1 Dec 2011


Tatizo kuu CCM si mafisadi pekee, bali hata wanaowalea

Evarist Chahali Uskochi

HATIMAYE mchezo wa kuigiza wa “kujivua gamba” umefikia kikomo. Baadhi yetu tulihisi tangu mwanzo kuwa usanii huo haukuwa tofauti na ahadi tamu zinazosheheni kwenye kila ilani ya uchaguzi inayotumiwa na CCM kuombea kura lakini mwisho wa siku ahadi hizo huishia kuwa porojo tu.

Kuna sababu lukuki kwa baadhi yetu kubashiri kwamba kama CCM itafanikiwa kuvua magamba basi chama hicho kitakuwa katika hatari kubwa ya kupoteza uhai wake. Japo magamba yaliyopaswa kuvuliwa na CCM hayakuwa mithili ya yale ya viumbe hai lakini kimsingi kiuhalisia kung’oa gamba la kiumbe kama kobe kunaweza kabisa kupelekea kifo cha kiumbe huyo. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa chama tawala.

Kwa muda mrefu sasa Chama Cha Mapinduzi kimekuwa tegemezi sana kwa watu wenye fedha pasipo kujali watu hao wamepataje fedha hizo. Yayumkinika kabisa kuhitimisha kuwa hata utaratibu usio rasmi kwamba ili kupata nafasi ya uongozi wa kisiasa nchini-hasa kwenye nafasi za udiwani na ubunge-mgombea anapaswa kuwa na mamilioni ya fedha za kununuliwa kura ni matokeo ya CCM kukumbatia wenye fedha, na hatimaye kupelekea uwezo wa kifedha kuwa kigezo muhimu cha ushindi kwa mgombea kuliko uwezo wake kiuongozi.

Lakini sababu kubwa kabisa iliyotengeneza kifo cha ajenda ya magamba tangu siku ya kwanza ni mwasisi wa wazo hilo, yaani Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete. Japo Watanzania tunasifika kwa usahaulifu lakini naamini wengi wetu tunakumbuka jinsi Rais Kikwete alivyopigana kufa au kupona kuwapigia kampenia na kuwatetea kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita, wanasiasa ambao baadaye waliitwa magamba.

Kikwete alisisitiza kwamba wanasiasa hao ni watuhumiwa tu na hawajafikishwa mbele ya vyombo vya sheria na hivyo hakuona ubaya kusimama majukwaani kuwaombea kura. Alikwenda mbali zaidi na kunadi uadilifu na uongozi wao bora, jambo lililoibua hisia kuwa hakuwa anawasaidia tu kupata kura, bali pia alikuwa anawatengenezea kinga pindi zikitokea jitihada za kuwachukulia hatua.

Ni hivi, laiti watuhumiwa hao wa ufisadi (au magamba) wangefikishwa mahakamani wangeweza kabisa kutumia hotuba za Kikwete kwenye kampeni zao kama utetezi wa tuhuma dhidi yao kwani sote tunajua kuwa kama Rais anaamini watu hao ni safi, basi hakuna hakimu au jaji ambaye angediriki kuwa na mtizamo tofauti.

Kwa lugha nyingine, Kikwete alikuwa akiwapatia watuhumiwa hao wa ufisadi kinga dhidi ya mashtaka ndani na nje ya Mahakama. Na kama wasemavyo Waingereza, hukumu ya umma ina nguvu kubwa zaidi ya hukumu halisi inayotolewa mahakamani. Hapa ninamaanisha kwamba “hukumu ya hawana hatia hadi watiwe hatiani” iliyotolewa hadharani na Kikwete kwa watuhumiwa wa ufisadi ilikuwa na nguvu kubwa kwa umma, hasa katika mazingira ya siasa za umungu-mtu wa Rais.

Kama ambavyo mara kadhaa nimeonyesha kutoelewa anayepaswa kubebeshwa lawama katika baadhi ya maamuzi ya Kikwete ni yeye mwenyewe au washauri wake nilipata tabu kumwelewa alipojipa jukumu la “kuwabeba” watuhumiwa wa ufisadi kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita. Haikuhitaji busara kwa Rais Kikwete kutambua kuwa wanasiasa hao waliokuwa wakituhumiwa kwa ufisadi hawakuamka tu ghafla na kujikuta wanatuhumiwa bali kulikuwa na mlolongo wa matukio uliowaingia katika tuhuma hizo.

Angeweza kabisa kuepuka hali ya kuonekana anawatetea na laiti busara zingetumika basi angewaachia jukumu la kuomba kura na kujisafisha kwa umma mikononi mwao. Ndiyo maana miezi michache baadaye alipokurupuka na ajenda ya kuwashughulikia watu hao hao aliowasafisha majukwaani ilikuwa ni dhahiri kuwa usanii huo usingezaa lolote la maana.

Lakini kuna kubwa zaidi lililojiri katika vikao vya CCM vilivyomalizika wiki iliyopita mjini Dodoma. Kwa mujibu wa vyombo vya habari, mmoja wa watuhumiwa wa ufisadi aliweka bayana jinsi Kikwete alivyofanya maamuzi ambayo hatimaye yalisababisha mwanasiasa huyo kuishia kuwa mtuhumiwa wa ufisadi. Kwa lugha nyingine, mwanasiasa huyo alikubali kubebeshwa mzigo wa lawama ambao kimsingi ulipaswa kubebwa na Kikwete.

Wakati usanii wa kujivua magamba unashika kasi kwenye vyombo vya habari kulizuka msamiati mpya wa “mapacha watatu” ambao ulimaanisha wanasiasa watatu waliokuwa wakituhumiwa kwa ufisadi na ambao kimsingi ndio walikuwa walengwa wakuu wa ajenda ya kujivua gamba. Wanasiasa hao ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Mbunge wa zamani wa Igunga, Rostam Aziz na Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge.

Kwa wanaofuatilia kwa karibu harakati za Rais Kikwete tangu aliposhindwa kwenye mchujo wa kupata mgombea urais kwa tiketi ya CCM mwaka 1985 hadi alipofanikiwa kuingia Ikulu mwaka 1995 ni wazi kuwa “mapacha watatu halisi” ni Kikwete, Lowassa na Rostam ambao kwa pamoja, waliweza kutengeneza mtandao wenye nguvu kubwa uliompa ushindi Kikwete.

Sasa katika mazingira ya kawaida tu, ingewezekanaje Kikwete ambaye kimsingi ndiye mwenye maamuzi ya mwisho ndani ya CCM awasaliti “mapacha wenzie” Lowassa na Rostam? Naomba ieleweke simaanishi kuwa angetaka kwa dhati kufanya hivyo asingeweza.

Nimesema “mazingira ya kawaida” kwa maana ya Kikwete tunayemfahamu sote: mwanasiasa anayeonekana kukumbuka sana fadhila alizofanyiwa na watu waliomsaidia kuingia Ikulu na kiongozi ambaye anachelea sana kuwaadhibu watendaji wake hata pale ambapo kuchelea huko kunaishia kumfanya aonekane kiongozi dhaifu na mwoga wa kuchukua maamuzi magumu.

Laiti Kikwete angetaka “liwalo na liwe” dhidi ya maswahiba zake ambao baadaye alionelea wanapaswa kuchukuliwa hatua ili kuinusuru CCM basi angeweza kabisa kuitumia Idara ya Usalama wa Taifa “kuwaandama” wanasiasa hao kwa minajili ya kuwadhibiti “wasimgeuke au kumdhuru.” Kama ambavyo taarifa za kiintelijensia zinavyosukuma haki za kikatiba za wananchi kuandamana kufinyangwa, basi ingewezekana kabisa kutumia mbinu hiyo kuhakikisha kuwa “magamba yakishang’olewa hayachipui tena.”

Na wala usidhani kwamba kungekuwa na haja ya matumizi ya “mbinu chafu” kuyadhibiti “magamba” bali wahusika wangeweza kukumbushwa “Rais ni nani” kwa njia nyepesi tu ya kile kinachofahamika kama ufuatiliaji wa waziwazi (overt surveillance).

Hii ni mbinu inayotumika kumfikishia ujumbe mlengwa kuwa anafuatiliwa, wafuatiliaji hawajihangaishi kujificha bali wanataka anayefuatiliwa afahamu kuwa anafuatiliwa na hivyo kumdhibiti kufanya jambo lolote lile “baya.”

Kwa hiyo laiti mwasisi wa wazo la kujivua magamba-Rais Kikwete angekuwa na dhamira ya kweli ya kutaka mkakati huo ufanikiwe basi wala kusingekuwa na haja ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, kupita huku na kule akiwahadaa Watanzania kuhusu umakini wa suala hilo.

Sina hakika kama Nape alikuwa anafahamu “ngoma aliyokuwa anaicheza” lakini kilicho dhahiri ni kwamba muda huu anatambua kuwa “hakuna mwenye uwezo au uthubutu wa kumtenganisha Kikwete na watu ambao hakufahamiana nao mtaani (bali wametoka mbali pamoja).”

Lakini kifo cha usanii wa “kujivua magamba” kinaweza kutoa fundisho kwa CCM kuacha mtindo wa kudandia hoja za vyama vya upinzani hususan CHADEMA. Wenye kumbukumbu nzuri watakuwa wanafahamu jinsi CCM ilivyopinga kwa nguvu zote madai ya CHADEMA kuwa chama hicho tawala si tu kinakumbatia mafisadi bali pia kimegeuka kuwa kichaka cha kuwahifadhi mafisadi.

Sasa baada ya kuona kuwa CHADEMA inapata umaarufu mkubwa kutokana na msimamo wake thabiti dhidi ya ufisadi, CCM nayo ikakurupuka na ajenda ya kusaka umaarufu ikisingizia inataka kujisafisha. Lakini hata kama chama hicho tawala kungekuwa na dhamira ya dhati kutekeleza mpango huo ingewawia vigumu kufanikiwa kwa sababu ufisadi na CCM ni kama samaki na maji; ukimtoa samaki majini umemuuwa na ukiwaondoa mafisadi CCM basi umeua chama.

Nimalizie makala hii kwa ushauri wa bure kwa chama tawala. Tatizo la msingi si magamba bali aliyeyawezesha magamba hayo kukomaa. Kama ambavyo ni vigumu kudhibiti malaria kwa kugawa vyandarua na dawa za kukinga au kutibu ugonjwa huo pasipo kuangamiza mazalia ya mbu, ndivyo ambavyo ni vigumu kwa CCM kupambana na mafisadi pasipo kuwabana viongozi ambao si tu wapo madarakani kwa msaada wa mafisadi bali pia uhai wao wa kisiasa umewekwa rehani kwa mafisadi hao.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.