23 Mar 2012


Mkapa, Wassira washitakiwe kwa kauli zao tata Arumeru Mashariki

Uskochi
Dk. Slaa, Nassari na Vincent Nyerere watangulie kortini
HUKO nyuma niliwahi kuandika makala ambayo ilijaribu kuangalia upande wa pili utawala wa Baba wa Taifa Mwalimu, Julius Nyerere. Katika makala hiyo ambayo baadhi ya wasomaji waliitafsiri visivyo kuwa ni kumkosea heshima Mwalimu, nilitanabaisha kuwa licha ya mazuri mengi ya Nyerere, kwa namna fulani alichangia kutufikisha katika mazingira hovyo ya sasa.
Kati ya mifano niliyotumia kuthibitisha hoja yangu ni baadhi ya viongozi walioaminiwa na Mwalimu wakati wa utawala wake lakini mara baada ya yeye kutoka madarakani na hatimaye kufariki waligeuka viumbe tofauti kabisa, huku baadhi wakijitahidi kubomoa kila msingi aliojenga Nyerere kwa manufaa ya Watanzania.
Nilitolea mfano wa mwanasiasa mkongwe na aliyekuwa rafiki wa karibu wa Mwalimu, Kingunge Ngombale Mwiru, ambaye mara kadhaa katika miaka ya hivi karibuni ameonekana kuwaunga mkono baadhi ya wanasiasa ambao ‘walikataliwa na Nyerere’ kutokana na wasifu wao usiopendeza.
Lakini pengine mfano hai na ‘mbichi’ kabisa ni wasifu wa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, ambaye siku chache zilizopita alizungumza mambo ya ajabu wakati akizindua kampeni za CCM, katika uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki.
Hata kabla ya kauli zake huko Arusha, Mkapa ameendelea kuonekana kama msaliti kwa Watanzania baada ya umma kufahamishwa mambo aliyokuwa akifanya ‘nyuma ya pazia’ wakati akiwa Ikulu.
Wakati Mkapa alikuwa akiwaaminisha Watanzania kuhusu umuhimu wa maadili bora na siasa za ukweli na uwazi, taarifa zilizopatikana baada ya kustaafu kwake ni tuhuma kwamba aliigeuza Ikulu kama kijiwe cha biashara.
Yayumkinika kuhisi kuwa laiti nchi yetu ingekuwa inazingatia utawala wa sheria, ni wazi muda huu Mkapa angekuwa matatizoni angalau kwa kuundiwa tume ya kuchunguza tuhuma kadhaa dhidi yake. Lakini kwa vile sheria zinazotawala Tanzania zipo katika makundi mawili - kwa vigogo na kwa walalahoi - Rais huyo mstaafu anaendelea kula pensheni yake nono kwa amani na utulivu, hasa baada ya Rais Jakaya Kikwete kuweka wazi msimamo wake kuwa mtangulizi wake huyo aachwe apumzike kwa amani.
Turejee Arumeru Mashariki. Katika uzinduzi huo wa kampeni za CCM, bila aibu na pasipo jitihada zozote za kutumia busara ya kumkumbusha kuwa pamoja na tuhuma za kuitumia vibaya Ikulu bado baadhi ya Watanzania wanamheshimu kama Rais wao mstaafu aliyewaongoza kwa miaka 10 mfululizo, Mkapa alizungumza maneno yaliyoshangaza wengi.
La kipuuzi zaidi ni kuingiza porojo za mtaani kwenye mambo ya msingi. Huku akitambua bayana kuwa uongozi ni haki ya kila Mtanzania bila kujali ametoka ukoo gani. Mkapa alitoa tuhuma nzito dhidi ya Mbunge wa Musoma Mjini (CHADEMA), Vincent Nyerere, kuwa hatoki katika ukoo wa Nyerere.
Ni kuzeeka vibaya au uthibitisho kuwa Nyerere alifanya kosa kubwa kumpigia debe apate urais mwaka 1995? Ukaribu wa Mkapa na Mwalimu hauwezi kuwa kigezo cha yeye kumfahamu kila mwana-ukoo wa Baba wa Taifa. Lakini hata kama angekuwa anafahamu kuwa Mbunge Vincent hatoki ukoo wa Nyerere, hilo linawasaidia vipi wapiga kura wa Arumeru?
Ni kwa nini Mkapa hajatoa ushirikiano kwa mamlaka husika iwapo alikuwa anafahamu kuwa Mbunge huyo wa Musoma Vijijini amedanganya kwa ‘kujipachika’ undugu na Baba wa Taifa?
Japo ninaamini kuwa sababu kubwa ya wapiga kura wa Jimbo la Musoma Mjini kumchagua Vincent ni imani yao katika uwezo wake kuwatumikia, lakini ukweli kwamba anatoka ukoo wa Nyerere unaweza kuwa ulimwongezea kura kadhaa (hasa kwa kuzingatia ‘siasa zetu za haiba ya mgombea’).
Kwa Rais mstaafu ‘kufahamu’ kuwa kuna mbunge anadanganya kuhusu wasifu wake lakini akakaa kimya hadi kwenye kampeni za uchaguzi ambapo Vincent ni mmoja wa waratibu wake kwa upande wa CHADEMA, inatueleza mengi kuhusu ubabaishaji wa Mkapa.
Lakini kubwa zaidi, kitendo cha mwenyekiti huyo mstaafu wa CCM kutokukifahamisha chama chake kuwa mgombea ubunge wa chama pinzani amedanganya kuhusu wasifu wake na hatimaye akafanikiwa kupata ubunge kinaweza kutafsiriwa kama usaliti dhidi ya chama alichokiongoza kwa mwongo mzima.
Sijui Mkapa alijisikiaje baada ya mmoja wa watoto wa Baba wa Taifa, Madaraka Nyerere kuwathibitishia Watanzania kuwa Vincent Nyerere anatoka ukoo wa Nyerere (kinyume cha uongo wa hadharani wa Mkapa).
Kilicho wazi ni kuwa upuuzi huo umeongeza sifa nyingine mbaya kwenye wasifu wake usiopendeza. Ni Mkapa pekee anayejua kwa nini alikurupuka kusema uongo hadharani lakini sote tunajua kuwa kitendo cha Rais mstaafu kusema uongo kwenye kadamnasi (tena pasipo hata haja ya kufanya hivyo) kimezidi kushusha hadhi ya kiongozi huyo.
Lakini kana kwamba  kasoro hiyo ya Mkapa kujifanya mwana-ukoo wa Nyerere na kumkana hadharani Vincent Nyerere, haitoshi kutueleza yeye ni binadamu wa aina gani, baadhi ya ahadi alizotoa kwa wapiga kura wa Arumeru Mashariki zinazua swali gumu, ilikuwaje yeye binafsi alifanikiwa kuwa Rais wetu kwa awamu mbili mfululizo.
Katika uzinduzi huo wa kampeni za chama tawala, Mkapa aliwaeleza wananchi kuwa amepokea taarifa za kuwapo kwa migogoro mikubwa ya ardhi inayosababishwa na baadhi ya wawekezaji kuhodhi maeneo makubwa na kusema atalifikisha kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na kumshauri achukue hatua kwa kuwawajibisha watendaji wa Serikali ambao wameshindwa kuwajibika na kuchukua hatua kwa wawekezaji waliokiuka masharti.
Hivi kweli Mkapa ameshasahau alikuwa Rais wetu kwa miaka 10 mfululizo na utawala wake ulifungua milango kwa kila mgeni kuja kuwekeza hata pale uwekezaji huo ulimaanisha uporaji wa rasilimali za nchi yetu?
Kama amesahau hilo lililojiri miaka michache tu iliyopita, kwa nini basi ajifanye kukumbuka kila kilichomhusu Baba wa Taifa kwa vile tu alikuwa msaidizi wake miaka mingi iliyopita?
Ni kwa vile tu CCM yenyewe inaendeshwa kimzaha ndio maana hadi sasa hakuna kiongozi yeyote wa chama hicho aliyediriki kumkemea Mkapa asimfarakanishe Kikwete na wananchi kwa ahadi za kumshauri Rais ashughulikie makosa yaliyofanywa na mtangulizi wake.
Na ni kwa sababu tu Kikwete ana huruma sana kwa viongozi wenye makosa ya wazi, ndio maana anaweza kuruhusu Mkapa ajipe wadhifa wa “mshauri” wa Rais katika kuwashughulikia wawekezaji feki waliokaribishwa wakati wa utawala wake. Vinginevyo, Kikwete asingeruhusu mtu aliyeshindwa kujishauri mwenyewe kuongoza nchi kwa maslahi ya umma atamke kuwa atambebesha Rais wa sasa mzigo wa kusafisha ‘uozo’ aliotenda.
Na kama CCM imekumbwa na virusi vinavyowafanya baadhi ya viongozi wake kuingilia mambo ya koo na familia za wanasiasa wa upinzani, mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Steven Wassira ameiga mfano wa Mkapa na kudai kuwa mgombea ubunge wa CHADEMA, Joshua Nassari hafai kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kuwa ni kijana mkorofi na mara kwa mara, baba yake mzazi amekuwa akimsihi kuachana na ukorofi tangu wakati akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Maneno haya yanatamkwa na mtu ambaye licha ya kuwa na wadhifa mkubwa ndani ya CCM pia ni waziri katika Ofisi ya Rais. Lakini tutegemee nini kwa mwanasiasa ambaye pengine ni maarufu zaidi kwa picha iliyosambaa mtandaoni akiwa kauchapa usingizi bungeni kuliko busara kutoka kinywani mwake!
Kama alimudu kusinzia wakati kikao cha Bunge kikiendelea, basi yayumkinika kuhisi hata huo wadhifa aliojipachika kuwa msemaji wa familia ya Nassari ni sehemu tu ya ndoto zake usingizini.
Lakini wito wa safu hii kwa familia ya Nassari ni huu, bila kujali matokeo ya uchaguzi wa Arumeru Mashariki ni muhimu kumfungulia Wassira kesi ya madai, awathibitishie Watanzania tuhuma alizotoa dhidi ya mgombea huyo. Ushauri kama huo unaelekezwa pia kwa Vincent Nyerere kwani kufanya hivyo kutatoa fundisho muhimu dhidi ya wanasiasa waropokaji.
Na kama tuhuma zake dhidi ya Nassari hazitoshi (na tayari baba wa mgombea huyo amezikanusha hadharani), Wassira amekaririwa akiendeleza matamshi yake tata kwa kudai kuwa Vincent Nyerere hawezi kutoka ukoo wa Nyerere eti kwa vile haiungi mkono CCM.
Huu ni uvivu wa kufikiri, kwa sababu hakuna sheria inayomlazimisha Mtanzania kufuata itikadi inayofuatwa na ndugu zake.
Kadhalika, Wassira ameendeleza kauli tata kwa kudai Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibroad Slaa alifanya ufisadi wa fedha za ziara ya Baba Mtakatifu John Paul wa Pili, alipozuru Tanzania mwaka 1990.
Japo Dk. Slaa hana tabia ya kufungua kesi za madai dhidi ya ‘wazushi’ wake, safari hii anapaswa kuangalia upya msimamo wake huo kwani njia pekee ya kuwafundisha ushirikiano kati ya ubongo na mdomo kwa watu aina ya Wassira ni kuwaburuza mahakamani.
Nimalizie kwa kutoa wito kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Kikwete kuwakumbusha wana-CCM wenzake kama Mkapa, Wassira na wengineo kuwa kampeni za uchaguzi Arumeru Mashariki ni za kupata mwakilishi bora bungeni na sio referendum (kura ya maoni) kuhusu ukoo wa Nyerere, familia ya Nassari au ziara ya Baba Mtakatifu mwaka 1990.
Na wito wangu kwa wana-Arumeru Mashariki ni huu, kiongozi yeyote anayeweza kuwadanganya hadharani hatosita kuwahujumu faraghani. Njia pekee ya kuwaadhibu wanasiasa kama Mkapa na Wassira ambao wanawafanya ninyi wapiga kura kuwa watu msiojua mnachotaka bali ni masuala kuhusu ukoo na familia ya fulani ni kumnyima kura mgombea wanayempigia kampeni.
Pengine kushindwa kwa mgombea wao kutawafanya wanasiasa hao kuwa makini kabla hawajaropoka chochote kile hadharani.



1 comment:

  1. Jambazi ni jambazi tu. Lakini mwalimu alishatuasa kuachana na majangili. Tukampuuza. Tukawapa hadi uwaziri mkuu. Tukayashuhudia. Subiri, kwa kuwa hatuna muda wa kufikiri vizuri tutawapa hata urais ili tuumie vizuri zaidi.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.