1 May 2011

Mimi ni Rais wenu,na huyu ndiye mwanangu mpendwa ninayependezwa na ufisadi,oops..ujasiriamali wake

na Mwandishi wetu

RAIS Jakaya Kikwete anakabiliwa na kashfa nzito kutokana na utajiri wa mtoto wake, Ridhiwani. Sasa anatuhumiwa kuitumia Ikulu kumtajirisha mwanawe, ambaye anasemekana ni bilionea.

Kwa nyakati mbalimbali, ukwasi wa mtoto huyo wa rais uliibuliwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa na Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila.

Katika moja ya mikutano yake ya hadhara hivi karibuni mkoani Tabora, Dk. Slaa alisema Ridhiwani amemaliza shule miaka michache iliyopita, lakini hivi sasa ni tajiri bilionea na kwamba ameupata utajiri huo katika mazingira ya kutatanisha.

Jana Mtikila alizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Travertine, akidai Ridhiwani amegeuka bilionea kwa muda mfupi “kwa mgongo wa baba yake.”
Akibainisha zaidi uwezo wa kifedha wa kijana huyo, Mtikila alisema hivi karibuni mtoto huyo ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UVCCM), aliingiza magari makubwa ya mizigo aina ya “semi trailer” zaidi ya 100 na kudai kuwa yanafanya kazi ya kusomba mizigo DRC na mengine ameyauza.

Alidai pia mtoto huyo wa rais anamiliki makampuni ya ujenzi wa barabara na maeneo mengi ya ardhi kwa lengo la kujenga maghorofa ya kupangisha.

“Huyu ni mtoto mdogo, kamaliza shule juzi, pesa za utajiri wote huu kazipata wapi?” alihoji Mtikila.

Hata hivyo, wiki iliyopita, Ridhiwani alikaririwa na moja ya vyombo vya habari akisema kuwa yuko tayari kutoa ushirikiano kwa Dk. Slaa kuonyesha kila anachomiliki.

Kutokana na tuhuma hizo, Mtikila alimtaka Rais Kikwete naye ajivue gamba kwa kuonyesha mfano, vinginevyo ni uendawazimu kujivua gamba bila mkuu huyo wa nchi kujiuzulu urais na uenyekiti wa CCM.

Huku akionekana kuwatetea Edward Lowassa (Monduli), Andrew Chenge (Bariadi Magharibi) na Rostam Aziz (Igunga), Mtikila alisema Kikwete anawachezea wana CCM na Watanzania kwamba ana nia ya kuwatimua makada hao kwa madai kuwa ni mafisadi wakati yeye ni mshirika wao.

“Kikwete aanze kutoka yeye ndipo awanyoshee vidole hawa Mapacha Watatu alioshirikiana nao kwenye ufisadi wa EPA, Richmond na Dowans, vinginevyo anawadanganya Watanzania. Aanze yeye,” alisema Mtikila.

Alisema anashangazwa na Kikwete kuibuka na dhana ya kujivua gamba kwa kuwatosa marafiki zake watatu wakati chama hicho kina mafisadi lukuki.

Mchungaji Mtikila pia aliorodhesha miradi ya ufisadi aliyomhusisha nayo Kikwete na watendaji wengine serikalini kuwa ni pamoja na IPTL, uuzaji wa iliyokuwa Benki ya NBC, Meremeta, Richmond, Dowans, EPA na nyingine, kwamba zinawahusu watendaji wengi na si mapacha watatu pekee.

”Kikwete aliunda tume kubaini waliochota fedha za EPA na kutakiwa warudishe, lakini hadi sasa hatujui kina nani wamehusika, na kiasi gani cha fedha kilichorudishwa. Kama rais hahusiki na ufisadi huu, usiri wa nini?” alihoji Mtikila.

Alisisitiza kuwa hana maana kuwa Lowassa, Rostam na Chenge ni wasafi, bali anataka orodha ya kuwatimua mafisadi wa CCM iwe kubwa, akiwamo Rais Kikwete kwani ndilo gamba kubwa kuliko yote.

Kuhusu hatima ya CCM na kile alichokiita usanii wa kujivua gamba, Mchungaji Mtikila alisema chama hicho kina ugonjwa wa ‘Nambulila’ ambao mgonjwa hufa na kuzikwa akijiona.

“Wapangwa wana ugonjwa unaitwa Nambulila. Ni ugonjwa unaotokana na tego la mke. Mtu akitembea na mke wa mtu anaupata na anapokufa, anawaona watu wanavyomlilia, wanavyomuingiza kwenye kaburi, lakini hana uwezo wa kusema, hivyo anazikwa akiwa hai, akiona kila kitu. Ndivyo ilivyo CCM, inakufa ikijiona. Hii ndiyo Nambulila,” alisema Mtikila.

Alisema usanii wa kujivua gamba hauwezi kuinusuru CCM kwani ni dhana ya uendawazimu yenye lengo la kuwaghilibu Watanzania.

Sambamba na hilo, Mtikila aliwataja mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye, Joseph Warioba na Cleopa Msuya, kuwa ni miongoni mwa watu wachache wasafi ndani ya CCM.

Alipobanwa kueleza usafi wa Sumaye wakati miaka sita iliyopita alipata kumtaja kwamba ni fisadi namba moja, Mtikila alikiri kutoa kauli hiyo na kuongeza kwamba baada ya kufuatilia walibaini kashfa dhidi yake zilikuwa za uongo na zilipikwa ili kumrahisishia Kikwete njia ya kuwa rais.

“Kweli niliwahi kumtaja kama fisadi namba moja, tulipofuatilia tulibaini kwamba haikuwa sahihi na ndiyo maana leo namtaja kama mmoja ya viongozi wachache wasafi,” alisema.

Aliwataka wana CCM kutobeza ushauri wa viongozi hao wachache wasafi na kutolea mfano wa Warioba na Sumaye walivyoshambuliwa na UVCCM walipotoa mawazo yao.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.