11 Nov 2011

Tatizo ni unafiki wetu, si ushoga

Uskochi
MOJA ya mambo yaliyonishitua sana nilipofika hapa Uingereza kwa mara ya kwanza ni jinsi Ukristo ulivyopoteza nguvu yake (hususan mahudhurio kanisani na watu wanaofuata Ukristo). Kilichonishitua ni ukweli kwamba Ukristo uliletwa huko nyumbani na “wazungu” hawa na nilitarajia wangekuwa wacha Mungu wakubwa.
Dalili za Ukristo kupoteza nguvu yake zinaonekana katika namna makanisa yanavyoishia kugeuzwa kumbi za starehe baada ya kukosa waumini. Kadhalika, asilimia kubwa ya waumini makanisani ni wageni kutoka nje ya nchi hii. Na japo Malkia wa Uingereza ni Mkuu wa Kanisa la Anglikana na Askofu Mkuu wa Canterbury ni mithili ya Baba Mtakatifu (Papa) kwa Kanisa hilo, idadi kubwa ya Waingereza inajitambulisha kama watu wasiofuata dini. Na kuna kundi kubwa tu la wanaojitambulisha kama Wakristo lakini wasiotia mguu kanisani.
Hakuna jibu jepesi kuhusu kwa nini Ukristo unazidi kupoteza nguvu nchini hapa lakini baadhi ya watu niliowahoji wanadai huenda maendeleo katika nyanja mbalimbali ni chanzo kwa baadhi ya watu “kupuuza” umuhimu wa imani katika maisha ya mwanadamu.
Lakini pamoja na Ukristo kupoteza nguvu yake miongoni mwa Waingereza, kwa kiasi kikubwa uadilifu katika nyanja mbalimbali za maisha umeendelea kuwa wa kiwango cha juu. Na hapa ndipo unaweza kubaini tofauti kubwa kati ya Waingereza “wanaopuuza dini” na akina sie huko nyumbani ambao dini inaonekana kuwa sehemu muhimu kwa maisha yetu.
Neno mwafaka linaloweza kuelezea tofauti hiyo ni UNAFIKI. Ni hivi, ni bora kuwa na watu wasio na dini au wasioabudu uwepo wa Mungu lakini wakaishi na kutenda mambo kiadilifu kuliko kuwa na ‘washika’ dini wasiokosekana makanisani au misikitini lakini uadilifu wao ni haba kama sio sifuri kabisa.
Na suala la unafiki linaweza kuchukua nafasi muhimu katika mjadala mkali uliosababishwa na kauli ya Waziri Mkuu wa Uingereza kuwa nchi yake itasitisha misaada kwa nchi zinazokiuka haki za mashoga. Tayari Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ameweka bayana msimamo wa Serikali kwamba Tanzania ipo tayari kukosa misaada ya Uingereza kuliko kubadilisha sheria za nchi zinazopiga marufuku ushoga.
Lakini kabla sijaingia kwa undani katika kujadili suala hili ni vema nikaweka wazi msimamo wangu. Imani yangu kama Mkristo wa madhehebu ya Katoliki (ambaye almanusura ningekuwa padre iwapo nisingeghairi kujiunga na seminari mwaka 1986) sio tu inapinga ushoga bali pia inauona kama dhambi. Kwa hiyo, naomba ifahamike kuwa lengo la makala hii si kuunga mkono ushoga.
Kwa upande mmoja, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, alikuwa na haki ya kuweka masharti katika misaada wanayotoa. Ifahamike kuwa misaada hiyo inatokana na fedha za walipa kodi wa Uingereza na inatarajiwa ielekezwe kwa nchi zinazoonekana machoni mwa Waingereza kama zinazoendana na maadili yao. Na moja ya masuala yanayopewa kipaumbele na nchi hii ni haki za binadamu (ikiwa ni pamoja na haki za mashoga).
Kwa hiyo basi si kwamba Cameron alikurupuka tu na tamko hilo ambalo baadhi ya wenzetu wamelitafsiri kama ajenda ya kueneza ushoga, bali anawakilisha hisia za wananchi wake ambao kimsingi ndio chanzo za fedha tunazopatiwa kama misaada.
Ni wazi kuwa kiongozi yeyote yule anayejua anachofanya atahakikisha anasimama upande wa wananchi wake. Kwa mantiki hiyo wananchi wake wanapotaka fedha yao wanayotupatia kama msaada ielekezwe tu kwa nchi zinazojali haki za binadamu (ikiwa ni pamoja na haki za mashoga) tu basi hana budi kufanya hivyo.
Japo siungi mkono ushoga lakini ninaelewa mantiki ya Cameron kutoa tamko hilo linaloakisi matakwa ya wananchi wake. Lakini kwa vile matakwa ya Waingereza kuhusu haki za binadamu hayaishii kwa mashoga pekee, ingeleta maana zaidi iwapo tishio la kukata misaada lingeelekezwa pia kwenye tatizo sugu la rushwa (na ufisadi kwa ujumla) ambalo si tu linakwaza haki za binadamu za masikini (ambao ni wengi kuliko mashoga) bali pia linaweza kusababisha wanyonge kupoteza maisha (kwa mfano rushwa inayowezesha  vyombo vya usafiri vyenye hitilafu kuendelea na kazi na hatimaye kusababisha ajali).
Sasa nigeukie unafiki unaoandamana na jinsi tamko la Cameron lilivyopokelewa. Haihitaji utafiti wa kina kubaini kwamba si tu Tanzania (na nchi nyingine zinazolengwa na tishio hilo la kukatiwa misaada) ina mashoga lakini pia ushoga unazidi kuongezeka. Hivi nani anayesoma magazeti ya burudani au blogu hajamwona shoga mmoja aliyejipachika jina Seduction ambaye ni kama yupo kwenye kila shughuli za mabinti maarufu jijini Dar?
