaya Kikwete. Nina hakika naye ameiimba, lakini hajaielewa barabara.

Kaulimbiu hii iliyoasisiwa na kina Samuel Sitta mwaka 2005, ilitumika kumtafutia urais mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete, kwa ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya.

Waliomjua vema uwezo na udhaifu wake walidokeza mapema kwamba maisha ya Watanzania chini ya CCM ya Kikwete yangedorora na kuwa magumu zaidi - kwa ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya.

Baadaye, sisi na baadhi ya watani wa CCM tuliifupisha kaulimbiu hiyo, tukaiita ANGUKA. Ni kweli! Miaka mitano baadaye, wameangukia pua.

CCM imeanguka. Rais Kikwete ameanguka. Mtandao wake umeanguka. Na kwa bahati mbaya, hata serikali yake imeanguka, ikaishia kuwa serikali kopa-kopa – hata mishahara ya watumishi – licha ya kodi kubwa tunazolipa.

Kuanguka huku, ndiko kumekuwa chanzo cha kura chache za mgombea urais wa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Kuanguka huku ndiko kumekuwa kichocheo cha vilio vya wananchi dhidi ya ufisadi. Kuanguka huku ndiko kumesababisha hata usanii mpya wa CCM wa ‘kujivua gamba.’

Kuanguka huku ndiko kumemkosanisha Rais Kikwete na maswahiba wake wa siku nyingi. Kuanguka huku ndiko kumemfanya Rais Kikwete aogope maandamano ya wananchi yanayoratibiwa na CHADEMA hata akalialia kwamba “wanataka kuniondoa kabla ya wakati.”

Kuanguka huku ndiko kumemwondoa Yusuf Makamba katika ukatibu mkuu wa CCM, yeye na sekretariati na Kamati Kuu. Kuanguka huku ndiko kumerutubisha na kukuza fitina na vita ya makundi ndani ya CCM.

Kuanguka huku ndiko kumewafanya Watanzania kuikataa CCM waziwazi kuliko wakati wote katika historia, na ndiko kumemwingiza Nape Nnauye (Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM) katika migogoro mipya ndani ya makundi ya CCM na kumwandalia anguko lake huko tunakokwenda, hasa baada ya Rais Kikwete kuondoka madarakani.

Anguko hili la ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya limewagusa wananchi wenyewe. Sasa wanakabiliwa na ukali wa maisha usiofanana kabisa na ahadi kemkemu walizopewa na CCM mwaka 2005 na 2010.

Bahati mbaya waliosababisha anguko hili, bado wanajitapa kwamba wameleta maendeleo. Vipofu!

Na kwa sababu ya upofu huu, wanakosa mikakati mipya ya kujikwamua. Wanarudiarudia yale yale yaliyoshindwa kuwanusuru miaka mitano iliyopita.

Kwa mfano, mwaka 2006 mwanzoni, Rais Kikwete aliingia na mbinu ya kutembelea wizara moja moja, kutoa maelekezo na kupiga picha na watumishi wa wizara hizo. Ilikuwa propaganda na mapambo ya magazeti na televisheni.

Baadaye, aliwaita mawaziri na watumishi waandamizi wa serikali (mara mbili) katika semina elekezi kwenye Hoteli ya kifahari, Ngurdoto, Arusha.

Leo tunapotazama nyuma, ni nani anaweza kujivunia semina elekezi za Ngurdoto?

Lakini watu wasiojifunza hawafichiki. Mwaka jana, rais yule yule akagombea kwa kaulimbiu ya ari zaidi, kasi zaidi na nguvu zaidi. Yaani, hawa jamaa hawakuridhika na ’anguko jipya’ la 2006. Waliona hilo halitoshi, wakatuandaa “kuanguka zaidi” mwaka 2010!

Haikumwongezea kura mgombea wao. Haikuvuta hisia za vijana wala kina mama. Ili kupata watu wa kuhutubia ilibidi CCM itumie pesa nyingi kuchapisha na kugawa sare, kuwagawia watu na kuwapakia kwenye magari kuwapeleka kwenye mikutano ya mbali.

Haikuwaunganisha watawala wawe na sauti moja, hata baada ya kurejea madarakani. Haikuwasaidia kupata hekima ya kumaliza matatizo ya muda mrefu, kama ukosefu wa umeme ambao umezungumzwa tena na tena bila ufumbuzi.

Sasa kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi, watawala wamerudi tena katika semina elekezi, chini ya mwelekezaji yule yule.

Walidhani zile zilishindikana kwa sababu zilifanyika Arusha. Sasa wamekimbilia Dodoma. Kwa wiki nzima, serikali iko Dodoma, imelala; inakula posho. Kazi zinakwama.

Rais naye, badala ya kuwaelekeza kwa hekima na ustadi, “akawananga” wasaidizi wake hadharani, kana kwamba huwa hapati fursa ya kukutana nao – wakati amekuwa akikutana nao kila mwezi katika vikao vya Baraza la Mawaziri. Ndio hao aliowatembelea na kuwasema wizarani kwao miezi miwili iliyopita, hata akawaamuru wengine waache ubabe.

Alitaka kuonewa huruma. Alitaka kuwashitaki kwa wananchi – waonekane wabaya, awe mzuri.

Rais anawasema mawaziri wake kama watoto wadogo wanaohangaika kuelewa kitu kidogo anachowafundisha. Anawaonyesha wananchi kwamba ana mawaziri mizigo, mbumbumbu – ambao kazi pekee wanayofanya ni “kumwangusha” rais.

Anataka turudi kwenye propaganda za kijinga walizoimba miaka mitano iliyopita, kwamba rais pekee ndiye anachapa kazi, bali mawaziri wake wanamwangusha.

Anawaambia mawaziri wake kuwa kama hawawezi kazi “waondoke,” kana kwamba hajui uwezo wao, hajui waliingiaje, wakati ndiye aliyewateua na ndiye ana mamlaka ya kuwaondoa.

Anataka “watoke” waende kwa wananchi kufafanua mafanikio ya serikali yake. Haamini kwamba wananchi wana uwezo wa kuona mazuri na mabaya ya serikali – bila kusubiri taarifa za mawaziri.

Haoni kwamba serikali inayofilisika na kulazimika kukopa hata mishahara ya watumishi wake, inahitaji kubana matumizi na kupunguza ziara na posho nono za viongozi hao waandamizi.

Lakini pia, tunapowatazama watu wenyewe aliokuwa anawapa somo, tunabaki kujiuliza: Rais amepata wapi hekima hii ya kudhani ana uelewa mpana kuliko mawaziri wake?

Amesomea wapi huko wasikojua wao, alikopata hicho cha kuwafunda? Tunapowatazama baadhi yao tunagundua kwamba kama rais angekuwa na busara ya kujifunza kutokana na miaka mitano iliyopita, asingewaita mawaziri kuwafunda, bali angewaita ili wakae kama timu, awaombe ushauri, awasikilize, wampe mang’amuzi yao na mipango mkakati; naye baada ya kuwasikiliza na kuongeza maono yake, awapangie kazi na kuwadai matokeo baada ya muda kadhaa.

Au basi angeunda kikosi kazi cha wasomi waliokubuhu kutoka taasisi mbalimbali zinazoheshimika, akawakutanisha na wasaidizi wake, wote pamoja wakavuna maarifa ya ziada katika kuboresha kazi zao na kukosoa kasoro za huko nyuma.

Angejenga mazingira ya kuambizana ukweli, naye akaambiwa kasoro zake; hasa kwamba serikali imekosa mipango mkakati mbadala na hata hiyo iliyopo imekosa msimamizi makini.

Kitendo cha rais kulialia mbele ya wateule wake na wananchi kupitia vyombo vya habari si ishara ya ushupavu anaostahili kuwa nao kiongozi mkuu wa nchi.

Ndiyo! Tuliona wameinama na kushika tama alipokuwa anafoka. Lakini ana uhakika gani kwamba walikubaliana naye? Ana uhakika gani kwamba walimwona shujaa?

Na kwa kiongozi ambaye ameongoza nchi kwa miaka mitano kwa hotuba na matamko yasiyotekelezeka, anadhani mawaziri wake watamwamini na kumheshimu baada ya kufokewa hadharani Dodoma?

Labda, watamshukuru kwa kuwatengenezea mazingira ya kula posho za safari. Lakini naamini mawaziri wenyewe wanajua fika kwamba hawana sababu ya kusafiri hadi vijijini kila mara, maana huko kuna watendaji wa ngazi za chini wanaopaswa kusimamia kazi na kuleta taarifa kwa ngazi za juu.

Sasa kama rais anaagiza mawaziri waende wenyewe vijijini, hao watendaji wa mikoani, wilayani na vijijini kwenyewe watafanya kazi gani?

Hivi waziri aliyekaa katika wizara ile ile kwa miaka mitatu au zaidi, ana kitu gani cha kujifunza kwa rais aliyekaa madarakani kwa miaka mitano bila maono na mafanikio yanayoshikika?

Rais Kikwete ana mfano gani wa utendaji uliotukuka anaoweza kuutumia kuwasuta mawaziri wake? Aliacha urithi gani katika wizara alizowahi kuongoza kabla hajawa rais?

Ni nani anayejua matatizo, changamoto, na suluhisho la matatizo yake, kati ya waziri aliye kwenye wizara hiyo hiyo, na rais “anayeishi kwenye ndege?”Baadhi yetu tunajua kwamba mkwamo mkubwa wa kiutendaji unatokana na madaraka makubwa ya rais, nidhamu ya woga ya wasaidizi wake na utovu wa uzalendo wa baadhi yao.

Zipo taarifa kwamba siku hizi wasaidizi wa rais wameamua kumwambia yale anayotaka kusikia, kwa sababu anawafokea hovyo hovyo wanapomweleza asiyotaka, au wanapompa mapendekezo magumu.

Wanadai rais hataki kuambiwa asichotaka; nao hawako tayari kupoteza kazi zao.

Kwa mantiki hii, haiwezekani kwamba baadhi ya wasaidizi wa rais wana nafuu kuliko yeye? Kwanini tusiamini, basi, kwamba rais ndiye anawaangusha wasaidizi wake?


1 May 2011



Ansbert Ngurumo

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinajitapa kwamba kinajivua gamba. Lakini sasa imeanza kudhihirika kwamba badala ya kujivua gamba kinajichuna ngozi. Kitakufa!

Bahati mbaya, kama baadhi yetu tulivyowahi kuandika huko nyuma, CCM kinashindwa kuwaaminisha watu wenye akili timamu kwamba kikiwafukuza ujumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu watu watatu – Andrew Chenge, Edward Lowassa na Rostam Azizi – kitakuwa safi. Kinajidanganya!

Taarifa zinaonyesha kuwa wanaoshabikia igizo hili la kujivua gamba ni Mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, na kundi linalofuata mkumbo kwa unafiki na woga.

Lakini wapo wana CCM wengi wenye akili timamu, na wananchi wengine, wanaosema wazi kwamba hata hao watatu wakiondoka, CCM haiwezi kuwa safi tena. Wala haitamsaidia Rais Kikwete kuonekana mwema kwa Watanzania. Na haitakifanya chama hicho kirejeshe mng’aro wake kwa umma.

Ni wazi, jitihada za Rais Kikwete na wenzake zinatokana na ukweli unaomuuma yeye binafsi kutokana na CCM kufanya vibaya katika uchaguzi mkuu uliopita.

Na ingawa kuna ukweli kwamba ufisadi umechangia kukifanya CCM kichukiwe na wananchi, hoja hiyo haiishii kwa watatu hawa. Mafisadi CCM ni wengi. Nimesema huko nyuma, kwamba hata Rais Kikwete mwenyewe, alitajwa kuwa miongoni mwao.

Hata jana alitajwa upya katika mkutano wa Mchungaji Christopher Mtikila na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, akimhusisha rais na utajiri wa ghafla wa mtoto wake.

Ufisadi huu wa rais unamnyima makali ya kuwashughulikia mafisadi wenzake. Na zaidi ya hayo unapanua wigo wa adui zake, maana sasa anagombana na watu wanaomfahamu vema; waliomsaidia na kumjenga, wakambeba hadi Ikulu.

Woga wake ni kwamba baadhi ya hawa waliombeba hadi Ikulu wana uwezo wa kutumia nguvu zile zile kumwondoa ama Ikulu au kwenye chama. Anachofanya sasa ni kuwashughulikia mapema ili kujinusuru.

Lakini nina hakika jitihada hizi hazitakinusuru chama chake. Na ingawa ameaminishwa kwamba mafisadi hawa ndio waliokifanya chama chake “kishindwe” uchaguzi mwaka jana, wapo wanaosema yale asiyotaka kusikia.

Anajiuliza zilikokwenda kura zake mwaka 2010, anapolinganisha na mwamko wa 2005. Anatafuta wachawi, lakini anasahau mambo kadhaa.

Kwa mfano, serikali imeshindwa kukidhi matakwa ya wananchi kama ilivyoahidi mwaka 2005. Kwa nini waipe CCM kura nyingi hata kama inawahonga mashati, kanga, kofia, pesa na pombe?

Wananchi walimsikia Rais Kikwete mwenyewe akiwaambia wafanyakazi ”sitaki kura zenu!” Wengi walikuwa waaminifu kwa kauli yake; wakamnyima. Si wao tu, bali hata rafiki zao, ndugu zao na wajuani wao, walikaa upande wa wafanyakazi. Kwa nini atarajie kura za CCM ziongezeke?

Mara kadhaa, Rais Kikwete alijikuta akigombana na baadhi ya viongozi wa dini kubwa zenye ushawishi kwa umma. Aliwadanganya Waislamu kuhusu Ofisi ya Kadhi Mkuu. Wamedai hadi wakakata tamaa. Hatimaye akawapatia ufumbuzi usioendana na ahadi yake. Wana sababu ya kumwamini na kumpa kura nyingi?

Serikali yake, kupitia kwa wasaidizi na washauri wake kadhaa, na hata yeye binafsi, ilijiingiza katika mzozo usio wa lazima na madhehebu kadhaa ya Wakristo, ikikerwa na jitihada zao za kukuza elimu ya uraia, na kuwahamasisha kuchagua viongozi waadilifu.

Sasa kama alikerwa na kampeni ya kuchagua viongozi waadilifu, tutamwaminije leo katika vita dhidi ya ufisadi? Na anapata wapi ujasiri wa kupiga vita mafisadi wale wale ambao alifika kwenye majimbo yao akawamwagia sifa na kuwanyanyua mikono kuwaombea kura?

Na kumbukumbu zinaonyesha kwamba katika wote, kama tunarejea ile orodha ya mafisadi ya awali (ambamo naye yumo), walishinda wote isipokuwa mmoja – Basil Mramba.

Zaidi ya hayo, walishinda wa kura nyingi. Maana yake ni kwamba wanakubalika katika majimbo yao, na hata nguvu yao inapenya katika vikao vya juu vya chama.

Ndiyo maana baadhi yao (kwa mfano Lowassa) wamefanikiwa hata kupata uongozi katika kamati za Bunge. Anajua nguvu yao ya ushawishi. Ndiyo inayomtisha.

Zaidi ya hayo, CCM kimetumia mabilioni ya shilingi kwa ajili ya “kununulia kura,” kinyume kabisa cha sheria ya gharama za uchaguzi. Ni mbunge gani wa CCM anaweza kujitapa kuwa amepita bila nguvu za ufisadi? Sasa rais na wenzake wanapiga vita ufisadi gani wakati wenyewe wamepita kifisadi, na chama kimejaa wabunge waliopita kifisadi?

Ndiyo maana sisi wengine tunakwenda mbali. Tunasema katika igizo la sasa la kujivua gamba, Rais Kikwete na wenzake, kama wana ujasiri wa kutosha, wasiishie tu kuwafukuza kwenye vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu.

Wawavue na ubunge. Wapoteze kila kitu. Tuanze upya. CCM igombee majimbo hayo bila nguvu ya rushwa. Je, CCM ina ujasiri huo?

Wapo wanaodokeza pia kwamba hata udhaifu binafsi wa rais kiafya ulichangia kupunguza imani na matumaini ya watu. Kwa mfano, madaktari wake walijaribu kufunika funika kwa taarifa zenye utata, lakini walishindwa kumzuia kuanguka hadharani mara kadhaa. Wanadhani hiyo ilikuwa mbinu ya kumwongezea kura?

Hizi ni chache tu, lakini zipo sababu nyingi za kuanguka kwa CCM katika uchaguzi uliopita. Hata maisha magumu yanayowakabili wananchi sasa hivi, ni kigezo kingine cha kuwahamasisha wananchi waichukie serikali na chama chake.

Ndiyo maana wenye akili wanapotazama kampeni hii ya kuvuana magamba wanasema bila woga kwamba tatizo la CCM si watu fulani, bali mfumo. Chama kimejikita katika mfumo wa ufisadi, kinaongoza kwa mazoea, kinakumbatia udikteta wa rais na mwenyekiti, na kinaogopa mabadiliko.

Mtu mmoja amenidokeza kwamba haikuwa kwa bahati mbaya Pius Msekwa kuteuliwa makamu mwenyekiti wa CCM. Ni Msekwa huyu aliyekuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa CCM mwaka 1977.

CCM haina muono mpya, au damu mpya za kushika nafasi ya Msekwa katika chama? Maana yake ni kwamba CCM iko nyuma ya wakati kwa miaka 34.

Hii ndiyo CCM inayoshabikiwa na kina Nape waliozaliwa ndani ya kipindi cha u-CCM wa Msekwa?

Ndiyo maana wanashindwa kujivua gamba, maana wao wenyewe ni magamba manene yaliyoshikamana na nyama za chama. Wakidiriki kuyavua, wataondoka na mnofu wa CCM.

Lakini hili haliwezekani kwa sababu CCM bila ufisadi, haiwezi kudumu. Ninachoona ni kwamba, ingawa wanaogopa kujichuna ngozi ili wasife, jitihada wanazofanya sasa ni sawa na kunywa sumu kali ambayo haiwezi kuwaepusha na mauti ya kisiasa. Wanalijua hilo?


17 Apr 2011



Chomoa, chomeka itainusuru CCM?

Ansbert Ngurumo

SAKATA la CCM kujivua gamba limezaa maswali mengi ambayo hayajajibiwa. Na limetusaidia kujua zaidi upeo wa watawala wetu, na uwezo wa kukabiliana na misukosuko ya ndani na nje ya chama tawala.

Na kwa kuwa wanapima upeo wa Watanzania kwa mizani ya upeo wao wenyewe, watawala wetu wamediriki kujitapa kwamba CCM imezaliwa upya. Wengine wanasema CCM imefufuka. Wamekosea!

Ni fursa kwa CCM ya Kikwete kujiuliza au kuulizwa. Kama CCM ya Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa ilionekana imara, ni nani ameidhoofika CCM ya Kikwete?

Mtu mmoja alinieleza miezi mitatu iliyopita, kwamba Rais Jakaya Kikwete alisikika akimweleza rafiki yake mmoja wa Iringa kwamba anavyoona chama kimeanza kumfia mikononi, na hilo ni jambo analoogopa sana. Je, mabadiliko haya ya kuchomoa na kuchomeka sura ndiyo yanaweza kuinusuru CCM inayokufa?

Tumesikia wanajitapa kwamba wameondoa mafisadi kwenye Kamati Kuu, na sasa wanataka waliobaki kwenye Halmashauri Kuu na vyombo vingine vya chama wajiondoe wenyewe, la sivyo watafukuzwa! Jambo jema.

Lakini CCM wameanza lini kukiri kwamba chama chao ni cha mafisadi au kina mafisadi? Si hawa hawa ndio walibeza na kulaani kauli ya wapinzani, iliyotolewa na Dk. Willibrod Slaa Septemba 2007, Mwembeyanga, Dar es Salaam, alipotaja orodha ya mafisadi na kufafanua ufisadi wa kila mmoja wao?

Si ndio hawa waliotishia, na baadaye wakaogopa kumshitaki Dk. Slaa, lakini wakaendelea kuwatumia mawaziri na makada wengine kuzunguka mikoani kushambulia wapinzani kwa kile walichoita ‘uzushi?’

Hoja ya ufisadi si ndiyo ilimfanya Rais Kikwete awabeze na kuwakejeli wapinzani akidai kelele za mlango hazitamzuia mwenye nyumba (yeye) kulala?

CCM hii si ndiyo iliwatuma Yusuph Makamba, Kingunge Ngombale-Mwiru, Jaji Joseph Warioba, Sofia Simba na makada wengine kubeza na kudhihaki wapinzani na vyombo vya habari, wakidai wanaendekeza habari za ufisadi badala ya masuala ya maendeleo?

Kama Rais Kikwete na wenzake wanasema kuwa umefika wakati chama kiondokane na mafisadi, basi wamethibitisha kwamba Dk. Slaa na wenzake walikuwa sahihi. Sasa tuwaamini CCM au akina Dk. Slaa?

Pili, dhana hii ya kujivua gamba bado ni tata hata kwa wenyewe wanaoipigia debe. Mwenyekiti mwenyewe aliyeianzisha alidhani CCM ina gamba moja tu inalopaswa kujivua; na akadhani inatosha tu kuvua gamba. Inasikitisha kwamba yeye anaishia hapo, lakini hata sisi tusio wana CCM tunajua kuwa CCM haikuhitaji kuvua gamba, bali kuwa na moyo mpya.

Lakini wale waliopenda kuendelea kuchambua hoja ya gamba wameshaorodhesha magamba ya CCM. Na wengine wamesisitiza kwamba Rais Kikwete, kwa staili yake ya uongozi, na baada ya kutathimni alikokitoa na alikokifikisha chama, naye ni gamba.

Kwa bahati mbaya, inavyoonekana, hata watawala wenyewe bado hawajajua idadi, na aina ya magamba wanayopaswa kukivua chama chao. Vile vile, hawajajua kwamba hata kama wangefanikiwa kuyatambua na kuyavua mgamba hayo, bado chama chao hakitaweza kuwa kipya.

Tatu, na hili ndilo la msingi kwangu, hivi watawala wanadhani kwamba nyoka anapojivua gamba anabadilika na kuwa mjusi au kinyonga?

Tunaona, na tunasema wazi kwamba CCM ya Kikwete, yenye gamba na isiyo na gamba, ni ile ile. Wanachofanya sasa ni kujaribu (na kufanikiwa kwa sehemu kubwa) kuwafukuza ’wabaya wao’ wa sasa na kuingiza marafiki wapya. Na bahati mbaya, ni sura zile zile tulizozizoea, tunazozifahamu, na ambazo tunapata shida kuzitenganisha na ufisadi uliowakumba kina Yusuph Makamba, Rostam Aziz, Andrew Chenge na wenzao.

Kikubwa zaidi ni mamlaka ya kimaadili yanayotumika kuwafukuza wengine na kuingiza wengine. Maana kama tunaendelea kukuza na kusisitiza hoja ya Mwembeyanga, waliotajwa kwenye orodha ya mafisadi ni hawa hapa:

1. Daudi Balali
2. Andrew Chenge
3. Basil Mramba
4. Gray Mgonja
5. Patrick Rutabanzibwa
6. Nazir Karamagi
7. Nimrod Mkono
8. Rostam Aziz
9. Edward Lowassa
10. Benjamin Mkapa
11. Jakaya Kikwete

Chama kinachojivua gamba, kwa mfano, kitajitapaje kwamba kimeondokana na mafisadi, wakati hata mwenyekiti mwenyewe yumo kwenye orodha?

Si hilo tu. Kwa misingi ya kikatiba, kihistoria na kitamadumi, CCM inaongozwa na mwenyekiti. Na hii ndiyo asili ya kaulimbiu ya siku nyingi ya CCM ya ‘zidumu fikra za mwenyekiti.’

Kwa mantiki hiyo, chama kinapofanikiwa au kinapokwama, mtu wa kwanza ambaye wana CCM wanapaswa kumhoji si katibu mkuu (maana utendaji wake unasimamiwa), bali mwenyekiti.

Sekretariti na Kamati Kuu ni zao la mwenyekiti. Ni mikono ya kazi anayotumia kuendesha chama. Ni kweli, Yusuph Makamba, kwa elimu na upeo wake, alibebeshwa mzigo mzito. Lakini ndiye huyo ambaye mwenyekiti aliridhika naye kwa miaka mitano.

Kwa hiyo, mwenyekiti ndiye aliyepaswa kubeba udhaifu wa katibu na chama kwa ujumla. Maana wana CCM walipohoji na kubeza uteuzi wa Makamba mwaka 2006 kurithi nafasi ya Philip Mangula, mwenyekiti hakujali.

Hata ilipopatikana fursa ya kubadilisha uongozi wa chama hapa katikati, Rais Kikwete aliridhika na utendaji wa Makamba. Huyu huyu hawezi kuibuka leo na kusema Makamba na sekretarieti yake hawajamsaidia kazi.

Nionavyo mimi, yaliyomkuta Makamba na Sekretarieti na Kamati Kuu yake ni sawa na yaliyomkumba Lowassa na Baraza la Mawaziri lililokuwa chini yake mwaka 2008.

Uamuzi wa kuondokana na Lowassa ilikuwa njia pekee ya kumnusuru Kikwete na anguko la kisiasa akiwa madarakani, kwa maana kashfa yenyewe iliyomsomba Lowassa iliwahusu wote.

Na hili la Makamba limeharakishwa na vuguvugu la mapinduzi ya ndani, baada ya mwenyekiti kuletewa taarifa kwamba kuna watu wananadi uenyekiti wake kwa maelezo kuwa ameshindwa kuongoza vema chama. Walitaka (na bado wanataka) abaki na urais, aachie uenyekiti.

Wanajua kuwa kwa utamaduni wao, mwenyekiti ndiye kiongozi wa chama. Anakotaka chama kiende, ndiko kinakokwenda. Na wandhani kuwa wakipata mwenyekiti mzuri watakuwa na chama kizuri.

Katika mazingira haya, njia pekee ya mwenyekiti kujinusuru ilikuwa kuwashughulikia walio chini yake ili ajipange upya, abadili hoja, na apate pa kuning’iniza propaganda za CCM mpya.

Na kwa maana hiyo, kujiuzulu kwa wajumbe wa Kamati Kuu na Sekretarieti (kwa shinikizo la mwenyekiti) ilikuwa faraja kwake binafsi si kwa CCM. Na ndiyo maana sisi wengine tunakataa kukubaliana na propaganda za akina Nape Nnauye eti chama kimezaliwa upya!

Nne, upya wa chama hauletwei na upya wa sura za wajumbe. Kama muono wa chama ni ule ule; itikadi ni ile il; sera zake ni zile zile; i wapi CCM mpya inayozungumzwa?

Bahati nzuri Katibu Mkuu mwenyewe ameshakiri kwamba hana jipya, bali anataka kurejesha na kusimamia misingi ile iliyokiasisi chama. Mwisho wa fikra!

Zaidi ya yote, kama huyu anayeteua, kupendekeza na kufukuza wajumbe wa kamati ndiye aliyesimamia waliopita, amepata wapi njozi mpya za kusimamia wapya kwa ufanisi? Au ni yale yale tuliyozoea kuona kila anapoteua baraza la mawaziri? Kama ndivyo, je, udhaifu wa uteuzi na utendaji tunaoshuhudia serikalini hautaendelezwa kwenye chama?

Kumwondoa Makamba na kumwingiza Mukama ni mabadiliko ya mwelekeo? Kumwondoa John Chiligati na kumwingiza Nape Nnauye ni kukipa chama dira mpya?

Kumwondoa Amosi Makala na kumwingiza Mwigulu Nchemba ni kukipa chama moyo mpya? Kumwondoa Bernard Membe na kumwingiza January Makamba ni kukipa chama katiba mpya? Kurejeshwa kwa Zakia Meghji kunakipa chama itikadi mpya?

Lililo wazi ni kwamba CCM ni chama kinacho kufa. Kina sura zile zile na mawazo yale yale. Na kwa sababu wameishiwa mapya, wamebaki katika siasa za kuwindana na kumalizana. Wanachomoa hawa na kuchomeka wale. Inatosha kuwanusuru?


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.