Nilipokuwa huko nyumbani mwaka 2005 na niliporejea tena mwaka 2008 nilishuhudia idadi kubwa tu ya mashoga katika maeneo mbalimbali ya burudani jijini Dar es Salaam. Na uchunguzi usio rasmi ulionesha kuwapo kwa mashoga kwenyekitchen parties ni kama suala la kawaida tu. Nilibaini kwamba kumbi za muziki wa mwambao zilikuwa ni chaguo kubwa la mashoga.
Lakini jambo moja la wazi ni kwamba hakukuwa na upinzani, chuki au hasira dhidi ya mashoga hao. Na sijawahi kusikia kuna shoga amekamatwa na polisi, kupelekwa mahakamani na hatimaye kufungwa kwa “kosa” la kuwa shoga. Na ukidhani hilo la kutokamatwa kwa mashoga ni la kushangaza sana, basi kubwa zaidi ni uteuzi wa kigogo mmoja (mstaafu sasa) wa shirika la umma ambaye kila aliyemjua alikuwa anafahamu  tabia yake ya ushoga (kwa maana ya tendo la ndoa na watu wa jinsia yake).
Nina hakika aliyemteua alikuwa anafahamu hilo lakini haikuzuia kigogo huyo kupewa nafasi ya kufisadi shirika hilo hadi alipoondoka huku akijimwagia sifa za vichekesho.
Tuache unafiki, hivi maadili tunayodai ni haya ya wengi wa vigogo wetu kutumainia waganga wa kienyeji katika kila wanalofanya? Maadili haya ya “wachunga kondoo wa Bwana” kuishi maisha ya kifahari kama matajiri wakubwa ilihali waumini wao hohehahe wakihimizwa kuongeza kiwango cha sadaka? Au maadili haya ya Wakristo na Waislamu wasiokosekana kwenye nyumba za ibada lakini ndio wahusika wakuu wa ufisadi? Au haya ya ushirikina kuwa muhimu kuliko kumtumainia Mungu?
Au maadili tunayodai kuwa nayo ni haya ya majambazi wanaotupora utajiri wetu kisha kuibukia makanisani au misikitini na kutoa sadaka au zaka kubwa (iliyotokana na fedha ileile waliyotuibia)? Au maadili tunayodai Waziri Mkuu Cameron anayapuuza ni haya ya wengi wa wasanii wetu wa kike kwenye fani ya filamu ambao licha ya kupendelea kuvaa nusu uchi, hawana mishipa ya aibu kutangazia umma uchafu wanaofanya katika maisha yao? Maadili haya ya wasanii wa Khanga Moja na Kitu Tigo wanaoigiza u-Sodoma na Gomora hadharani kwa kisingizio cha burudani lakini hakuna wa kuwachukulia hatua?
Ni maadili gani anayozungumzia Kikwete na Waziri wake Membe ilihali katika hotuba yake iliyogusia mafisadi wa EPA alikumbushia umuhimu wa haki zao za binadamu (na ikambidi aliyekuwa Spika, Samuel Sitta, amkumbushe Rais kuwa haki za wananchi ni muhimu kuliko za mafisadi)?
Mbona hakukuwa na maandamano ya kumlaani Kikwete kwa kutetea haki za binadamu ambao ni mafisadi lakini leo tunawalaani Waingereza kwa kutishia kutunyima fedha zao kama tusipofuata matakwa yao?
Lakini unafiki mkubwa zaidi ni huu: viongozi hawa hawa ambao licha ya kukiri hadharani kuwa hawajui kwa nini nchi yetu ni masikini (labda pia hawajui kwa nini waliamua kutuongoza) pia ni washiriki wakubwa wa ufisadi unaotufanya tuishi kwa kutegemea fadhila za wafadhili kama Uingereza, wanatuhadaa kuwa ni bora tunyimwe misaada kuliko kukiuka maadili yetu. Lakini wababaishaji hawa hawatuambii jinsi watakavyofidia pengo litakalotokana na kukatwa misaada hiyo.
Na hawatuambii kwa sababu hajui watafidia vipi na hawajali kwa vile wao hawataathiriwa na kukatwa misaada hiyo. Na kama ambavyo tatizo la umeme linavyodumishwa na mafisadi ili kujaza akaunti za vijisenti huku nje, si ajabu tukikatiwa misaada mafisadi watapata kisingizio kipya cha “imebidi mabilioni haya ya shilingi yatumike kufidia pengo lililotokana na uamuzi wa Uingereza kutukatia misaada.”
Nimalizie makala hii kwa kutamka bayana kuwa kama ambavyo sipingi uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi kwa vile hainihusu mie Mkristo, sina tatizo na kurekebisha sheria za ushoga kwa vile si tu mashoga wapo na wanazidi kuongezeka (na hakuna anayewachukulia hatua kwa kuvunja sheria) lakini pia sheria hizo hazinihusu mimi au yeyote yule asiye shoga.

1 comment:

  1. Siku tutakayoondoa unafiki pengine tutapiga hatua, UNAFIKI unatusmubua sana, si kwenye suala hili tu bali mengi yanayoendelea hapa nchini yanatawaliwa na unafiki na si uhalisia, wengi wanaounga ama kupinga jambo fulani ukiangalia ama kuwakuta faragha hawaongei kile walichokuwa wakiongea mbele ya kadamnasi, ni UNAFIKI MTUPU.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube